Tuesday, June 21, 2016

SUBRA (kusubiri)



SUBRA (kusubiri)
Mwaanadamu kama kiumbe wa Allah hakuachakuwa ni mwenyekupita katika mitihani mikumbwa ya  huzuni na hata furaha, kiasi kwamba njia pekee ya kufaulu katika mitihani hiyo ni kushikamana tu na kamba ya Subra.  Mwenyezi mungu (S.W) anasema;
كُلُّ نَفْسٍ ذَائِقَةُ الْمَوْتِ وَنَبْلُوكُم بِالشَّرِّ وَالْخَيْرِ فِتْنَةً وَإِلَيْنَا تُرْجَعُونَ
(Kila nafsi itaonja mauti; na tunakujaribuni kwa shari na kheri. Na kwetu sisi mtarejeshwa. (Al-Anbiyaa (17: 35).
Subra ambayo itamnufaisha mwanadamu ni ile tu, iliyojengwa juu ya misingi ya kisheria. Yaani inayoendana na mafundisho sahihi, nayo ni muongozo wa Allah (S.W) na maelekezo ya bwana mtume (SAW).
Misingi ya subra
Subra  ijengwe juu ya misingi ya:
a)    Imani                    
b)    Ikhlaaswi     
c)     Kushukuru
Bwana Mtume (S.A.W)  anasema:
عجبا لأمر المؤمن إن أمره كله خير ، وليس ذاك لأحد إلا للمؤمن ؛ إنأصابته سرّاء شكر؛ فكان خير له····
Ajabu  ya  jambo  la  Muumin  kwamba  kila  jambo  lake  ni  kheri.  Na halipatikani  hili  isipokuwa  kwa  Muumin.  Anapofikwa  na  jambo  zuri hushukuru nayo ni kheri kwake na anapofikwa na jambo lenye madhara husubiri nayo ni kheri kwake))

Tahadhari
Wapo baadhi ya watu wanamtazamo potofu juu ya mitihani ambayo Allah (S.W) huwajaribu waja wake.  Kwa mfano, wapo wanaoamini kwamba, kwa kadri mja anapopatwa na mitihani hasa ya kuondokewa na ndugu zake wa karibu, upungufu wa mali, watoto na mithili ya hayo, ni kutokana na kukasirikiwa na Allah (S.W).

Yapasa ieleweke kuwa jambo hilo halitokuwa sahihi, na ni sawa na hadithi za sungura na fisi tu.   Mtume (S.A.W) amesema:
            Kutoka kwa Anas kwamba Mtume   amesema:  ((Allaah Anapompendelea  mja  Wake  kheri,  Humharakishia  adhabu  duniani.  Na Allaah  Anapomtakia  mja  Wake  shari  Humzuilia  dhambi  zake  hata Amlipe  Siku  ya  Qiyaamah)).
Na  amesema  Mtume   (S.A.W):
            (Hakika malipo makubwa kabisa yapo pamoja na mtithani mkubwa, na hakika Allaah Anapopenda watu Huwapa mtihani. Basi atakayeridhika atapata radhi (za Allaah)na atakayechukia atapata ghadhabu)) At-Tirmidhiy (Hadiyth Hasan Swahiyh).
“Aidha, imesimuliwa, kutoka kwa Sa’iyd bin Abi Waqaasw (R.A) amesema: Nilimuuliza Mtume (S.A.W): “Ee Mjumbe  wa  Allaah!  Watu  gani  wanaopata  mitihani  migumu  zaidi? Akasema: ((Mitume, kisha mfano wake, na mfano wake. Hupewa mtihani mtu  kulingana  na  Dini  [imani] yake.  Ikiwa  Dini  yake  ni  imara,  mtihani wake  huwa  mkubwa.  Na  ikiwa  Dini  yake  ni  dhaifu  hupewa  mtihani kulingana  na  Dini  yake.  Husibiwa  sana  na  mtihani  mmojawapo  hadi atatembea ardhini bila ya kuwa na dhambi)) At-Tirmidhiy (Hadiyth  Hasan  Swahiyh) .
Vilevile, kutoka kwa ‘Aaishah (R.A) (amesema: “Mtume  akisema:  ((Hakuna  msiba  wowote  unaomsibu  Muislamu  isipokuwa tu Allaah Humfutia madhambi hata mwiba unaomchoma)) Al-Bukhaariy na Muslim

SUBIRA NI SIFA ZA WAJA WEMA WA ALLAH
a)      Nabii Ismail, Idrisa na Dhal Kifli.
وَإِسْمَاعِيلَ وَإِدْرِيسَ وَذَا الْكِفْلِ كُلٌّ مِّنَ الصَّابِرِينَ
 Na [taja] Ismaa’iyl na Idriys na Dhal-Kifl, wote ni miongoni mwawenye kusubiri)) Al-Anbiyaa (17: 85).
b) Nabii Ayyub
إِنَّا وَجَدْنَاهُ صَابِرًا نِعْمَ الْعَبْدُ إِنَّهُ أَوَّابٌ
 Tumemkuta ni mwenye subira sana, uzuri ulioje wa mja, hakika yeye ni mwenye kurudiarudia kutubia [Kwetu])) (Swaad (38: 44).
b)      Ulu-l azmi Mina rrusul
            ((Basi subiri [ee Muhammad] kama walivyosubiri Mitume wenye ustahmilivu mkubwa)) (Al-Ahqaaf (46: 35).

Vigawanyo vya  Subira
Subira imegawika katika sehemu kuu nne:

1.      Subira katika utiifu. Yaani kusubiri katika ‘amali anazotenda mja kwa kutumia mwili au ulimi wake (kumdhukuru Allaahi). Allah ana sema;
وَاسْتَعِينُواْ بِالصَّبْرِ وَالصَّلاةِ وَإِنَّهَا لَكَبِيرَةٌ إِلاَّ عَلَى الْخَاشِعِينَ
 ((Na tafuteni msaada kupitia subira na Swalah; na hakika hilo ni kubwa isipokuwa kwa Khaashi’iyn [wanyenyekevu])) Al-Baqarah (2: 45).
Aidha Mwenyezi mungu anasema katika Suuratu Twaahaa:
وَأْمُرْ أَهْلَكَ بِالصَّلاةِ وَاصْطَبِرْ عَلَيْهَا لا نَسْأَلُكَ رِزْقًا نَّحْنُ نَرْزُقُكَ وَالْعَاقِبَةُ لِلتَّقْوَى
((Na waamrishe watu wako kuswali, na uendelee mwenyewe kwa hayo)) Twaahaa (20: 132).
2.      Subira katika maasi. Kusubiri katika kuacha kutenda jambo lisilokuwa lenye kuridhisha kwa kutumia mwili au ulimi wako.

3.      Subira katika Qadhwaa (Yaliyopangwa) na Qadar (Yaliyokadiriwa) ya Allaah. Kusubiri katika kuizuia nafsi isiungulike au isimahanike au isighadhibike kutokana na mitihani inayomsibu mja. Allah (S.W) anasema;
 . وَنَبْلُوكُم بِالشَّرِّ وَالْخَيْرِ فِتْنَةً
((Na Tunakufanyieni mitihani kwa [mambo ya] shari na ya kheri)) Al-Anbiyaa (17: 35)
Katika suuratul Al – Fajri  (89: 15 – 16 )Allah (S.W) anasema;
فَأَمَّا الإِنسَانُ إِذَا مَا ابْتَلاهُ رَبُّهُ فَأَكْرَمَهُ وَنَعَّمَهُ فَيَقُولُ رَبِّي أَكْرَمَن وَأَمَّا إِذَا مَا ابْتَلاهُ فَقَدَرَ عَلَيْهِ رِزْقَهُ فَيَقُولُ رَبِّي أَهَانَنِ  
Ama binaadamu anapojaribiwa na Mola wake, Akamkirimu na Akamneemesha, husema: Mola wangu Amenikirimu!  Na ama Anapomjaribu Akampunguzia riziki yake, husema: Mola wangu Amenitia unyonge!”
Na katika Suuratul-Baqara, Allah (S.W) anasema;
وَلَنَبْلُوَنَّكُمْ بِشَيْءٍ مِّنَ الْخَوْفْ وَالْجُوعِ وَنَقْصٍ مِّنَ الأَمْوَالِ وَالأنفُسِ وَالثَّمَرَاتِ وَبَشِّرِ الصَّابِرِينَ···

Na bila shaka Tutakujaribuni kwa kitu katika khofu na njaa na upungufu wa mali na nafsi na mazao. Na wabashirie wenye kusubiri. Wale ambao unapowafika msiba husema: (Innaa liLlaahi wa Innaa Ilayhi Raaji’uwn) “Hakika sisi ni wa Allaah na hakika sisi Kwaketutarejea”. Hao juu yao zitakuwa Baraka kutoka kwa Mola wao na Rehma, na hao ndio wenye kuongoka)) Al-Baqarah (2: 155-157).

5. Subira kutokana na maudhi ya watu
Ni kuzuia nafsi, ulimi na viungo visilipize maovu anayotendewa mtu.  
     
وَإِنْ عَاقَبْتُمْ فَعَاقِبُواْ بِمِثْلِ مَا عُوقِبْتُم بِهِ وَلَئِن صَبَرْتُمْ لَهُوَ خَيْرٌ لِّلصَّابِرِينَ
((Na mkilipiza [kuadhibu adui au Waumini] basi lipizieni [kuadhibu] kulingana na vile mlivyodhuriwa. Na mkisubiri basi bila shaka hivyo ni ubora kwa wenye kusubiri.

وَاصْبِرْ وَمَا صَبْرُكَ إِلاَّ بِاللَّهِ وَلاَ تَحْزَنْ عَلَيْهِمْ وَلاَ تَكُ فِي ضَيْقٍ مِّمَّا يَمْكُرُونَ
           
Na subiri. Na kusubiri kwako kusiwe ila kwa ajili ya Allaah. Wala usihuzunike kwa ajil yao, wala usiwe katika dhiki kutokana na hila wanazozifanya.  (An-Nahl (16: 126-127).
Katika Suuratu – Luqmaan, Luqmaan anamuusia mwanawe;
يَا بُنَيَّ أَقِمِ الصَّلاةَ وَأْمُرْ بِالْمَعْرُوفِ وَانْهَ عَنِ الْمُنكَرِ وَاصْبِرْ عَلَى مَا أَصَابَكَ إِنَّ ذَلِكَ مِنْ عَزْمِ الأُمُورِ
((Ee mwanangu! Simamisha Swalah, na amrisha mema, na kataza maovu, na subiri kwa yanayokupata. Hakika hayo ni katika mambo ya kuazimiwa) Luqmaan (31: 17)

Kwa nini subra?
i.                    Wenye kusubiri ni wapenzi ya Allaah
((…na Allaah Anawapenda wanaosubiri. Al- Imran 146))
ii.                  Wenye kusubiri siku zote wapo pamoja na Allaah:
           
            (….hakika Allaah Yu Pamoja na wanaosubiri . Al-baqara 246))

iii.                Allaah    amewatunukia  bishara njema;  Baraka  [na  Maghfirah],  Rehma  Yake, 
            Na bila shaka tutakujaribuni kwa kitu katika khofu na njaa na upungufu wa mali na nafsi na mazao. Na wabashirie wenye kusubiri. Wale ambao unapowafika msiba husema: Innaa liLlaahi wa Innaa Ilayhi Raaji’uwn. (Hakika sisi ni wa Allaah na hakika sisi Kwake tutarejea)”. Hao juu yao zitakuwa Baraka kutoka kwa Mola wao na Rehma, na hao ndio wenye kuongoka) (Al- Baqara 155-157)
iv.                Allaah  Ameahidi  kuwalipa  malipo  mazuri  kabisa  kwa sababu ya kusubiri kwao.  
مَا عِندَكُمْ يَنفَدُ وَمَا عِندَ اللَّهِ بَاقٍ وَلَنَجْزِيَنَّ الَّذِينَ صَبَرُواْ أَجْرَهُم بِأَحْسَنِ مَا كَانُواْ يَعْمَلُونَ
            (Mlivyo navyo vitakwisha na vilivyoko kwa mwenyezi Mungu ndivyo vitakavyobakia. Na kwa yakini Sisi Tutawalipa ambao wamesubiri ujira wao kwa mazuri waliyokuwa wakitenda)) An-Nahl (16: 96).

v.                  Allaah   Ameahidi  Maghfirah  na  ujira  mkubwa  kwa wenye kusubiri na wakatenda mema.
إِلاَّ الَّذِينَ صَبَرُواْ وَعَمِلُواْ الصَّالِحَاتِ أُوْلَئِكَ لَهُم مَّغْفِرَةٌ وَأَجْرٌ كَبِيرٌ
(Isipokuwa ambao wamevumilia wakatenda mema, hao watapata Maghfirah na ujira mkubwa) Huwd (11: 11).

vi.                Allaah ameifanya  subira  kuwa  ni  kinga  kubwa  kwa maadui na hila zao, kama walivyoaahidiwa Maswahaba katika vita vya Uhud.
إِن تَمْسَسْكُمْ حَسَنَةٌ تَسُؤْهُمْ وَإِن تُصِبْكُمْ سَيِّئَةٌ يَفْرَحُواْ بِهَا وَإِن تَصْبِرُواْ وَتَتَّقُواْ لاَ يَضُرُّكُمْ كَيْدُهُمْ شَيْئًا إِنَّ اللَّهَ بِمَا يَعْمَلُونَ مُحِيطٌ
(Na ikikupateni kheri huwaudhi. Na ikikupateni shari wanafurahi. Na nyinyi mkisubiri na mkawa na taqwa haitakudhuruni chochote katika hila zao. Hakika Allaah kwa wayatendayo ni Mwenye Kuzunguka yote wayatendayo. (Aal-‘Imraan (3: 120).
Na Allah ni mjuzi zaidi

Monday, June 20, 2016

IFAHAMU IBADA YA FUNGA (SAUMU) YA RAMADHANI

AL-AKHY MUBARAKA GHULAAM


01.         MAANA YA FUNGA

Funga (Saum) kilugha maana yake ni ni kujizuilia.  
Kisheria funga (Saumu) ni ibada ya kujizuilia kula, kunywa, na vyote vinavyo funguzisha kama vile kuvuta sigara, kujamii, kujitoa manii, kujitapisha  na mengineyo, kwa kipindi cha kati ya Al-fajri ya kweli mpaka kuingia magharibi kwa kunuilia kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Ta’ala).

Ili saumu ya mfungaji iwe na maana na yenye kufikia lengo, hana budi mfungaji kukizuilia (kukifungisha) kila kiungo chake cha mwili - macho, ulimi, masikio, mikono, miguu, pamoja na fikra na hisia zake na matendo yote aliyokataza Allah (Subhaanahu wa Ta’ala).

a)      Funga ya macho ni kujizuilia na kuangalia aliyoyakataza Allah (Subhaanahu wa Ta’ala);
b)      Funga ya ulimi ni kujizuilia na mazungumzo yote aliyoyakataza Allah (Subhaanahu wa Ta’ala) kama vile kusengenya, kusema uwongo au kugombana.
c)      Funga ya masikio ni kujizuia kusikiliza yale yote aliyoyaharamisha Allah (S.W).
d)     Funga ya miguu ni kujizuilia na kuyaendea yale yote aliyoyakataza Allah (Subhaanahu wa Ta’ala)
e)      Funga ya fikra na hisia ni kujizuia na fikra na dhana mbaya ambazo zinampelekea kuvunja amri na makatazo ya Allah (Subhaanahu wa Ta’ala).  
Mtume (Swalla Allaahu ‘alahyi wa aalihi wa sallam) anasema:
 من لم يدع قول الزور والعمل به فليس لله حاجة في أن يدع طعامه وشرابه

  “Yule ambaye haachi kusema uwongo na haachi kufanya vitendo viovu, Allah hana haja na kuona kuwa anaacha chakula chake na kinywaji chake’’ yaani Allah (Subhaanahu wa Ta’ala) hana haja na funga yake.

02.  NAFASI YA FUNGA YA RAMADHANI KATIKA UISLAMU

Funga ya Ramadhani ni miongoni mwa nguzo za Uislamu na ni faradhi kwa Waislamu kama inavyobainika katika aya ifuatayo:
أَيُّهَا الَّذِينَ ءَامَنُواْ كُتِبَ عَلَيْكُمُ الصِّيَامُ كَمَا كُتِبَ عَلَى الَّذِينَ مِن قَبْلِكُمْ لَعَلَّكُمْ تَتَّقُونَ
‘’Enyi mlioamini! Mmefaradhishiwa kufunga (saumu) kama walivyofaradhishwa waliokuwa kabla yenu ili mpate kumcha Mungu’’ (2:183)

Kama ilivyo katika nguzo nyingine za Uislamu, mtu atakapoivunja makusudi nguzo hii hatabakia kuwa Muislamu japo atajiita Muislamu na watu wakaendelea kumwita hivyo.

 

03.         kuTHIBITI KUINGIA MWEZI WA RAMADHANI

kuthibiti kuingia mwezi Mtukufu wa Ramadhani kutategemea moja ya mawili yafuatayo:
a)      Kukamilika siku thelathini (30) za mwezi wa Shaabani.
b)      Kuonekana mwezi mwandamo siku ya  29 ya mwezi wa Shaabani.
Angalizo;
Mwezi wa kuingia Ramadhani inatosha kuonwa na Muislamu mmoja mwadilifu ama mwezi wa kumalizika Ramadhani ni lazima uonwe na Waislamu waadilifu wawili au zaidi.

04.        NANI iNAmuWAJIBIKiA FUNGA YA RAMADHANI?

Funga ya Ramadhani inamuwajibikia kila Muislamu, ambaye ni:
i)                    Baleghe
ii)                   Mwenye akili
iii)                Alie katika mji wake (asiwe msafiri)
iv)                Mwenye siha (afya- asiwe mgonjwa)
v)                  Asiwe na mambo yanayozuia kusihi kwa funga (kama hedhi na nifasi kwa wanawake).
Zingatio.
Inatakikana kwa wazazi kuwafundisha kufunga watoto wao wanapofikia umri wa miaka  saba (7) na kuwalazimisha hadi ikibidi kuwapiga wanapofikia umri wa mika kumi (10).  

 

05.          Ni akina nani WALIORUHUSIWA KUTOFUNGA

i.                    Walio katika safari na wagonjwa wa kawaida.
Hawa ni wale ambao kufunga kwao kutawafanya wawe wagonjwa zaidi. Haipendezwi kwa watu hao kufunga badala yake itawawajibikia kuja kulipa siku hizo wasizofunga baada ya Ramadhaan.
Ama kwa upande wa Msafiri, ni safari ya siku mbili kwa kutumia kipando cha ngamia yaani (mar-hala mbili) kwa lugha ya kitaalamu, ambayo ni sawa na umbali wa takribani kilomita (85km).

ii.                  Wanawake walio katika hedhi na Nifaas. Hawaruhusiwi kufunga, na wakifunga katika hali hio, basi Swawm yao haitokubaliwa. Nao pia ni lazima walipe kila siku walizoacha baada ya Ramadhaan.

iii.                Wanawake wajawazito na wanaonyonyesha (ikiwa watakhofu kuwa Swawm itawadhuru watoto wao au wenyewe). Na ni lazima wafunge baada ya Ramadhaan kulipa siku zao. Na ikiwa waliacha kufunga kwa sababu tu ya kukhofia afya ya watoto wao, basi wanapaswa kulipa na kumlisha maskini mmoja kwa kila siku moja iliyowapita katika Ramadhaan.

iv.                Vikongwe (Vizee) na wenye maradhi sugu (yasiyotarajiwa kupona). Kwa wao inawatosheleza kulisha maskini mmoja kwa kila siku moja wanayoshindwa kufunga.  

v.                  Iliyemzidi njaa na akahofia kuangamia. Huyu pia ni mwenye udhuru katika nyudhuru za kuruhusiwa kuacha kufunga, na itamuwajibikia kuja kulipa kama kundi la kwanza la wagonjwa wa kawaida.

06.        YANAYOBATILISHA (YANAYOHARIBU) SWAWM

        i.            Kula na kunywa kwa makusudi. Na sio kwa kusahau wala kwa bahati mbaya au kwa kulazimishwa, katika mchana wa ramadhani.
      ii.            Kujitapisha kwa makusudi.  
    iii.            Mume kumuingilia Mke wake. Na pia kumkumbatia au kumchezea hadi yakamtoka manii.
    iv.            Kujitoa manii kwa makusudi kwa njia yoyote ile.  .
      v.            Kupatwa na Hedhi au Nifasi kwa Mwanamke. Hata kukiwa kutokea huko kuwa ni wakati wa kukaribia kufuturu/kufutari.
    vi.            Mwenye kutia Nia ya kula wakati amefunga, kwa sharti kuwa kaazimia tendo hilo hata kama hakulitekeleza

07.        YASIYOBATILISHA (YASIYOHARIBU) SWAWM

i.                     Kula au kunywa kwa kusahau, kimakosa au kulazimishwa.

ii.                   Kuingia maji ndani ya matundu ya mwili bila kukusudia, kwa mfano wakati wa kuoga.

iii.                Kudungwa sindano mwilini wakati wa maradhi.

iv.                Dawa ya maji idondoshewayo machoni.

v.                  Kuoga na kujimwagia maji mwilini wakati wa joto kali.

vi.                Kuonja chakula kwa mpishi kwa sharti asimeze kile akionjacho.

vii.              Kumbusu au kumkumbatia mkeo, kwa sharti awe mtu ana uwezo wa kujizuia na kudhibiti matamanio yake.

viii.             Haitobatilika Swawm ya mtu atakayeamka na janaba (lakini akishaamka akoge) au atakayeota mchana wa ramadhan akatokwa na manii.
ix.                Kukoga, kupiga mswaki, kusukutua au kusafisha pua kwa kutia maji puani bila kuzidisha.

08.        BAADHI YANAYOSUNIWA KWA MFUNGAJI


1.  Kula daku.
 Imepokewa hadithi kutoka kwa Anas Ibn Maalik (Radhiya Allahu ‘anhu) kuwa amesema Mtume (Swalla Allaahu ‘alahyi wa aalihi wa sallam): ‘’Kuleni daku kwani hakika chakula cha daku kina baraka ndani yake’’ (Al Bukhariy na Muslim). Na inasuniwa kuchelewesha kula daku mpaka kukaribia alfajiri.

2.  Kuharakisha kufutari (mara tu likizama jua).
Imepokewa hadithi kutoka kwa Sahl ibn Saad (Radhiya Allahu ‘anhu) kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alahyi wa aalihi wa sallam) amesema: ‘’Watu watakuwa bado wapo katika kheri muda wa kuwa wanaharakisha futari’’ (Al Bukhariy na Muslim).
   
3.  Kuanza kufutari kwa tende au maji.
 Imepokewa hadithi kutoka kwa Salmaan Ibn‘Aamir (Radhiya Allahu ‘anhu) kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alahyi wa aalihi wa sallam) amesema: ‘’Anapofutari mmoja wenu basi na afuturu kwa tende na kama hakupata (tende) basi na afutari kwa maji kwani hakika ya maji ni kitoharisho (kisafisho)’’ ( Wameipokea Maimamu watano).

4.  Kuzidisha kuomba dua.
Pia inasuniwa kwa mfungaji kuzidisha kuomba dua na hasa wakati wa kufutari, kwani dua ya mfungaji na hasa wakati wa kufutari ni katika dua zinazokubaliwa na Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa  Ta’ala).

09.        BAADHI YANAYOTAKIWA AYAKITHIRISHE MUISLAMU KATIKA MWEZI WA RAMADHANI

1.  Kisimamo cha usiku (Swalah ya tarawehe)
Amesema Mtume (Swalla Allaahu ‘alahyi wa aalihi wa sallam):
من قام رمضان إيماناً واحتساباً غُفر له ما تقدم من ذنبه    

‘’Mwenye kusimama (kwa ibada) katika mwezi wa Ramadhani kwa imani (thabiti) na hali ya kutaraji malipo toka kwa Allah (Subhaanahu wa Ta’ala) husamehewa yale aliyoyafanya katika madhambi yake’’.

Na inafaa kwa wanawake kuhudhuria Swalah katika misikiti maadamu watachunga na kufuata taratibu za dini (sharia). Na haifai kwa wanaume kuwazuilia wanawake walio katika usimamizi wao kuhudhuria ibada hizo bila ya kuwa na sababu za kimsingi zinazo kubalika kisheria, amesema Mtume(Swalla Allaahu ‘alahyi wa aalihi wa sallam):
‘‘wakiwaombeni ruhusa wanawake zenu kwenda msikitini basi waruhusuni’’ (Muslim).

2.  Kuzidisha kusoma Qur-aan.
Mwezi wa Ramadhani ni mwezi wa Qur-aan na ndio mwezi ulioteremshwa ndani yake Qur-aan, Amesema Allah (Subhaanahu wa Ta’ala):

إِنَّا أَنزَلْنَاهُ فِي لَيْلَةِ الْقَدْرِ
‘’Hakika tumeiteremsha (Qur-aani) katika laylatul-Qadr (usiku wenye heshima kubwa), (usiku wa mwezi wa ramadhani)’’ (97:1).
Na

شَهْرُ رَمَضَانَ الَّذِيَ أُنزِلَ فِيهِ الْقُرْآنُ هُدًى لِّلنَّاسِ وَبَيِّنَاتٍ مِّنَ الْهُدَى وَالْفُرْقَانِ
‘’Mwezi huo mlioambiwa mfunge ni mwezi wa Ramadhani ambao imeteremshwa katika (mwezi) huo hii Qur-aani…’’ (2:185).

3.  Sadaka.
Pamoja na fadhila zake katika masiku yote huzidi fadhila na thawabu zake katika mwezi wa Ramadhani. Na katika sadaka zinazotiliwa mkazo katika mwezi wa Ramadhani ni kuwafuturisha waliofunga, amesema Mtume (Swalla Allaahu ‘alahyi wa aalihi wa sallam):

من فطَّر صائما كان له مثلُ أجرِه غيرَ أنه لا ينقص من أجر الصائم شيئا
‘’Mwenye kumfutarisha aliyefunga anakuwa na malipo mfano wa malipo ya aliyemfutarisha na hayapungui malipo ya aliyefunga kitu chochote’’. (Ahmad na Annasaiy).

4.  Kufanya Umrah.
Amesema Mtume (Swalla Allaahu ‘alahyi wa aalihi wa sallam):
‘’Umrah katika mwezi wa Ramadhani una malipo sawa na Hijjah’’ (Muslim).

5.  Itikafu
Itikafu ni kubaki msikitini bila ya kutoka ukijishughulisha na ibada mbalimbali, inasuniwa kufanya itikafu na hasa katika kumi la mwisho la mwezi wa Ramadhani. Imepokewa hadithi kutoka kwa Ibn ‘Umar (Radhiya Allahu ‘anhuma)  amesema;

كان رسول الله صلى الله عليه وسلم يعتكف العشر الأواخر من رمضان .اخرجه البخاري
Alikuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alahyi wa aalihi wa sallam) akifanya itikafu siku kumi za mwisho za mwezi wa Ramadhani. (Al Bukhariy).

6.  Kuutafuta usiku wa cheo (laylatul-qadr).
Zaidi katika kumi la mwisho la Ramadhani, imepokewa hadithi kutoka kwa Mama ‘Aishah (Radhiya Allahu ‘anha)  amesema: Amesema Mtume (Swalla Allaahu ‘alahyi wa aalihi wa sallam):
‘’Utafuteni usiku wa cheo (laylatul-qadri) katika siku kumi za mwisho za Ramadhani’’ (Al Bukhariy na Muslim)

Na amepokea Abu Hurayrah (Radhiya Allahu ‘anhu) kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alahyi wa aalihi wa sallam) amesema:
’Mwenye kusimama katika usiku wa cheo (laylatul-qadri) kwa imani thabiti na kwa kutaraji malipo kutoka kwa Allah (Subhaanahu wa Ta’ala) husamehewa madhambi alioyafanya (kabla ya hapo’’ (AlBukhariy na Muslim).

7.  Toba.
Nako ni kurudi kwa Allah (Subhaanahu wa Ta’ala) kutokana na makosa aliyoyatenda mja na kuomba msamaha kutoka kwake, kujuta na kuazimia kutokuyarudia tena makosa hayo.  

10.         FADHILA ZA SWAUMU

1. Funga inamuokoa mtu kutokana na moto
    Mtume (Swalla Allaahu ‘alahyi wa aalihi wa sallam) amesema:
   "Swawm ni kinga itamukoa mja kutokana na moto (siku ya Qiyaamah)’’

   Na katika hadithi nyingine Mtume (Swalla Allaahu ‘alahyi wa aalihi wa sallam) amesema:
  "Mwenye kufunga siku kwa ajili ya Allah Mwenyeezi Mungu Atamuokoa uso wake kutokana na moto kwa  umbali wa miaka sabini"

2. Swawm ni kinga kutokana na matamanio
    Amesema Mtume (Swalla Allaahu ‘alahyi wa aalihi wa sallam):
    ‘’Enyi kundi la vijana miongoni mwenu atakae kuwa na uwezo wa kuoa basi na aoe, (kufanya hivyo) kutampelekea kuinamisha macho yake na kuhifadhi tupu yake. Ikiwa hana uwezo wa kuoa basi na  afunge  kwani hiyo ni kinga kwake’’.


 3. Swawm ni njia ya kumpelekea mtu peponi
     Kutoka kwa Abu Umamah (Radhiya Allahu ‘anhu) amesema kumwambia Mtume (Swalla Allaahu ‘alahyi wa aalihi wa sallam);
“Ewe Mtume wa Allah Niamrishe mimi jambo litakalonifaa mbele ya Allah”. Akasema Mtume (Swalla Allaahu ‘alahyi wa aalihi wa sallam) “Ni juu yako kufunga kwa hakika hakuna  mfano wake"

4. Funga itamuombea mtu siku ya Qiyaamah:
    Amesema Mtume (Swalla Allaahu ‘alahyi wa aalihi wa sallam

الصيام والقرآن يشفعان للعبد يوم القيامة، يقول الصيام: أي رب، منعته الطعام والشهوات بالنهار فشفِّعني فيه، ويقول القرآن: منعته النوم بالليل فشفعني فيه، قال: فيُشفَّعان   
 "Funga na Qur-aan zitamuombea mja siku ya Qiyaamah, itasema funga: ewe Mola amejizuilia kutokana na chakula chake na matamanio yake wakati wa mchana, basi nnamuombea msamaha, na itasema Qur-aan: amejizuilia kutokana na usingizi wake wakati wa usiku ninamuombea msamaha. Atasema  wamesamehewa’’

5. Swawm ni kafara na msamaha kutokana na madhambi:
  Mtume (Swalla Allaahu ‘alahyi wa aalihi wa sallam) amesema:

 : من صام رمضان إيمانا واحتسابا غفر له ما تقدم من ذنبه
 
    "Mwenye kufunga Ramadhaan kwa imani na akatarajia malipo atasamehewa madhambi yake
    aliyoyatanguliza"

 


11.  YANAYOPASWA KUJIEPUSHA NAYO MFUNGAJI.


1.  Tabia chafu na maneno maovu, kama kusengenya, kusema uongo, na kadhalika.

2.  Kuzidisha usingizi (kulala kupita kiasi) ambao unampotezea Muislamu fursa ya kufanya ibada zaidi.

3.  Kupoteza wakati mwingi katika michezo na maongezi yasiyo na faida, na kuacha kuutumia wakati huo katika kazi na ibada mbali mbali.

4.  Kuacha kula daku au kuchelewa kufuturu baada ya kutwa kwa jua.

5.  Kufanya israfu katika vyakula na vinywaji wakati wa kufutari.

6.  Kufutari kwa vyakula vyenye harufu ya kuchukiza, kama: vitunguu thaumu,vitunguu maji, doriani, na kadhalika kwa kuhofia kuwaudhi Waislamu wakati mnapojumuika  kwa Swalah.

7.  Kutokuswali tarawehe kwa utulivu na unyenyekevu.

 

 

12. YANAYOTAKIWA KWA KUMALIZIKA RAMADHANI.


1.      Kutoa zakatul-fitri, nayo ni wajibu kwa kila Muislamu, (mwanamume, mwanamke, mkubwa, mdogo, muungwana (huru) au mtumwa).
Watoto wadogo,Watumwa na pia Wanawake waliochini ya usimamizi wa Wanaume itawalazimikia zakah hio wasimamizi wao. Ama Wanawake wanaojitegemea itawalazimikia wao wenyewe.  Na inatakikana itolewe zakatul-fitri kabla ya Swalah ya iddi.
Imepokewa hadithi kutoka kwa Ibn ‘Umar (Rradhiya Allahu ‘anhuma)  amesema:
‘’Amefaradhisha Mtume (Swalla Allahu ‘alayhi wa sallam) Zaka ya fitri (ya kumalizika Ramadhani) pishi ya tende au pishi ya shairi kwa mtumwa na huru (muungwana), mume na mke, mdogo na mkubwa katika waislamu, na akaamrisha (hiyo zakah ya fitri) itolewe kabla ya kutoka watu kuelekea katika Swalah (ya iddi)’’. (Al Bukhariy na Muslim).

Na wajibu ni kutoa pishi ya chakula maarufu katika mji uliopo (ambayo ni sawa na uzito wa kilo mbili na gramu mia nne (2.4 kg) takribani kwa nafaka kama mchele na mfano wake au thamani yake.

2.  Takbir; inasuniwa kuleta takbir baada ya kuandama (kuonekana) mwezi wa kumalizika Ramadhani, kuanzia kuchwa (kuzama) kwa jua mpaka wakati wa Swalah ya iddi. Na inasuniwa kunyanyua sauti kwa wanaume njiani, masokoni na hata majumbani.


3.  Kuhudhuria swalah ya iddi, kwa wanaume na wanawake.

4.  Inasuniwa kula tende kwa idadi ya (witri) au chakula chengine hafifu kabla ya kutoka kwa ajili ya Swalah ya iddi al-fitri.

5.  Inasuniwa kubadilisha njia wakati wa kwenda na kurudi kwenye Swalah ya iddi. Imepokewa hadithi kutoka kwa Jaabir (radhiya Allahu ‘anhu)  amesema: Alikuwa Mjumbe wa Allah (Swalla Allahu ‘alayhi wa sallam) inapokuwa siku ya iddi akibadilisha njia (ya kwenda na ya kurudia). (Al Bukhary).

6.  Kuvaa mavazi bora zaidi anayoyamiliki Muislamu.
Na inatakikana kwa wale wenye familia kuwaandalia mavazi mazuri watu wa familia zao (bila ya kufanya israfu).

7.  Pia inasuniwa baada ya kumalizika Ramadhani kufunga siku sita katika mwezi wa mfunguo mosi (shawwali).
Amesema Mtume (Swalla Allahu ‘alayhi wa sallam):

 من صام رمضان ثم أتبعه ستاً من شوال، كان كصيام الدهر


{Mwenye kufunga Ramadhani kisha akaifuatilizia siku sita katika mwezi wa shawwali (mfunguo mosi) inakuwa kama aliyefunga mwaka (mzima kamili).(Muslim).

Tanbihi:
Ni haramu kufunga ndani ya siku ya Iddi. Imepokewa hadithi kutoka kwa Abu Said Al khudriy (radhiya Allahu ‘anhu) :( Hakika Mjumbe wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allahu ‘alayhi wa sallam) amekataza kufunga katika siku mbili: Siku ya (iddi) alfitri na siku ya (iddi) ya kuchinja (iddi l-adh‘ha).(Al Bukhariy na Muslim).


Na allah ni mjuzi zaidi.