DALILI ZA KUKARIBIA KWA SIKU YA QIYAAMAH
IMETAYARISHWA NA MUHAMMAD FARAJ
SALEM AL SAIY
Mwenyezi Mungu Amemleta Mtume wake Muhammad (Swalla
Llaahu ‘alayhi wa sallam) akiwa kama ni mletaji habari njema na muonyaji ambaye
hakuacha jambo lolote la kheri isipokuwa ametujuulisha nalo na kutuhimiza
kulikimbilia, na hakuacha jambo lolote la shari isipokuwa ametutahadharisha
nalo.
Na kwa vile Ummah huu ni Ummah wa mwisho, basi
Mtume huyu mtukufu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) ametuletea kutoka kwa Mola
wake dalili za kutosha zilizo wazi, zenye kutujuulisha juu ya kukaribia kwa
Siku ya Qiyaamah. Akatubainishia kwa ulimi wake, tena kwa ufasaha kabisa, juu
ya baadhi ya yatakayotokea katika mwisho wa zama. Akatuhakikishia kuwa yote
hayo lazima yatatokea, haya yote yakiwa ni dalili juu ya ukweli wa Utume wake
(Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) utakayowafanya watu wajitayarishe vizuri na
Siku hiyo. Siku ambayo mtu hatovuna isipokuwa kile alichochuma, na hatokuwa na
wakumlaumu isipokuwa nafsi yake.
Mwenyezi Mungu Anasema:
{{“Isije ikasema nafsi (asije akasema
mtu); “Eee majuto yangu kwa yale niliyopunguza upande wa Mwenyezi Mungu, na
hakika nilikuwa miongoni mwa wanaoyafanyia mzaha (mambo ya diyn)”.
Au ikasema; “Kama Mwenyezi Mungu
angeniongoa bila shaka ningekuwa miongoni mwa wenye kumcha Mwenyezi Mungu”.
Au ikasema ionapo adhabu; “Kama ningepata
marejeo (ya kurejea tena duniani)
ningekuwa miongoni mwa wafanyao mema”.
(Ataambiwa) “Kwa yakini! Bila shaka
zilikujia Aayah (dalili) zangu ukazikadhibisha na ukajivuna na ukawa miongoni
mwa wanaotakabari”.}}
[Az-Zumar: 56-59]
Katika kuzijua dalili hizo kisha kuziona
zikitendeka hapa duniani kunampatia mtu faida nyinigi sana zikiwemo zifuatazo:
·
Kuwa na uhakika juu ya ukweli wa
Utume wake Muhammad (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam).
·
Kujitayarisha vizuri na Siku ya
Qiyaamah. Kwani kwa mfano mtu anapopewa
habari juu ya meli inayokaribia kuwasili bandarini, huingoja meli hiyo huku akiwa na wasi wasi mwingi.
Lakini anapoisika sauti ya selo ya
meli hiyo, anakuwa na uhakika usio na shaka kuwa meli sasa imekaribia kweli kuwasili.
Mfano huu ni sawa na mtu aliyejuulishwa juu ya
dalili ya kukaribia kwa Siku ya Qiyaamah, kisha akaziona dalili hizo
zikitendeka mbele ya macho yake kama zilivyoelezwa na Mtume wa Mwenyezi Mungu
(Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam). Mtu huyo anakuwa na uhakika usio na shaka wa
kuwepo kwa siku ya Qiyaamah.
·
Kwa ajili hiyo, kuzijua na
kuziona dalili za kukaribia kwa Siku ya Qiyaamah
kunaongeza pia yakini juu ya ukweli wa kukaribia kwa Siku hiyo.
·
Kunamsaidia mtu kutoyumbishwa na
masaibu, mitihani na machafuko yanayotekea
kila siku. Kwani akirudi katika mafundisho ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) ataona kuwa
yote hayo yamekwishatajwa kuwa yatakuja kutokea.
·
Kunamsaidia mtu aliyejisahau
akawa anaikimbilia dunia, anapoziona dalili
hizo zikitokea kikweli humkumbusha mtu huyo akawa anaifanyia kazi Akhera yake badala ya kuikimbilia
dunia.
Kutokana na haya na mengi mengineyo, Mwenyezi Mungu
Akamfunulia Mtume wake (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) baadhi ya dalili ya
yale yatakayotokea kabla ya kuja kwa Siku ya Qiyaamah.
Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa
sallam) alikuwa anapozungumza juu ya dalili za kukaribia kwa Siku ya Qiyaamah,
mashavu yake yanageuka kuwa mekundu huku akiipaza sauti yake juu kwa ghadhabu
mfano wa Amiri Jeshi mwenye kulipa amri jeshi lake.
Alikuwa pia akisema:
((“Nimeletwa baina yangu na Qiyaamah
kiasi kama hiki”, huku akiashiria kwa kidole chake cha shahada na cha pili
yake.))
Zipo dalili zinazoitwa ‘dalili ndogo’ na zipo pia
‘dalili kubwa’ za Siku ya Qiyaamah. Nyingi katika dalili ndogo zimekwisha tokea
na kuonekana, jambo lililowafanya Waislamu waongezeke imani na kumsadiki zaidi
Mtume wao (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam). Wakati zitakapoanza kuonekana
dalili kubwa, basi zitatunga na kufuatana moja baada ya nyingine mpaka Qiyaamah
kitakaposimama. Lakini sisi tutazitaja hapa baadhi yake na chache sana miongoni
mwa ‘dalili ndogo’ tu.
Fitan
Neno ‘Fitan’ ambalo ni wingi wa (plural ya) Fitnah;
maana yake ni Mitihani. Lakini neno hili linaongezeka maana yake kila
linapozidi kutumika. Kwani neno hili linaweza kumaanisha misiba, madhambi,
kufru, mauaji, kuchomwa moto n.k.
Neno ‘Fitan’ pia linamaanisha vita vya wenyewe kwa
wenyewe (civil wars). Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam)
ametujuulisha juu ya Fitnah nyingi sana zitakazotokea baada yake zikiwa kama ni
dalili ya kukaribia kwa Siku ya Qiyaamah. Fitnah zitakazomfanya mtu asiweze
kutambua ipi haki na ipi baatwil. Fitnah zitakazozitetemesha nyoyo na
kuiyumbisha imani, hadi kufikia kwamba mtu anaweza akaamka asubuhi akiwa ni
Muislamu na jioni yake akageuka kuwa kafiri, au anaweza kuamka asubuhi akiwa
kafiri na jioni yake akawa Muislamu.
Kila inapotokea fitnah, mtu hudhani kuwa hii ndiyo
itakayoangamiza, kisha humalizika na kutokea nyingine kubwa kuliko ile. Na hali
itaendelea hivyo mpaka kitakaposimama Qiyaamah.
Anasema Abu Muusa Al-Ash’ary (Radhiya Allaahu
‘Anhu) kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:
((Kinapokaribia Qiyaamah zitatokea
Fitnah nyingi mfano wa vipande vya usiku wenye kiza kizito, mtu ataamka ndani
yake akiwa Muislamu na jioni yake anakuwa kafiri, au anakuwa wakati wa jioni
Muislamu na asubuhi anakuwa kafiri. Aliyekaa katika mtihani huo anakuwa bora
kuliko aliyesimama, na aliyesimama anakuwa bora kuliko mwenye kutembea taratibu,
na mwenye kutembea anakuwa bora kuliko anayekwenda mwendo wa kukazana.)) [Imepokewa na Imaam Ahmad, Ibni Maajah, Al-Haakim
na wengineo]
Imetolewa na Muslim pia kutoka kwa Abu Hurayrah
(Radhiya Allaahu ‘Anhu) kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa
sallam) amesema: ((Kimbilieni kufanya ‘amali njema
kabla ya kuja kwa Fitnah mfano wa vipande vya usiku wenye kiza kizito, mtu
ndani yake anaamka akiwa Muislamu na jioni yake anakuwa kafiri, au jioni
anakuwa kafiri na asubuhi anakuwa Muislamu. Mtu ndani ya Fitnah hizo anaiuza
diyn yake kwa thamani ndogo ya dunia.)) [Imepokewa na Muslim]
Na maana ya neno ‘vipande vya usiku wenye kiza
kizito’, ni ule ubaya wa Fitnah hizo utakaomfanya mtu achanganyikiwe asiweze
kutambua baina ya haki na baatwil.
Kutoka kwa Ummu Salamah (Radhiya Allaahu ‘Anha)
amesema kuwa usiku mmoja Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa
sallam) aliamka akiwa na hofu nyingi huku akisema: ((Subhaana
Llaah! Hazina ngapi alizoteremsha Mwenyezi Mungu, na mitihani mingapi
aliyoiteremsha Mwenyezi Mungu? Nani atakayewaamsha waliolala vyumbani mwao
(akimaanisha wake zake), huenda mtu akawa amevaa duniani akaenda uchi Akhera.))
Maulamaa wamelitafsiri neno ‘amevaa duniani akaenda
uchi Akhera’, tafsiri nyingi sana zikiwemo zifuatazo:
·
Mtu tajiri mwenye nguo nyingi
hapa duniani lakini hana ‘amali njema za kumsitiri
huko Akhera.
·
Wengine wakasema kuwa maana yake
ni mtu mwenye kuvaa nguo
zisizomsitiri hapa duniani na huko Akhera hatokuwa
na cha kumsitiri.
Kuvunjwa
Kwa Mlango
Nitaanza kwa kutaja baadhi ya Hadiyth
alizozungumzia ndani yake Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa
sallam) Fitnah za mwanzo katika Uislamu, Fitnah zilizotokea miaka michache
baada ya kufariki kwake, mara baada ya kuuliwa kwa Khaliyfah wa pili wa
Waislamu ‘Umar bin Khatwaab (Radhiya Allaahu ‘Anhu).
Kutoka kwa Hudhayfah (Radhiya Allaahu ‘Anhu)
amesema kuwa:
‘Umar bin Al-Khattwaab (Radhiya Allaahu ‘Anhu)
aliuliza siku moja: “Yupi kati yenu aliyehifadhi
kauli ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) juu ya
Fitnah?”.
Hudhayfah akasema: “Mimi
nimehifadhi kama alivyosema”.
‘Umar (Radhiya Allaahu ‘Anhu) akamwambia: “Tuhadithie, kwani wewe ni jasiri”.
Hudhaifah (Radhiya Allaahu ‘Anhu) akasema: “Fitnah ya mtu katika ahli yake (watu wa nyumba yake) na
mali yake na jirani zake zinaondoka kwa kuswali na kutoa Sadaka na kwa
kuamrisha mema na kukataza mabaya”.
‘Umar akasema: “La, mimi
sikusudii (fitnah) hizi, bali zile zinazorusha mawimbi (makubwa) kama mawimbi
ya bahari”.
Akasema: “Ewe Amiri wa
Waislamu! Wewe umeepukana nazo Fitnah hizo, kwani baina yako na baina yake
(Fitnah hizo) upo mlango uliofungwa”.
‘Umar akauliza: “Mlango
huo utafunguliwa au utavunjwa?”
Akasema: “La, bali
utavunjwa”.
‘Umar (Radhiya Allaahu ‘Anhu) akasema: “Kwa hivyo hautofungika tena...” Na katika riwaya
nyingine akasema: “Kwa hivyo hautofungika mpaka
Siku ya Qiyaamah?”
Wakamuuliza (waliokuwa wakimsikiliza Hudhayfah
baada ya kufa kwa ‘Umar): “Aliujua?” Na
katika riwaya nyingine: “’Umar alikuwa akiujua
mlango huo?”.
Hudhayfah (Radhiya Allaahu ‘Anhu) akawaambia: “Naam kama (anavyojua kuwa) usiku wa leo unakuja kabla ya
usiku wa kesho)”.
Masruuq bin Al Ajda-a alipomuuliza Hudhayfah
(Radhiya Allaahu ‘Anhu): “Nani mlango huo”.
Akasema: “(Mlango huo ni)
‘Umar.”
Kisha Hudhayfah (Radhiya Allaahu ‘Anhu) akawaambia:
“Mimi nilimuhadithia ‘Umar Hadiyth (hii) kama
nilivyomsikia Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) bila
makosa.”
Ikawa kama alivyotujuulisha Msemakweli Muhammad
(Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam), kwani mlango huo ulivunjwa mara baada ya
kuuliwa Khaliyfah wa pili wa Waislamu ‘Umar bin Al-Khattwaab (Radhiya Allaahu
‘Anhu). Kuanzia hapo Fitnah zikafunguka na kuenea na kukithiri, na Fitnah ya
mwanzo ilikuwa kuuliwa kwa Khaliyfah wa tatu wa Kiislamu- Mwenye Nuru mbili
‘Uthmaan bin ‘Affaan (Radhiya Allaahu ‘Anhu).
[Imepokewa na Al-Bukhaariy, Muslim na At-Tirmidhiy]
Kuuliwa
Kwa ‘Uthmaan (Radhiya Allaahu ‘Anhu)
Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa
sallam) aliwahi kumbashiria ‘Uthmaan bin ‘Affaan (Radhiya Allaahu ‘Anhu) kuwa
atakumbwa na mtihani mkubwa.
Kisa chenyewe ni kama ifuatavyo:
Anasema Abu Muusa Al-Ash’ary (Radhiya
Allaahu ‘Anhu) kuwa siku moja alimuona Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam)
akielekea katika kisima kilichozungushiwa ukuta.
Abu Musa Al-Ash’ary anasema: “Nikasema: Leo mimi nitakuwa mlinzi wa Mtume (Swalla
Llaahu ‘alayhi wa sallam).” Nikamuona Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa
sallam) akielekea kisimani, akakidhi haja yake kisha akakaa juu ya kisima huku
akining’iniza miguu yake.
Akaja Abu Bakr akataka ruhusa ya
kuingia ndani, nikamwambia: “Hapo hapo ulipo, ngoja
kwanza usiingie mpaka nikakuombee ruhusa kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla
Llaahu ‘alayhi wa sallam)”. Nikamwendea Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa
sallam) na kumwambia: “Abu Bakr anataka ruhusa ya
kuingia”, Akanambia: ((Mruhusu aingie, na
mbashirie Pepo)). Nikafanya hivyo, akaingia na kukaa juu ya kisima
kuliani kwa Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) na kuining’iniza miguu yake
kama alivyofanya Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam).
Mlango ukagongwa tena. Nikatamani
mgongaji awe ndugu yangu. Nikauliza: “Nani?”,
“’Umar bin Al-Khattwaab”, Nikamwambia: “Hapo
hapo ulipo, usiingie mpaka kwanza nimjulishe Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla
Llaahu ‘alayhi wa sallam)”. Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam)
akanambia: ((Mruhusu aingie, na mbashirie Pepo)). Nikafanya
hivyo, na ‘Umar naye akaingia na kukaa juu ya kisima kushotoni kwa Mtume
(Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) na kuining’iniza miguu yake kama walivyofanya
wenzake.
Haujapita muda mlango ukagongwa tena:
Nikatamani mgongaji awe ndugu yangu. “Nani?”
“‘Uthmaan bin ‘Affaan”. Nikamwambia: “Hapo hapo
ulipo, usiingie mpaka kwanza nimjulishe Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu
‘alayhi wa sallam)”. Nilipomjulisha, Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa
sallam) akanyamaza muda kidogo, kisha akanambia: ((Mruhusu
aingie na mbashirie Pepo baada ya kupambana na mtihani mkubwa)).
Nilipomwambia hivyo, ‘Uthmaan akasema: “Allaahul-Musta’an”,
(na katika riwaya nyingine alisema: “Tutakuwa
na subira In shaa Allaah”). Kisha akaingia, lakini ‘Uthmaan hakupata pa
kukaa, akaenda upande wa pili akakaa akiwa amekabiliana nao.
Anasema Abu Muusa (Radhiya Allaahu
‘Anhu): “Nikahisi kama hivi ndivyo makaburi yao
yatakavyokuwa, na nikatamani ndugu yangu naye aje”.
[Imepokewa na Al-Bukhaariy]
Ingawaje ‘Umar bin Khattwaab (Radhiya Allaahu
‘Anhu) aliuliwa kama alivyouliwa ‘Uthmaan (Radhiya Allaahu ‘Anhu), lakini ‘Umar
aliyeuliwa na kafiri anayeabudu moto wakati akiswalisha Swalah ya Alfajiri
hakupata misukosuko kama aliyopata ‘Uthmaan (Radhiya Allaahu ‘Anhu) kabla ya
kuuliwa kwake.
Baada ya kuuliwa ‘Uthmaan (Radhiya Allaahu ‘Anhu)
Fitnah zikawa nyingi, khitilafu zikaongezeka, hata Maswahaabah (Radhiya Allaahu
‘Anhu) walishiriki katika vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Mnayaona
Ninayoyaona Mimi?
Siku moja alipokuwa akisimamia ujenzi wa ngome
katika mji wa Madiynah, Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa
sallam) aliyekuwa akiyajuwa yote hayo kuwa yatatokea, aliwauliza Maswahaba
wake: ((Mnaona ninayoyaona?))
Maswahaba (Radhiya Allaahu ‘Anhum) wakasema: “Hatuoni (kitu) ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu.”
Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa
sallam) akasema: ((Mimi naona mapigano mengi yakitokea
baina ya nyumba zenu, wingi wa nyumba kubwa kubwa (zinazowakusanya watu wengi
ndani yake).))
Fitnah nyingi zilizowakumba Waislamu zilitokea
upande wa Mashariki ya dunia, na Fitnah ya mwanzo iliyoleta mfarakano baina ya
Waislamu ilitokea upande huo wa Mashariki, jambo ambalo bila shaka
lilimfurahisha sana Shaytwaan. Na haya yanakubaliana na maneno ya Mtume wa Mwenyezi
Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) aliyetujuulisha kuwa huko ndiko kwenye
pembe ya Shaytwaan.
Kutoka kwa Ibn ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘Anhu)
amesema kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) amesema
huku akiashiria upande wa Mashariki: ((Fitnah ipo
huku, Fitnah ipo huku, kutakapotokeza pembe ya Shaytwaan.)) [Imepokewa na
Al-Bukhaariy na Muslim]
Habari hizi alizotujuulisha Mtume wa Mwenyezi Mungu
(Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) zilianza kuonekana tokea mwanzo wakati
yalipotokea mapigano ya wenyewe kwa wenyewe, jambo ambalo bila shaka yoyote
lilimfurahisha sana Shaytwaan.
Anasema Shaykh Yuusuf bin ‘Abdillaah Al-Waabil
kuwa: “Kutoka upande wa mashariki Fitnah nyingi sana zilitokea. Kwani huko
ndiko yalipoanza mapigano ya wenyewe kwa wenyewe baina ya Waislamu. Kutoka huko
umekuja Ukadiani, Ukoministi. Matartar pia wametokea huko katika karne ya saba
ya Hijriyyah, wakaangamiza na kueneza shari kubwa sana”.
“Hadi hii leo”, anaendela kusema Shaykh Yuusuf:
“Fitnah zinaendelea kutujia kutokea upande huo wa Mashariki ya dunia na hata
Yajuju na Majuju watatokea upande huo huo”.
Kupotea
Kwa Amaanah
Kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘Anhu)
kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) amesema: ((Uaminifu utakapoondoka basi isubirini Sa’ah (kingojeeni
Qiyaamah).)) Akaulizwa: “Vipi unapotea
(uaminifu) ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu?”
Akasema: ((Mambo
yakiegemezwa kwa wasiostahiki, basi isubirini Sa’ah.)) [Imepokewa na
Al-Bukhaariy, Kitaabur-Riqaaq]
Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam)
akatubainishia pia kuwa uaminifu utatoweka katika nyoyo na kubaki athari yake
tu.
Imepokewa kutoka kwa Hudhayfah (Radhiya Allaahu
‘Anhu) kuwa amesema: “Mtume wa Mwenyezi Mungu
(Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) amenihadithia mambo mawili, na mojawapo
katika hayo nimekwishaliona likitokea na ninalisubiri la pili (nilione pia). Amenihadithia
kuwa uaminifu utatoweka. Amenihadithia kuwa amaanah (ilipoteremshwa),
iliteremshwa ndani ya mizizi ya nyoyo za watu, kisha iilipoteremshwa Qur-aan
wakaijua zaidi, kisha wakaijua (vizuri zaidi) kupitia katika Sunnah (Mafundisho
ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam)).”
Kisha akatuhadithia juu ya kunyanyuliwa (kupotea) kwa
amaanah akasema: ((Mtu analala usingizi huku amaanah
inafutwa moyoni mwake na kubaki athari yake tu, mfano wa doa lisilokuwa na
rangi. Kisha analala usingizi (mwingine) na amaanah inafutwa (‘tena’ - yaani
hilo doa lililobaki). Kisha itabaki amaanah mfano wa alama (ya ngozi
iliyokunjika) inayobaki mkononi baada ya mtu kunyanyua kitu”, (inayotoweka
baada ya kupita muda mdogo) (au) maumivu yanayobaki mguuni baada ya kukanyaga
kijinga kidogo cha moto (pakafanya lenge lenge kisha likakauka).))
Kisha Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam)
akasema: ((Kisha watu watakuwa wanafanya biashara na
hapana hata mmoja kati yao atakayekuwa muaminifu, itafika hadi kusemwa; “Katika
watu wa kabila Fulani yupo mtu mmoja muaminifu. Na hata itafika hadi watu watakuwa
wakimsifia mtu huku wakisema: ‘Mwanamume kweli huyu, mkarimu kweli huyu, ana
akili kweli huyu’, (atapewa sifa zote hizo) wakati mtu huyo hana imani (wala
uaminifu) hata yenye uzito wa hardali.))
Hudhayfah (Radhiya Allaahu ‘Anhu) akaendela kusema:
“Nimekwishaiona zama ambayo ndani yake uaminifu
baina ya watu ulikuwepo. Na sikuwa nikijali ninafanya biashara na nani (kwa
sababu watu wote waaminifu), akiwa mtu huyo ni Muislamu basi Uislamu wake
utamfanya asiipoteze amaanah yake. Na kama mtu huyo ni Mkiristo au Myahudi,
basi atakuwa anafanya kama anavyotakiwa (kutonidhulumu haki yangu). Ama wakati
huu wa leo, uaminifu umeondoka, na khiyaanah imedhihiri na sitofanya biashara
isipokuwa na fulani au fulani (tu)”.
Yaani alikuwa akifanya biashara na baadhi ya watu
wachache tu alokuwa akiwaamini.
Hudhayfah (Radhiya Allaahu ‘Anhu) aliishi muda
baada ya kuuliwa kwa ‘Uthmaan bin ‘Affaan (Radhiya Allaahu ‘Anhu).
[Imepokewa na Al-Bukhaariy na Muslim]
Anasema Shaykh Yuusuf bin ‘Abdillaah Al-Waabil
aliyeandika kitabu cha Ashraatwus-Sa’ah
kuwa: “Miongoni mwa dalili za kupotea kwa amaanah ni kule kupewa ufalme,
uongozi au uhakimu watu wasiokuwa waadilifu wala waaminifu. Kwani viongozi
wanapotengenea, raia nao hutengenea. Ama huko juu kukiharibika, basi chini nako
kutaharibika pia. Na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam)
amekwishatujuulisha kuwa utafika wakati wa hadaa, mambo yatakapokwenda kinyume.
Wakati huo, muongo ndiye atakayesadikiwa na mkweli atakadhibishwa, na muaminifu
ataitwa haini na haini ndiye atakayeaminiwa”.
Kubebeshwa mzigo wa uongozi watu wasioijali Dini
yao, ni dalili ya watu kutojali maamrisho ya Dini yao. Na dalili ya upungufu wa
Ma’ulamaa na kuongezeka kwa ujinga, na hizi pia ni katika dalili za kukaribia
kwa Qiyaamah alizozitaja Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa
sallam).
Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa
sallam) amesema: ((Katika dalili za kukaribia kwa
Qiyaamah ni kupotea kwa elimu na kuongezeka ujinga.)) [Imepokewa na
Al-Bukhaariy]
Kushindana
Na Kujisifia Katika Kuipamba Misikiti
Imepokelewa kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla
Llaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:
((Katika dalili za kukaribia kwa
Qiyaamah ni watu kushindana na kujisifia katika kuipamba misikiti.)) [Imepokewa na An-Nasaaiy]
Anasema Al-Bukhaariy: Amesema Anas (Radhiya Allaahu
‘Anhu) kuwa: “Watu wataipamba (Misikiti) lakini
hawaendi kuswali ndani yake isipokuwa wachache”.
‘Umar bin Al-Khattwaab (Radhiya Allaahu ‘Anhu)
alikataza watu kuipamba sana Misikiti kwa sababu mapambo yanawababaisha watu
ndani ya Swalah zao. Alipokuwa akisimamia utengenezaji wa Msikiti wa Mtume
(Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) alikuwa akiwaambia wajenzi:
“Wakingeni watu na mvua na msitie
rangi nyekundu wala manjano mkawababaisha watu”. [Imepokewa na Al-Bukhaariy]
“Mwenyezi Mungu Amrehemu ‘Umar bin Khattwaab
(Radhiya Allaahu ‘Anhu)”, anasema Shaykh Yuusuf Al-Waabil, “kwani watu
hawakutoshelezeka na kuwakinga watu na mvua wala hawakutoshelezeka na rangi za
manjano na nyekundu, bali Misikiti siku hizi inapambwa na kujazwa nakhshi mfano
wa nguo inavyonakshiwa”.
Mauaji
Kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘Anhu)
amesema kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:
((Qiyaamah hakitosimama mpaka ‘Haraj’ ikithiri.))
Wakamuuliza: “Ni nini hii ‘Haraj’ ewe Mtume wa
Mwenyezi Mungu?” Akasema: ((Mauaji, mauaji!.))
[Imepokewa na Muslim]
Na katika riwaya nyingine iliyosimuliwa na Abu
Muusa (Radhiya Allaahu ‘Anhu) kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu
‘alayhi wa sallam) amesema: ((Kabla ya Qiyaamah
kusimama kutatokea ‘Haraj’.)) Wakamuuliza: “Ni
nini hii ‘Haraj’ ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu?” Akasema: ((Mauaji)). Wakamuuliza: “Kuliko
tunavyoua? Tunaua (vitani) katika mwaka mmoja zaidi ya alfu sabini?”
Akasema: ((Si kama kuuwa kwenu washirikina, bali huko
ni kuuana nyinyi wenyewe kwa wenyewe.)) Wakasema: “Tutakuwa na akili zetu siku hiyo?” Akasema: ((Zitaondolewa akili za wengi wa watu wa zama hizo. Watakuwa
na wafuasi wengi kama vumbi, wengi wao watadhani kuwa wameshika chochote
(katika haki), lakini (ukweli ni kuwa) hawana chochote.)) [Imepokewa na
Imaam Ahmad na Ibn Maajah]
Halikadhalika, imesimuliwa kutoka kwa Abu Hurayrah
kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) amesema: ((Naapa kwa Yule ambaye nafsi yangu imo mikononi mwake,
haitotoweka dunia mpaka iwajie watu siku ambayo ndani yake muuaji hatojua kwa
ajili gani ameua na wala aliyeuliwa kwa ajili gani ameuliwa.)) Akaulizwa:
“Yatakuwaje hayo?” Akasema: ((Al-Haraj! aliyeuwa na aliyeuliwa (wataingia) Motoni.))
Haya yote yashatokea kweli katika zama zilizopita
na tunayaona yakitokea katika zama zetu hizi pia. Hasa baada ya kuvumbuliwa kwa
silaha zinazoangamiza.
Na katika Hadiyth sahihi iliyomo katika Mustadrak ya Al-Haakim, Mtume wa
Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) amesema: ((Ummah wangu ni Ummah utakaohurumiwa, hawatokuwa na adhabu
huko Akhera, kwani adhabu zao ni za dunia, mauaji na mashaka na mitetemeko.))
Mtu
Atatamani Kufa
Imepokelewa kuwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu
‘Anhu) amesema kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam)
amesema: ((Hakitosimama Qiyaamah mpaka mtu atakapopita
penye kaburi la mtu akasema: “Yareti mimi ndiye ningelikuwa mahali pake”.))
[Imepokewa na Al-Bukhaariy]
Na kutoka kwa Abu Hurayrah pia, kuwa Mtume wa
Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) amesema: ((Naapa kwa yule ambaye nafsi yangu imo mikononi Mwake,
dunia haitotoweka mpaka mtu atakapopita penye kaburi akasimama na kusema:
‘Yareti ningelikuwa mimi ndani ya kaburi hili”. Si kwa ajili ya Dini, bali kwa
ajili ya mitihani.)) [Imepokewa na Al-Bukhaariy]
Amesema Ibni Mas’uud (Radhiya Allaahu ‘Anhu): “Utakupitikieni wakati, mtu akiyakuta mauti yanauzwa,
basi atayanunua”.
Wanasema Ma’ulamaa kuwa mambo kama haya si lazima
yatokee katika kila nchi. Lakini yanaweza kutokea katika zama mbali mbali
kutokana na mitihani mizito mbali mbali. Mtu anapokumbwa na mitihani hiyo
atakapopita makaburini atahisi kama kwamba yule aliyelala ndani mule ndiye
aliyestarehe. Ama yeye anajiona yumo katika adhabu, misukosuko mashaka na
mitihani mikubwa isiyomalizika.
Kupigana
Na Warumi (Wakiristo)
Kutoka kwa ‘Awf bin Maalik Al-Ashjaiy (Radhiya Allaahu
‘Anhu) amesema kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam)
amesema: ((Hesabu mambo sita, lazima yatatokea kabla
ya kusimama Qiyaamah, miongoni mwa mambo sita hayo akasema: Kisha vita
vitasimamishwa baina yenu na watu wa manjano (Wakiristo), kisha watakufanyieni
khiana, watakujieni chini ya bendera themanini, chini ya kila bendera (watu)
elfu kumi na mbili.)) [Imepokewa na Al-Bukhaariy]
Siku moja alikuja mtu kwa ‘Abdullaah bin Mas’uud
(Radhiya Allaahu ‘Anhu) akamwambia: “Ewe ‘Abdullaah! Qiyaamah kitasimama
(karibu sana)”. ‘Abdullaah bin Mas’uud (Radhiya Allaahu ‘Anhu) aliyekuwa amekaa
akiwa ameegemea, akakaa vizuri kisha akamwambia: “Hakika ya Qiyaamah
hakitosimama mpaka kwanza mirathi isigawiwe na ngawira isifurahiwe”.
Kisha akasema huku akiashiria upande wa Shaam
(upande wa Mashariki): “Maadui watajikusanya kuwapiga vita Waislam, na Waislam
watajikusanya kwa ajili ya kupambana nao”. Nikamuuliza: “Warumi? (Wakristo?)”
Akasema: “Ndiyo, na katika vita hivyo wengi watartaddi, na Waislamu
watatayarisha jeshi litakalokuwa tayari kufa lisilokubali kurudi nyuma bila
ushindi, watapigana vita mpaka usiku utakapoingia, kisha watarudi nyuma hawa na
wale, hapana mshindi kati yao, kisha jeshi litaangamia. Kisha Waislamu
watatanguliza jeshi (lingine) litakalokuwa tayari kufa, watapigana vita mpaka
wakati wa jioni, kisha watarudi nyuma hawa na wale, hapana mshindi kati yao,
kisha litaangamia jeshi. Itakapoingia siku ya nne, Waislamu waliobaki watakuja
kuwasaidia, na Mwenyezi Mungu Atawajaalia ushindi uwe upande wao, watapigana
vita visivyopata kuonekana namna yake, hata ndege akipita juu yao, basi
ataanguka akiwa amekufa”. [Imepokewa na Muslim]
Kuja Kwa
Qahtwaaniy
Imepokelewa kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla
Llaahu ‘alayhi wa sallam) amesema: ((Hakitosimama
Qiyaamah mpaka kwanza aje mtu kutoka kabila la Qahtwaan (kabila la watu wa
Yemen), atawaongoza watu kwa bakora (yaani atawaongoza na wataongoka vizuri na
wote watampenda).)) [Imepokewa na Imaam Ahmad, Al-Bukhaariy na Muslim]
No comments:
Post a Comment