Uchaguzi wa wanafunzi
wa kuingia Kidato cha Tano katika shule za Serikali na Vyuo vya Ufundi kwa
mwaka 2014 umekamilika. Uchaguzi umefanyika kwa kuzingatia takwimu za matokeo
ya watahiniwa waliofanya Mtihani wa Kidato cha Nne Tanzania Bara mwaka 2013.
2.0 WATAHINIWA
WALIOFANYA MTIHANI WA KIDATO CHA NNE, MWAKA 2013
Jumla ya
watahiniwa 427,679 walisajiliwa kufanya Mtihani wa Kidato cha
Nne 2013, wakiwemo wasichana 199,123 sawa na asilimia 46.56 na
wavulana 228,556sawa na asilimia 53.44. Kati
yao watahiniwa 404,083 sawa na asilimia 94.48 walifanya
mtihani na watahiniwa 23,596 sawa na asilimia 5.52 hawakufanya
mtihani huo.
2.1 Watahiniwa wa Shule
(School Candidates)
Kwa Watahiniwa wa
Shule, watahiniwa 367,163 walisajiliwa kufanya mithanikati yao
wavulana ni 198,099 na
wasichana ni 169,064. ambapo watahiniwa 352,614sawa
na asilimia 96.04 walifanya mtihani; kati yao wasichana
walikuwa 162,412 sawa na asilimia 96.07 na wavulana 190,202 sawa
na asilimia 96.01. Watahiniwa14,549 sawa na asilimia 3.96 hawakufanya
mtihani kwa sababu mbalimbali.
2.2 Watahiniwa wa
Kujitegemea (Private Candidates)
Kati ya watahiniwa60,516 wa
kujitegemea waliosajiliwa kufanya mtihani, watahiniwa 51,469 sawa
na asilimia 85.05 walifanya mtihani na
watahiniwa 9,047 sawa naasilimia 14.95 hawakufanya
mtihani kwa sababu mbalimbali.
Jumla ya watahiniwa 235,227 sawa na
asilimia 58.21 ya watahiniwa waliofanya Mtihani wa Kidato cha
Nne 2013 walifaulu. Mwaka 2012 watahiniwa waliofaulu walikuwa 185,940 kati
ya 431,650 waliofanya mitihani; hii ni sawa na
asilimia 43.08. Matokeo haya yanaonesha kuwa mwaka 2013 ufaulu
umeongezeka kwa asilimia 15.13.
3.1 Ufaulu wa
Watahiniwa wa Shule
Mwaka 2013 Watahiniwa wa Shule waliofaulu
ni 201,152 sawa na asilimia 57.05 ya
watahiniwa 352,614 waliofanya mtihani. Kwa mwaka
2013 kuna ongezeko la ufaulu wa watahiniwa 41,405, sawa na asilimia 25.91
ikilinganishwa na ufaulu wa mwaka 2012 ambapo watahiniwa 159,747 walifaulu.
3.2 Ufaulu wa
Watahiniwa wa Kujitegemea
Takwimu zimeonesha kuwa kumekuwa na ongezeko la ufaulu
kwa watahiniwa wa kujitegemea kutoka 26,193, sawa na
asilimia 43.07 mwaka 2012 hadi kufikia watahiniwa 34,075, sawa
na asilimia 66.21 kwa mwaka 2013; Kwa kulinganisha na mwaka
2012 lipo ongezeko la asilimia 30.09 kwa ufaulu wa watahiniwa wa
kujitegemea.
Ufaulu wa watahiniwa wa shule kwa mwaka 2013 katika
madaraja ya I -III umefikia watahiniwa 71,527 sawa na
asilimia 20.28 ya watahiniwa waliofanya mtihani Tanzania
Bara.Hivyo kuna ongezeko la ufaulu wa asilimia 106.73 ikilinganishwa
na matokeo ya ufaulu kwa mwaka 2012, kwa kuwa watahiniwa wa shule waliofaulu
katika madaraja I-III kwa mwaka huo walikuwa 34,599 sawa na
asilimia 9.67 ya watahiniwa waliofanya mtihani.
5.0TARATIBU ZA UCHAGUZI
WA WANAFUNZI WA KIDATO CHA TANO 2014.
Kulingana na utaratibu
uliowekwa na Serikali, mwanafunzi anayeomba kuchaguliwa kuendelea na elimu ya
sekondari kidato cha tano na vyuo vya Ufundi, hulazimika kujaza ‘Selform’ ambayo
ndiyo fomu rasmi ya maombi. Kwa kutumia fomu hiyo, mwanafunzi huchagua
maombi matano ya tahasusi (Combinations)za masomo anayotaka kusoma
na shule anayotarajia kujiunga nayo kwa kila chaguo.
Kamati ya uchaguzi humpanga mwanafunzi katika machaguo
yake ya masomo na shule
kwa kuanzia na chaguo la kwanza. Kama mwanafunzi atakuwa hana sifa katika
machaguo yote aliyoomba, mwanafunzi husika hupangiwa chaguo la somo alilofaulu
zaidi na katika shule iliyopo karibu na wilaya yake ya makazi kulingana na
tahasusi na nafasi zilizopo katika shule husika.
6.0 IDADI YA WANAFUNZI
WALIOCHAGULIWA KUINGIA KIDATO CHA TANO
Jumla ya Wanafunzi 54,085 sawa na
asilimia 75.61 ya wanafunzi 71,527 waliostahili
kuingia Kidato cha Tano Tanzania Bara kwa mwaka 2014 wamechaguliwa; hilo ni
ongezeko la wanafunzi 20,402 kwa kulinganisha na wanafunzi 33,683 waliochaguliwa
mwaka 2013. Kati ya wanafunzi waliochaguliwa 2014 wavulana ni 31,352na
wasichana ni 22,733.
Wanafunzi wamechaguliwa kujiunga kidato cha Tano
katika jumla ya shule 241 zikiwemo shule 33 zilizopangiwa
wanafunzi kwa mara ya kwanza mwaka 2014.
Nawashukuru sana wadau wote wa elimu katika
Halmashauri mbalimbali kwa kuimarisha miundombinu ya shule hizo, ikiwemo
maabara.
Wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha Tano
2014 ni kutoka shule za serikali na zisizo za serikali. Kati yao wavulana 14,826 sawa
na asilimia27.41wamechaguliwa kusoma masomo ya sayansi na
wavulana 16,526 sawa na asilimia 30.56 wamechaguliwa
kusoma masomo ya sayansi ya Jamii. Aidha,wasichana 7,859 sawa
na asilimia 14.53wamechaguliwa kusoma masomo ya sayansi na
wasichana 14,874 sawa na asilimia 27.50 wamepangwa
kusoma masomo ya Sayansi ya Jamii.
Nawapongeza walimu wote kwa juhudi walizozifanya
katika ufundishaji kwa kuzingatia mbinu za ufundishaji walizopata kupitia
mpango wa mafunzo kazini (INSET)kwa walimu wa sayansi na lugha
(Kiswahili na Kiingereza) unaosimamiwa na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi
kwa kushirikiana na Ofisi ya WaziriMkuu, Tawala za Mikoa na Serikali ya Mitaa.
Aidha nawapongeza wanafunzi wote waliochaguliwa kujiunga na kidato cha Tano na
Vyuo vya Ufundi. Hali hiyo inaonesha kuwa jitihada za Serikali za kuhamasisha
vijana kusoma masomo ya Sayansi zimeanza kuzaa matunda.
Natoa wito kwa wanafunzi wa jinsi zote kujisomea
kwa bidii masomo yote, yakiwemo
ya Sayansi na Sayansi ya Jamii, kwani yanategemeana.
Walimu wa masomo ya Sayansi, Sayansi ya Jamii na Hisabati wanakumbushwa kutumia
mbinu shirikishi za kitaalam na kisaikolojia katika kufundisha
ili kuwavutia wanafunzi wengi zaidi kusoma na kufaulu mitihani yao. Aidha
walimu wa masomo ya Sayansi, waendelee kuwahamasisha wanafunzi kusoma masomo ya
Sayansi wakiwemo wanafunzi wa kike. Aidha, wanafunzi wa kike
wanapaswa kujiamini kuwa wanaweza masomo yote yakiwemo ya Sayansi, kwani siri
ya kujifunza ni utayari.
7.0 WANAFUNZI
WALIOCHAGULIWA KUJIUNGA NA VYUO VYA UFUNDI, MWAKA 2014
Jumla ya
wanafunzi 472wakiwemo wavulana 355na wasichana 117
wamechaguliwa kujiunga na Vyuo vya
Ufundi. Idadiya wanafunzi hao imepungua kutoka 530 mwaka
2013 hadi 472 mwaka 2014 kwa sababu kwa sasa vyuo hivyo
vimeanza kuchukua wanachuo wa shahada ya kwanza. Aidha, kutokana na ufaulu
kuongezeka idadi ya wanafunzi wa kike waliochaguliwa kujiunga
na vyuo hivyo imeongezeka kutoka wanafunzi 114 mwaka 2013 hadi
wanafunzi 117mwaka 2014 sawa na ongezeko la asilimia 2.63.
Natoa wito kwa wanafunzi kuendelea kusoma kwa bidii
masomo ya sayansi ili mwakani idadi ya wanafunzi wanaojiunga na mafunzo ya
ufundi iongezeke ili Taifa lipate wataalam wa kutosha wa ngazi zote.
8.0 SABABU ZA
WANAFUNZI KUKOSA KUCHAGULIWA KUINGIA KIDATO CHA TANO
Jumla ya wanafunzi 16,800 wakiwemo watahiniwa
wa kujitegemea 10 waliokuwa na sifa za msingi hawakuchaguliwa kwa
sababu mbalimbali zikiwemo: ufinyu wa nafasi za shule za Kidato cha Tano
(wanafunzi 16,400) na kukosa tahasusi - Combination (wanafunzi 400).
Serikali inatarajia kufanya uchaguzi wa awamu ya pili
baada ya kubaini nafasi zitakazokuwa wazi zinazotokana na wanafunzi ambao
hawakuripoti awamu ya kwanza. Aidha, Serikali imeweka utaratibu wa kuwapatia
nafasi ya kusoma kidato cha Tano na cha Sita kwa pamoja na shahada ya Ualimu
wanafunzi wenye sifa.
Shule za Kidato cha Tano na Sita zinatakiwa kuwa na
mahitaji ya msingi, ikiwemo miundombinu yenye uwiano sahihi wa vyoo,
bafu, vyumba vya madarasa, bweni, jiko, bwalo, maktaba, maabara, chumba cha
Jiografia; pamoja na samani kulingana na idadi ya
wanafunzi.
Shule zenye Kidato cha Kwanza mpaka cha
Nne ambazo zinahitaji kuanzisha kidato cha Tano, zinatakiwa kuwa na miundombinu
na mahitaji kamilifu yanayotosheleza kidato cha Kwanza hadi cha Nne kabla ya
kuanza kujenga miundombinu ya Kidato cha Tano na Sita.
Natoa wito kwa Makatibu Tawala Mikoa wawaelekeze
Wakurugenzi wa Halmashauri, Miji na Majiji kuhakikisha azma ya Serikali ya kila
Tarafa kuwa na shule ya Kidato cha Tano inatekelezwa ili kupunguza idadi ya
wanafunzi wanaokosa nafasi. Kutokana na ongezeko la ufaulu wa masomo ya sayansi
tunahimiza shule zitakazoanza Kidato cha Tano ziwe na maabara ili kuongeza
idadi ya wanafunzi wa tahasusi za sayansi.
Aidha, shule ambazo hazikupangiwa wanafunzi kutokana
na mapungufu mbalimbali, Makatibu Tawala wa Mikoa husika wanahimizwa kuwaelekeza
Wakurugenzi kusimamia kwa karibu ukamilishwaji wa shule hizo ili ziweze kupokea
wanafunzi wa chaguo la pili (Second selection).
Natumia nafasi hii kuwahimiza wadau wote wa Elimu
kuhakikisha kuwa shule zote zinazoanzishwa kwa ajili ya kidato cha Tano ziwe za
bweni kwa kuwa wanafunzi wa kutwa ni wachache na ni lazima watoke eneo
husika. Kwa mfano, mwaka huu shule ya sekondari Buswelu ya mjini
Mwanza imekosa wanafunzi kwa kuwa ni ya kutwa na Mwanza kuna shule 3 za kutwa.
Hivyo ilikuwa vigumu kupata wanafunzi wa eneo hilo wa kutosheleza shule hizo.
Wakuu wa Shule wahakikishe kuwa wanafunzi wa kidato cha nne wote wanajaza
‘Selforms’ kwa umakini na kwa usahihi ili kurahisisha zoezi la uchaguzi. Aidha,
wazazi kwa kushirikiana na walimu wawaelekeze watoto wao kuwa na dira,
kuwasaidia kusoma kwa malengo na kufanya machaguo ya tahasusi kulingana na dira
walizonazo.
10.0 WANAFUNZI KURIPOTI
KATIKA SHULE WALIZOPANGWA
Muhula wa kwanza kwa wanafunzi wa Kidato cha Tano
mwaka huu 2014,utaanza mwezi Julai tarehe 10. Wanafunzi wamepangwa
katika shule zenye miundombinu na walimu kwa masomo husika. Aidha, iwapo baadae
mapungufu yatajitokeza, wakuu wa shule wameelekezwa kutoa taarifa kwa uongozi
wa Halmashauri husika kuhusu upungufu huo.
Uchaguzi wa wanafunzi
wa kujiunga na kidato cha tano umefanyika kwa kutumia mfumo wa kompyuta kwa
kuzingatia machaguo ya wanafunzi pamoja na ufaulu hivyo hakutakuwa na
mabadiliko yoyote.
Kwa nafasi hii, naagiza wanafunzi wote
kuripoti katika shule walizopangwa tarehe 10 Julai, 2014. Wanafunzi ambao
watashindwa kuripoti shuleni hadi tarehe30 Julai, 2014 nafasi zao
zitajazwa na wanafunzi ambao wamekosa nafasi.
Mwisho ninachukua nafasi hii kuwapongeza wanafunzi
waliochaguliwa kujiunga Kidato cha Tano na Vyuo vya Ufundi mwaka 2014, walimu,
wazazi, Bodi za Shule, viongozi, jamii na wadau wote wa elimu kwa jitihada za
kuwaandaa wanafunzi, na kufanikiwa kuingia Kidato cha Tano. Ushirikiano wa
wadau wote unatakiwa ili kuboresha elimu hapa nchini.
Wataalam wa elimu kuanzia ngazi ya shule wawe na
utaratibu endelevu wa kuelimisha wadau katika utekelezaji wa malengo
yanayopimika. Katika utaratibu wa ”Matokeo Makubwa Sasa (Big Results
Now)”; kila mmoja anatakiwa kuacha utendaji wa mazoea na
afanye kazi kwa malengo na viwango, kuwa na mipango
inayotekelezeka ya muda mfupi na muda mrefu na kuwa na vipindi
vya tathmini kwa kila lengo kabla, kati na mwisho wa utekelezaji.
Ni matumaini yangu kuwa wakuu wa shule na viongozi wote wa elimu
wakizingatia taratibu hizi, elimu inayotolewa hapa nchini itaendelea kuwa bora
zaidi.
Orodha ya wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na Kidato
cha Tano mwaka 2014 inapatikana katika tovuti zifuatazo: -
Ahsanteni kwa
kunisikiliza.
Mhe. Kassim M. Majaliwa
(MB)
OFISI YA WAZIRI MKUU -
TAMISEMI
No comments:
Post a Comment