UTANGULIZI WA MWANDISHI
تشى الله اهرضي اهرض ىٖ
BISMILLAHIR-RAHMANIR-RAHIYM
Kila sifa njema zinamstahikia Mwenyezi Mungu mwingi wa Rehma, Mwenye Kurehemu.
Pia Rehema na Amani zimfikie Mtume wetu Muhammad (Swalla Allaahu „alayhi wa aalihi wa sallam), yeye pamoja na watu wa nyumba yake tukufu na Masahaba wake watukufu. Aidha Radhi za Mwenyezi Mungu ziwafikie wafuasi wake wema hadi siku ya Qiyaamah.
Baada ya hayo, haitakuwa kosa kwa upande wetu kukiri kwamba kitabu hiki ni jaribio maalum katika nyanja za Shari‟ah ya Diyn ya Kiislam. Ni matarajio yetu kwamba kitaweza kuwanufaisha Waislam japo kwa uchache.
Ufafanuzi wa kitabu hiki unajitokeza katika mambo mawili makubwa:
Kwanza kabisa, katika ile maudhui yake ambayo ni mgogoro wa suala la kuandama kwa mwezi. Jambo ambalo licha ya kuwa ni miongoni mwa masuala yanayosababisha Waislam kugawika katika makundi yenye mitazamo tofauti, bali pia ni miongoni mwa masuala yanayowababaisha mno Waislam hususan kila unapoingia mwezi wa Ramadhaan na wakati wa kuingia sikukuu mbili za 'Iydul-Fitri na 'Iydul-Hajj.
Kitabu hiki kimejaribu kuyashughulikia maudhui hayo ingawa kwa uchache kuyachambua na kuyawekea hoja pande zote zinazotofautiana katika suala hili pamoja na kuonesha ama uzito au udhaifu wa hoja hizo zilizotolewa.
Pili, ufafanuzi wa kitabu hiki unaonekana katika ile fani ya uandishi wake iliyotumiwa. Lugha iliyotumika ni ya Kiswahili sanifu ambayo tunataraji msomaji ataweza kukisoma na kukielewa bila ya usumbufu.
Sura na mada za kitabu hiki zimepangwa kwa mantiki maalumu ambayo itaweza kumvuta msomaji, ambapo kwanza kabisa atakutana na Msimamo wa Qur-aan juu ya mada ya mwezi, kisha anaingia katika Hadiyth za Mtume (Swalla Allaahu „alayhi wa aalihi wa sallam), halafu anakutana na mtazamo wa Maswahaabah (Radhiya Allaahu „Anhum), hatimae anaingia katika mitazamo ya wanavyuoni wengine. Kwa hivyo, itaonekana kuwa mtiririko wa mada za kitabu hiki ni wenye kumuongoza msomaji hadi kufikia kwenye kilele cha maudhui yenyewe.
Pamoja na kuwa mgogoro wa kuandama kwa mwezi umeanza kuonekana hadharani katika jamii za Waislam wa hapa Afrika ya Mashariki katika miaka ya hivi karibuni, lakini historia inaonesha kuwa mgogoro huo umekuwepo zama za nyuma sana. Imethibitika kwamba tokea kuwepo tofauti kati ya wanavyoni wa Kiislam juu ya mtazamo wa kufuata miandamo ya mwezi hadi hivi sasa si chini ya karne kumi, yaani zaidi ya miaka (1000) alfu moja iliyopita. Kwa sababu ya kukosekana mawasiliano ya kutosha, wanavyuoni wenye mtazamo usemao kuwa
vii
pawepo na muandamo mmoja ulimwenguni hawakuweza kutekeleza kikamilifu msimamo huo. Ndio maana mtazamo huu ukaanza kutekelezwa vizuri zaidi na baadhi ya Waislam wa karne ya kumi na tisa ambapo mawasiliano yamekuwa yakipamba moto na kuifanya dunia kuwa kama mtaa mmoja tu kwa mawasiliano ya haraka yaliyozaliwa na maendeleo ya sayansi na teknolojia mpya. Lakini jambo moja la kuhuzunisha ni kule kuonekana na baadhi ya Waislam kama kwamba jambo hilo ni kosa au kwamba halikuwepo! Watu hao wameonesha kubishana na kuupinga vikali msimamo huu ambao kwa kweli ni msimamo uliojengwa juu ya hoja imara na unaowiana vyema na maendeleo ya Ulimwengu. Bila shaka ubishani huo wa baadhi ya Waislam hususan wa hapa Afrika ya Mashariki umetokana na kutofahamu baadhi ya Aya za Qur-aan na Hadiyth za Mtume (Swalla Allaahu „alayhi wa aalihi wa sallam). Mara nyingi wamekuwa wakizifasiri Aya na Hadiyth hizo kwa mitazamo finyu isiyo ya kitaalamu jambo ambalo husababisha kupotosha maana halisi ya madondoo hayo ya Qur-aan na Hadiyth za Mtume (Swalla Allaahu „alayhi wa aalihi wa sallam).
Kitabu hiki ni jaribio la kutaka kulitolea ufumbuzi suala hilo la “kuandama kwa mwezi” na kujaribu kuonesha njia ya kufuatwa na Waislam katika kufunga mwezi wa Ramadhaan, siku ya „Arafay na kula 'Iyd.
Kwa upande wetu tumejitahidi kutoa hoja za pande zote zinazohusika katika mjadala wa kuandama kwa mwezi na tumejaribu kusisitiza vya kutosha kila penye uzito na kuonesha dosari pale penye udhaifu. Aidha tumeorodhesha kauli za Wanavyuoni mbali mbali waliopita ambao wanategemewa katika ulimwengu wa Kiislam na pia hatukuwadharau wale tulionao katika zama hizi. Kama ambavyo tumetaja baadhi ya semina na makongamano ya wanavyuoni yaliyowahi kufanyika nchini Tanzania/Zanzibar na hata katika mataifa mengine ya Ulimwenguni pamoja na kutaja maazimio yaliyowafikiwa katika semina na makongamano hayo.
Tunatumai mambo yote hayo yatamsaidia msomaji kulielewa kwa uzito na umuhimu suala hili pamoja na kumuwezesha kujua ni mtazamo gani unaofaa kufuatwa na Waislam.
Mwisho hatuna budi kukiri kwamba kitabu hiki ni zao la bidii na juhudi ya muda mrefu sana, muda ambao haupungui miaka saba ingawa ukusanyaji na uandishi wa mambo yaliyomo humu umechukua karibu miaka miwili.
Pia hatuna budi kukiri kwamba kitabu hiki ni mjumuiko wa michango ya watu mbali mbali. Kwa kweli si kazi ya mtu mmoja wala kumi na moja, bali ni wengi mno ambao kwa njia moja au nyengine wameiwezesha kazi hii kutoka katika sura ya kitabu. Ni wajibu wetu kuwashukuru kwa dhati kabisa watu wote hao kwa mchango wao huo.
Ni tumaini letu pia kuwa kitabu hiki kitapokelewa na kusomwa na Waislam kwa mikono miwili kwa lengo la kujiongezea maarifa ya Diyn na kuyatekeleza kwa nia ya kuleta ufanisi mzuri zaidi badala ya kuleta mabishano yasiyokuwa na msingi.
viii
Tunamuomba Mwenyezi Mungu Atuoneshe Haki na Atuwezeshe kuifuata, na Atuoneshe Baatwil na Atuwezeshe kuiepuka. “Amiyn”.
Nassor A. Bachoo
Zanzibar
29 Rabiul-Awwal 1418 H.
2/8/1997 M.
CHANZO. ALHIDAYA.COM
No comments:
Post a Comment