Monday, June 2, 2014

ATHARI ZA KUWEPO MIANDAMO MINGI YA MWEZI



TAATHIRA ZIPATIKANAZO KWA KUKUBALI
 
KUWEPO TOFAUTI ZA KUANDAMA MWEZI

Yapo mambo au matokeo ambayo yanahusu jamii ya ulimwengu mzima kwa wakati mmoja. Mathalan, hili jambo la kuwa na tarehe moja kwa ulimwengu mzima ni jambo linalowezekana kabisa. Kukubalisha ulimwengu huu mmoja kuwa na tarehe nyingi kunasababisha taathira mbali mbali za migogoro na matatizo. Hapa tutaja baadhi ya taathira hizo kama zifuatazo:


1.      Kubadilika Kwa Tarehe Ya Hijiriya
Tarehe ya Hijiriya bila shaka imeasisiwa kutokana na lile tukio maarufu la Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) la kuhama Makkah na kuhamia Madiynah yeye mwenyewe pamoja na Maswahaba wake (Radhiya Allaahu ‘Anhum) kama neno lenyewe linavyojionesha. Hijiriya linatokana na neno “Hijra” ambalo ni kuhama. Kwa kuwa tukio lenyewe ni moja tu, tena lilitokana na Mtume wa ulimwengu mzima, bila shaka litakuwa ni tukio la tarehe ya ulimwengu mzima, kama ilivyo kwa matokeo ya tarehe nyengine. Kwa mfano katika tarehe ya “Miladiya” ambayo imechukuliwa kutokana na tukio la ‘kuzaliwa kwa Nabii ‘Iysa (‘Alayhi swalaatu was-Salaam). Bila shaka tunakubaliana kuwa Nabii ‘Iysa (‘Alayhi swalaatu was-Salaam) alizaliwa na mama yake ‘siku moja’ kwa ‘mara moja’ tu na kwa hivyo dunia nzima imefuata tarehe moja ya Miladiya. Ndio maana imewafikiana tarehe moja tu kwa dunia nzima kutokana na tukio hilo moja tu.

Kwa hivyo tarehe ya Hijiriya si tarehe ya watu wa Makkah na Madiynah peke, yao bali ni tarehe ya umma (Waislam) wote ulimwenguni. Bila shaka yoyote kama tutafuata ile kauli ya kwamba kila nchi ione mwezi wake kutegemea tofauti za matlai, masafa ya Qasr na nyenginezo basi kila nchi au kila eneo litakuwa na tarehe yake na Hijiriya yake ya kitaifa au kinchi, siyo ile Hijiriya iliyoasisiwa na mwenyewe Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

Mbali na kwamba kila nchi au kila eneo lenye matlai moja liwe na tarehe yake, bali pia jambo hilo linaweza kusababisha tarehe zaidi ya moja kwenye nchi moja. Kwani katika nchi moja inawezekana kuwa na tofauti za matlai zaidi ya moja. Tukichukulia mfano wa nchi kubwa kama ya Urusi ambayo imeanzia tokea Bara la Asia hadi kumalizikia kwenye Bara la Ulaya. Je unadhani nchi kama hiyo itakuwa na matlai ngapi na kwa hivyo itakuwa na tarehe ngapi za Hijiriya? Mbali na mfano huo wa Urusi, kuna nchi kama Canada ambayo pekee ni kubwa kuliko Bara zima la Ulaya. Je Ulaya ina matlai ngapi na Canada nayo itakuwa na ngapi? Sikwambii tena nchi kama China, USA, Brazil, Australia au Bara Hindi (India) zitakuwa na matlai ngapi na tarehe ngapi za Muandamo!

Kisha tupige mfano mwengine wa eneo moja la Afrika ya Mashariki (Kenya, Uganda na Tanzania) ambalo limechukuwa eneo hilo kama kwamba ni kigezo cha sehemu ya Matlai moja. Ambayo pia itakuwa na uwezekano wa kuwa na tarehe moja ya Hijiriya. Hapa pana masuala mengi yanayoweza kujitokeza mbele yetu.

Kwanza: Tujiulize ni mantiki gani iliyotumika kujitambulisha kwamba Afrika ya Mashariki iwe na tarehe yake tofauti na nchi zilizo jirani (zilizopakana) kama Somalia, Ethiopia, Sudan, Rwanda, Burundi, Zaire, Malawi, Mozambique na Zambia?

(Tazama: Ramani Na. 1 ya Afrika Mashariki).

KIELELEZO NA 1: Ramani ya Afrika Mashariki inavyoonekana kupakana kwake na nchi zote jirani.

Pili: Mfano mwengine ni wa Kusini mwa Somalia ambapo sehemu hiyo imeingiliana sana na Kaskazini ya Kenya. Basi itakuwaje Kenya na Somalia ziwe na tarehe mbili tofauti za Hijiriya? Hali ya kwamba sehemu hizo kama si kutenganishwa na mipaka hapana shaka ingalikuwa ni sehemu ya Kenya –Afrika ya Mashariki.

Tatu: Nchi kama Burundi na Rwanda ambazo hapo awali zilikuwa ni sehemu ya Tanganyika ya zamani, hivi sasa nchi hizi mbili hazitajwi sana katika mjumuiko wa nchi za Afrika ya Mashariki. Kutokana na mgawanyo wa tawala na mipaka iliyoasisiwa na wakoloni (Wafaransa, Wabelgiji,  Wajerumani na Waingereza), watu wanathubutu kusema kwamba nchi hizo zina Matlai tofauti na kwa hivyo zitakuwa zinafunga tarehe zao tofauti na Kenya, Uganda na Tanzania. Ambapo pia ukiangalia mikoa ya Kagera na Kigoma iliyoko Tanzania, inakuwa karibu zaidi na Rwanda na Burundi hata kuliko ilivyo baina ya kagera na Nairobo, au Kagera na Dar-es-Salaam zilioko kwenye Tanzania.

(Tazama Ramani Na. 2 ya Afrika Mashariki).


KIELELEZO NA 2: Ramani ya Afrika Mashariki inavyoonekana baadhi ya miko yake iliyo karibu na nchi jirani. (Angalia mikoa ya Kigoma na Kagera – Tanzania ilivyo karibu zaidi na nchi za Burundi na Rwanda na jinsi ilivyo mbali na Dar es Salaam).

Nne: Je kama itachukuliwa Afrika ya Mashariki hii kama ni kipimo cha matlai moja – yenye tarehe yake moja ya Hijiriya. Je unadhani zinaweza kutoka Afrika ya Mashariki ngapi ndani ya ukubwa wa Urusi, Marekani, Canada, Brazil, China, Australia au India?

(Tazama Ramani Na. 3 ya Ulimwengu, kwa ufafanuzi zaidi).




KIELELEZO NA 3: Ramani ya Ulimwengu, angalia ukubwa wa Afrika ya Mashariki ukilinganisha na maeneo ya nchi nyengine duniani.

Tano: Pia kuna mfano mwengine hai ambao umetokea hivi karibuni ambapo mwezi uliandama siku ya Ijumaa katika nchi ya Saudi Arabia na nyingi nyenginezo ulimwenguni. Mwezi ambao, huku kwetu Afrika ya Mashariki ulionekana siku ya pili yake ambayo ilikuwa Jumamosi. Hapa pana tukio muhimu la kuzingatiwa, ambalo ni tarehe mbili tofauti kwa siku hiyo hiyo moja. Kutokana na jambo la kukubalisha kila nchi na tarehe yake ya Hijiriya lilisababisha siku hiyo moja ya Jumamosi kwa Saudia na Tanzania kuwa na ‘Tarehe Tofauti’, ‘Mwezi Tofauti’ na ‘Mwaka Tofauti’. Ilikuwa Ijumaa tarehe 17/5/1996 AD (30/12/1416 H) siku ulipoandama mwezi nchini Saudi Arabia. Kwa bahati mbaya siku hyo haukuonekana mwezi huku Afrika ya Mashariki ambapo ilikuwa ni tarehe 29 Dhul Hijjah 1416 (29/12/1416 H).

Siku ya pili yake (Jumamosi) ikapambazukiwa Saudi Arabia na nchi nyengine nyingi duniani kuwa ni ‘mwaka mpya’ (New Year) yaani tarehe 1 Muharram 1417 H (1/1/1417 H) wakati ambapo siku hiyo hiyo (ya Jumamosi) huku Afrika ya Mashariki ilikuwa bado ni tarehe 30 Dhul Hijjah 1416 H (30/12/1416). Jumamosi 18/5/1996 AD muafaka na 1/1/1417 - Saudi Arabia, 30/12/1416 - Tanzania. Siku moja katika nchi mbili (Saudi na Tanzania) tarehe tofauti, mwezi tofauti na mwaka tofauti.

Kwanini siku moja yenye masaa 24 iwe na tarehe, mwezi na mwaka tofauti? Tena basi kama ukizingatia nchi hizi mbili za Saudi Arabia (Makkah na Madiynah) utaona zinafata nyakati ‘time’ moja na Tanzania (Zanzibar). Hata nyakati zao za Sala zote tano ni (moja) sawa sawa. Watu wa Makkah na Madiynah wakisali Adhuhuri saa 7 na Zanzibar watasali ile ile saa 7. Utatanishi huu ambao unaifanya siku moja ya hapa duniani kuwa na tarehe tofauti, mwezi tofauti, na mwaka tofauti unaweza kuzusha matatizo na migogoro mingi kama hii ifuatayo:

Passport: Tujaalie mtu anaondoka Jiddah - Saudi Arabia saa moja asubuhi kwa ndege kuja Zanzibar. Bila shaka wakati huo huku Zanzibar itakuwa ni saa moja asubuhi vile vile. Kwa kawaida ndege huchukua masaa manne kufika hapa Zanzibar.

Kwa hivyo, mtu huyo kama ameondoka Jiddah saa moja asubuhi, atafika hapa Zanzibar saa tano asubuhi hiyo hiyo ya siku hiyo hiyo. Ikiwa alipoondoka Jiddah ‘Airport’ aligongewa muhuri wa magresheni katika passport yake ikionesha tarehe ya huko itakuwa kama ifuatavyo:

JIDDAH, SAUDI ARABIA
السبت المحرم ١٤١٦ ﻫ
Jumamosi
Jumamosi 1/1/1417 H.
18/5/1996 AD
Saa 1:00 asubuhi


Pia alipofika huku Zanzibar, siku hiyo hiyo ya Jumamosi saa tano asubuhi hiyo hiyo amegongewa muhuri wa tarehe ya huku ambayo ni:

ZANZIBAR, TANZANIA
السبت٣٠  ذوالحجة ١٤١٦
Jumamosi
Jumamosi  30/12/1416 H.
18/5/1996 AD
Saa 5:00 asubuhi


Kwa hivyo mtu huyo, asubuhi hiyo hiyo atakuwa ameondoka Jiddah ‘Mwaka huu’ 1417 amefika hapa Zanzibar ‘Mwaka jana’ 1416 kwa ndege!

Unaweza pia kufikiria mifano ya matatizo mbali mbali yanayoweza kujitokeza kwa kutumia rekodi mbali mbali katika computer, fax, telex, simu, TV, redio, barua, nyaraka, mikataba na mengi mengineyo baina ya nchi mbili zenye tarehe, mwezi na mwaka tofauti kwa siku moja.

Kwa hivyo, ili tuwe tunakwenda sambamba na tarehe moja tu ambayo ndiyo aliyo akiitumia Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) itabidi kuondoa kabisa wazo la tofauti za Matlai na mambo yote yanayokubaliana kuwepo tofauti ya siku nzima, yaani masaa 24. Jambo ambalo halipo kabisa katika ulimwengu huu. Hakuna nchi yoyote iliyo tofauti na nyengine kwa masaa 24. La si hivyo! Kama ndio tutakubalisha kwa kulazimisha kuwepo tofauti ya siku nzima, ina maana kuwa tunakubalisha kwenda kinyume na tarehe zote zilizohusiana au zilizoasisiwa na kufuatwa na yeye mwenyewe Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) pamoja na Maswahaba wake (Radhiya Allaahu ‘Anhum).

Hapa pana mfano mmoja muhimu ambao sote tunakubaliana nao, mfano wenyewe ni ile siku aliyokufa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), yaani Jumatatu 12, Rabiul-Awwal 11 H. Sasa tujiulize masuala yafuatayo:

  • Je alipokufa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) huko Madiynah tunadhani huku kwetu ilikuwa ni tarehe ngapi?
  • Ikiwa huku kwetu ilikuwa ni tarehe 11 Rabiul-Awwal, 11H (siku moja nyuma). Hivyo, basi itakuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikufa ama ‘kesho yake’ au ‘jana yake’, kwa hapa kwetu. Yaani tukikubali tarehe 12, siku itakuwa mbele – Jumanne. Na tukikubali siku ya Jumatatu, tarehe itakuwa nyuma yaani 11.

Ama: Jumanne, 12 Rabiul-Awwal
Au: Jumatatu 11 Rabiul-Awwal

Jambo hili ni la kusikitisha sana! Watu kujiweka kinyume na mipango ya Mwenyezi Mungu na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Ta’ala) Ametuumba sisi wanadamu kisha akatupangia ‘nyakati’ maalum ili kutekeleza ibada mbali mbali juu ya maamrisho yake. Mwenyezi Mungu Mtukufu Amesema katika Qur-aan Tukufu kwamba:

إِنَّ عِدَّةَ الشُّهُورِ عِنْدَ اللَّهِ اثْنَا عَشَرَ شَهْرًا فِي كِتَابِ اللَّهِ يَوْمَ خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ مِنْهَا أَرْبَعَةٌ حُرُمٌ
 
{{Idadi ya miezi (ya mwaka mmoja) mbele ya Mwenyezi Mungu ni miezi kumi na mbili katika elimu ya Mwenyezi Mungu (mwenyewe) tangu Alipoumba mbingu na ardhi. Katika hiyo imo minne iliyo mitukufu kabisa (nayo ni Rajabu, Dhulkaadah, Dhul-Hijjah na Muharram}} (At-Tawbah 9: 36)[1][1].

Kisha Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliwahutubia watu siku ya tarehe 10 Dhul Hijjah, katika Hadiyth waliyoisimulia Maimaam Al-Bukhaariy na Muslim kutoka kwa Abu Bakr amesema:

((خطبنا النبي صلى الله عليه وسلم يوم النحر، قال: "إن الزمان قد استدار كهيؤته يوم خلق الله السماوات والأرض، السنة اثنا عشر شهرا منها أربعة حرم، ثلاث متواليات، ذوالقعدة و ذوالحجة والمحرم، ورجب مضر الذى بين جمادى وشعبان"))

((Alituhutubia Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika siku ya kuchinja (‘Iydul-Adh-haa) akasema: “Wakati unakwenda kama ulivyopangwa tangu zilipoumbwa Mbingu na Ardhi, mwaka una miezi 12, minne katika hiyo ni mitukufu, (ambayo) mitatu imefuatana (nayo ni) Dhul-Qaadah, Dhul-Hijjah na Muharram. (Wa nne ni) Rajab uliyopo baina ya Jumaadah na Sha’abaan”.))

((وقال: "أي شهر هذا؟ قلنا الله ورسوله أعلم، فسكت حتى ظننا أنه سيسميه بغير اسمه، قال أليس ذو الحجة؟ قلنا: بلى، قال: أي بلد هذا؟ فلنا الله ورسوله أعلم، فسكت حتى ظننا أنه سيسميه بغير اسمه، قال: أليست البلدة؟ قلنا: بلى، فأي يوم هذا؟ قلنا: الله ورسوله أعلم، فسكت حتى ظننا أنه سيسميه بغير اسمه، قال: أليس يوم النحر؟ قلنا: بلى.)) (متفق عليه)

((Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akauliza: “Ni mwezi gani huu?” Tukamjibu “Mwenyezi Mungu na Mtume wake ndio wajuwao”. Akanyamaza kitambo hadi tukadhani ataupa jina jengine kisha akasema: “Huu sio Dhul-Hijjah?” Tukamjibu: “Ndio” Akauliza: “Ni siku gani hii?” Tukamjibu: “Mwenyezi Mungu na Mtume wake ndio wajuwao”. Akanyamaza kitambo hadi tukadhani ataipa jina jengine kisha akasema: “Hii siyo siku ya kuchinja?” Tukamjibu: “Ndio”.)) (Al-Bukhaariy na Muslim).

(Angalia Kitabu: Arrahiqul-Makhtuum, uk. 519)

Utaratibu huo wa Mwenyezi Mungu kuhusu ‘nyakati’ haukubadilika tokea alipoziumba Mbingu na Ardhi.

Siku ni nyakati tano:
Asubuhi, Adhuhuri, Alasiri, Magharibi na Ishaa.

Wiki ina siku saba:
Yaumu: Assabt, Al-Ahad, Al-Ithnayn, Athulathaa, Al-Arbi’aa, Al-Khamiys, Al-Jumu’ah.

Mwezi una wiki nne:
Wiki I, Wiki II, Wiki III na Wiki IV.

Mwaka una miezi 12:
Muharram, Safar, Rajab, Rabi’ul-Awwal, Rabi’u-th-Thaaniy, Jumaadal-Uwlaa, Jumaadal-Aaakhirah, Rajab, Sha’abaan, Ramadhaan, Shawwaal, Dhul-Qa’idah na Dhul-Hijjah.

Mwaka Wa Kiislam unaotumia hesabu za mwezi una (kiasi cha) siku 354.
Mwaka Wa Kikristo unaotumia hesabu ya jua una siku 365 au 366.

Kwa kawaida mwaka wa mwezi (سنة القمرية) unaohesabiwa kuandama kwa mwezi hadi mwezi mwengine ambao kwa kawaida huchukua kiasi cha siku 29 1/2. Ambao mwaka wake mmoja una siku 10 ukiulinganisha na Mwaka wa Jua (سنة الشمسية) ambao kwa kawaida dunia hukamilisha kulizunguka jua kwa kiasi cha siku 365 au 366. Hali hiyo husababisha mwezi wa Ramadhaan kusonga mbele siku kumi katika kila mwaka kama utalinganisha na idadi ya hesabu za mwaka wa jua.

Kutokana na jambo hilo, Muislam yeyote atakayebahatika kujaaliwa kufunga kwa muda wa miaka 36 mfululizo maishani mwake, hatokuwa na msimu wowote wala siku yoyote katika mwaka ambayo hakuifunga. Yaani atakuwa ameonja ladha ya kuzifunga siku zote za misimu yote ya mwaka – msimu wa jua na mvua, wakati wa kipupwe na kiangazi, siku za upepo, shwari, vuli, mchoo, kusi, kaskazi na kadhalika.

Kwa bahati mbaya, na pengine bila kujijua, sisi Waswahili (watu tunaozungumza lugha ya Kiswahili) tumeyageuza majina ya siku za wiki. Imekuwa kinyume na vile aliyoakitumia Mtume wetu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Halikadhalika tumegeuza majina ya miezi ya mwaka na baya zaidi ni kule kugeuza ule mpangilio wenyewe wa miezi hiyo katika mwaka. Kwa ufafanuzi zaidi angalia jadweli ifuatayo:

MAJINA YA SIKU ZA WIKI



MAJINA YA KIISLAM (Aliyo akiyatumia Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam))
MAJINA YA KIKWETU (Uswahilini)
  1.  
Siku ya Kwanza
يوم الأحد
Jumapili
  1.  
Siku ya Pili
يوم الأثنين
Jumatatu
  1.  
Siku ya Tatu
يوم الثلاثاء
Jumanne
  1.  
Siku ya Nne
يوم الأربعاء
Jumatano
  1.  
Siku ya Tano
يوم الخميس
Alkhamisi
  1.  
Siku ya Sita
يوم الجمعة
Ijumaa
  1.  
Siku ya Saba
يوم السبت
Jumamosi

MAJINA YA MIEZI

         



MAJINA YA KIISLAMU - Aliyo akiyatumia Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)
MAJINA YA KIKWETU (Uswahlini)




  1.  
Mwezi wa Kwanza
محرم
Mfunguo Nne




  1.  
Mwezi wa Pili
صفر
Mfunguo Tano




  1.  
Mwezi wa Tatu
ربيع الأول
Mfunguo Sita




  1.  
Mwezi wa Nne
ريع الثانى
Mfunguo Saba




  1.  
Mwezi wa Tano
جماد الأولى
Mfunguo Nane




  1.  
Mwezi wa Sita
جماد الأخر
Mfunguo Tisa




  1.  
Mwezi wa Saba
رجب
Rajab




  1.  
Mwezi wa Nane
شعبان
Shaaban




  1.  
Mwezi wa Tisa
رمضان
Ramadhaan




  1.  
Mwezi wa Kumi
شوال
Mfunguo Mosi




  1.  
Mwezi wa Kumi na moja
ذوالقعدة
Mfunguo Pili




  1.  
Mwezi wa Kumi na mbili
ذوالحجة
Mfunguo Tatu

Mambo haya ya kugeuza geuza kusiko kuwa na mpangilio na hoja madhubuti ndio kumetufanya tusiwe na msimamo makini wa siku na tarehe za Kiislam. Hebu na tujiulize ni kitu gani hasa kilichofanya Yaumul-Ahad kuitwa Jumapili? Au Yaumul-Arbi'aa kuitwa Jumatano? Kisha Yaumul-Khamis ikaitwa vile vile Al-Khamis! Kwa nini Yaumul-Khamis isiitwe Jumasita? Yaonesha kwenye hii ‘wiki ya kikwetu’ kuna siku za ‘Tano’ mbili: Jumatano na Al-Khamis. Neno ‘Alkhamisi’ lina maana ya ‘Tano’ katika lugha ya Kiarabu.

Katika majina na mpangilio wa miezi ya mwaka mzima, watu wamekwenda kinyuma nayo; ‘Muharram’ ambao ndio mwezi wa mwanzo Kiislam, umeitwa mfunguo nne, ‘Dhul-Hijjah’ mwezi wa 12 ambao ndio mwezi wa mwisho, umeitwa mfunguo tatu.

Jamii kubwa ya Waislam wa pande hizi za Afrika ya Mashariki hawawezi kupambanua kwamba mwezi wa Ramadhaan ni mwezi wa 9 katika mpangilio wa mwaka wa Kiislam.

Jambo la kushangaza hapa, ni misingi gani hasa iliyotufanya Waislam twende kinyume na majina ya miezi iliyoasisiwa na Mwenyezi Mungu Mtukufu (Subhaanahu wa Ta’ala) kisha ikatumiwa na Mjumbe wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)?

Mwezi wa 'Dhul-Hijjah’ umepewa jina hilo kutokana na utukufu wa ibada maalum ya Hijjah inayofanyika Makkah nchini Saudi Arabia kila ufikapo mwezi huo wa 12 katika kila mwaka.

Mwezi wa Ramadhaan ndio mwezi pekee uliotajwa kwa jina lake mahususi katika Qur-aan Tukufu. Qur-aan ambayo imeteremka huko huko Makkah na Madiynah ambayo ni uongofu kwa Ulimwengu mzima. Pia hio Qur-aan yenyewe imeteremka katika huo mwezi wa Ramadhaan.

Alimradi ibada hizi mbili za Hijjah na Saumu ndizo pekee zinazowaunganisha watu wa Ulimwengu mzima kwa wakati mmoja – maalum katika kila mwaka.
Tukirudi katika jambo letu la kutokuwa na msimamo wa pamoja baina ya Waislam wa miji tofauti hata walio majirani, tunaona inavyosababisha matatizo mengi ya kitarehe, mwezi na mwaka. Mpaka imedhaniwa kwamba Dini hii ya Kiislam si dini yenye msimamo. Hali ambayo imepelekea mambo mengine yasiyokuwa ya Kiislam kuonekana mepesi na bora zaidi kufuatwa! Waislam wa leo, hawaoni aibu wala fedheha kufuata tarehe na miezi ya Kikristo, lakini wanaona muhali kufuata tarehe na miezi iliyoasisiwa na Nabii Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ambayo ndio inayofuatwa na ndugu zetu wanaoishi katika Miji Mitakatifu ya Makkah na Madiynah.

Kuna jambo moja muhimu la kuzingatia ambalo ni uzinduzi kwa Waislam wote. Kwanza kabisa ingekuwa vyema kujiuliza nini hasa chanzo cha hizi tarehe za Miladiya? Na nani hasa aliyeweka tarehe hizo?

Tunaziandika siku na miezi kwa majina ya waungu wa shirk, February, April, May, June, July na August. Hayo ni majina ya waungu wa shirk. ‘Saturday’ ni sanamu lenye kuashiria mungu wa kilimo, ‘Sunday’ ni siku iliyo ikiabudiwa jua. ‘Monday’ ni siku iliyo ikiabudiwa mwezi.

Waislam tunaiandika miezi na siku hizo bila ya kujua, kwenye vitabu vya Dini na juu ya Qur-aan Tukufu. Hiyo ni aibu na fedheha isiyo na mpaka!

Kwa maelezo zaidi: Angalia:

i)                   Pears Encyclopaedia.
ii)                 Encyclopaediea Britannica.



2.      Kupatikana Ramadhaan Zaidi Ya Moja

Kama ndio tutakubali kuwepo tofauti ya siku nzima baina ya sehemu moja na nyengine hapa duniani, hapana shaka zitapatikana Ramadhaan mbili au zaidi. Kwani nchi moja inaweza kufunga siku 29 na nyengine siku 30. Hali hii inatokea mara nyingi, jambo ambalo linasababisha kuwa na mfungo wa Ramadhaan tofauti tofauti. Hizo zitakuwa Ramadhaan mbili tofauti kwani kila moja ina hesabu ya idadi yake ya siku za kufunga. Isitoshe kila Ramadhaan moja kati ya hizo imeanza na kumaliza siku za tarehe tofauti na nyengine.

Ni vyema tuelewe kwamba ikiwa tutakubali kwamba kila nchi ione mwezi wake basi hakutokuwa na Ramadhaan moja. Pia kama tutasema kuwa tofauti hiyo katika kuanza kufunga kwa baadhi ya nchi kabla ya nyengine ni Ramadhaan moja tu, basi jambo hilo linaweza kutupelekea kuamini kwamba mwezi unaweza kuwa na siku 31 au 32. Kwani kama utaandama tarehe 29 kwa kundi la mwanzo, basi kundi la pili au la tatu litakuwa nyuma kwa siku moja au mbili. Kwa hivyo ni kusema kwamba baada ya mwezi kuandama tarehe 29 kwa lile kundi la mwanzo, kutakuwepo na siku mbili zaidi kwa yale makundi mawili yaliyochelewa kufunga. Jambo hili litazifanya idadi ya siku zilizofungwa duniani kuwa 31. Aidha kama mwezi utaandama tarehe 30 kwa lile kundi la mwanzo, kisha ukaongeza siku 2 kwa yale makundi mawili mengine yaliyochelewa, patapatikana idadi ya siku 32 zilizofungwa. Na katika idadi sahihi ya siku za mwezi hakuna mwezi wenye siku zaidi ya 30. Kama alivyosema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

((عن ابن عمر رضي الله عنهما عن النبي صلى الله عليه وسلم قال: "إنا أمة أمية لا نكتب ولا نحسب الشهر هكذا وهكذا" وعقد الإبهام قي الثالثة)) (رواه مسلم)

((Sisi ni umma wa kimaumbile, aghlabu yetu hatuandiki wala kuhesabu; mwezi ni hivi... na hivi... na hivi...”, akafitika kidole gumba katika ile mara ya mwisho)) (Muslim)

Maelezo: Aliposema ((hivi...na hivi....na hivi...)) na ishara ilionesha vidole vyake ‘kumi’ vya mikono kwa ‘mara mbili’ na mara ya tatu yake akafitika kidole chake cha gumba na kuviacha ‘tisa’ vikionekana.

Maana ya ishara hii ni kuwa kwa kawaida mwezi una siku 29.

(10+10+9=29)

((وعنه رضي الله عنهما قال: قال رسول الله صلى الله عليه وسلم "إنا أمة أمية لا نكتب ولا نحسب الشهر هكذا وهكذا" ويعنى مرة تسعة وعشرين ومرة ثلاثين.)) (رواه البخاري)
((Sisi ni umma wa kimaumbile, aghlabu yetu hatuandiki wala kuhesabu mwezi ni hivi... na hivi... na hivi... yaani wakati mwengine ni (siku) 29 na wakati mwengine ni (siku) 30)) (Al-Bukhaariy).

Hadiyth hizi zimekuja nyingi kwa lafdhi mbali mbali zote zikiashiria mwezi wa Kiislam una siku 29 au 30 tu. (Angalia: Sahihi Muslim, J. 7, uk. 196).



3.      Utata Kuhusu Funga Ya 'Arafah

Neno 'Arafah au 'Arafah ni jina la uwanja/viwanja maalum vilioko nje kidogo ya Mji Mtukufu wa Makkah. Mahujaji wote wanapokuweko Makkah, hutekeleza ibada maalum ya kwenda kusimama mchana katika viwanja hivyo. Jambo hilo la kwenda kusimama kwenye viwanja hivyo kwa kuomba dua na kumtaja sana Mwenyezi Mungu ni katika nguzo muhimu (kubwa) ya ibada hiyo ya Hijja.

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amebainisha hayo kwa kusema:
((الحج عرفة))
((Hijja ni 'Arafah))

Jambo hilo linamaanisha kwamba mtu asiyetekeleza nguzo hiyo wakati akiweko Makkah, atakuwa hakuipata ibada ya Hijja.

Watu humiminika na kusimama kwenye uwanja wa 'Arafah siku ya tarehe ‘9 Dhul-Hijjah’ ya kila mwaka. Ikumbukwe kwamba tarehe 9 hiyo ni ya Makkah siyo ya pahala pengine popote duniani.

Watu hao waliosimama hapo siku hiyo wameharamishwa kufunga funga yoyote. Ama watu wote wengine ambao si katika mahujaji waliosimama hapo wamependezeshwa wafunge siku hiyo ya 'Arafah ili kuadhimisha utukufu wa siku hiyo na ili kuweza kushirikiana kwa kuungana na wenzao waliosimama huko popote pale walipo duniani.

((وعن أبى هريرة رضى الله تعالى عنه أن النبى صلى الله عليه وسلم: نهى صوم يوم عرفة بعرفة))
 (رواه الخمسة غير الترمذي)

((Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amekataza kufunga siku ya 'Arafah katika (viwanja vya) 'Arafah))

Kufunga siku ya 'Arafah kuna fadhila kubwa, kama alivyosema Mjumbe wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwenye Hadiyth ifuatayo:

عن أبي قتادة الأنصاري رضي الله تعالى عنه، أن رسول الله صلى الله عليه وسلم سؤل عن صوم يوم عرفة فقال: "يكفر السنة الماضية والباقية")) (رواه مسلم)

((Aliulizwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuhusu funga ya 'Arafah, akasema ‘hufuta madhambi ya mwaka uliopita na mwaka ujao)) (Muslim)

Jambo moja la kusikitisha ni kwamba ikiwa Waislam watakubali kuwepo tofauti ya siku na tarehe baina yao, hapana shaka watakuwa wanafunga saumu ya 'Arafah siku tofauti na inavyotakiwa.

Kwa hivyo lengo na faida ya funga yenyewe litakuwa halikupatikana. Mbali na kukosekana huko Makkah, jambo baya zaidi ni kwamba watakuwa wanafunga siku ya pili yake ambapo watakuwa wanafunga siku ya ‘Iydul-Adh-ha’; siku ambayo ni haramu kufunga.

Ni vyema tuzingatie kwamba funga hii ya 'Arafah pamoja na ‘Iyd yake ni vitu ambavyo havina mahusiano na kuandama mwezi kutokana na kila nchi inavyoona mwezi wake. Bali chanzo cha funga ya 'Arafah ni uhusiano wa ile siku ambayo mahujaji wanaposimama katika uwanja wa 'Arafah. Na jambo la kusimama 'Arafah linapatikana sehemu moja ulimwenguni ambayo ni siku inayosadifu tarehe 9 Dhul-Hijjah huko Mji wa Makkah, siyo tarehe 9 ya nchi nyengine yoyote ile.

Kwa maneno mengine ni kuwa tutakapotofautiana kufunga siku ya 'Arafah baina yetu na kula kwetu ‘Iyd, ina maana kama kwamba kila nchi ina uwanja wake wa 'Arafah na Makkah yake. Kwa uthibitisho zaidi wa funga ya siku ya 'Arafah tunajifunza kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipotueleza umuhimu wa siku hii, na kila alipotaja siku hii ya 'Arafah alitumia neno ‘siku’ wala hakutamka neno ‘tarehe’:

 ((الحج عرفة))
((Hijja ni 'Arafah))

‘Siku ya 'Arafah imejaaliwa kuwa ni moja tu kwa mwaka mzima na uwanja wenyewe ni mmoja peke yake ulimwenguni. Hakuna 'Arafah zaidi ya hiyo. Ndio maana huzingatiwa siku ile wanaposimama mahujaji mahala hapo. Yatupasa kutega masikio ili tupate kujua ni lini mahujaji wanasimama hapo ili na sisi tulioko sehemu zote ulimwenguni tufunge ili tupate kushirikiana nao katika ibada hiyo. Jambo ambalo ndio lengo hasa la ibada yenyewe mbali na kule kupata ujira wa kufutiwa maovu ya miaka miwili.

Katika siku hiyo ya 'Arafah pia pana mazingatio mengine makubwa kwamba Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakuweka kabisa jambo la kutofautisha siku, tarehe na mwaka kwa Waislam wote. Vile vile alionesha kwamba Mji huu Mtukufu wa Makkah ndio marejeo (Reference) au muelekeo kwa Waislam wote ulimwengu mzima. Hebu tuzingatie kwa makini maneno ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) wakati aliposimama katika uwanja wa 'Arafah, siku ya 'Arafah katika ‘Hijjatul-Wadaa’ (Hijja ya Kuaga) ambapo siku yenyewe ilikuwa Ijumaa, tarehe 9 Dhul-Hijjah mwaka wa 10 H. Kisha akawahutubia kwa kuwaita “Enyi Watu!”أيها الناس  Huku akisistiza katika khutba yake ndefu kwa maneno kama:

((... كحرمة يومكم هذا، فى شهركم هذا، فى بلدكم هذا...))

((...katika hali ya heshima yenye utakatifu wa siku yenu hii, mwezi wenu huu na katika mji wenu huu))

Kisha baada ya hapo Mwenyezi Mungu mwenyewe Akaipiga muhuri (akaifunga) siku hiyo kwa jambo la kuwakamlishia watu wote, dini yao. Wala haikuwa kwa watu wa Makkah peke yao bali kwa Walimwengu wote. Qur-aan Tukufu imethibitisiha hayo kwa kusema:

{{الْيَوْمَ أَكْمَلْتُ لَكُمْ دِينَكُمْ وَأَتْمَمْتُ عَلَيْكُمْ نِعْمَتِي وَرَضِيتُ لَكُمُ الْإِسْلَامَ دِينًا }}

{{Leo nimekukamilishieni dini yenu, na kukutimizieni neema zangu, na nimekupendeleeni Uislam uwe dini yenu}} (Al-Maaidah 5: 3)


4.      Kufunga Siku Ya Shaka (Yawmush-Shakk)

“Yawmush-Shakk” ni ile siku inayofuatia baada ya tarehe 29 ya mwezi wa Shaabani, kisha pakawa na tetesi (maneno yasiyokuwa rasmi) kwamba mwezi umeandama. Kama itakuwa habari zenyewe si za kuaminika kisheria, jambo hilo litakuwa lina mashaka. Halina uhakika.

Ama itakapokuwa siku hiyo ya tarehe 29 Shaabani hapakupatikana habari yoyote ya kuonekana mwezi hata kama kutakuweko na mawingu yaliyotanda mbinguni, hiyo haitoitwa “Yawmush-Shakk”, na itawabidi Waislam waukadirie (waukamilishe) mwezi wa Shaabani kwa siku 30.

Yaani wangoje siku ya shaka ipite ndio waanze kufunga kwa pamoja bila ya wasi wasi na bila ya kuwepo michafuko (chaos) ya kwamba hawa wameanza kufunga leo, wengine kesho na pengine katika nchi moja. Na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametukataza kufunga siku ya shaka na akalinasibisha jambo hilo kuwa ni uasi kwa atakayelifanya.

((عن عمار بن ياسر قال: "من صام اليوم الذي يشك فيه فقد عصى أب القاسم صلى الله عليه وسلم"))
 (أبو داوود والترمذي)

((قال رسول الله صلى الله غليه وسلم: من صام اليوم الذي شك فيه فقد عصى أبا القاسم صلى الله عليه وسلم)) (البخاري ومسلم)

((Mwenye kufunga siku ya shaka atakuwa ameamuasi Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).)) (Al-Bukhaariy na Muslim).

Ni vyema kueleza kama tulivyoeleza hapo awali kwamba “Yawmush-Shakk" ni ile siku ambayo kuna minong’ono nong’ono ya kwamba mwezi umeonekana lakini habari zenyewe haikuthibiti (hazikuaminika), hapa itakuwa haramu kufunga siku ya pili yake. Ama zitakapopatikana habari za kuaminika kwamba mwezi umeandama sehemu fulani siku hiyo, basi hiyo haitokuwa tena siku yenye shaka. Itawabidi watu sehemu nyengine wafunge madamu wamepata habari za uhakika. Mtu yeyote anayepinga kufuata watu wa nchi nyengine, na pengine ni habari zilizopatikana kutoka nchi jirani, bila ya sababu za msingi, basi aelewe kwamba; huko ni kukata kichwa mchungwa tu.


5.      Utata Juu Ya Siku Ya Mwanzo Wa Ramadhaan

((عن أبي هريرة رضي الله عنه قال: قال رسول الله صلى الله عليه وسلم: إذا دخل رمضان فتحت أبواب السمآء وفي رواية: فتحت أبواب الجنة وغلقت أبواب جهنم وسلسلت الشياطين وفي رواية: فتحت أبواب الرحمة)) (متفق عليه)

((Kutokana na Hadiyth aliyoipokea Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘Anhu) amesema: “Amesema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwamba inapoingia Ramadhaan, hufunguliwa milango ya mbinguni. Na katika mapokeo mengine: Hufunguliwa milango ya peponi na kufungwa milango ya motoni na mashetani hufungwa minyororo. Na katika mapokeo mengine hufunguliwa milango ya Rehma”.)) (Imewafikiwa).

((عن ابن عمر أن النبي صلى الله عليه وسلم قال: "... فإذا كان أول يوم من رمضان هبت ريح تحت العرش من ورق الجنة على الحور العين...")) (متفق عليه)

((Kutokana na Ibn ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘Anhu) kwamba: Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “... Inapoingia siku ya mwanzo ya Ramadhaan, huvuma upepo chini ya Ardhi kutoka kwenye majani ya peponi kuwaelekea Mahurul-‘Ayn...”)) (Al-Bayhaqiy).

Kutokana na Hadiyth hizo za Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) tunaweza kuona namna zinavyoashiria uingiaji na upatikanaji wa neema mbali mbali mara tu inapoingia siku ya kwanza ya Ramadhaan.

Kwanza: Inatufahamisha wazi kuwepo kwa Ramadhaan moja tu aliyo akiitambua Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

Pili: Inatufahamisha kwamba inapoingia siku ya mwanzo ya Ramadhaan, dunia nzima hupata neema hizo kama za kufunguliwa milango ya mbinguni, kufunguliwa milango ya peponi, kufungwa kwa milango ya motoni, mashetani kufungwa minyororo, kufunguliwa milango ya rehma na kuvuma upepo maalum toka kwenye ‘Arshi ya Mwenyezi Mungu.

Yote haya hupatikana katika ile siku ya mwanzo ya Ramadhaan mara tu unapoonekana mwezi muandamo yaani tarehe 29 au 30 Shaabani.

Kwa kawaida mwanzo wa siku kwa Kiislam huanza kuingia wakati wa Magharibu mara tu jua linapokuchwa (linapotua). Ndio maana Sala za Tarawehe huanza usiku ule ule ulioandama mwezi, ikiashiria kwamba usiku ule ni usiku wa mwanzo wa Ramadhaan.

Hapa pana mambo mengi ya utata tunayoweza kujiuliza:

  • Tujaalie Ramadhaan imeanza kuingia sehemu moja hapa duniani kwa kuwa watu wa sehemu hiyo wameuona mwezi muandamo. Ikatokea watu wa upande mwengine wasiukubali mwezi huo, yaani kwao wao Ramadhaan haikuthibiti (haikuingia bado). Je katika hali kama hiyo tutaamini kwamba hizo Rehma na Neema zilizotajwa katika Hadiyth zitawashukia wale waliouna mwezi tu au ni Rehma kwa dunia nzima?
  • Inapotokea nchi fulani kama Saudia (Makkah na Madiynah) imeingia katika Ramadhaan, Tanzania bado wanangoja mwezi wao. Je inaaminika kwamba wale mashetani walioko nchini Saudi Arabia yatakuwa yamefungwa na mashetani yalioko nchini Tanzania yatabaki huru? Au tudhani mashetani yalioka Saudi Arabia yatakimbilia huku Tanzania mbio kuja 'kuvunja jungu' kwa kuwa Ramadhaan haijaingia huku bado?
  • Je kama itatokea mtu ameanza kufunga Ramadhaan siku ya mwezi akiwa Saudia, kwa bahati siku ya pili amefanya safari kuja Tanzania alipofika Tanzania bado watu wanakula mchana, Ramadhaan haijaingia bado. Je mtu huyu atapataje Barka na Rehma za kufunguliwa milango ya peponi, kufungiwa milango ya motoni na kufungiwa mashetani wakati ambapo bado mashetani yanazurura ovyo mitaani huku Tanzania? Au tusema mashetani yatafungwa kwa ajili yake peke yake mtu mmoja huyu?
  • Mtu huyu alieanza kufunga Ramadhaan akiwa Saudia, alipokuja Tanzania bado Ramadhaan haijaingia. Je ataambiwa amefunga kweli Ramadhaan au amefunga Ramadhaan alipokuwa Saudia kisha amekuja kufunga Shaabani huku Tanzania?

Kwanza ameanza kufunga Ramadhaan kisha amekuja kufunga Shaabani! Nini hukumu ya saumu yake mtu huyu?

Kwa hakika, njia ya Salama na wepesi katika hukumu hii ya kufunga mwezi mtukufu wa Ramadhaan ni pale mara tu unapoingia kwa mara ya mwanzo mwezi wenyewe wa Ramadhaan. Hoja zote za kielimu na kiakili zinakubali kwamba Ramadhaan huingia siku moja kwa dunia nzima mara tu unapoandama mwezi. Mwezi wa Ramadhaan uko katikati baina ya kumalizika mwezi wa Shaabani na kuingia mwezi wa Shawwaal.

Sha'abaan                                                    Shawwaal
Ramadhaan



Kama mtu hakupata habari kwamba mwezi umeonekana hata kama umeonekana katika nchi yake, huo ni udhuru wala hatokuwa na lawama. Lakini kama mtu amesikia kuwa mwezi umeandama itambidi afunge. Au ikiwa ndio hataki au hakubaliani na watu waliouona mwezi na kwa hivyo hayuko tayari kufuata bila sababu za msingi atakuwa amekwenda kinyume na mafundisho ya Bwana Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Na atakuwa ametenda jambo ambalo litamkosesha ujira mkubwa mno alioekewa na Mola wake. Kama vile Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alivyosema kwamba:

((عن أبي هريرة رضي الله عنه أن رسول الله صلى الله عليه وسلم قال: "من أفطر يوما من رمضان من غير رخصة ولا مرض لم يقضه صوم الدهر كله وإن صامه")) (الترمذي)

((Kutokana na Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘Anhu) kwamba Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: "Mwenye kufuturu siku moja (kula mchana) katika Ramadhaan bila ya ruhusa wala maradhi, hawezi kukidhi (kuilipa) funga hiyo hata kama atafunga dahiri (milele).)) (At-Tirmidhiy).

Pia Sayyidna 'Aliy bin Abi Twaalib (Radhiya Allaahu ‘Anhu) ameonesha umuhimu wa kufunga Ramadhaan mara tu inapoingia kwa kusema:

((أخرج الشافعي عن علي رضي الله عنه قال: لأن أصوم يوما من شعبان أحب إلي من أفطر يوم من رمضان))

Maneno haya ameyataja Imamu Ash-Shaafi’iy (Rahimahu Allaahu) kwamba Sayyidna 'Aliy (Radhiya Allaahu ‘Anhu) amesema: ((Ni bora mno kwangu kufunga siku moja ya Shaabani kuliko kula (mchana) siku moja ya Ramadhaan))

Vile vile Ibn 'Umar (Radhiya Allaahu ‘Anhu) amekuja na msimamo wake kuhusu kuingia siku ya mwanzo wa Ramadhaan. Angalia Hadiyth ifuatayo iliyoandikwa kwenye kitabu Naylul-Awtaar, J. 4, uk. 262 kama ifuatavyo:
((قال نافع وكان عبدالله إذا مضى من شعبان تسع وعشرون يوما يبعث من ينظر فإن رآى فذلك وإن لم يرو لم يحل دونه منظره سحاب ولا قتر أصبح مفطرا وإن حال دون منظز سحاب أو قتر أصبح صاؤما)) (رواه أحمد)

((Bwana Nafii (Radhiya Allaahu ‘Anhu) anasimulia kuwa ‘Abdullaah bin 'Umar alikua inapofikia tarehe 29 Shaabani humtuma mtu kwenda kutizama mwezi. Mtu huyo iwapo ameuona mwezi basi Ibnu 'Umar (Radhiya Allaahu ‘Anhu) hufunga. La ikiwa hakuuona (Ibnu 'Umar) huangalia mazingira yaliyopo kama pana wingu au utando wowote angani, hufunga; la kama hayapo mambo hayo ndio huendelea kula (siku ya pili yake) kama kawaida".)) (Ahmad)


6.      Laylatul-Qadr Ni Ngapi?

Mwenyezi Mungu Mtukufu Ameufadhilisha umma huu wa Nabii Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa kuwapa usiku maalum wenye baraka, hadhi na cheo kikubwa. Usiku huo mmoja umefadhilishwa kuliko miezi elfu moja.

Amesema Alkhattabiy kwamba: "Wamewafikiana wanavyuoni kwamba usiku huu wa 'Laylatul-Qadri' haukuwepo katika ummati zote zilizopita, bali umefanywa ni makhsusi kwa ummati huu (wa mwisho)".

Mwenyezi Mungu Mtukufu (Subhaanahu wa Ta’ala) ameyataja hayo kwa kueleza fadhila na utukufu wa usiku huo kwa kusema:

{{إِنَّا أَنزَلْنَاهُ فِي لَيْلَةِ الْقَدْرِ (1) وَمَا أَدْرَاكَ مَا لَيْلَةُ الْقَدْرِ (2) لَيْلَةُ الْقَدْرِ خَيْرٌ مِّنْ أَلْفِ شَهْرٍ (3) تَنَزَّلُ الْمَلَائِكَةُ وَالرُّوحُ فِيهَا بِإِذْنِ رَبِّهِم مِّن كُلِّ أَمْرٍ (4) سَلَامٌ هِيَ حَتَّى مَطْلَعِ الْفَجْرِ (5)}}

{{Hakika tumeiteremsha (Qur-aan) katika Laylatul-Qadr (usiku wenye heshima kubwa) (1) Na jambo gani litakalo kujulisha (hata ukajuwa) ni nini huo usiku wa Laylatul-Qadr? (2) Huo usiku wa heshima, ni bora kuliko miezi elfu (3) Huteremka Malaika na Roho katika usiku huo kwa idhini ya Mola wako kwa kila jambo (4) Ni amani (usiku huo) mpaka mapambazuko ya alfajiri (5)}} (Al-Qadr 97: 1-5)

Ama kuhusu ni lini hupatikana usiku huo, hapo wametofautiana wanavyuoni kwa namna mbali mbali. Wapo miongoni mwao waliosema kwamba usiku huo umefichwa ndani ya mwezi mzima wa Ramadhaan. Lakini kwa bahati nzuri Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametubainishia kuwa hutokea usiku huo katika kumi la mwisho wa mwezi wa Ramadhaan.

((فعن عائشة رضي الله عنها قالت: كان رسول الله صلى الله عليه وسلم يجاور في العشر الأواخر من رمضان ويقول "تحروا ليلة القدر في العشر الأواخر من رمضان")) (رواه البخاري ومسلم)

((Kutokana na mama wa Waumini 'Aaishah (Radhiya Allaahu ‘Anha) amesema: "Alikuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akijitenga katika (siku za) kumi la mwisho wa Ramadhaan na (alikuwa) akisema: "Itafuteni Laylatul-Qadr katika (siku za) kumi la mwisho wa Ramadhaan".)) (Al-Bukhaariy na Muslim).

Kutokana na maelezo hayo inatubainikia kwamba "Usiku wenye Cheo" hutokea katika kumi la mwisho wa Ramadhaan, lakini jee ni siku ipi hiyo katika kumi la mwisho? Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakuwacha kutubainishia kwamba hutokea usiku huo katika usiku ulio na tarehe ya 'Witri' (Odd Numbers) yaani 21, 23, 25, 27 au 29.

Kama alivyosema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwamba:

(("تحروا ليلة القدر في الوتر من العشر الأواخر من رمضان"))

((Itafuteni Laylatul-Qadr katika (siku ya) witri kwenye kumi la mwisho wa Ramadhaan)) (Al-Bukhaariy na Muslim)

Hata hivyo Mwenyezi Mungu Ameuficha usiku huo, hakuna anayejua ni usiku gani hasa katika hizo witri za kumi la mwisho? Lakini wanavyuoni wengi wanakubaliana kwamba huenda usiku huo ni usiku wa tarehe 27. Kama alivyopokea Imaam Ahmad kutoka kwa Ubay bin Ka'ab amesema:

((سمعت رسول الله صلى الله عليه وسلم يقول: "ليلة القدر سبع وعشرين"))

((Nimemsikia Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: 'Usiku wenye cheo ni usiku wa ishirini na saba (27)'.))

Jambo la msingi hapa tunajifunza kwamba Laylatul-Qadr hupatikana usiku mmoja tu kwa mara moja tu katika hilo kumi la mwisho wa Ramadhaan. Usiku huo unawakilisha kumbukumbu ya kuteremka kwa Qur-aan Tukufu. Kama alivyotaja Mwenyezi Mungu Mtukufu:

{{إِنَّا أَنزَلْنَاهُ فِي لَيْلَةِ الْقَدْرِ}}

{{Hakika tumeiteremsha (Qur-aan) katika 'usiku wenye cheo' (Laylatul-Qadr)}} (Al-Qadr 97: 1)

Bila shaka Qur-aan yote kwa ujumla imeelezwa kwamba iliteremka siku moja kwa ukamilifu wake kutoka kwenye Lawhil-Mahfuudh kuja kwenye Samaa-Dunya kisha baada ya hapo ikawa inateremshwa kidogo kidogo kwa kutegemea haja, matokeo au sababu mbali mbali kwa muda wote wa miaka 23 ya Utume wa Mtume wetu Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

Tukikumbuka Hadiyth zilivyokuja kutaja kuwa kuna uwezekano wa kutoka Laylatul-Qadr usiku mmoja katika kumi la mwisho wa Ramadhaan, tena uwezekano mkubwa ni tarehe 27. Sasa kama tutakadiria hivyo, kwamba Mwenyezi Mungu Amejaalia Laylatul-Qadr itokee usiku wa 27.


  • Suala la kujiuliza hapa, Je ni tarehe 27 ya nchi gani hiyo ikiwa tutakubali kuwepo tofauti ya siku na tarehe baina ya nchi mbali mbali?
  • Au tusema ikiwa kila nchi itateremkiwa na Laylatul-Qadr kwa 27 yake. Je kutakuwepo na Laylatul-Qadr ngapi ulimwenguni?
  • Pindipo itatokea Laylatul-Qadr usiku wa 27 kule nchini Saudi Arabia ambapo huku kwetu Afrika Mashariki usiku huo huo bado ni 26. Je tatahukumu vipi, Laylatul-Qadr itatokea kesho yake kwa hapa Afrika Mashariki au ndio tutajumuika nao kuipata Laylatul-Qadr siku hiyo hiyo moja? Je, 27 = 26?
  • Kama tutakubali kuwa inawezekana kutokea Laylatul-Qadr usiku wa 26 au 28, tuelewe kwamba tunahukumu kinyume na maneno ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) pale aliposema kwamba hutokea Laylatul-Qadr katika Witri ya kumi la mwisho wa Ramadhaan.
  • Na kwa vile Laylatul-Qadr huweza kutokea tarehe 29 kwa mwezi ulioonekana Tanzania. Je zile nchi zilizo mbele ya Tanzania kwa tarehe kutokana na mwezi ulivyoonekana kwao ndio tusema zitakosa Laylatul-Qadr? Kumbuka nchi hizo zitakuwa zimeshatoka katika mwezi wa Ramadhaan na zimeshaingia katika Shawwaal.

Je itapotokea kwenye nchi moja kama Tanzania ambapo kuna makundi kama matatu yaliyoanza kufunga kwa tarehe tofauti tofauti, lakini kwa makundi yote matatu bila shaka yamo ndani ya usiku mmoja usio na tofauti hata ya sekunde moja na wapo katika sehemu moja. Ndio tukadirie watakuwa na Laylatul-Qadr tatu tofauti? Au ndio wengine wataupata usiku wa Laylatul-Qadr na wengine wataukosa? Hasa kama tutachukulia Laylatul-Qadr imetokea usiku wa 29 wa kundi moja wapo.


Maelezo Juu Ya Kupatikana Kwa Usiku

Ni vyema kujikumbusha kwamba maelezo ya kisayansi yaliyopatikana kwenye Qur-aan Tukufu yanazingatia kwamba 'nyakati' hupatikana kutokana na mipinduko ya jua, mwezi na dunia. Hapana shaka yoyote dunia ina mizunguko yake miwili. Kwanza kuna ule mzunguko wa dunia kulizunguka jua ambapo mzunguko huu husababisha mabadiliko ya miongo (seasons) mbali mbali kama vile mchoo, vuli, kipupwe au kiangazi.
Pili ni ule mzunguko wa dunia kujizunguka yenyewe katika mhimili (axis) wake. Mzunguko huo wa pili ndio unaosababisha kupatikana usiku na mchana. Kwa kawaida dunia hujizunguka yenyewe kamili kwa muda wa masaa 24 ambayo hupatikana 'siku' moja yenyewe usiku mmoja na mchana mmoja.
Usiku na mchana ni nyakati mbili zinazopatikana mara moja kila siku ya hapa duniani. Mwenyezi Mungu ameziumba nyakati mbili hizo kama Alivyoumba jua na mwezi. Qur-aan Tukufu imetaja hayo kwa kusema:

{{وَهُوَ الَّذِي خَلَقَ اللَّيْلَ وَالنَّهَارَ وَالشَّمْسَ وَالْقَمَرَ ۖ كُلٌّ فِي فَلَكٍ يَسْبَحُونَ }}

{{Na yeye ndiye aliyeumba usiku na mchana na jua na mwezi, vyote vinaogelea katika duara (zao).}} (Al-Anbiyaa 21: 33)

{{لَا الشَّمْسُ يَنْبَغِي لَهَا أَنْ تُدْرِكَ الْقَمَرَ وَلَا اللَّيْلُ سَابِقُ النَّهَارِ ۚ وَكُلٌّ فِي فَلَكٍ يَسْبَحُونَ}}

{{Haliwi jua kuufikia mwezi, (wakati wa nguvu zake) wala usiku kuupita mchana, (ukaja kwa ghafla kabla ya wakati wake). Na vyote vinaogelea  katika njia (zao).}} Yaasiyn (36:40)

Angalia pia aya zifuatazo kwa ufafanuzi zaidi:

Yunus 10: 5, Al-Jaathiyah 45: 13, Ar-Rahmaan 55: 5, Al-An-'Aam 6: 96, Ibraahiym 14: 33, An-Nahl 16: 12, Al-Furqaan 25: 61, Nuuh 71: 15-16, An-Nabaa 78: 12-13, At-Tawbah 9: 36, Al-Aaraf 7:54.

Habari zifuatazo zimenukuliwa kutoka gazeti la An-Nuur, toleo nambari 79, Jumaadath-Thaaniy, 1417 – Oktoba 1996 ukurasa 10. Habari hizo zimeandikwa kama ifuatavyo:

"Kupishana kwa mchana na usiku:"

Qur-aan iliyoteremka zama ambazo watu walidhani kuwa Dunia ndio katikati ya ulimwengu, na kwamba jua ndio lilikuwa linaizunguka dunia. Aya za Qur-aan zikatoa maelezo yafuatayo:

(Angalia: Al-Aaraf 7: 54, Yasiyn 36: 37, Luqman 31: 29, Az-Zumar 39: 5)

Neno lililotumika katika Qur-aan ni "Kawwara" yaani "kufunika". Kwa asili yake neno hilo lina maana ya kuviringisha kilemba kichwani. Maana hii ya kufunika kwa kuzungushwa imo katika msemo wa Qur-aan hasa tukizingatia kinachotokea katika kupishana kwa usiku na mchana.

Wanaanga wa Marekanani wameona na kupiga picha kinachotokea iwapo mtu ataangalia dunia kutokea mbali sana, tuseme iwapo mtu yupo mwezini. Waliona jinsi ambavyo mwanga wa jua unavyoangazia daima ile sehemu ya dunia inayokabiliana na mwanga huo.

Na ile sehemu isiyopata mwanga huo inakua gizani. Sasa dunia inapozunguka katika mhimili wake nusu moja huwa mwangani na mwengine gizani. Na baada ya muda, ile iliyokuwa gizani huwa mwangani. Ukiangalia kwa mbali unaona kama kwamba mchana na usiku vinajiviringisha katika ile sayari ya dunia".

Kielelezo Nam 4: Ramani ya dunia inavyoonesha kupishana kwa usiku na mchana.

http://www.alhidaaya.com/sw/UserFiles/MWEZI%204.jpg


7.      Uharamu Wa Kufunga Siku Ya ‘Iyd

Kama tulivyokwishaeleza sehemu nyingi hapo awali kwamba masuala ya tarehe, siku na mwezi yanahusiana zaidi na ulimwengu mzima kwa pamoja, isitoshe ni jambo la watu wote.

Jambo la kupishana masaa machache baina ya nchi moja na nyengine, sio sababu ya kudai kuwepo kwa tofauti ya siku nzima au nchi hizo zimetofautiana kitarehe.

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kila alipoakizungumzia amri za kufunga na kufungua alikuwa anazitaja kama ni amri kwa watu wote ulimwenguni. Hakutaja hata amri moja ya kufunga au kufungua kwa kuhusisha watu wa Makkah na Madiynah peke yao.

Kuhusu siku za ‘Iyd yaani sikukuu, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) pia hakuwacha kutuhutubia kuwa ni jambo la pamoja yaani kwa Waislam wote ulimwenguni:

((و عن عائشة رضي الله عنها قالت: قال رسول الله صلى الله عليه وسلم: "الفطر يوم يفطر الناس، والأضحى يوم يضحى الناس")) (رواه الترمذي)

((Na kutoka kwa mama wa Waumini 'Aaishah (Radhiya Allaahu ‘Anha) amesema: Amesema Mjumbe wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwamba: ‘Iydl-Fitri ni siku ya watu kula na ‘Iydl-Adh-ha ni siku ya watu kuchinja (wanyama).)) (At-Tirmidhiy)

Katika Hadiyth hii pana mazingatio yafuatayo:

a)    ‘Iyd zote mbili zimehusishwa moja kwa moja kwa tamko la 'watu', kwa hivyo sikukuku hizi ni kwa ajili ya Waislam wote ulimwenguni, sio watu wa nchi au kijiji kimoja.
b)    Siku zote mbili zina uhusiano wa matukio maalum kwa dunia nzima kwanza kumalizika kwa mwezi Mtukufu wa Ramadhaan ambao ni mfungo wa duniani kote. Pili ibada ya kuchinja inatokana na kumalizika kwa Hijjah ambayo pia ina uhusiano wa moja kwa moja na dunia nzima.
c)     Ibada ya Funga imefaradhishwa Madiynah katika mwaka wa pili Hijiriya na ibada ya Hijjah imefaradhiswa huko katika mwaka wa sita[2][2] Hijiriya. Kwa hivyo marejeo (References) ya ibada hizi mbili ni kuangalia kwamba ibada zenyewe zina mahusiano ya moja kwa moja na Miji hiyo. Kama Mwenyezi Mungu Alivyotuthibitishia juu ya jambo la kuandama kwa mwezi kuwa ni jambo la 'watu' wote pamoja na ibada ya Hijja, kama Alivyosema kwenye Qur-aan Tukufu:

{{يَسْأَلُونَكَ عَنِ الْأَهِلَّةِ ۖ قُلْ هِيَ مَوَاقِيتُ لِلنَّاسِ وَالْحَجِّ}}

{{Wanakuuliza juu ya miezi. Sema: "Hiyo ni vipimo vya nyakati kwa ajili (ya mambo) ya watu na (mengine) ya Hija (zao).}} (Al-Baqarah 2: 189)

Kwa kuzingatia maana halisi ya kuwekewa Siku Kuu mbili hizi, utaona kwamba kuna mazingatio maalum ya kujenga umoja baina ya watu na kukirimiana. Katika siku hizi tukufu Waislam hupeana mikono ya furaha, hupeana sadaka na hutembeleana. Furaha hizo hufanyika tokea baina ya mtu na mtu, familia hadi jamii nzima. Katika wakati wetu wa sasa, utawaona Waislam wanawasiliana sehemu mbali mbali ulimwenguni kupeana mkono wa ‘Iyd kwa kupigiana simu, kupelekeana posti kadi na mengineyo. Jambo hilo linaonesha dhahir kwamba Siku Ya ‘Iyd inawezekana kabisa kusherehekewa siku moja tu ulimwenguni kote.

Mifano mizuri ni siku kuu zote za kilimwengu – za dini nyengine, za kisiasa, za kiuchumi na nyingi nyenginezo husherehekewa kimataifa na huadhimishwa kwa siku moja duniani kote bila ya kuzingatiwa tofauti za masaa baina ya nchi moja na nyengine. Hili ni jambo linalowezekana kabisa, na ndivyo itakiwavyo.

Kwa upande wa mas-ala ya uingiaji wa ‘Iyd yenyewe, kitu cha msingi ni kwamba ziwe zimepatikana habari kuwa mwezi umeonekana na Waislam. Kama tulivyokwishaeleza kwa kirefu hapo nyuma kuwa watu wawili tu hutosheleza kutoa ushahidi wa kuona mwezi wa Shawwaal. Yaani ndio uthibitisho wa kuingia ‘Iydl-Fitri.

Kwa hivyo, mtu yeyote ambaye amepata taarifa rasmi kwamba ‘Iyd imeingia, haimuwajibikii tena kisheria kuendelea kufunga funga ya aina yoyote siku hiyo. Kwa maana nyengine, ni haramu kufunga siku ya ‘Iyd kama alivyotukataza Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika Hadiyth zifuatazo:

((عن أبي سعيد الخذري رضي الله عنه قال: أن رسول الله صلى الله عليه وسلم: نهى عن صيام يومين، يوم الفطر ويوم النحر)) (متفق عليه)

((Na kutoka kwa Abu Sa'iyd al-Khudriy (Radhiya Allaahu ‘Anhu) ni kwamba: Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amekataza kufunga siku mbili: Siku ya ‘Iyd-Fitri na Siku ya ‘Iyd ya kuchinja)) (Al-Bukhaariy na Muslim)

((... عن النبي صلى الله عليه وسلم قال: "لا تسافر المرأة يومين إلا معها زوجها أو ذو محرم. ولا صوم في يومين: الفطر و الأضحى...)) (البخاري)

((…Asisafiri mwanamke siku mbili peke yake ila awe pamoja na mumewe au mahrimu yake. Wala msifunge siku mbili: ‘Iydul-Fitr na ‘Iydul-Adh-haa)) (Al-Bukhaariy)

CHANZO: www.alhidaaya.com




No comments:

Post a Comment