Sifa njema zote zinamstahikia Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Ambaye Ameumba vitu
vyote kisha Akavipangia hali zake tofauti tofauti. Tunakiri kwamba hakuna jambo
lolote lililoweza kutokea huko nyuma au linalotokea wakati huu wala
litakalotokea baadae isipokuwa kwa Amri yake Mola pekee.
Ndiye Yeye Aliyemleta Nabii Muhammad
(Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ambaye ndiye kipenzi chake, ili
awe ni kigezo cha kufuatwa na walimwengu wote kwa ajili ya uongofu. Naye Nabii
ametekeleza haki ya ujumbe wa Mola wake ambao
alitusisitiza Waislamu sote tuwe wamoja katika kila jambo kwa hali
yoyote inayowezekana. Lakini
kutokana na kuwa
wanaadamu wameumbwa katika hali tofauti-tofauti zisizokamilika ndio panajitokeza tofauti za kifikra na
kimatendo. Bila shaka hayo yanatokana na
mapungufu tuliyonayo sisi wanaadamu hata katika kuifahamu Amri
iliyokamilika ya Mola wetu.
Kitabu hiki ni kama nasaha kwa Waislamu
wote ili kuweza kudumisha umoja wetu hususan pale ambapo pamejitokeza misimamo
tofauti katika mambo ya ibada. Wala lengo la kitabu hiki sio kuendeleza
malumbano baina ya Waislamu wenyewe kwa
wenyewe hata kwa wale wenye misimamo
tofauti. Kutajwa ndugu yetu Juma
Muhammad Rashid lilikuwa ni jambo lisilobudi wala hapakuwa na lengo la
kumkashifu au kumuumbua bali ni kutokana
na kuwa hapakuweza kupatikana njia
mbadala kwa vile ameshaandika kitabu ambacho ameshakichapisha chapa ya
kwanza na ya pili.
Msisitizo wetu mkubwa katika kitabu
hiki ni ile nukta muhimu ya kwamba suala la kufunga na kufungua kwa muandamo
mmoja kwa dunia nzima si jambo jipya kama wanavyodhani baadhi ya watu, ni jambo la
kale mno ambalo linaweza kutekelezeka na
kwamba huo ndio uliokuwa msimamo wa
‘Jamhur’ ya wanavyuoni.
Mwisho tunatarajia kwamba wasomaji wetu
wapendwa watakaokisoma kwa makini kitabu hiki wataweza kuzitumia vyema akili
zao huru bila kuweka (taasub) dhana potofu ya aina yoyote ile.
Tunamuomba Allaah (Subhaanahu
wa Ta’ala)
Atuonyeshe mema na Atuwezeshe kuyafuata na Atuonyeshe mabaya na Atuwezeshe
kuyaepuka. Amiyn.
KAMATI YA TAALUMA,
MASJID SUNNAH,
KIKWAJUNI,
TAREHE: 26/Jumadal Akhar/1430,
19/06/09.
Ndugu yetu Juma
Muhammad Rashid Al-Mazrui amejitahidi kuandika kitabu alichokiita: “Ushahidi
Uliowekwa Wazi Katika Suala La Miandamo Ya Mwezi.”
Makusudio yake
yalikuwa ni kutaka kukijibu kitabu kilichoandikwa na Shaykh Naaswir Abdullah
Bachuu kinachojulikana kwa jina la “Ufafanuzi Wa Mgogoro Wa Kuandama Kwa
Mwezi.” Kutokana na jambo hilo, sisi kwa upande mmoja tunashukuru kwa juhudi
yake hiyo na kwa upande wa pili tunatuma masikitiko yetu kwake kwa kutokuwa
makini na muadilifu katika kulifafanua jambo hilo muhimu.
Kwani kitabu
chake hicho kimeandikwa katika mfumo wa chuki, kibri, kejeli na malumbano huku
akisisitiza kwa mara nyingi kauli chafu ambazo muandishi hapaswi kuzitumia
katika kitabu au katika mijadala ya Dini.
Mfano wa kauli
zake mbaya ni kama zifuatazo:
((vuta-nikuvute)) [uk. 6]
((hii ni ajabu katika ajabu za dunia!)) [uk. 124]
((Kwa
hivyo, uwezekano huo alioutoa Sheikh hauwashi wala hauzimi …)) [uk. 124]
((Ninasema: Enyi walimwengu wenzangu tazameni hoja za kielimu
hizo!!!!!!! Kwani nyinyi Wazanzibari kabla ya kuja fikra hio ya Sheikh Nassor
Bachoo ya kufunga kwa muandamo mmoja,))
((Utaona kwamba masuala yote haya si yenye kima katika soko la
elimu, bali ni masuala ya kuwababaisha watu wasiojua nini cha kujadiliwa katika
mas-ala haya ya funga.)) [uk. 167]
((Hoja nyengine – nayo pia ni hoja ya mitaani – ni kuwa watu
wengi wa kawaida wanapouona mwezi mkubwa husema: "E basi ule ndio mwezi
wa leo ule?!!!"))
((Jawabu hii ya mwisho, inaufanya upinzani mzima wa Sheikh
Bachoo kuwa hauna maana yoyote.)) [uk. 132]
((Kwa ufupi ni kuwa hicho walichokidai
watetezi wa rai pinzan…)) [uk. 32]
((utaona jinsi gani mwanamume alivyokuwa bingwa wa kubadilika!
Na hili si jengine bali ni lile Waswahili wanalolisema: "Mfa maji hukamata
maji.")) [uk. 128]
((Hakuna hapa kinachoonesha mas-ala ya
kufunga kwa muandamo mmoja wala kumi na moja.)) [uk. 125]
((haina maana kwamba usiku ukiingia sehemu moja ndio umeingia
dunia nzima. Kwa ufupi ni kuwa hii ni hoja ambayo haina faida yoyote ya
kielimu, lakini tunaijadili kwa ajili ya watu wa mitaani tu.))
Kwa hakika
katika kitabu chake hicho kwenye uk. 6, anajionyesha alivyo na kauli mbili
tofauti: Kwanza anakubali kwamba suala la muandamo wa mwezi lina ikhtilafu
katika kufunga kwa kumuelezea Shaykh Naaswir Bachuu kwamba: ((Tunampongeza kwa juhudi…))
Kisha pale pale
anageuka kwa kusema: ((madamu hili ni suala la khilafu –
basi ilikuwa ni kutolizungumza kabisa,)) Sasa hebu
tumuulize ndio anapongeza nini? Na ni nani aliyemwambia kwamba jambo lenye
khitilafu halizungumzwi? Yeye angezungumza nini katika kitabu chake kama si
masuala ya ikhtilafu? Pia anatwambia haya ni katika mambo ya furui
(matawi) za Kidini, kwa hivyo zisizungumzwe. Kwani ni nani aliyemwambia kuwa furui
za Kidini hazizungumzwi?
Sisi tunapenda
kumfahamisha kuwa suala hili la kwamba mwezi ukiandama sehemu moja unatosheleza
kufuatwa kwa kufunga au kufungua ulimwengu mzima, si suala jipya bali ni jambo
la kale. Tunasikitika kwamba hakuangalia vizuri maoni ya Wanavyuoni wakubwa
walivyoelezea msimamo huo. Angalia katika kitabu cha Shaykh Naaswir Bachuu uk.
51-58. Hapa tunanukuu baadhi ya kauli hizo:
Imamun-Nawawy
aliyekisherehesha Kitabu cha Sahihi Muslim anasema:
والصحيح عند أصحابنا أن الرؤية لاتعم
الناس بل تختص بمن قرب على مسابقة لاتقصر فيها الصلاة، وإلا فلا. وقال بعض أصحابنا
تعم الرؤية في موضع جميع أهل الأرض.
“Na jambo lililo sahihi kwa wenzetu (Mashaffi)
ni kuwa muandamo mmoja hauwahusu watu wote bali unawahusu wale walio karibu kwa
kiasi ambacho hawaruhusiki kupunguza Sala (Sala ya safari). Pia imesemwa kuwa
iwapo matlai ni mamoja watalazimika (watu) kufunga pamoja. Pia imesemwa kuwa
ikiwa (wanaishi) katika eneo la Iklimu moja (maili 72 au km 89) (watalazimika
kufunga pamoja) vyenginevyo kila mmoja atafunga kwa muandamo wake. Na
wakasema wenzetu wengine (Mashaffi) kuwa muandamo katika sehemu moja utawahusu
wote wa dunia nzima”.
Shaykh
Jaadul Haq wa chuo kikuu cha Al-Azhar katika kitabu chake “Bayaanullinnas” J. 2
uk. 203 - 204 ameandika yafuatayo juu ya kauli hiyo ya Imamun-Nawawy:
“….Hapa Imamu An-Nawawy
ametaja kwa mukhtasari kauli zilizomo katika madhehebu ya Kishaffi (juu ya
kuandama kwa mwezi) na ambazo pia zimo katika madhehebu mengine ya Kiislamu.
Kauli hizo tunaweza kuzigawa katika mafungu matatu makuu:
“...Hapo Imamu An-Nawawy
ametaja kwa mukhtasar kauli zilizomo katika madhehebu ya Shaffi (juu ya
kuandama kwa mwezi) na ambazo pia zimo katika madhehebu nyengine za Kiislam.
Kauli hizo tunaweza kuzigawa katika mafungu matatu makuu:
Kauli ya kwanza: “Kila
nchi iwe na matlai yake, wala muandamo wa nchi moja hautalazimu nchi nyengine
ya mbali wala karibu”.
Kauli ya pili:
“Muandamo wa nchi moja unalazimu nchi zote za dunia hata kama ziko mbali”.
Kauli ya tatu:
“Muandamo wa nchi moja unalazimu nchi iliyo karibu nayo au inayowafikiana
kimatlai”.
Kisha, Shaykh Jaadul-Haq akaendelea kusema kwamba:
...وكلها آزاء التهادية لاتقوم على دليل قطعى ثبوتا
ودلالة. فيحتار منها ما يتفق المصلحة العامة.
“...Na (kauli) zote hizo ni maoni yatokanayo
na Ijtihaadi ambazo hazikusimama juu ya hoja kat-ii, si sanad wala matni. Kwa
hivyo ingefaa ichaguliwe kauli ambayo inakubaliana na maslahi ya (Waislam wote
wa) dunia nzima kwa jumla”.
Tungependa
kumueleza ndugu yetu kwamba hata hapa Afrika ya Mashariki jambo hili
hakulianzisha Shaykh Naaswir Bachuu kama alivyodai mwenyewe (Nd. Juma) kwamba: ((Muafrika wa Mashariki wa kawaida kusikia sauti ya mgogoro)) Inasikitisha hakuweza kuangalia katika kitabu cha Shaykh Naaswir Bachuu
uk. 161-163 wametajwa walioonyesha kwa vizuri kabisa misimamo hiyo tofauti.
Mashaykh wenyewe ni hawa wafuatao: Al-marhuum Shaykh Juma Abdul Waduud (wa
Zanzibar), Shaykh Abdillahi Naaswir (Nairobi Kenya), na Shaykh Naaswir Khamis
Abdul Rahman (Mombasa Kenya).
Pia Shaykh
Ahmad Al Khalil, Mufti wa Omani amethibitisha kwamba Ikhtilaf hii ya muandamo
wa mwezi katika hukmu ya kufunga au kufungua ipo na kwamba ni jambo la kale.
Kama alivyosema maneno yake yaliyotafsiriwa na Shaykh Muniir Sulayman 'Aziz
kwamba:
“Hakuna madhehebu iliyokuwa imesalimika na
kuwa na Khitilafu baina ya Wanavyuoni wake juu ya suala la kutafautiana
miandamo ya mwezi.”
Jee ndugu Juma
anataka kusema kwamba Shaykh Naaswir Bachuu ndiye mwalimu aliyeanzisha
madhehebu zote? Au ndiye aliyeanzisha mtafaruku huu kama alivyouita mwenyewe
ndugu Juma?
Katika
kudhihirisha udhaifu wake wa kumuandama mtu fulani; Ndugu Juma anasema: ((Kama tunavyojua kwamba Sheikh Nassor
Bachoo, ni mmoja wa wenye kusisitiza ulazima wa kuwa na muandamo mmoja.))
Sisi kwa upande
wetu tunasema: Katika kitabu cha Shaykh Naaswir Bachuu hakuna pahala
alipolazimisha watu wafuate huo aliouita ndugu Juma (msimamo wa Shaykh
Naaswir). Bali yeye ameonesha mitizamo ya Wanavyuoni kwa kutumia Aya za
Qur-aan, Hadiythi na vitabu vinavyokubalika. Lugha aliyotumia Shaykh Naaswir
katika huo unaonekana ni msimamo wake ni maneno yaliyozimuliwa kilugha (polite
language) kama vile: ((inawezekana…))
((inaonyesha…))
Aliyelazimisha
rai ni ndugu Juma mwenyewe kama anavyosema: ((Lakini kilicho lazima na ambacho tunatakiwa tukubaliane ni
kuwa muandamo wa mbali hautendewi kazi mbali.)) [uk. 112]
Kisha katika
uk. 85 ndugu Juma anataja kwamba msimamo huu wa muandamo mmoja kwa dunia nzima
ni ((kitu kipya))
na kwamba jambo hilo halitekelezeki
na ni kauli iliyobaki vitabuni
tu baada ya kutaja baadhi ya nchi zinazofuata miandamo yao – yaani kila
nchi na muandamo wake kama Al-yaman, Oman, Misri na Saudia. Kisha hapo hapo
akataja: ((isipokuwa Imarati katika miaka ya
mwisho wamekuwa wakifata Saudia.))
Inafaa ndugu
Juma aulizwe masuala yafuatayo:
i)
Kama ni jambo lisilotekelezeka vipi tena Imarat wanalitekeleza?
ii)
Je hawa wa Imarat nao ni wanafunzi wa Shaykh Naaswir
Bachuu?
iii)
Kwani hiyo sio
kauli ya Jamhuur ambayo ndio msimamo wa
maimamu wakubwa wakiwemo Ahmad
bin Hanbal, Malik na Abu Hanifa? (Angalia
pia sehemu ya 11 na 13 za kitabu
hiki)
Na sisi
tunamuongezea habari moja ambayo ni vyema kuielewa, kwamba nchi ya Uganda iliyo
katika Afrika ya Mashariki pia inafuata rasmi muandamo mmoja wa duniani. Pia
aelewe kwamba huo msimamo wa kila nchi na mwezi wake huku Afrika ya Mashariki
haukuwepo tokea zamani. Mashaykh wote wa huku wanakubaliana mwezi ukionekana
popote katika nchi hizi tatu (Kenya, Uganda na Tanzania) wanafunga pamoja. Yeye
anaendelea kushika msimamo wake: ((Al-yaman wanafata muandamo wao, Oman
wanafata muandamo wao, Saudia wanafata muandamo wao,)). Lile
analoliona yeye halitekelezeki, basi ndio linatekelezeka.
Kuna suala moja
la nyongeza tunapenda tumuulize ndugu yetu Juma: Hata kama hizo nchi
alizozitaja (Al-Yaman, Oman, Misri na Saudia) hazijakubaliana kufuata muandamo
mmoja, je hakuna uwezekano (japo wa sadfa) unaoweza kutokea kufunga siku
moja ijapokuwa kila mmoja ameona mwezi katika nchi yake? Sasa tuseme kila nchi
katika hizo imeona mwezi usiku wa Alkhamisi kuamkia Ijumaa - Wote si watafunga
siku moja ya Ijumaa? Basi huo ndio utekelezaji aliosema hautekelezeki. Ni wazi
kuwa unatekelezeka.
Tunapenda
kumfahamisha ndugu Juma kwamba mara nyingi inaweza kutokezea katika jambo moja
watu kutofautiana lakini hawapingani. Ni vyema kuelewa kwamba upinzani umo
katika Siasa za kilimwengu na mambo
mengine sio katika masuala ya Dini. Katika Dini hutokea Ikhtilafu. Masahaba (Radhiya Allaahu
‘Anhum) pia walikuwa wakikhitilafiana katika baadhi ya mambo,
lakini hawakuwa wakipingana. Kila mmoja aliweza kushika mwendo wake bila
kugombana na mwenzake. Ama pale ulipotokea upinzani kwa bahati mbaya –
jambo hilo liliwapelekea kugombana au kupigana vita, kwani jambo hilo ni katika
amali za Kishetani. Lakini mara walipotanabahi juu ya udhaifu huo waliomba toba
kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) na kutakana misamaha baina yao. Na huo bila shaka ndio mwendo wa watu
wema.
Kwa bahati
nzuri semina na makongano yote yaliyofanyika ndani na nje ya Zanzibar
hapajatokea kuitwa ‘pinzani’ wala neno ‘upinzani’ halijatumika hata mara moja.
Bali semina zote zilizowahi kufanyika zimekuwa zikisisitiza maneno ya ‘umoja’
na ‘kuelimishana’ wala sio ‘kupingana.’
Neno ‘upinzani’ haliko katika midomo ya
Wanavyuoni. Tanasikitika sana kuwa Ndugu yetu Juma Muhammad Rashid amelitumia
neno ambalo si zuri la ‘upinzani’ na kulikariri katika kitabu chake zaidi ya
mara 33. Kwa kweli hizo si kauli za wenye busara na hikma, bali ni kama
alivyozoea kuzitumia. Kwa mfano pale alipokuwa akimlalamikia Shaykh Naaswir
Bachuu, alisema:
((Tazama
pia katika uk. 109-110 uone upinzani alioutoa hapo halafu linganisha upinzani
huo na upinzani alioutoa kabla ya hapo, utaona jinsi gani mwanamume alivyokuwa
bingwa wa kubadilika! Na hili si jengine bali ni lile Waswahili wanalolisema:
"Mfa maji hukamata maji." ))
Tunamshukuru
Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) kwamba kwa upande wa hapa kwetu Tanzania watu wanaruhusiwa kufunga na
kufungua kwa mujibu wa misimamo yao (yote miwili) bila ya kugombana. Swala za
'Iyd kwa upande wa watu wanaofuata mwezi unapoonekana popote duniani wamekuwa
wakiswali misikitini na viwanjani bila ya bughudha yoyote. Bali hata katika
familia moja yenye misimamo hiyo tofauti, watu hawagombani. Huko ndiko kukhitilafiana
sio kupingana.
Jambo jengine
la kusikitisha ni kuwa ndugu Juma haonyeshi kuwaheshimu Wanavyuoni au kuwapa
hadhi zao wanazostahiki. Wanavyuoni wana heshima zao hata pale wanapokosea. Ni
vyema kuelewa kwamba Al Imam Shawkani alikuwa ni miongoni mwa Wanavyuoni
wakubwa kama ilivyoelezwa kwenye historia yake fupi katika kitabu cha “Kuandama Kwa Mwezi” cha Shaykh Naaswir Bachuu Uk. 35. Al
Imam Shawkani aliandika vitabu vingi vya kukubalika pamoja na Tafsiri yake ya
Qur-aan Tukufu inayojulikana kwa jina la “Fathul Qadir.”
Ndugu Juma
katika kujikweza kama kwamba yeye ana elimu kubwa zaidi na kwamba anakubalika
zaidi kuliko Al Imam Shawkani, anathubutu kusema: ((Huo ndio upinzani wa pili wa Al-imamu Al-shaukaniy, lakini
kama unavyoona jawabu yetu ya kwanza inajibu baadhi ya nukta zilizomo katika
upinzani huu.)) [uk: 111]
Kisha
akamfananisha Al Imam Shawkani na watu wa kawaida (yaani labda ni mtu wa
mitaani asiyekuwa na elimu) kwa kusema: ((Maneno haya ya Al-imamu
Al-shaukaniy – kama yalivyo maneno ya watu wengi wa kawaida.))
Ndugu Juma
katika kumuandama Al Imam Shawkani anaendelea kusema: ((Penye andiko huwa hapana ijtihadi;)) kama kwamba Al Imam Shawkani alikuwa hajui Qur-aan wala Hadiyth. Au
kama kwamba Al Imam Shawkani anampinga Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).
Angalia katika
kitabu chake Ndugu Juma kwenye uk. 108 - 109 ameeleza misimamo ya Wanazuoni
wawili mashuhuri; yaani Al Imam Badru Din na Shaykh Al Khalil ambao wamejaribu
kuukosoa msimamo wa Al Imam Shawkan lakini kwa njia nzuri. Wote wawili
wameonyesha kwamba ile ni Ijtihadi ya Al- Imam Shawkani katika kumfahamu Ibni
''Abbas katika kisa cha Kuraib wala hawakumfanya Al Imam Shawkani kama ni
mpinzani. Ni vyema kuelewa pia kwamba wanaweza kutokea Wanavyuoni wengine
wanaoweza kusema pia kwamba na hizo ni Ijtihadi za Al Imam Badru Din na Shaykh
Al Khalil katika kumfahamu Al Imam Shawkani. Wala huwezi kusema kuwa Al Imam
Shawakani alikuwa halifahamu andiko, Shaykh Al Khalil ndio amelifahamu andiko.
Hizo zote ni Ijtihadi katika kukifahamu kisa cha Kuraib.
Katika kitabu
chake alichokiandika, Ndugu Juma ameonyesha udhaifu wake wa kulazimisha
kujaribu kujibu hoja za kitabu cha Shaykh Naaswir Bachuu. Maneno yake mengi
yametawaliwa na ubinafsi. Hakupenda kuwa muadilifu katika kueleza hoja zake
ingawa yeye mwenyewe anapokwama kihoja hujifanya kumgomba Shaykh Naaswir Bachuu
huku akimwambia:
((Kwa ufupi ni kuwa hii ni hoja ambayo haina faida yoyote ya
kielimu, lakini tunaijadili kwa ajili ya watu wa mitaani tu.))
Ni kweli kwamba
mlango wa Ijtihadi uko wazi, lakini si vyema katika wakati wetu huu mtu kutoa
rai binafsi za kujikweza bila kunukuu hoja za Wanazuoni waliotangulia tena
wanaokubalika. Katika kitabu cha Shaykh Naaswir Bachuu kuna hoja nyingi mno
zilizotajwa kutoka kwenye vitabu vya Wanazuoni wakubwa ambao wameonyesha
misimamo mbali mbali juu ya maudhui haya ya muandamo wa mwezi, lakini Ndugu
Juma hakuijibu hata moja zaidi ya kumponda Al Imam Shawkani. Angalia misimamo
ya Wanazuoni waliotajwa katika kitabu cha ‘Kuandama Kwa Mwezi’ cha Shaykh Naaswir Bachuu uk. 5 - 11, 51 –
56, 59 – 74, 129 - 133.
Pia angalia: ‘Makubaliano Katika Mikutano Ya Wanavyuoni’
yalivyoelezwa ambayo ndugu Juma ameyafumbia macho uk. 134 - 155.
Angalia Ndugu
Juma alivyokuwa akijenga baadhi ya hoja zake binafsi (za umimi) pale aliposema:
((Nasi tunasema kwamba Aya ndio, lakini hoja yake katika Aya
hio ni hoja dhaifu sana.)) [uk. 71]
((Isipokuwa upinzani ambao – mimi kwa upande wangu – nauona
kuwa una muelekeo juu ya tafsiri hii tulioitoa hapa,)) [uk. 62]
Ziko wapi hapa
hoja za Wanavyuoni wanaokubalika zaidi ya kudai: ((Mimi
kwa upande wangu nauona)) au: ((Ninasema bila shaka…))
Kama kawaida yake ndugu yetu Juma
amezusha dhana mpya katika mas-ala ya mwezi ambayo inakwenda kinyume kabisa na
mitazamo ya Wanavyuoni, katika kulihusisha suala hilo na utaratibu wa kufunga
na kufungua Ramadhaan. Amejaribu kuugawa muuandamo wa mwezi katika sehemu mbili
kama alivyodai mwenyewe katika kitabu chake uk. 18 kwa kusema: ((Hali ya kwanza: ni ya muandamo wa kifalaki.)) na ((Hali ya pili: ni ya muandamo wa Kisharia.))
Hatujui dhana hii potofu ameitoa wapi
kwani hakuweza kuthibitisha hata kauli moja ya Mwanachuoni yeyote aliyegawa
muandamo au aliyesema kuna miandamo miwili (ya Kifalaki na ya Kisheria). Hoja
sio kusema unavyoona wewe binafsi, kama mara nyingi alivyojaribu kuonya yeye
mwenyewe ndugu Juma kwamba pasitumike 'hoja za mitaani’ lakini
bahati mbaya yeye mwenyewe anakwenda kinyume na kauli zake hizo.
Ukiangalia katika kitabu cha “Kuandama Kwa Mwezi” uk. 6 - 7 cha Shaykh Naaswir Bachuu, utaona
kwamba yeye hakuporoja, bali amenukuu hoja za Wanavyuoni katika vitabu zaidi ya
kumi. Baadhi yao ni kama vifuatavyo:-
Imam as-Suyuuty katika tafsiri yake iitwayo “Durul-Manthuur”
ameandika hivi “Amepokea Al-Khalib katika vitabu vya nyota kutoka kwa Ibn
‘Abbaas (Radhiya Allaahu ‘Anhu) kwamba kauli ya Mungu isemayo:
“Na mwezi tumeupanga vituo
husafiri (vituoni humo) hadi kurudi ukiwa kama karara la mtende.”
Amesema: “Ni vituo ishirini
na nane ambavyo mwezi hutua humo kwa muda wa mwezi mzima, kumi na nne kati ya
hivyo vipo magharibi na kumi na nne vyenginevyo viko mashariki.”
Baada ya kuvitaja vituo hivyo akaendelea kusema:
“Utakapomaliza (kusafiri
katika) vituo ishirini na nane, hurudi ukiwa kama karara la mtende, kama
ulivyokua mwanzo wa mwezi.” (Durul-Manthuur: J. 5, uk. 495)
Naye Imam Al-Qurtubiy amesema haya yafuatayo:
“Na vituo vilivyotajwa
katika aya hii ni ishirini na nane....” Akavitaja kwa majina kisha akasema:
“Mwezi unapofika katika
kituo cha mwiisho hurudi tena katika kituo cha mwanzo, kwa hivyo humaliza
mzunguko mmoja katika siku ishirini na nane, kisha hufichika, kisha huchomoza
tena katika sura ya uchanga (mwandamo) na kurejea katika safari yake kwenye
vituo vilivyotajwa”. (Tafsirul-Qurtubiy J. 8, uk. 21)
Wala haina maana kwamba Shaykh Naaswir
Bachuu, kwa kuzinukuu tafsiri hizo anaashiria kuwa watu wafunge kwa kutumia huo
alioita ndugu Juma 'Mwezi wa falaki.'
Kwanza ni vyema kuelewa kwamba hakuna
hiyo dhana ya muandamo wa kifalaki lakini kitaaluma kuna:
“mwezi mpya”
usioonekana (the invisible new moon) na “mwezi mchanga”
unaonekana
(the visible young crescent ).
Ndio maana Shaykh Naaswir Bachuu
akaandika katika kitabu chake uk. 87 - 88 kwa kusema hivi:
Tukirejea katika mada yetu ya kuandama kwa mwezi, itakuwa vizuri
hapa kama tutamnukuu mtaalamu wa elimu hii ya annga (Astronomy), Dr. S. K.
Abdali katika makala yake iliyochapishwa katika gazeti la Al-Ittihad la Mombasa
Kenya, litolewalo mwaka mara nne; la kipindi cha Januari – Julai 1979. Amesema:
“... Huu ‘mwezi mpya’
usioonekana (the invisible new moon) ambao majira yake hupatikana katika
makalenda na magazeti, usichanganywe na mwezi mchanga unaoonekana (the visible
young crescent) ambao (kutokana na mwezi huo mchanga) huanza mwezi mpya katika
kalenda ya Kiislam...”.
Hapa tunajifunza jambo moja muhimu kuwa ‘mwezi mpya’ (new moon)
ni tofauti na ‘mwezi mchanga’ (young crescent). Na mwezi mchanga ndio
tunaoutumia Waislam kujua kalenda (tarehe) yetu.
Kwa hivyo hapa Shaykh Naaswir
anasisitiza jambo la kutumika mwezi
unaoonekana katika hukumu ya muandamo.
Pili: Katika kitabu kizima
cha Shaykh Naaswir kimeandikwa kwa msisitizo wa kutosha wa kwamba hukumu ya
kufunga na kufungua ni lazima uonekane mwezi muandamo au kukamilisha siku 30
kama patapatikana udhuru wa kutoonekana mwezi siku ya tarehe 29. Ameyasema hayo
Shaykh Naaswir akiwa anajua fika kwamba huo mwezi (aliouita ndugu Juma wa
Falaki) hauna hukumu ya kufanya mtu afunge au afungue, kwani hauonekani kwa
macho ya kawaida (the invisible new moon). Unajulikana kwa mahesabu ya
Kitaalamu au kwa kuangaliwa kwa vyombo vya Kitaalamu.
{{هُوَ الَّذِي جَعَلَ الشَّمْسَ ضِيَاء
وَالْقَمَرَ نُورًا وَقَدَّرَهُ مَنَازِلَ لِتَعْلَمُواْ عَدَدَ السِّنِينَ
وَالْحِسَابَ}}
{{Yeye (Mwenyezi Mungu) ndiye aliyelifanya jua (kutoa) mwangaza
na mwezi (kuakisi) nuru na akaupangia
(huo mwezi) vituo (vya kusafiria) ili
mpate kujua idadi ya miaka na
hesabu (ya nyakati).}} (10: 5)
Ndugu Juma anaona mwezi na jua ni vitu
sawa sawa na kama kwamba vinafanya kazi moja kwa kuwa vimetajwa kwenye Aya moja
ya Qur-aani. Huku akisisitiza kwamba: ((Sasa utaona kwamba Aya hii imetaja vitu viwili: jua na
mwezi. Na vyote hivi vinazunguka katika falaki (orbits) zake na vinapita
katika manazil (vituo) yale yale na vinapita katika buruji (constellations)
zile zile.))
Pia anaona hukumu ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)
kusema kwamba ((Fungeni kwa
kuuona mwezi)) ni sawa
sawa na kauli ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Aliposema kuwa: {{Swalini kwa kutenguka jua.}}
Sisi tunajibu
hivi:
a) Mwezi na jua ni vitu viwili tofauti
vinavyofanya kazi tofauti katika huo wakati (time). Kila kimoja kinafanya kazi
yake maalumu kwa kuashiria huo wakati maalumu uliopangiwa.
b) Hukumu ya ((Fungeni kwa kuona mwezi na Swalini kwa kutenguka
jua)) ni vitu viwili tofauti kwa sababu zifuatazo:
i.
Hadiyth ya kufundisha nyakati za Swala aliteremka Sayyidna Jibriyl (‘Alayhi swalaatu
was-salaam) kuja kumfundisha Mtume (Swalla
Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) wala haina khitilafu ya mahala kwa
Wanavyuoni karibu wote. Angalia pia Qur-aan
Tukufu (17: 78).
ii. Hukumu ya mgonjwa au mtu aliye
safarini anayo ruhusa ya kutokufunga hata kama ameona mwezi lakini hana ruhusa
ya kutokuswali kabisa hata akiwa mgonjwa
au aliye msafiri.
iii. Mwanamke aliye katika siku
zake ambaye amepewa ruhusa ya kutofunga Swaum ya Ramadhaan na kutokuswali
atakuja kulipa Swaum, lakini hatolipa Swala.
iv. Hutokezea (ijapo kwa Sadfa) watu wa
eneo kubwa kama nchi zote za Kiarabu hufunga Swaum zao kwa siku moja kutokana
na muandamo wa mwezi. Lakini hawaswali Swala zao za faradhi kwa wakati mmoja –
kwa kufuata jua wala hilo halina pingamizi wala mjadala kama ilivyokuwa
hakuna ikhtilafu katika kufuturu wakati wa kuzama jua.
v. Kumbuka kilichozungumzwa ndani ya
kitabu cha Shaykh Naaswir Bachuu pamoja na Wanavyuoni wote wakubwa waliokuja na
hoja ya kufunga pamoja. Wameelezea uwezekano wa kufunga dunia nzima katika siku
moja, sio dakika au saa moja ya siku. Kwa mfano, dunia nzima inaswali Swala ya
Ijumaa siku moja ya Ijumaa. Hakuna Ijumaa mbili duniani bali kuna kupitana na
kutanguliana na hayo yanakuwa hata katika nchi moja.[1][1]
vi. Nyakati za Swala zimetengenezewa
Jadweli (Time table) zinazolingana na mitenguko ya jua lakini suala la kufunga
(Swaum) halikubaliki kufanyiwa jadweli au kalenda za muandamo wa mwezi sharti
mwezi uonekane japo kwa macho ya mtu mmoja.
vii. Si sharti kuliona jua kwa macho
hata kwa mtu mmoja wakati wa kuchomoza au kutua (kuzama) katika hukumu ya
kuanza na kumaliza kufunga. Unahakikisha muda wake tu kama umefika.
viii. Mwezi una Manazil (vipimo maalumu
kwa ajili ya mwezi peke yake sio jua). Angalia
Qur-aan (36: 39).
Mwezi: Umejaaliwa
kuashiria hesabu ya masiku 1, 2 … 28, 29 au/na 30. Kuingia kwa siku
iliyoashiriwa na muandamo wa mwezi ndio unaufanya Ummah wa Kiislamu ufunge au
ufungue Ramadhaan.
Jua: Limejaaliwa kuashiria hesabu ya
sekunde, dakika, saa, siku, wiki, miezi (months),
miaka pamoja na miongo (Seasons) kwa ujumla. Mwenendo wa jua ndio unaofafanua
nyakati za Swala, kula daku na kufuturu. Wala huwezi kutumia mienendo ya mwezi
au Manazil yake katika kuashiria nyakati za Swala, kula daku au kufutari.
Kusema: ((jua likitenguka Makka watu wa Zanzibar wasali?!)) kama alivyosema ndugu Juma katika
kitabu chake uk. 20, hizo ndio hoja za mitaani anazozikataa, kisha akawa
anazitumia mwenyewe.
Sisi tunamjibu hivi: Basi wakiswali Dar es Salaam na Kigoma
waswali? Nizwa wakiswali na Ruwi waswali? Maana wanafunga siku moja.
Katika kuelezea mada hii Shaykh Naaswir
Bachuu kwenye kitabu chake ameelezea kama ifuatavyo:-
Lakini hakuna Aya hata moja katika Qur-aan (bali hata Hadiyth
moja iliyokuja) kujuzisha (kukubalisha) kuwepo kwa tofauti za Matlai ya mwezi.
Kwa hivyo basi hakuna hoja hata moja ya kisheria iliyokuja kukubalisha kuwepo
kwa Matlai ya mwezi ‘Matlial-Qamar’. Neno Matlai mara zote katika Qur-aan limekuja likiambatanishwa pamoja na Jua ‘Matlai-shamsi’. Zifuatazo ni baadhi ya
Aya zilizotaja habari za Matlai:
{{Unaliona jua
linapochomoza....}} (18: 17)
{{Hata ilipofika
matokea ya jua ...}} (18:
90)
{{Na umtukuze Mola
wako pamoja na kumsifu kabla halijatoka jua ...}} (Taha 20: 130)
{{Na Mtukuze Mola
wako kwa kumsifu, kabla ya kutoka jua...}} (50:
39)
Kwa upande wa Ndugu Juma, yeye anayaona
maelezo hayo siyo sahihi, lakini kwa bahati mbaya kama kawaida yake hakuweza
kutoa hata Aya moja kuthibitisha hoja yake. Tahamaki anajaribu kutoa hoja ya
kuwepo “Matlail – Qamar” kwa hoja za mashairi, maneno ya kiarabu pamoja na
kutukumbusha kipande cha Qasida maarufuطلع البدر علينا .
Sasa ukirejea tena katika maelezo ya
Shaykh Naaswir Bachuu utakuta kuwa bado ndugu yetu Juma ana deni kubwa juu ya
uthibitishaji wake katika mas-ala haya. Kwa kuwa Shaykh Naaswir ametulia katika
misingi miwili imara ya Qur-aan na Sunnah. Ingetarajiwa Ndugu Juma naye angetoa
hoja katika misingi hiyo hiyo lakini anaonesha umahiri wake katika kuhifadhi
beti za Qasida wala Shaykh Naaswir hakusema hakuna aliyesema “Mat-lail-Badru” katika Qasida. Kwani
Qasida au mashairi hata ndugu Juma anaweza kusema atakavyo wala hakatazwi.
Alichosema Shaykh Naaswir ni kwamba hapakutajwa lafdhi ya “Matlail–Qamar” ndani ya Qur-aan lakini pametajwa: “Matlai–Shams."[2][2]
Kwa upande mwengine, Ndugu yetu Juma
amejaribu kutaka kuonyesha kwamba yapo Matlai ya mwezi kwa kuinukuu Aya ya
Qur-an isemayo:
{{Na alipouona mwezi
unachomoza alisema: "Huu ndio Mola wangu."}} (6: 77)
Hapa ingefaa aelezwe Ndugu Juma kama
anakusudia kwamba ni dalili katika Aya hiyo kuwepo kwa “Matlail – Qamar” basi kwa mujibu wa mtiririko wa Aya
zilizotangulia kabla ya Aya hiyo, hazina uhusiano wowote katika masuala hayo.
Wala hajulikani mfasiri hata mmoja aliyeifasiri hivyo Aya hiyo hata Ndugu Juma
akapata kigezo hicho. Ama kama anakusudia kutujuulisha mtindo wa lugha ya
Kiarabu kuhusu neno بَزَغَ
atakuwa amekwenda kinyume
na kanuni, kwani tujuavyo sisi kitabu chake alichokiandika ni cha mas-ala ya
mwezi wala hakihusiani na lugha.
Ufafanuzi wa Aya ya Qur-aan:
{{Wanakuuliza juu ya
miezi. Sema: “Hiyo ni vipimo vya nyakati kwa ajili (ya mambo) ya watu (mengine)
na ya Hijja (zao).}} (2: 189)
Hapa Ndugu yetu Juma katika kosoa kosoa
zake anaona kama hivi ifuatavyo kwa mujibu anavyosema katika kitabu chake uk 56
- 57:
((Kwa hivyo ni wazi kwamba kinachozungumziwa hapa ni miandamo
yenyewe ya mwezi: wala si hali tafauti za mwezi, kwani vipimo vya nyakati na
hija ni miandamo yenyewe: si hali tafauti za mwezi: hali tafauti za mwezi za
kuwa mkubwa na mdogo haziwezi kuwa vipimo vya nyakati na hija.))
Sisi tunajibu
kama ifuatavyo:
Neno 'yas-aluunaka' ambalo tafsiri yake ni “Wanakuuliza” tunaweza kuligawa sehemu tatu zifuatazo:-
1. Wenye kuuliza (waulizaji).
2. Mwenye kuulizwa (muulizwaji).
3. Chenye kuuliziwa (kinachouliziwa).
1. Wenye kuuliza (Waulizaji): Kwa hapa
bila shaka ima itakuwa ni Waislamu waliokuwa katika hadhara ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)
– yaani Masahaba au kama sio Waislamu watakuwa ni makafiri. Lakini kwa mujibu
wa Tafsiri nyingi za Wanavyuoni wengi wenye kutegemewa katika fani hii ya
tafsiri na baadhi ya vitabu vyengine – vimeeleza kwamba Masahaba ndio
waliomuuliza Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi
wa aalihi wa sallam).
2. Mwenye kuulizwa hapa bila shaka
yoyote atakuwa ni mwenyewe Mtume (Swalla
Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Kwani yeye ndiye aliyeteremshiwa
hiyo Qur-aan Tukufu. Na Aya kama hizi zipo nyingi katika Qur-aani Tukufu. Angalia: (2: 215, 217, 219, 220, 222).
3. Chenye kuuliziwa kwa hapa ni zile
hali za mwezi kama yalivyobainishwa hayo na Wanavyuoni katika tafsiri zenye
kutegemewa katika fani hii ya tafsiri. Ni vyema kuelewa kwamba Qur-aan ina
utaratibu wake maalumu wa kuitafsiri, hususan inapokuwa katika mjadala wa
kielimu au katika kutoa hoja juu ya hukumu ya jambo fulani, lazima yatolewe
madondoo ya tafsiri za Wanavyuoni wenye kutegemewa. Wala sio busara mtu yeyote
kutoa fikra zake binafsi hasa kama mtu huyo hajafikia katika daraja ya “Ijtihaad.”
Kwa mantiki hiyo, ndio maana ukaona
katika kitabu cha “Kuandama Kwa Mwezi”
cha Shaykh Naaswir Bachuu kila anapotoa hoja ya jambo fulani huwa anatoa
madondoo maalumu hata pale anapotaja tafsiri ya baadhi ya Aya za Qur-aan.
Kitu cha msingi hapa ni kujua kwamba:
Je suala liliulizwa au halikuulizwa? Hata kama waliouliza ni Masahaba au
Mayahudi. Bila shaka Aliyesema kwamba paliulizwa suala ni Mwenyewe Mwenyezi
Mungu Mtukufu Aliposema: {{يَسْأَلُونَكَ}}
{{Wanakuuliza}}
Masahaba walitaka kujua kwa kina juu ya
hali za miezi, mbona mara unakuwa mkubwa, mara mdogo, mara unapotea hauonekani
kabisa, mara hali hii mara hali ile? Bila shaka jawabu ingetarajiwa iwe yenye
kufafanua hali halisi ya matokeo hayo lakini jawabu ilikuja kutaja “hikma” ya kupatikana hali hizo nazo
ni kujua nyakati za Ibada za watu. Yaani kuweza kujua wakati wa kufunga
(Swaum), Hijja, Zakka na shughuli nyengine za kimaisha. Ikumbukwe kwamba
utaratibu kama huu wa kuulizwa suala na jawabu ikataja hekima ya jambo lenyewe
badala ya kufafanuliwa hilo jambo lenyewe ni jambo maarufu katika fani ya "Balagha" ijulikanayo kwa
jina la “Uslubul-Hakiim” (أسلوب الحكيم) . Angalia kwa
makini baadhi ya madondoo kutoka katika kitabu Al-Balaghal – Waadhihah (البلاغة الواضحة) kama ifuatayo:
إن
أصحاب الرسول (صلى الله عليه وسلم) سألوه عن الأهلة لم تبد صغيرة ثم تزداد يتكامل نورها ثم
تتضاءل حتى لا تُرَى وهذه مسئلة من مسائل علم الفلق يحتاج في فهمها إلى دراسة
دقيقة طويلة فصر فهم القرآن الكريم عن هذا بيان أن الأهلة وسائل للتوقيت في المعملات
والعبادات ...
Masahaba
walimuuliza Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)
kuhusu (hali za) miezi, vipi mwezi huonekana mdogo kisha unakamilika
nuru yake (kwa kuwa mkubwa) kisha
unakuwa mdogo katika hali ya kutoonekana. Mas-ala haya ni miongoni mwa mas-ala
yanayohusu elimu ya nyota yanayohitajia uchambuzi mrefu na wa kina, ndio maana
Qur-aan Tukufu ikawacha uchambuzi huo, na badala yake ikabainisha kuwa (hali hizi) za miezi ni njia za kujua nyakati
za kazi na ibada mbali mbali”.
Kwa hiyo tukichunguza Aya hiyo {{يَسْأَلُونَكَ}}
{{Wanakuuliza}} tutaona kuwa, Aya yenyewe
inatuthibitishia wazi kwamba Mtume
(Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliulizwa, na waliomuuliza
walikuwa ni Masahaba na
alichoulizwa ni hali za miezi kama tulivyokwishaelezea.
Kwa vyovyote vile kushikamana na
Qur-aan ni jambo bora zaidi (aula) hususan inapotokezea khitilafu juu ya jambo
au hukumu fulani. Shaykh Saalimiy
katika kitabu chake الجامع
الصجيح
anasisitiza
zaidi katika jambo la kushikamana na Qur-aan hasa pale zinapopatikana ikhtilafu
juu ya jambo fulani katika Umma:
... فمن تمسك
بظاهر كتاب الله عند اختلاف الأمة في حكم او خبر فقد تمسك بالعروة الوثقى التي لا
انفصام لها...(صفحة:
29)
Mwenye
kushikamana na dhahir (ya maneno) ya
kitabu cha Mwenyezi Mungu wakati
ambapo Umma (wa Kiislam) umetafautiana
juu ya hukumu ya jambo (fulani) au habari (fulani) bila shaka (mtu huyo)
atakuwa ameshika kishiko madhubuti
kisichovunjika.
Ama kuitolea hoja Aya hiyo {{يَسْأَلُونَكَ}} {{Wanakuuliza}} kuwa ni dalili ya kuthibitisha kuwepo
kwa muandamo wa kisheria au kuwa ni dalili ya kwamba kila nchi ifunge kwa
muandamo wake au kuthibitisha kuwepo kwa 'miandamo mingi’ huko ni kushindwa kuifahamu makusudio ya Aya. Vile
vile ni kwenda kinyume na maelezo ya Wanazuoni katika vitabu vyao vya tafsiri,
kwani Qur-aan ni lazima itafsiriwe kwa kuzingatia misingi yake maalum na kanuni
zake zinazokubalika katika hiyo fani ya tafsiri.
Shaykh Ahmad Al-Khaliil (Mufti Mkuu wa
Oman) alipokuwa akielezea rai za Wanavyuoni juu ya aina za tafsiri ya Qur-aan-
ameeleza haya yafuatayo:
... وبهذا يتضح رجحان القول بجواز التفسير بالرأي لمن جمع الشرائط
التي يلزم توفرها في المفسر كما أسلفنا ولم يصدر رأيه عن هوى وإنما كان ناتجا عن
النظر والتأمل في مصادر التفسير مع مراعاة الظرف الذي نزلت فيه آية المفسرة ...
Kauli yenye
nguvu ni kuwa inafaa kutafsiri Qur-aan kwa kutumia rai (lakini) kwa yule
aliyekusanya sharti ambazo lazima Mfasiri awe nazo. Sharti zenyewe
tumeshazieleza katika darsa iliyopita. Wala Mfasiri huyo asitie (katika tafsiri
yake hiyo) matamanio ya nafsi yake. Bali rai yake hiyo iwe ni faida itokanayo
na madondoo ya tafsiri za Wanavyuoni zenye kutegemewa katika fani hii ya
tafsiri. (Sio kubuni tafsiri isiyoeleweka wala isiyokubalika katika misingi ya
Dini) vile vile azingatie vizuri tokeo lililosababisha kuteremshwa Aya hiyo
anayoifasiri, (lazima) aangalie “Sababun - Nuzuul”
Katika maudhui hii, ndugu yetu Juma
amechanganyikiwa kwa kuwa tabia yake anaona ni bora kupinga tu vyovyote iwavyo! Yeye anaona katika Aya
hiyo neno ‘Ahilla’
(أهلة) halizungumzii hali tofauti za mwezi
bali linazungumzia miandamo yenyewe – yaani kama kwamba kusema: Omani itazame mwezi wake, Dubai itazame mwezi
wake, Yemen itazame mwezi wake, Saudia itazame mwezi wake na kila nchi itazame
mwezi wake. Angalia katika kitabu chake uk. 56 – 57.
Anasema hivi:
((Kwa hivyo ni wazi kwamba
kinachozungumziwa hapa ni miandamo yenyewe ya mwezi: wala si hali tafauti za
mwezi,))
Kisha akasema: ((lafdhi Ahilla (أَهِلَّةٌ) (miezi miandamo), ni dalili ya
kuwepo kwa miandamo mingi wakati mmoja.)) Angalia uk. 56 ndani ya kitabu chake.
Jambo jengine; ndugu Juma anaona kazi
za mwezi na jua ni sawa sawa na kwamba kwa kuwa mwezi una ‘Manazil’ basi hivyo hivyo na jua lina
‘Manazil’. Pia anaona kwamba kwa kuwa jua lina ‘Matlai’ basi na mwezi vile vile una Matlai. Angalia katika kitabu chake hicho (uk. 153 - 157).
Jambo jengine ni kwamba ndugu Juma
anaona katika tafsiri ya Aya hiyo{{يَسْأَلُونَكَ}}
{{Wanakuuliza}} imetumika Hadiyth ‘maudhui’ yaani ya
uongo katika hilo linalobainishwa kwenye sababu ya kushuka Aya hiyo (سباب النزول)[3][3] na kwamba waliouliza
hawakuwa ni Maswahaba bali ni Mayahudi.
Sisi tunamuelimisha hivi ndugu yetu
huyu kwa kumwambia kwamba kwa upande wetu tunazithamini sana tafsiri za watu
wenye elimu ambao hapana shaka, wao hiyo Hadiyth wameshaiona na wameitumia
baada ya kuipima kwa viwango vya kielimu zao. Halafu hapa katika Aya {{يَسْأَلُونَكَ عَنِ
الأهِلَّةِ}}
hapana mjadala wala
utatanishi wowote unaohitaji maelezo makubwa ya sababu ya kushuka kwa Aya hiyo,
kwani dhahiri ya Aya iko wazi mno kwamba Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Mwenyewe
Anathibitisha kwamba: {{Ewe
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): (watu) wanakuuliza kuhusu
(hali za) mwezi….}}
Hebu
tumuangalie mwanachuoni Al- Imam
Abil-Hawaary Muhammad Binil - Hawaary Al-Omaniy Al-Ibadhy anayetajwa kama ni
mwanachuoni wa karne ya tatu
Hijriyah aliyeandika kitabu chake
alichokiita:
Katika kuitafsiri Aya hiyo ya Qur-aani:
{{يَسْأَلُونَكَ عَنِ الأهِلَّةِ}}
Aliandika ifuatavyo kwenye uk. 99:
نزلت
فى معاذبن جبل، وثعلبة بن عنمة، وهما الأنصار، سألا النبي ( صلى الله عليه وسلم)
عن الأهلة، فقال معاذ: يانبي الله مابال الهلال يبدو مثل الخيط ثم يزيد ويمتلىء
حتى يستوى تم لايزال ينقص حتى يعود كم بدأ؟
فنزلت : {{يَسْأَلُونَكَ عَنِ الأهِلَّةِ قُلْ هِيَ
مَوَاقِيتُ لِلنَّاسِ}} يعن: فى حل دينهم، وعدة نسا ئهم،
وصومهم، واشروط التي بينهم إلى أجل مسمى، ثم قال: والحج
يعنى : وقت حجهم، فالأهلة مواقيت فى ذلك.
Imeteremshwa
Aya hii kwa Muadh bin Jabal na
Tha’alabah bin Anama ambao ni katika Maansar. Walimuuliza Mtume (Swalla
Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuhusu miezi miandamo. Akasema Muadh: “Ewe
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) wa Mwenyezi Mungu una nini huu mwezi mbona
unakuwa (mwembamba) kama
uzi kisha unazidi (wembamba huo) tena unajaa (unakuwa
mnene) mpaka unakuwa sawa sawa baada ya
hapo unapungua unakuwa kama ulivyoanza?”
(Baada ya suala hilo, Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Akamteremshia Mtume wake aya hiyo: {{Wanakuuliza kuhusu miezi
miandamo. Sema hiyo ni
vielelezo vya nyakati kwa ajili
(ya mambo) ya watu}} kama kutaka (kujua) nyakati za eda
zao, swaum zao, Mikataba yao
(na mambo mengine ) na
Hijja - yaani kujua
nyakati za Hija
zao. Kwa hivyo miezi
ni vielelezo vya nyakati
kwa mambo hayo”.
Sasa tuangalie Wanavyuoni wetu ambao ni
wazaliwa wa Zanzibar wenye kutegemewa ambao wameandika tafsiri zao za Qur-aan
tukufu:
1. Shaykh Abdalla Saleh Al-Farsy aliyeandika tafsiri ya Qur-aan Takatifu alikuwa na haya
yafuatayo katika kuifasiri (yas-aluunaka), {{يَسْأَلُونَكَ عَنِ الأهِلَّةِ}} alitoa maelezo
yafuatayo:
“Maswahaba
waliuliza nini sababu ya kukhitalifu sura ya mwezi – mara mdogo, mara mkubwa.
Wakajibiwa kwa wepesi tu kuwa ‘Ipate kuwa kipimo ili wapate watu kujua kuwa
sasa wako katika mwanzo wa mwezi au kati yake au mwisho wake.’
2.
Shaykh Said Muusa Muhammad
Al-Kindy katika Tafsiri yake ya Qur-aan aliyoiita: منابع الهدى “Asili ya uongofu”
Katika kuifasiri Aya hiyo; {{يَسْأَلُونَكَ
عَنِ الأهِلَّةِ}} Alikuwa na maelezo yafuatayo:-
“Kaulizwa
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuhusu namna ya mwezi kwamba
ukiandama mwanzo wa mwezi unakuwa mdogo kisha baada ya siku unakuwa nusu, kisha
mkubwa, kisha unapunguka urudi kuwa nusu, na mdogo, na kuwa kama uzi; Jee nini
hekima yake?”
Waulizaji
waliouliza ni Muadh bin Jabal na Thaalabah bin Ghanam. Wakazidi kumuuliza Mtume
(Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwamba, kwa nini unabadilika hivyo
mwezi? Na kwa nini jua halibadiliki kama mwezi? Ndio ikateremka Aya hii: “Wanakuuliza
juu miezi, sema: “Ewe Nabii Muhammad uwaambie kwamba: ‘Hiyo’ kuwa mwezi mara
mdogo mara mkubwa: “Ni vipimo vya nyakati kwa ajili ya mambo ya “watu.”
Yanayohusu mambo yao ya dunia na pia ya Dini. Kwa ajili wajue: madeni yao
wanayodaiana, na kodi zao wanazolipana katika mambo mbali mbali, na hesabu zao
na za kujua siku na mwezi na mwaka na nyakati.”
“Na wajue eda
ya hedhi za wake zao, na wajue siku za Swaum yao, na wajue siku za ‘Hijja’ zao
na… na… Ameulizwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) sababu ya
kubadilika mwezi mara kwa mara. Ndio akawajibu kwamba ingekua mwezi utabaki
namna moja tu kama jua, haitajulikana hisabu ya mwezi.”
“Na muradi wa
mwezi yaani ni “Takwimu” au kalenda ya kujua hisabu ya wakati za siku na
nyakati za wiki na nyakati za miezi na nyakati za miaka, na mambo mengi ya watu
ya maisha yao ya duniani kupeana kama: kodi za nyumba, au mashamba au
mfanyakazi au… au... Na mengi mengineyo.”
“Na kama
mambo ya Dini ambayo tumekwisha kuyataja. Yote hayo ya dunia na ya Dini
yamehusika na hesabu ya mwezi kubadilika kwake mara kuwa mdogo na mara kuwa
mkubwa.”
3. Al -Marhuum Shaykh Ali Muhsin Al-Barwani katika Tafsiri yake ya
Qur-aan Tukufu ijulikanayo kwa jina la "Tarjama Ya Al-Muntakhab” ( (ترجمة المنتخبkatika kuifafanua Aya hiyo {{يَسْأَلُونَكَ عَنِ
الأهِلَّةِ}} ameeleza yafuatayo:-
“Na watu
wanakuuliza habari za mwezi, unaanza mwezi mchanga kama uzi, kisha unakuwa
mpaka unatimia kamili. Tena unapungua mpaka unakuwa kama ulivyoanza. Haukai
katika hali moja kama jua. Nini maana ya kugeuka huku hata inakuwa kila siku 29
au 30 unakuja mwezi mpya?”
“Waambie huku
kutokea hivi kuandama mwezi na kugeuka yapo ndani yake maslaha ya Dini na dunia
pia. Hizi ni alama za kuonyesha nyakati za mambo ya maisha yenu. Zinaonyesha nyakati
za Hijja, ambayo ni moja katika nguzo za Dini yenu. Na lau kuwa mwezi
ungelibaki namna moja tu kama jua msingelitambua nyakati za maisha yenu na
Hijja zenu. Wala huko kutojua hekima ya kugeuka mwezi kusikupelekeeni kutilia
shaka hekima ya Muumba.”
“Uislamu unahisabu mwezi unapoandama na
kugeuka Sura kwa watu kupimia nyakati za ibada, na pia kwa mambo yao ya
kidunia, kwa sababu hayo ni mambo ya kuonekana, na kwa hivyo tarehe inajulikana
kwa sura ya mwezi. Mwezi kwa hakika ni kama kioo kinachoonyesha mwangaza wa jua
huku duniani. Mwezi ukiwa kati baina ya jua na dunia hauonekani, na baadae
mwezi mchanga unaandama na wakaazi wa dunia wanajua kuwa mwezi mpya umeanza.
Ukifika mwezi katika upande unaokabiliana baina ya jua na dunia ndio unapokuwa
wakati wa mbaamwezi, mwezi mpevu. Halafu unaendelea kupungua kama ulivyokuwa
kwanza ukizidi kukua. Kwa hivyo tarehe inaanza tangu pale ulipokuwa mwezi
mchanga. Pale unapoonekana mwezi mchanga kama uzi ndio mwezi umeandama,
huonekana upande wa magharibi, hata kwa dakika chache baada ya kuchwa jua nao
hupotea. Hivyo hivyo siku baada ya siku huhisabiwa mpaka zipite siku 29 au 30.”
4. Shaykh Al-Amin bin 'Ally Al-Mazrui: “Katika tafsiri yake uk. 67 ya
Qur-aan Tukufu juu ya Aya isemayo: {{يَسْأَلُونَكَ
عَنِ الأهِلَّةِ}}
Alikuwa
na haya ya kusema:
{{Wanakuuliza
wewe habari ya miezi!}}
Kisha akaendelea kufafanua:
“Baadhi ya
Masahaba walimuuliza Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) habari
ya miezi – kwa nini huanzia mwembamba, ukaongezeka kidogo kidogo hata
ukakamilika kengee yake, kisha ukaanza kupungua mpaka ukapotea kabisa kabisa?
Kama suala hili lingejibiwa kisayansi ingewafungulia watu mlango wa kuuliza
mengi ambayo hayahusiani na kazi ya Mitume. Kwani Mitume kazi yao ni kuwaongoza
watu na kuwafunza yale ambayo hawawezi kuyajua ila kwa Wahyi. Ama mambo
yawezayo kujulikana kwa ilimu, kama Falaki (astronomy), utabibu na kadhalika,
si mambo ya kufaa kuulizwa Mitume, wala hayahusiani na kazi yao kamwe. Kwa
sababu hii Allaah, badili ya kujibu suala lao, Ameeleza faida ya mwezi
iliyofungamana na baadhi ya mambo ya manufaa, Shari'ah na mambo ya ibada. Hili
lilitosha kuwafunza Masahaba lifaalo kumuuliza Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa
aalihi wa sallam) na kuwakomesha wasiulize suala zisizofaa. Wakaambiwa kuwa
mwezi huwajulisha watu nyakati za muamala wao na maslaha yao ya kilimwengu na
nyakati za ibada zao kama Hijja, Swaum na kadhalika.”
Kama kawaida yake, Ndugu Juma ametoa
dhana yake binafsi kwamba si lazima mwezi ukithibiti kuandama sehemu moja uwe
umethibiti sehemu nyengine, na kwamba kwa mawazo yake ni lazima tusalim amri
kwa hilo, yaani yeye anataka kila nchi ifunge kwa muandamo wake. Kwani aonavyo
yeye katika jambo hilo kuna andiko.
Hilo andiko je alinukuu?
Alilolichukua yeye ni katika kisa cha Ibnu ''Abbas na Kuraib.[4][4]
Sisi tunamfahamisha mambo yafuatayo
kwamba:
1.
Hakuna andiko Takatifu zaidi ya Qur-aan Tukufu, lakini bado Wanavyuoni
wakubwa wametofautiana katika baadhi ya tafsiri za Aya nyingi pamoja na Hadiyth
sahihi.
2.
Maswahaba pia walitofautiana katika kufahamu tafsiri za Aya za Qur-aan
na Hadiyth. (Angalia tafsiri ya Shaykh
Ahmed Al-Khaliil J. 1)
3. Kama Wanavyuoni waliopita wangekuwa
na msimamo kama wa ndugu Juma kwamba katika kisa cha Kuraib kuna andiko, basi kungekuwa hakuna mjadala.
Kama ilivyo katika nyakati za Swala hazina tofauti kubwa, kila eneo linaswali
kwa mitenguko yake ya jua.
4.
Kama kisa chenyewe ni andiko,
mbona ndugu Juma anatoa mawazo kwamba suala la umbali gani ndio linatakiwa
Ijtihadi? Sasa tunakujibu kwamba hapa ndipo penye mjadala wote wa mwezi, maana
mpaka leo hii hapakupatikana makubaliano ya kweli ya kisheria, isipokuwa kila
eneo linafuata matakwa yake ya kisiasa na kifalme za nchi zao.
Hapa chini tutaonyesha namna Wanavyuoni
wenye kutegemewa ambao hawakukichukua kisa cha Kuraib kama ni hoja ya kwamba
kila nchi au kila eneo lifunge au lifungue kwa muandamo wake. Wanavyuoni
wamekhitalifiana kwa sababu kisa chenyewe cha Ibnu ''Abbas na Kuraib kina
utata, hakikueleweka kwa mtazamo mmoja. Chambilecho alivyosema Shaykh Ahmed
Al-Khaliil kwamba: “Hakuna madhehebu iliyosalimika.”
Habari hizi zimepatikana katika khutba
yake iliyorikodiwa katika kanda (audio cassette) alipozungumza Shaykh Ahmed Al-Khaliil
kwenye msikiti Istiqama Zanzibar iliyotafsiriwa na Shaykh Munir Sulayman
'Aziiz.
1. Rawdhatun-Nadiyyah:
وأما
استدلال من استدل بحديث كريب عند مسلم وغيره فغير صحيح لأنه لم يصرح ابن عباس بأن
النبي (صلى الله عليه وسلم) أمرهم بأن لا يعمل برؤية غيرهم من أهل الأقطار.
"Ama hoja ya aliyetegemea Hadiyth ya Kuraib iliyopokelewa na Muslim na
wengineo, (hoja hiyo) sio sahihi kwa sababu Ibnu 'Abbas hakueleza kama Mtume
(Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amewakataza kufuata mwandamo wa
nchi nyengine.”
2. Aunul-Maabud,
Sherhe Sunanu Abu-Daud:
قوله
"هكذا أمرنا" يحتمل أن المراد
به أنه أمرنا أن نعتمد على رؤية أهل بلدنا ولا نعتمد عن وؤية غيرهم إلا
المعنى الثاني تميل ترجمة المصنف إذ الإحتمال يفسد الإستدلال.
Yaani: aliposema: “hivi ndivyo alivyotuamrisha.”
kama anakusudia: Ametuamrisha kukubali ushahidi wa watu wawili sio mtu mmoja
katika kufungua (siku ya 'Iydl-fitri). Aidha inawezekana pia kwamba anakusudia
ametuamrisha tufungue kwa kufuata mwandamo wa nchi tuliyopo siyo nchi nyengine.
Abu Daudi ameitegemea hii maana
ya pili lakini Ibnul-Qayyim
anaona kuwa maneno haya: هكذا أمرنا "hivi ndivyo
alivyotuamrisha"
yana utata – yaani yanaweza kukusudiwa kwa maana ya kwanza au ya pili. Kwa
maana hiyo, maneno hayo hayawezi kuwa hoja kwani hoja haitakiwi kuwa na utata
(yaani maana zaidi ya moja). Wanavyuoni wa Usulil - Fiqhi wanasema hivi:
"الدليل
إذا طرقه الإحتمال سقط به الإستدلال"
“Dalili ikiwa na maana (nyingi) zaidi ya moja,
ushahidi wake huporomoka.”
3. Imamu
Suyuti:
Aliyesherehesha
"Sunanun-Nisai" ametumia maneno yale yale ya Ibnul–Qayyim:
Kwa hivyo Imamu Suyuti naye amekuja na
msimamo ule ule wa Ibnul-Qayyim wa kwamba maneno ya Ibnu ''Abbas (Radhiya
Allaahu ‘Anhu): “Hivi
ndivyo alivyotuamrisha ….” Yana utata, kwa hivyo si hoja ya kutegemewa
kisheria.
Baada ya kupimwa maneno ya Ibnu-'Abbas
(Radhiya Allaahu ‘Anhu) katika mezani ya Usul-Fiqhi na kuonekana kwamba hayaeleweki kwa maana moja, sasa
tuyatie kwenye mezani ya Hadiyth ambapo tutaona maneno ya Ibnu-'Abbas (Radhiya
Allaahu ‘Anhu) aliyoyasema: “Hivi ndivyo
alivyotuamrisha Mjumbe wa Mwenyezi
Mungu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam),” yanapewa ‘Hukmu Arafi’ (حكم الرافع) yaani yanapewa nafasi sawa na Hadiyth
ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa
aalihi wa sallam) katika hukmu. Hapa mezani ya Mustwalahul-Hadiyth inatoa jawabu ifuatayo:
i. Katika kitabu خبر الواحد وحجيته cha الشنقطى kimeandika yafuatayo:
“Itakapogongana ‘Marfuu-hukman’ na ‘Marfuu-Saraaha’
hutangulizwa (katika hukmu) ‘Marfuu-Saraaha.”
ii. Pia katika tafsiri ya Qur-aan ifuatayo:
imeandikwa ifuatavyo:
“Marfuu–Saraaha ni bora zaidi (aula) kutangulizwa
(katika hukmu) kuliko Marfuu-hukman.”
Kwa ufafanuzi zaidi wa maelezo hayo ni
kwamba Hadiyth za Mtume (Swalla Allaahu
‘alayhi wa aalihi wa sallam) zilizotajwa hukmu ya kufunga na kufungua
zimetaja hukmu hiyo kwa (saraaha) uwazi: “Fungeni kwa kuona mwezi.” Hilo ni agizo la ujumla – yaani kwa
watu wote. Lakini tukiyachunguza maneno ya Ibnu ''Abbas (Radhiya Allaahu ‘Anhu)
tutayagundua ingawaje kayategemeza kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) bado hayako wazi –
yana utatanishi.
Baada ya kuyaona maneno ya Ibnu 'Abbas
(Radhiya Allaahu ‘Anhu) kwamba hayako wazi na kama mezani ya fani ya Hadiyth
inavyojionesha – ni vyema kuwauliza Wanavyuoni ambao ni wapokezi wa Hadiyth: Je
Ibnu 'Abbas (Radhiya Allaahu ‘Anhu) hajawahi kupokea Hadiyth inayotaja kadhia
hii ya miandamo ya mwezi nyengine isiyokuwa ile ya Kurayb? Wanavyuoni watajibu
kuwa ipo riwaya iliyopokelewa na Ibnu 'Abbas (Radhiya Allaahu ‘Anhu) mwenyewe
juu ya suala hili la muandamo wa mwezi.
Ifuatayo ndiyo riwaya yenyewe:
وعن ابن عباس رضي الله عنهما أن أعرابيا جاء إلى النبي (صلى الله عليه
وسلم) فقال إني رأيت الهلال، فقال: أتشهد أن لا إله إلا الله وأن محمدًا رسول
الله؟ قال: "نعم" قال: "فأذن في الناس يا بلال أن يصوموا
غدًا" (رواه مسلم)
((Kutoka kwa Ibnu 'Abbas (Radhiya Allaahu ‘Anhu)
kwamba bedui mmoja alikuja kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa
sallam) akasema: “Nimeuona mwezi.” Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa
sallam) akamwambia: “Unashuhudia kwamba hakuna anayepaswa kuabudiwa isipokuwa
Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala)?” akasema: “Ndio.” Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)
akasema: “Ewe Bilal watangazie watu kesho wafunge.”)) (Muslim).
Kama tulivyoona kwamba Ibnu 'Abbas
(Radhiya Allaahu ‘Anhu) ndiye aliyeipokea Hadiyth hiyo ya bedui na alivyokuja
bedui huyo kumpa habari Bwana Mtume (Swalla
Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), naye Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akazikubali habari
hizi za kuambiwa. Jambo alilofanya ni kuzithibitisha tu kwamba yule aliyezileta
habari zile ni Muislam. Wala hakumuuliza kwamba bedui yule anatokea wapi, wala
pahala alipouona mwezi, wala kutokea masafa gani. Inawezekana kuwa alitokea
maeneo ya karibu au vile vile inawezekana alitokea maeneo ya mbali na inaelekea
kabisa kuwa Mtume (Swalla Allaahu
‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakuwa akimjua bedui yule ndio maana
akamtamkisha shahada ili kuhakikisha kama alikuwa ni Muislamu.
Ilivyokuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)
hakumuuliza bedui jambo lolote katika hayo tuliyoyataja, Shari'ah ya ‘Usulul-Fiqhi’ Wanavyuoni wanasema yafuatayo:
“Kuacha kuuliza pahala ambapo ilikuwa inayumkini
kuuliza basi inamaanisha kuwa hii ni hukmu ya jumla ('aam) isiyokuwa na
mipaka.”
Habari hizi zimenukuliwa katika Tafsiri
ya Qur-aan Tukufu:
i. أضواء البيان – الجزء الخامس
ii. الفقه الاسلامي وأدلته
Na ndio njia inayoelekea kuwa sahihi
kuliko kufuata jambo lenye utatanishi (ihtimaalati). Bora kushikamana na
mafunzo sahihi ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ambayo
yako wazi na yaliyo mepesi.
“Jambo la asli halihitaji (kuletewa) dalili, (lakini
dalili inahitajika katika jambo lisilo la asili).”
Kwa hivyo ilivyokuwa Ibnu 'Abbas
(Radhiya Allaahu ‘Anhu) alipokea (Hadiyth) maneno ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)
ya kwamba alimkubali bedui bila
ya kumuuliza anatokea wapi; halafu Ibnu 'Abbas (Radhiya Allaahu ‘Anhu) huyu
huyu hakuukubali mwezi ulionekana na Kuraib huko Sham, hapa inaonyesha wazi
kwamba kitendo cha Ibnu 'Abbas (Radhiya Allaahu ‘Anhu) kimetafautiana na yale
aliyoyapokea kwa Mtume (Swalla Allaahu
‘alayhi wa aalihi wa sallam).
Je nini hukmu ya kadhia hii? Ni vyema
tusogeze karibu mezani yetu ya Mustalahul-Hadiyth
ili tuone kipimo sahihi na chenye uzito mkubwa kipo upande gani:
إذا
خالف الروي مرويه هل يقدم مذهب الراوي أو يقدم الخبر، ذهب الجمهور من أهل الأصول
والفقهاء ومنهم السافعي وأبو الحسن إلى أنه يجب العمل على ظاهر الخبر دون تأويل
الراوي. والعبرة بما روى لا بما رأى
1- الإحكام في أصول الأحكام _ الجزء الثاني،
3-
خبر الواحد وحجبته،
4-
الفتاوى الصلاة – الزكاة – الصوم – الحج.
“Atakapokwenda kinyume mpokezi (wa Hadiyth) kwa kile
alichokipokea; Je hutangulizwa (katika hukmu ya jambo hilo) njia (madhehebu) ya
mpokeaji (namna alivyofanya yeye) au itatangulizwa habari (yaani) kile
alichokipokea? Jamhuri ya Wanavyuoni wa Usulul–Fiqhi na Wanavyuoni wa Fiqhi -
wakiwemo Imamu Shafi na Abul-Hassan wameonelea kwamba kilicho wajibu kutendewa
kazi ni ile habari aliyoipokea mpokeaji sio ile tafsiri (ya tendo) la mpokezi.
Kwani chenye kuzingatiwa juu ya kadhia hii ni kile alichokipokea (Swahaba
kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) sio kile
anachokiona yeye katika rai yake au alichokitenda.”
Habari hizi
zinapatikana katika vitabu vifuatavyo:
1. Al –
Ihkamu Fii Usulil-Ahkam J. 2
2. Irshadul-Fuhul.
3.
Khabaril–Waahid Wahujjiyatuh.
4. Al-Fatawa-Swala,
Zakka, Swaum wa Hajj – kitabu cha 1 uk 268.
Baada ya
kuona uzito uliopo katika mezani ya Mustalahul-Hadiyth. Ni vyema
tuangalie tena mfano mwengine ufuatao:-
Kuhusu Sahaba Abu Hurayra (Radhiya
Allaahu ‘Anhu) alivyopokea hukmu ya chombo kilichorambwa na mbwa. Sahaba huyu
ndiye aliyepokea Hadiyth kutoka kwa Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwamba chombo
kilichorambwa na mbwa kisafishwe kwa kuoshwa kwa maji mara saba; moja kati ya hizo isafishwe kwa mchanga.
Katika mapokezi mengine Abu Hurayra
(Radhiya Allaahu ‘Anhu) huyu huyu ameshuhudiwa kutoka kwa Sa'iyd bin Musayab
kwamba yeye Abu Hurayra alikiosha chombo mara tatu katika sehemu ambayo ilitiwa mdomo na mbwa.
Imeonekana kitendo hicho cha Abu
Hurayra (Radhiya Allaahu ‘Anhu) kimetofautiana na maneno aliyoyapokea kutoka
kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa
aalihi wa sallam). Kwa jambo hilo, Wanavyuoni wote wa Kishafi wamesema
chombo kilichorambwa na mbwa kioshwe mara saba na wala sio mara tatu. Kwa
mantiki hiyo wameona washike yale maneno yake Abu Hurayra aliyoyapokea kutoka
kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa
aalihi wa sallam) na wameacha kushika kile kitendo chake. Kwa hivyo cha
kuzingatia ni yale maneno yaliyopokewa na wala sio kitendo cha aliyepokea.
Kwani huenda mpokeaji akaghafilika, lakini maneno yakabaki vile vile na ndiyo
yanayostahiki kutendewa kazi. Haya ni kwa mujibu wa misingi ya Shari'ah,
Qur-aan na Sunnah.
Tokeo hili ni sawa katika hukmu na
tokeo la Ibnu 'Abbas (Radhiya Allaahu ‘Anhu) katika kisa cha Kuraib, kama vile
Ibnu 'Abbas (Radhiya Allaahu ‘Anhu) alipokea kwamba Mtume (Swalla Allaahu
‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikubali habari za mwezi zilizoletwa na bedui
asiyetambulika na bila ya kumuuliza anatokea wapi au mwezi aliuona wapi. Halafu
Ibnu 'Abbas (Radhiya Allaahu ‘Anhu) huyu huyu hakuukubali mwezi ulioonekana na
Kuraib pamoja na watu wengine huko Sham.
Hapo ndipo tunapowajibika kushika yale
maneno aliyoyapokea Ibnu 'Abbas (Radhiya Allaahu ‘Anhu) na kukiacha kitendo
chake. Lililo bora ni kushika yale maneno ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa
aalihi wa sallam) yaliyo wazi kuwa mwezi ukionekana (popote) watu wafunge au
wafungue na hivyo ndivyo alivyofanya mwenyewe Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa
aalihi wa sallam) bila ya kuzingatia wapi umeonekana mwezi.
Kauli yake ilikuwa kama ifuatavyo:
((Fungeni kwa kuonekana mwezi - muandamo na fungueni
kwa kuonekana mwezi – muandamo.))
Suala
Jengine:
Je masimulizi ya Kuraib na Ibnu 'Abbas
(Radhiya Allaahu ‘Anhu) ndio yanakuwa makhsusi (خاص) katika Hadiyth za
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) zilizotaja habari za kufunga
na kufungua?
Ni vyema kuweka wazi kwamba Hadiyth
zote za Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ambazo ni nyingi mno
(Mutawaatir) zilizotaja habari ya kufunga na kufungua mwezi wa Ramadhaan zote
zimekuja kwa ujumla – (‘aam) (عام). Bila kuhusisha
watu wa nchi fulani, masafa au matlai ya aina yoyote.
Angalia:
i. Ahkamul–Qur-aan
Cha Al-Jaswas J. 1 uk. 305.
ii. Fiqhi–Sunnah
Cha Sa'iyd Saabiq J. 1 uk. 436.
iii. Rawaaiul–Bayaan
J. 1 uk. 211.
iv. Naylul-Awtaar
J. 4 uk. 195
v. Sharhu
Subulu Sawiyyah Lifiqhi Sunanil –
Marwiyyah
vi. Fatawa
Za BAKWATA uk. 10 - 11 Mada 14/70
Masimulizi ya Ibnu 'Abbas (Radhiya
Allaahu ‘Anhu) na Kuraib yalitokea zaidi ya miaka 30 baada ya kufa kwa Mtume
(Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na kwamba Makhalifa wote wanne
walikwishaondoka duniani. Kwa hivyo kuyafanya masimulizi hayo ya Kuraib kuwa
ndiyo ‘Khaas’ (خاص) katika Hadiyth hizo
za kufunga na kufungua Swaum ni kinyume na kanuni za kifani. Ni vyema
kuwaangalia Wanavyuoni wa fani ya Usulil-Fiqhi
wanasema nini katika vitabu vyao kwenye huu mlango wa ('aam) ( عام) – yaani maana ya
ujumla na upamoja kwa watu wote:
... اما احتمال التخصيص دون أن ينهض دليل على هذا الإحتمال فهو مما
لا يؤبه به. ولا يلتفت إليه، ولا يعمل عليه، فتبقى دلالة العام على شمول أفراده
قطعية، ولا يؤثر فيها مجرد احتمال التخصيص بلا دليل إذا أن هذا الإحتمال من قبيل
التوهم، ولا عبرة بالوهم ولا التوهم.
Ifuatayo ni tafsiri kwa njia ya maana
bila ya kutafsiri neno kwa neno:
“Ili khaas (خاص) ikubalike katika
misingi ya Shari'ah kama ni hoja sahihi lazima khaas hiyo iepukane na utata.
Kuwepo kwa utata ndani ya khaas kutaifanya kukosa kuwekwa mbele kwenye safu za
hoja. Kwa hivyo (kielimu) haitaweza kutegemewa kwa namna yoyote ile. Na badala yake itabakia kuwa ni ya ujumla ('aam)
( عام) katika kuwajumuisha
watu wote popote walipo. Kwani kuwepo kwa utata ni tuhuma zisizo na ushahidi imara zinazoifanya khaas hiyo kwa
mujibu wa kanuni za Usulil-Fiqh kutoweza kuzingatiwa.
i). Kwa kuwa masimulizi ya Ibnu 'Abbas
(Radhiya Allaahu ‘Anhu) na Kuraib yana utatanishi – hayaeleweki kwa maana moja;
hayawezi kuchukuliwa kama ni hoja kama walivyoeleza hayo Wanavyuoni wa Usulil-Fiqhi na Mustalahul–Hadiyth.
ii). Kwa kuwa Ibnu 'Abbas (Radhiya
Allaahu ‘Anhu) ameonyesha kinyume na vile alivyopokea Hadiyth ya Mtume (Swalla
Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakiwezi tena kuchukuliwa kitendo chake
kama ni hoja.
iii). Katika Hadiyth iliyopokelewa
habari ya kuonekanwa mwezi muandamo na bedui ambapo ingeyumkinika kuulizwa
aliuona wapi mwezi muandamo lakini hakuulizwa. Jambo hilo linapewa hukmu ya
'aam (عام) ujumla katika fani ya Usulil-Fiqhi.
Wanavyuoni wamekuwa wakisema haya yafuatayo:
"إن العبرة عند تعارض مذهب الصحابى وروايته بروايته دون مذهبه
فإن رأيه لا يوجب حكمًا بخلاف روايته ولو نقل رايه تواترًا وهو معنى قولهم: العبرة
بما روى الصحابى لا بما رأى"
“Hakika chenye kuzingatiwa baina ya njia aliyopita
Sahaba (katika kutenda jambo fulani) na kile alichokipokea kutoka kwa Mtume
(Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam); jambo la kufaa kuzingatiwa katika
hukmu ni kile alichokipokea (wala sio kile alichokitenda). Hata kama kitendo
chake hicho kimepata umaarufu na kujulikana sana.”
Hiyo ndio maana ya maneno ya Wanavyuoni
wa Shari'ah yasemayo:
“Chenye
kuzingatiwa ni kile alichokipokea Sahaba kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu
‘alayhi wa aalihi wa sallam) wala sio kile alichokitenda kutokana na riwaya
hiyo.”
iv). Ameandika mwanachuoni mmoja
anayeitwa Shaykh Aadaud bin Ibrahim bin Umar kitabu cha Kiibadhi cha Usulul-Fiqh kinachosomeshwa mashuleni.
Katika J. 2 uk. 15 ameandika yafuatayo:
"فإذا
حكي عن النبي (صلى الله عليه وسلم) حكم _ وكان
في الحال المحكية معه أكثر من احتمال واحد، وسكت النبي (صلى
الله عليه وسلم)
كتاب أصول الفقه – للسنوات المتوسطة، تأليف: الشيخ: آدود بن
ابراهيم بن عمر، الجزء الثانى صفحة: 10.
إذا
حكى عن النبي (صلى الله عليه وسلم) حكم، وكان في
الحال المحكية معه أكثر من احتمال واحد كان الحكم عامًّا مع كل تلك الإحتمالات.
Tafsiri yake ni kama ifuatavyo:-
“Atakapoeleza
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) juu ya hukmu ya jambo
(fulani) na hukmu hiyo ikawa ina utata (yaani ina tafsiri zaidi ya moja) kisha
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akanyamaza bila ya kutoa
ufafanuzi mwengine wowote juu ya hukmu ya jambo hilo; itakuwa hukmu ya jambo
hilo ni ‘aam – yaani ni hukmu ya jambo lenye kuwajumuisha Waumini wote kwa
pamoja, pamoja na kuwa jambo hilo lina utata.”
Ndugu Juma amekuwa na mtazamo wake juu
ya yale aliyoyasema Shaykh Naaswir Bachuu kwamba kwa muda wa miaka 30 ya
Makhalifa waongofu hapakupatikana utatanishi wowote juu ya suala la muandamo wa
mwezi. Haikuthibiti kwamba Masahaba waliwahi kuzingatia suala la masafa au
matlai katika suala la kuandama kwa mwezi.
Ndugu Juma anasema: ((Kama ilivyokuwa hakuna ushahidi kwamba wao waliwaamrisha watu
wasifate miandamo yao, pia hakuna ushahidi kwamba wao waliwakataza wasifate
miandamo yao, au kwamba waliwaamrisha kufata muandamo wa Madina.))
Kwa upande
wetu tunasema hivi:
Ni kweli kuna uwezekano kwamba Masahaba hawakuwaamrisha watu wasifuate miandamo
yao au waliwakataza watu kufuata miandamo yao.
Bila shaka jambo hilo linawezekana sana,
kwani Masahaba hawana mamlaka ya kuwaamrisha au kuwakataza watu kwani wao
hawakuwa wakipata Wahyi. Mwenye mamlaka hayo ni mwenyewe Mtume (Swalla Allaahu
‘alayhi wa aalihi wa sallam). Isipokuwa Sahaba akisema: “Tumeamrishwa kadha” au “Tumekatazwa kadha.” Jambo
hilo hupewa hukumu ya “Rafii.”
Juu yao Masahaba ni kumsikiliza Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa
sallam) anavyowaamuru na kumuuliza pale panapotokea mushkeli wowote.
Kwa mantiki hiyo tunapenda kusema kuwa
hakuna Riwaya hata moja iliyo Sahihi
inayoeleza kuwa labda Masahaba walimuuliza Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa
aalihi wa sallam) kuwa tufunge vipi au wenzetu walioko mbali nao wafunge vipi
na wafungue namna gani. Hii ina maana kwamba Masahaba walimuelewa vyema Mtume
(Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika maagizo yake hasa katika
suala hili la kufunga walielewa vyema kuwa agizo hili ni la Waumini wote, mahala popote walipo.
Riwaya itegemewayo juu ya suala hili
linalo zingatiwa matlai ni masimulizi ya Kuraib tu. Tukio lililotokea zaidi ya
miaka 30 baada ya kufa Bwana Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa
sallam). Pia Makhalifa wote wanne walikwisha ondoka Duniani.
Masimulizi ambayo yana utata mkubwa na hayana ufafanuzi wa kina, hususan yanapopimwa katika mezani mbili – mizani ya Usulul Fiqhi na mezani ya Mustalahul- Hadiyth. Baada ya kupimwa vizuri uzito wake katika mezani zote mbili, inabainika kwamba hapana uzito unaostahili kuchukuliwa kama ni hoja sahihi za kutegemewa katika mdahalo huu wa muandamo wa mwezi.
Ama tukichukua maneno sahihi ya Mtume
(Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliyoyasema: ((Fungeni kwa kuuona mwezi
muandamo…)) katika mezani, tutaona kina cha uzito wa maneno haya ni
kikubwa mno. Ndio maana tukasema kushikamana na maneno ya Mtume (Swalla Allaahu
‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni bora na ndiyo hasa Sheri'ah inavyotuagiza
kuliko kushika maneno yenye utata na yenye khitilafu.
Kama tukijadili uwezekano wa
utekelezaji wa agizo hilo la kufunga na kufungua katika zama ambazo mawasiliano
yalikuwa duni na hafifu sana;
tungejiuliza, Masahaba wangewezaje kupeana taarifa za kuandama kwa mwezi
katika nchi za mbali? Wengewezaje kwa pamoja kuamka wakiwa wamefunga na hasa
pakizingatiwa kuwa taarifa zenyewe zinatakiwa ziwafikie wengine kabla ya
kupambazukiwa na alfajiri? Bila shaka jambo hilo lilikuwa ni gumu kiutekelazaji
hata katika nchi moja pekee. Lakini ni vyema kuelewa kwamba hilo lilikuwa ni
jambo la dharura kwa wakati huo.
Msisitizo wetu mkubwa ni kuwa katika
masimulizi ya Kuraib hapakupatikana maafikiano ya Wanavyuoni kwa hivyo si jambo
la kutegemewa. Kama wanavyosema Wanavyuoni wa ‘Usulil-fiqhi.’
“Dalili ikiwa na maana (nyingi) zaidi ya moja,
huporomoka ushahidi wake.”
Ikumbukwe kuwa Sunnah ya Mtume (Swalla
Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni (aula) bora kwa hali yoyote iwayo.
Kinachotakiwa ni kuifuata sio kuibeza. Shaykh Al–Qanubiy wa Kiibadhi anasema
katika kitabu chake kuwa:
"... فإذا تعارض أمر رسول الله (صلى
الله عليه وسلم) وأمر غيره، فأمر رسول الله (صلى
الله عليه وسلم) أولى أن يتقدم ويتبع"
“Itakapogongana amri ya Mtume (Swalla Allaahu
‘alayhi wa aalihi wa sallam) na amri nyengine yoyote, basi amri ya agizo la
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni (aula) bora zaidi
kutangulizwa (mbele) na kufuatwa.”
Shaykh Ahmed Al-Khaliil (Mufti Mkuu wa
Omani) naye amesema:
"ولا عبرة بقول قائل يخالف الحديث الصحيح فالسنة حجة على
غيرها ولا يكون غيرها حجة عليها"
“Hakuna kuzingatiwa kauli itakayopingana na Hadiyth
sahihi, kwani Sunnah ni hoja juu ya jambo la Kidini, wala jambo jengine lolote
haliwezi kuwa ni hoja dhidi ya Sunnah.”
"...
فالواجب يحتم أن يكون الأصل الذي يرجع إليه مادل عليه صريح الكتاب العزيز والسنة
الصحيحة..." الحق الرامغ (صفحة: 103)
Anachokieleza Shaykh Ahmed Al-Khaliil
ni kuwa:
“Lazima
marejeo ya asili (katika misingi ya Kidini) ni kila kilichoelezwa kwa (saraha)
uwazi katika Qur-aan Tukufu na kilichoelezwa katika Sunnah Sahihi.”
"وكان السلف الطيب يشتد نكيرهم وغضبهم على من عارض حديث رسول
الله (صلى الله عليه وسلم) برأى أو قياس أو
استحسان أو قول أحد من الناس كأننا من كان..."
“Walikuwa wanavyuoni wema wakionyesha kukereka kwao
na hasira zao juu ya yule mtu ambaye anaipuuza (anaibeza) Hadiyth ya Mtume
(Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa (kuifuata) rai (ya
mwanachuoni) au Qiyaas au mapendekezo ya Wanavyuoni au kauli ya mtu yeyote kwa
kuipuuza Sunnah ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)”
Katika maudhui yetu hayo ya muandamo wa
mwezi, katika kadhia ya kufunga na kufungua kwa kuonekana mwezi, ni vyema
kuachana na vitu vyenye utata na kusisitiza kushikamana na maneno katika
Hadiyth Sahihi ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) isemayo: ((Fungeni kwa kuonekana mwezi –muandamo…))
Katika maelezo yaliyopita tumeeleza
kwamba Hadiyth zote za Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)
zilizotaja amri hii ya kufunga na kufungua ni Sahihi na ni zenye kukubalika mbele ya Wanavyuoni wala hazina
khitilafu yoyote juu ya usahihi wake. Hadiyth zote hizo zimetaja amri hii ya
hukumu ya kufunga na kufungua kwa ujumla – yaani ni jambo linalotekelezeka kwa
watu wote katika siku moja. Wala agizo hilo halihusishi nchi fulani pasi na
nchi nyengine. Ni agizo la ujumla ‘aam
(عام). Pia ni wazi kwamba
agizo hilo la Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) halikutaja
suala la kuwepo kwa matlai wala masafa gani, wala chengine chochote. Wala
hakuna katika maelezo sahihi ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa
sallam) ambayo yanakubalika na Wanavyuoni yaliyotaja kwamba ‘kila nchi ifunge
na ifungue kwa miandamo yao!’
Kama ilivyoelezwa kwamba hoja
inayotegemewa na baadhi ya Wanavyuoni wachache juu ya mas-ala haya ni kisa cha
masimulizi ya Kuraib, masimulizi ambayo hayana ufafanuzi wa kina kama
walivyoeleza hayo baadhi ya Wanavyuoni wengine na kuonyesha kuwa yana
utatanishi (ihtimaalati). Jambo
ambalo linaifanya hoja yake kuwa dhaifu. Kama yalivyoelezwa hayo na Wanazuoni
wa fani ya “Usulul-Fiqhi.”
Kwa hivyo agizo hilo la kufunga na kufungua
kwa pamoja litaendelea kuwa hivyo kwani hakuna riwaya sahihi isiyo na utata
yenye kuvua ujumla huu. Tamko hili ni:
Ama jambo la kusema kila watu na
mtenguko wao wa jua kwa hivyo wana wakati wao wa kuswali na kufunga (Swaum)
ndio hivyo hivyo; ni vyema ieleweke hivyo ni vitu viwili tofauti. Swala
imeambatana na mitenguko ya jua na Swaum imeambatana na kuandama kwa mwezi.
Mas-ala ya nyakati za Swala yameshaelezwa na kufafanuliwa na Mwenyewe Mwenyezi
Mungu katika Qur-aan na pia Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)
amelibainisha kwa uwazi kabisa katika Hadiyth. Wala hakuna ikhtilafu yoyote
mbele ya Wanazuoni juu ya jambo hilo. Ijmai ya Wanazuoni wamekubaliana kuwa
kila sehemu, wala si kila nchi nzima inaweza kusali kwa wakati mmoja. Kwani
mtenguko wa jua unaweza kutofautiana hata katika nchi moja. Angalia Dar es
Salaam na Kigoma wanaswali na kufuturu tofauti, lakini wanafunga kwa mwandamo
mmoja.
Kila sehemu itaswali kwa wakati wake
kwa kutegemea mtenguko wake wa jua. Mwenyezi Mungu Amebainisha hayo katika Surat Bani Israil (17: 78) kama
ifuatavyo:
{{Simamisha Swala jua
linapopinduka (likaenda magharibi) mpaka giza la usiku.}}
Kwa upande wa Swaum hapakupatikana
ufafanuzi wa kina ambao unakubalika mbele ya “Jamhur” ya Wanazuoni. Hakuna hoja
isiyokuwa na utata katika jambo la kuanza kufunga na kufungua kwa kutegemea
kila nchi au kila eneo moja peke yake. Kwa mantiki hiyo ndio maana “Jamhur” ya
Wanavyuoni wetu wakaonelea ni bora kutegemea Sunnah, yaani Hadiyth za Mtume
(Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) zilizo wazi ambazo zinaashiria
umoja katika kufunga kwa pamoja.
Kukamata andiko sahihi (نص صحيح)ni bora kuliko kung’ang’ania jambo
lisilofahamika ambalo lina utatanishi.
“Kutumia madondoo ( النص ) kama Qur-aan au Sunnah ni bora zaidi ( أولى ) kuliko kuiwacha (au kuipuuza na kuzingatia dalili zenye utata)”.
Ama suala la kuingia alfajiri na
kujizuilia kula na kunywa katika hukmu ya kuanza kufunga au kuanza kufuturu
wakati wa kuzama kwa jua, mambo hayo hayana mjadala au khitilafu kama hizo
kwani Mwenyewe Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Ameshayafafanua katika Qur-an Tukufu
kama ifuatavyo:
{{وَكُلُوا وَاشْرَبُوا حَتَّىٰ يَتَبَيَّنَ
لَكُمُ الْخَيْطُ الْأَبْيَضُ مِنَ الْخَيْطِ الْأَسْوَدِ مِنَ الْفَجْرِ}}
{{Na kuleni na kunyweni
mpaka ubainike kwenu weupe wa Alfajiri katika weusi wa usiku. Kisha timizeni
Swaum mpaka usiku.}} (2: 187)
Jambo hilo la kutokuwepo khitilafu
yoyote katika mas-ala haya, inamaanisha kwamba kila sehemu itajizuilia kula na
kunywa kutokana na kuingia alfajiri yake na kila sehemu itafuturu baada ya
kuzama jua kwa upande wake.
Ama ile hoja inayotolewa na baadhi ya
ndugu zetu kama Juma isemayo: “Mbona
watu wa nchi fulani wakifuturu nyinyi hamfuturu nao?" Au “Wakifuturu watu wa Saudia na nyinyi mufuturu basi.” Bahati nzuri kwa upande wetu tumeshajibu mara
nyingi katika makala haya kwamba jambo hili haliingizwi katika mjadala kama huu
kwani jambo hilo halizungumzwi hata katika nchi moja yenye kufuata muandamano
mmoja. Tumetoa maelezo kwamba katika Tanzania, Mji wa Dar-es-salaam hauwezi
kufuturu sawa na mji wa Kigoma kwani kuna tofauti ya zaidi ya dakika 40.
Jua linazama au kuchomoza dakika 40
kabla ya Kigoma. Kwa hivyo, Dar es Salaam wanaanza kufuturu mwanzo wakati bado
jua halijatua Kigoma.
Al-Marhuum Shaykh Abdulla Al-Farsy
alipokua akiifasiri Aya ya Quran isemayo:
{{Kisha timizeni Swaum
mpaka usiku.}}
Aliitolea maelezo yafuatayo:
“Na ilipoambiwa: {{Fungeni
Swaum mpaka usiku.}} Muradi ni magharibi – jua likishakuchwa tu, ndio
usiku wenyewe uliokusudiwa, kama alivyobainisha hivi Mtume (Swalla Allaahu
‘alayhi wa aalihi wa sallam), na akahimiza watu wafungue jua tu likishakuchwa,
na wakawie kula daku…”
Kwanza ni vyema kuelewa kwamba mjadala
huu wa mwezi katika hukumu ya kufunga na kufungua ni mkongwe wala haukuanza
leo. Wala hii si fikra aliyoianzisha Shaykh Naaswir Bachuu kama walivyofahamu
hayo baadhi ya watu kama akina ndugu Juma. Ukweli ni kuwa Shaykh Naaswir ni
miongoni mwa Mashaykh wanaoendeleza harakati hizi za kufuata muandamo mmoja.
Mtazamo huu wa kufunga kwa pamoja uliokuwepo tokea karne nyingi zilizopita
umeshaelezwa katika kitabu cha “Kuandama
kwa Mwezi” cha Shaykh Naaswir Bachuu uk. 129 - 133.
Wanavyuoni wakubwa kama Dr. Wahbah
Zuhailiy, Shaykh 'Abdur-Rahmaan Al-Juzairy, Alqanuji, Sayyid Saabiq, Ibnu
Taymiyah, Ibnu Quddama Almaqdisiy, Shaykh Muhammad 'Aliy Assaabuniy na wengine
wengi ni miongoni mwa waliosema kuwa msimamo wa kufunga kwa muandamo mmoja ndio
“Rai ya Jamhur.”
Msimamo huu kwa kweli umejengeka katika
misingi imara uliopokewa moja kwa moja kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi
wa aalihi wa sallam) pale aliposema:
((Fungeni kwa kuona mwezi – muandamo…..))
Wanavyuoni wa Shari'ah wameieleza “Jamhur” kwa maana ya kukubaliana
jambo “Maimamu wanne wa Kisunni”
na hata kama ikitokea kujitoa Imamu mmoja katika hao wanne kwenye jambo fulani
bado jambo hilo litachukuliwa ni la msimamo wa “Jamhur” midam watatu kati yao wana msimamo mmoja.
Ama tukichunguza katika kitabu cha
ndugu Juma tunakuta ameeleza maana ya Jamhur
kinyume na hivyo. Ameieleza “Jamhur”
katika mtindo usioelezwa katika vitabu vya Shari'ah. Miongoni mwa udhaifu
alioutaja ndugu Juma katika kueleza maana ya “Jamhur” ni vile alivyoeleza kuwa ((…tunasema kwamba kusema kwamba kauli ya muandamo mmoja ni
kauli ya Jumhuri ya Umma, ni jambo la kufikiriwa.)). Sisi tunasema kwamba kitu cha kwanza
cha kufikiriwa ni hii tafsiri ya ndugu Juma katika maana ya neno “Jamhur.” Tunamuomba ndugu Juma
asijifanye kama yule kipofu aliyeingia kwenye nyumba ya mtu na kujigonga kwa
vitu vilivyokuwemo ndani, kisha akawalaumu sana wenye nyumba. Sasa inafaa
kujiuliza ni nani wa kulaumiwa baina ya kipofu na mwenye nyumba? Bila shaka wa
kulaumiwa ni yule bwana kipofu kwani vitu vilikwishapangwa vizuri na mwenye
nyumba lakini kwa sababu ya kutokuona kwake ndio akamtupia lawama mwenye
nyumba.
Kwa hivyo nasi tunamtanabahisha ndugu
Juma kuwa Wanavyuoni wenye kuaminika wamekwishakuieleza maana halisi ya “Jamhur” katika matumizi ya Shari'ah
ingawa yeye kwa makusudi akajitia upofu na kuanza kusema: ((…naona watu hapa wamekuwa wakipiga
kampeni kwa kutumia jina Jumhuri nayo si sahihi.)) Kisha akaendelea kusema: ((basi atatokea mtu anayetaka kuipamba rai yake, anasema:
"Umma umekubaliana juu ya jambo hili!"))[5][5]
Kama kweli ndugu Juma ni msomi ingekuwa
jambo la busara atoe majina ya vitabu vya Wanavyuoni wenye kukubalika waliosema
kuwa rai ya kufuata muandamo mmoja sio rai ya Jamhur. Pili tunamuuliza
ndugu Juma ni rai ipi aliyoikuta yeye ambayo imetajwa kuwa ni rai ya Jamhur kisha isiwe ni rai ya Jamhur? Ilikuwa ni wajibu wake kama
anataka kuikosoa atoe ushahidi wa maandiko na madondoo ili uwe ushahidi. Kwani
tunavyojua sisi ni kuwa kila rai iliyotajwa kuwa ni ya Jamhur panakuwa na
maandiko yenye kukubalisha jambo hilo, hata kama ipo khitilafu ya baadhi ya
Wanazuoni.
Tunamnasihi ndugu yetu Juma kuwa
anapojaribu kuelezea mas-ala yoyote ya kielimu, basi ni vyema apite katika njia
zake zenye kukubalika kitaalamu wala asidhani kuwa anaweza kufaulu bila ya
kupita katika njia hizo. Ni vyema aelewe kwamba asipopita katika njia hizo
atapotea. Mshairi mmoja wa kiarabu anasema hivi:
“Unatarajia kuokoka (kufaulu) bila ya kupita katika
njia zake (Elewa kwamba) jahazi haiwezi kwenda kwenye nchi kavu.”
Mshairi mwengine anasema:
“Ukiliendea jambo (ukitaka kulifanya jambo) bila ya
kupita katika njia zake utapotea (na kuwapoteza wenzako). Na ukiliingia jambo
katika njia zake utaongoka (na utaongoza wenzako).”
Tukiendelea kumfahamisha ndugu Juma juu
ya kauli zake alizoziandika kwenye kitabu chake ambazo sio za kielimu ni kule
kusema kwake kwamba: ((kama tulivyotangulia kusema kwamba
mas-ala ya kufunga kwa muandamo mmoja yamo katika vitabu tu: si katika matendo:
kimatendo ni Waislamu wachache sana duniani wanaofata rai hio.))[6][6]
Tunamfahamisha ndugu Juma kwamba kitu
cha msingi kinachofaa kuzingatia katika mas-ala yoyote yale ya Dini ni ule usahihi wake, sio kuangalia wingi au
uchache wa wafuasi. Mfano mzuri ni haya madhehebu ya Ibadhi yenye wafuasi
wachache mno duniani ukilinganisha na madhehebu mengine kama Hanafi na
mengineyo. Je kwa sababu ya uchache wao ndio unataka kusema Ibadhi hawako
katika haki?
Kwa hiyo uchache wa wafuasi sio kipimo
cha haki au batil. Ni vyema ndugu Juma awe makini katika uandishi hususan katika
jambo la kujenga hoja, asikubali kutawaliwa na taasub za aina hizo.
(1) Msimamo wa kufunga na kufungua kwa
muandamo mmoja duniani ndio rai ya Jamhur. Wala si rai itokayo kwa Shaykh Naaswir
Bachuu. Ndugu Juma hakuwa makini katika kukisoma kitabu alichokiandika Shaykh
Naaswir Bachuu: “Kuandama Kwa Mwezi” uk. 162 - 163. Wafuatao ni baadhi ya
Mashaykh wa Afrika Mashariki waliowahi kubainisha jambo hilo:-
i) Al-Marhuum Shaykh Juma 'Abdul-Waduud
wa Zanzibar katika kuelezea msimamo wa kufunga pamoja alisema ifuatavyo:
“Hii ni rai
nayo na wengi wamesema (hivyo) kama Imamu Malik, Ahmad na kundi kubwa la
Hanafi….”[7][7]
ii) Shaykh Abdillahi Naaswir wa Kenya
ameeleza yafuatayo:
“Wako
wanaosema kwamba mwezi ukionekana mji mmoja, basi Waislamu wengine popote
walipo wafunge. Hayo ni maoni ya Hanbali, Maliki na Hanafi…” (Imenukuliwa kutoka kitabu chake
Swaum--Nguzo Ya Nne uk. 22 - 23 chapa ya 1985.)
iii) Al-Marhuum Shaykh Hemed bin Juma
bin Hemed –aliyekuwa Mufti Mkuu Wa Tanzania Katika hotuba yake iliyonukuliwa
neno kwa neno na gazeti la Al-Jihaad toleo No: 4 la tarehe 18/03/1994 sawa na
6/Shawaal/1416 lililotolewa na MSAUD. Katika maelezo mengi aliyoyatoa Shaykh
Mkuu huyo kwenye kadhia iliyosababisha kuandama mwezi siku iliyo ikiaminika
kuwa ni mwezi (tarehe) 28 ya Ramadhaan alikuwa na haya ya kusema:
“Nyinyi
Waislamu wezangu, mwaniambia mimi, kwa ile tukio lenyewe lote, kadhia
nilivyoeleza, mwaweza nambia nimewafungisha siku ishirini na nane? Basi
tumefungua, Alhamdulillah rabbil aalamin. Linalofuata, mimi nitoe shukrani
kubwa kwa watukufu, kutusaidia namna hiyo, na kuondosha tatizo hilo. Pia
nashukuru sana, kwa bahati kubwa tuliyoipata mwaka huu, ya kihistoria, kufungua
siku moja, sisi na wa Saudia, Cairo na Muscat Oman na wapi, kufungua siku moja,
nadhani kihistoria, mimi mpaka leo, nina miaka, huu wa sitini na sita, lakini
sikumbuki kupata bahati hii. Sikumbuki kupata bakhti hii. Nimemuuliza mzee
wangu, Mzee Gumsani, una miaka mingapi, ananiambia themanini na nne, sijui themanini
na ngapi! Je iko siku umebahatika hivyo, asema bado sijapata. Je, bahati
iliyoje hii? Hadhi kubwa tuliyoipata ya kufungua siku moja, wa Saudia, Cairo,
Maskati Oman na miji kadha kadhaa ya Kiarabu.
Tunamuomba
Mwenyezi Mungu Aiendeleze bahati hii, ili kuimarisha umoja huu. Mungu ajaalie
'Arafah pia iwe moja. Ndio zina matatizo, na 'Iyd ya mfunguo mosi iwe moja.
Matatizo haya yaondoke InshaAllaah!”
Mwisho wa kunukuu.
(2) Imeshawahi kutokezea mara nyingi
dunia nzima (au sehemu kubwa ya dunia) kufunga na kufungua kwa pamoja, yaani
katika siku moja. Mfano mzuri uliowahi kutokea ni huo hapo juu alioueleza Mufti
Mkuu Shaykh Hemed bin Juma katika tokeo la mwaka 1994.
Pia katika mwaka wa 2007 takriban dunia
nzima ilifunga siku moja ya tarehe 13/09/2007.
{{Atakayeuhudhuria mwezi afunge!}} (2: 185)
Uchambuzi wa neno “shahida” (شهد) na neno (الشهر ) “Shahra”; baadhi ya watu wamedhani
kwamba maana ya shahida ni ‘kuona kwa
macho’ na neno Shahra wanadhani kuwa ni ‘mwezi – muandamo.’
Kwa mujibu wa Wafasirina takriban wote
wamelifasiri neno ‘shahida’ kwa maana ya “kuwepo” au “kuhudhuria” wala sio
maana ya ‘kuuona mwezi’ hata Shaykh Muhammad 'Aliy Assaabuniy ameona ni makosa
kitafsiri kulifasiri neno hilo kwa maana ya “Kuuona mwezi muandamo” kama
alivyosema:
“Na wala sio maana ya neno ‘shahida’ (liliyomo
katika Aya hiyo) kwa maana ya kwamba: ‘ameuona mwezi.”
Neno ‘shahra’ lililomo katika Aya hiyo
linaleta maana ya ‘mwezi - siku’ yaani ‘month’ kwa lugha ya Kiingereza. Ni
mwezi unaoashiria tarehe kuanzia 1 mpaka 29 au 30. Wala neno hilo halina maana
ya ‘mwezi-sayari’ yaani ‘crescent’ au ‘moon’ kwa lugha ya Kiingereza.
Kitu muhimu ni kuelewa kwamba maneno
mawili hayo yaani ‘shahida’ na ‘shahra’ yaliyomo katika aya hiyo, yana maana
tuliyoieleza hapo juu na ndivyo walivyoeleza Wafasirina wakubwa wote. Ni vyema
mtu anapoingia katika mjadala kama huu atoe madondoo sahihi yenye kukubalika
sio kuingiza fikra zake tu, hususan katika suala hili la tafsiri. Tukianza
kutumia utamaduni huo wa kila mmoja kubuni tafsiri yake mwenyewe na tukaziacha
tafsiri za Wanazuoni wenye kutegemewa, jambo hilo litatufanya tuwe na idadi
kubwa ya wafasiri ‘bandia’ ambao sio wafasiri wa kweli.[8][8]
Vile vile ukizingatia neno ‘shahra’ (الشَّهرَ) utaliona katika
herufi yake ya mwisho ambayo ni ‘Re’ imetiwa ‘fat-ha’ (َ رَ), hio haina maana
kwamba neno hilo lina maana ya ‘mtendwa’ (مفعول به) – kama wanavyodhania
baadhi ya watu. Ingawaje neno hilo limemalizikia ‘fat-ha’, lakini halina maana ya ‘mtendwa’ bali neno hilo linaashiria maana ya ‘wakati’ (ظرف الزمان). Ni muda maalumu
kama mfano mtu akisema: “Nitakuja mwezi
wa Ramadhaan” hapa hakuna kitu chenye kuonekana bali muda au wakati tu. Kinyume na akisema: “Nimeuona mwezi” hapa ndio itakuwa neno ‘mwezi’ ni ‘mtendwa.’
Kwa hiyo, wanaotumia Aya hiyo kwa maana
ya ‘kuuona mwezi kwa macho’ sio
sahihi kama alivyothibitisha hayo Mwanachuoni – Mufasir katika tafsiri ya
‘Al-Kashaaf’:
الشهر:
منصوب على الظرف وكذلك الهاء في "فليصمه" ولا يكون مفعول به كقولك: شهدت
الجمعة، لأن المقيم والمسافر كلاهما شاهدان للشهر _ (الكشاف، صفحة: 226 الجزء
الأول)
Na vile vile katika kitabu:
‘Rawaaiul-Bayaan’ yameelezwa hayo hayo:
قوله
تعالى: {{فَمَنْ شَهِدَ مِنْكُمُ الشَّهْرَ
فَلْيَصُمْهُ}} الشهد منصوب على الظرف وكذلك الهاء في "فليصمه"
ولا يكون مفعولا به لأنه يلزم حينئذ المسافر لأنه شهد الشهر قال الزمخشرى: المعنى
فمن كان شاهدًا أي حاضرًا مقيمًا غير مسافر فليصم في الشهر ولا يفطر.
{{فَمَنْ شَهِدَ مِنْكُمُ الشَّهْرَ فَلْيَصُمْهُ}} المراد شهود الوقت لا شهود رؤية
الهلال. إذ قد لا يراه إلا واحد أو اثنان ويجب صيامه على جميع المسلمين. وشهد
بمعنى حضر وفيه إضمار أي من شهد منكم الشهر مقيما غير مسافر ولا مريض فليصمه.
Takriban wafasirina wote wa Qur-aan
tukufu wameifasiri Aya hiyo kwa maana ya ‘atakayekuwa katika mji katika huu mwezi wa Ramadhaan afunge.’
Hakuna hata mmoja aliye Mwanachuoni wa kweli aliyeifasiri Aya hiyo kwa maana ya
‘atakayeuona' au 'atakayeushuhudia’ mwezi afunge. Wala
hakuna khitilafu katika tafsiri za Wanavyuoni hao juu ya Aya hiyo. Khitilafu
iliyopo ni moja tu: Je mwezi ukiandama sehemu moja duniani italazimu kufunga
sehemu nyengine zilizobaki au kila sehemu na muandamo wake?
Kinyume na maneno ya ndugu Juma
aliposema: ((Aya hii inawezekana kuchukua tafsiri zote: kushuhudia kwa
maana ya kuona na kushuhudia kwa maana ya kuwepo katika mji. Na zote
zinakubalika kwa mujibu wa fani za tafsiri…))
Inasikitisha sana mara nyingi kumuona
ndugu yetu Juma anavyotoa tafsiri ya baadhi ya Aya za Qur-aan bila kuwapa
nafasi Mashaykh wenye kutegemewa katika ulimwengu wa Kiislam. Anachokifanya
yeye ni kuingiza fikra zake binafsi katika kufasiri Aya za Qur-aan tukufu.
Kitendo ambacho hakikubaliki. Kwani ingekuwa inakubalika hali hiyo bila shaka
kusingelikuwa na haja ya kutegemewa tafsiri yoyote, kwani kila mmoja wetu
angelikuwa bingwa wa kubuni tafsiri aitakayo mwenyewe – jambo ambalo
lingetufikisha pahala pabaya na baya zaidi ni kumsingizia uongo Mwenyezi Mungu
katika Maneno Yake Matukufu.
Wala hatukusudiwi kwamba hao wafasiri
pekee walikuwa kama kwamba wakipata ‘Wahyi’ na kwamba maneno yao yalikuwa
hayawezi kuwa na dosari au kupingwa. La hasha! Kinachokusudiwa ni kuwa
anapoingia mtu yeyote katika mjadala wa kutetea hoja juu ya jambo fulani lazima
aonyeshe madondoo sahihi yenye kuthibitisha dai lake hilo, sio kutoa fikra zake
na zikakubalika. Kinachosisitizwa ni ule umuhimu wa kuonyesha madondoo ya
tafsiri ya Aya za Qur-aan alizotegemea sio nafasi ya mtu kutumia akili yake
katika maeneo hayo.
Mantiki hiyo ndiyo aliyotumia Shaykh
Naaswir Bachuu kila anapotaja tafsiri ya Aya za Qur-aan tukufu huwa anaonesha
pahala alipoitoa tafsiri hiyo. Kwa hivyo hakwenda kinyume na kanuni za kielimu
na misingi sahihi ya Dini yetu.
Alichosisitiza Shaykh Naaswir Bachuu
katika Hadiyth isemayo:
((Fungeni kwa kuuona mwezi – muandamo…))
Ni kuwa Hadiyth hii ni 'aam – yaani ya ujumla, kwa hivyo
popote mwezi utakapoonekana na habari hizo zikathibitishwa usahihi wake, basi
watu wote wafunge. Kadhalika wafungue kama ni mwezi wa kufungua.
Pia Shaykh Naaswir ameonesha msimamo wa
Wanazuoni juu ya masimulizi ya Kuraib kwamba hayawezi kuwa “hoja sahihi” katika mas-ala haya.
Ndugu Juma yeye amezitaja baadhi ya
tafsiri za Quran na baadhi ya vitabu vilivyotaja Aya inayoelezewa:
Akidhania kuwa tafsiri hizo
zimeitafsiri Aya hiyo kuwa:
Ukichunguza vyema utaona kuwa ndugu
Juma hakuelewa kinachokusudiwa katika tafsiri hizo. Kwanza utaona kuwa kila
anapojaribu kulitolea tafsiri neno شهد ‘shahida’
huliwacha kama lilivyo kwa kusema ‘atakayeushuhudia’. Ni kama kusema شهد بمعنى شهد Yaani: “Atakayeushuhudia” maana yake
“atakayeushuhudia.”
Hebu na tuangalie Wanavyuoni
walivyolifasiri neno shahida: شهد
شهد
بمعنى حضر _ اى من شهد منكم الشهر مقيمًا غير مسافر ولا مريض فليصمه.
Mwanachuoni Dr. Zuhaily ameeleza
yafuatayo:
... وشهود شهر رمضان سبب لوجوب الصيام في قوله تعالى: {{فَمَنْ شَهِدَ مِنْكُمُ الشَّهْرَ فَلْيَصُمْهُ}}
“Kuuhudhuria mwezi wa Ramadhaan ni sababu ya
kuwajibika kufunga (Swaum) kama ilivyoelezwa katika Qur-aan Tukufu: {{Atakayekuwa katika mji katika huu mwezi (wa Ramadhaan) afunge.}}
Dr. Zuhaily aliendelea kutoa dalili ya
kuonesha wajibu wa kufunga kwa kuonekana mwezi – muandamo kwa kuyanukuu maneno
ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) pale aliposema: ((Fungeni kwa kuonekana mwezi –
muandamo…)) Na jambo la kuonekana mwezi japo na mtu mmoja katika Hadiyth
hiyo ni la wote ('aam).
Wala hakuna Mwanachuoni yeyote
aliyesema kuwa Hadiyth hii inaashiria kila pahala pafuate muandamo wake.
Kutegemea maneno matupu ya mwanachuoni
kama ni Khaas (خاص) bila ya kuonyesha
dalili zenye kukubalika kifani, huo utakuwa udhaifu.
Shaykh Al-Amin 'Aliy Mazrui: katika
kuifasiri Aya isemayo: {{فَمَنْ شَهِدَ مِنْكُمُ
الشَّهْرَ فَلْيَصُمْهُ}}
ameeleza
yafuatayo:
“Basi mwenye
kuwemo katika mwezi huu na afunge.” Kisha akaendelea
kusema:
Mwanachuoni Shaykh
Al-Jassas katika kitabu chake
Ahkamul–Qur-aan ameweka
mlango unaitwa Kayfiyati
Shuhudi Shahri “mlango unaolelezea
namna ya kuhudhuria
mwezi” Shaykh Al-Jassas akaanza
kunukuu aya mbili, ya kwanza “Famman Shahida minkum… na
aya ya pili “Yas-alunaka
'anil-ahilah…"
Ifuatayo ni
tafsiri sahihi ya aya hizo kama ilivyo katika
vitabu vya tafsiri,
tafsiri ya aya ya
mwanzo:
{{Atakayekuwa katika Mji katika mwezi huu
mwezi (wa Ramadhaan afunge).}}
Tafsiri ya aya ya pili:
{{wanakuuliza miezi miandamo
sema hiyo ni (vielelezo vya) nyakati kwa ajili (ya mambo) ya watu na hija
zao.}}
Ufuatao ni ufafanuzi wa aya hizo.
Tunaanza na aya ya mwanzo wanazuoni wengi sana wameitafsiri aya hiyo kwa maana
iliyo hapo juu. Ingawa ukilichukua neno mojamoja katika aya hiyo na
ukaliangalia katika makamusi ya Kiarabu utalikuta lina maana zaidi ya moja, utaratibu huu sio mgeni katika lugha
ya Kiarabu, kanuni ya lugha inasema:
“Neno halina
maana (moja) mpaka liwemo
ndani ya
sentensi”,
kwa hivyo neno
“Shahida” liliyomo ndani ya aya
hiyo lina maana ya “Kuwepo” (sio maana
ya kuona). Na neno “Shahri” lina maana ya mwezi siku, sio maana ya mwezi sayari[10][10] hiyo ndiyo
tafsiri sahihi ama kuitafsiri kwa maana ya “atakayeuona mwezi na afunge” hiyo
ni tafsiri ya kuilazimisha.
Ama uchambuzi wa aya
ya pili
kama ulivyo katika vitabu vingi
vya tafsiri, kwanza wameeleza
sababu ya kuteremshwa aya hiyo ni kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)
ameulizwa na kama aya yenyewe inavyothibitisha tokeo hilo.[11][11]
Na vilevile Wanazuoni hao wakaeleza
kuwa kilichoulizwa hapo ni hali halisi ya mabadiliko ya miezi. Kwa maelezo
zaidi rudi katika tafsiri, itakutosha tafsiri ya Dr. Zuhaily.[12][12]
Kwa mantiki hiyo hapa
hapazungumziwi kuwepo miandamo mingi wala kuwepo muandamo wa kisheria, wala Aya hii maana ya kuwa kila
nchi ifunge na ifunguwe kwa mujibu wa
matlai yao, vile vile Aya hii haina maana ya kuwa ni “Khaas” katika zile
Hadiyth zilizotaja kwa ujumla kuhusu
suala la kufunga na kufungua.
Alichokisisitiza Shaykh Al-Jassas katika kitabu
chake ni ule wajibu wa
kufunga na kufungua kwa kuzingatia “Suala zima la
kuonekana mwezi”
Na
ndio maana Shaykh
Al-Jassas akanukuu Hadiyth zenye
kutaja wajibu wa kufunga na kufungua kwa
kuonekana mwezi.
Na Hadiyth zote
hizo zimetaja jambo
hilo kwa njia ya Ujumla,
yaani hukumu yake
inawaenea Waumini wote popote walipo.
Katika kuielezea kauli hii ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)
Shaykh Al-Jassas anasema:
“ni
jambo linaloeleweka kuwa
kauli ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) isemayo: ((Fungeni kwa
kuonekana mwezi na
Fungueni kwa kuonekana mwezi)) ni ya ujumla
haiwahusishi watu wa
nchi moja peke yao pasi na wengine.
Na vilevile msimamo kama huu wa kufunga
pamoja ameuweleza Dr. Zuhaily katika
kitabu chake Al-Fiqhul- Islamiy.
Katika kitabu cha ndugu Juma chapa ya
pili uk. 143 amenukuu hoja nyengine ambayo haikuwemo katika chapa yake ya
kwanza. Katika hoja hiyo ya Abu Ammar imegundulika kwamba imejengeka katika
msingi wa ibara isemayo: “inawezekana.” Kwa hivyo ni ibara yenye utata
(ihtimal) – yaani inawezekana hivi au kinyume na hivi. Ibara kama hizi
zimeshaelezewa mara nyingi kuwa sio za kuzijengea hoja sahihi kama
walivyothibitisha hayo Wanavyuoni wa Usulul-Fiqhi.
Ingawa hoja hiyo imesemwa na
Mwanachuoni mkubwa anayeheshimika sana na InshAllaah Allaah (Subhaanahu
wa Ta’ala)
Atamlipa kwa jitihada yake hiyo. Lakini kama alivyoandika ndugu Juma katika
kitabu chake baada ya kuinukuu hoja moja ya Shaykh Naaswir Bachuu iliyomo ndani
ya kitabu chake uk. 37, hatimae kuonyesha mshangao katika hoja hiyo na kuandika
hivi: ((…shubuhati kama hizi hazifai kujadili mambo
ya kielimu.)) Nasi tunasema shubuhati kama hizi za kina Abu Ammar
hazifai kujadili mambo ya kielimu.
Ikumbukwe kuwa maneno ya Mtume (Swalla
Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika jambo hili la kufunga na kufungua
ni ya pamoja ('aam) kwa watu wote. Hakuna kabisa maneno mengine ya Mtume
(Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) yaliyo “sahihi” yenye kutufunza
kuwa kila nchi ifunge na ifungue kwa muandamo wake. Kitu kilichoelezwa juu ya
mas-ala haya ni upatikanaji wa mawasiliano ya habari za kuaminika katika
utaratibu unaokubalika kishari'ah.
Maneno ya Abu Ammar yasemayo: “Kwa
sababu lau ingelikua Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)
kafundisha kutendewa kazi muandamo wa mbali….” Hayo ni maneno dhaifu sana.
Hakuweza kutoa dalili sahihi isiyokua na utata inayoonesha kuwa amri hiyo ya
kufunga na kufungua ina mipaka maalum, au ni ya watu maalumu au inahusisha nchi
moja na kuacha nchi nyengine.
Mwanachuoni Al-Jassas katika kitabu chake Ahkamul-Qur-aan J. 1, uk. 305 katika kuieleza kauli hii ya Mtume
(Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema hivi:
“Ni jambo linaloeleweka kuwa kauli
ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) isemayo: ((Fungeni kwa kuonekana mwezi –muandamo na fungueni kwa
kuonekana mwezi-muandamo)) ni ya ujumla '(aam), inawahusisha watu wa
pande zote za dunia na kwamba haihusu watu wa nchi moja peke yao pasi na
wengine.”
Aidha Shaykh Sayyid Saabiq katika kitabu chake Fiqhus-Sunnah J. 1 uk. 436 baada ya kuitaja kauli hiyo ya Mtume
(Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ameandika hivi:
"وهو خطاب عام لجميع الأمة فمن رآه منهم في أي مكان كان ذلك
رئية لهم جميعا ..."
“Na
kauli hii ni agizo la ujumbe linalojumuisha umma wote (wa Kiislam), kwa hivyo
yeyote miongoni mwao atakayeuona (mwezi-muandamo) popote pale; kuonekana huko
kutakuwa ni kwa wote…”
Kwa marejeo mengine zaidi kama haya
angalia:-
1. Rawaaiul-Bayan
J. 1, uk. 211
2. Naylul-Awttar
J. 4, uk. 195
3. Sharhu
Subulu Sawiyah Li Fiqhi Sunanil Marwiyah
4. Fatawa
ya BAKWATA uk. 110:.11 mada 14/70
Kuna baadhi ya watu kama ndugu yetu
Juma ambao wamejenga hoja ya kuwepo miandamo mingi ya mwezi kwa vile maneno ya
Ibnu 'Abbas (Radhiya Allaahu ‘Anhu) katika kisa cha Kuraib yalinyamaziwa.
Hakuna Sahaba yeyote aliyetoa kauli tofauti na ile ya Ibnu 'Abbas (Radhiya
Allaahu ‘Anhu). Jambo hilo limechukuliwa kama ni hoja kwamba Masahaba wote
walikubaliana na Ibnu 'Abbas (Radhiya Allaahu ‘Anhu).
Ni vyema kuelewa kuwa Wanavyuoni
wameigawa Ijma' kwenye sehemu mbili kuu:
i)
Ijma' Sariyh. الإجماع الصريح
ii) Ijma' Sukutii. الإجماع السكوتى
Ni Ijma' ambayo Jamhuri ya Wanavyuoni
wa Fiqhi wamekubaliana juu ya usahihi wake kwa vile iko wazi, haina utata
wowote. Hoja ya Ijma' hii ni madhubuti na yenye kukubalika zaidi mbele ya Umma
wa Kiislamu na wala hakuna khitilafu yoyote juu ya Ijma' hii.
Katika kuielezea Ijma' hii, Imam Shaffi
(Rahimahu Allaahu) anasema hivi:
لست
تقول ولا أحد من أهل العلم هذا مجتمع عليه إلا لما تلتقى عالما أبدًا إلا قاله لك
... (أصول الفقه – أبو زهرة)
Anachosema Imam Shaffi hapa, juu ya umuhimu
wa Ijma' hii kwa ufupi ni kuwa:
“Hakuna
yeyote atakayeweza kusema (juu ya umuhimu wa Ijma' hii Sariyh) kinyume na vile
ambavyo Wanazuoni wote walivyosema (kuhusu uzito wa Ijma' hii Sariyh). Kwa
maneno mengine ni kuwa: “Mwanachuoni yeyote atakayeonana naye na kumuuliza
uzito wa Ijma' hii Sariyh bila shaka jawabu ya Mwanachuoni huyo itakuwa ni ile
yenye kuthibitisha umuhimu wa Ijma' – Sariyh, kuliko Ijma' - Sukutiy katika
hoja.”
Ni makubaliano ambayo mmoja husema kitu
na wengine wakanyamaza wasimpinge.
Takriban ukiviangalia vitabu vyote vya Usulul–Fiqh kuhusu Ijma' hii Sukutiy utaona
kwamba ni Ijma' yenye khitilafu (mvutano) mkubwa, hakuna maafikiano ya pamoja.
Tofauti na Ijma'-Sariyhi ambayo ina
makubaliano yenye uzito wa hoja za kutegemewa katika misingi ya Shari'ah.
Chanzo cha khitilafu hizi katika Ijma' Sukutiy ni kule kupatikana ndani
yake utata; jambo ambalo huifanya hoja yake kuwa dhaifu. Kama kanuni ya Usulul-Fiqhi inavyosema:
“Dalili inapokuwa ina maana nyingi huporomoka
ushahidi wake.”
Shaykh Abu Zuhra amesema:
إنه
لا يصح أن يعتبر السكوت موافقة، لأن السكوت يحتمل أن سكوت الموافقة ويحتمل أنه سكت
لأنه لم يجتهد في الموافقة، ويحتمل أنه اجتهد ولم يئده اجتهاده إلى الحزم بشئ، ومع
كل هذه الإحتمالات لا يمكن أن يعتبر السكوت حجة..."
Ifuatayo ni tafsiri kwa njia ya maana:
“Ijma'
Sukutiy (makubaliano ya kunyamaza) ina khitilafu kubwa mbele ya Wanavyuoni wa
‘Usulul-Fiqhi.’ Kwa kuwa Wanavyuoni wengi hawakuizingatia Ijma' hii ni dalili
imara katika mas-ala ya kielimu. Al-Imam Shaffi ni miongoni mwa wale
wasioizingatia Ijma' hii kuwa ni hoja, kama alivyoeleza hayo mwanachuoni M. Abu
Zuhra katika kitabu chake cha Usulul–Fiqh. Sababu za msingi zilizoifanya Ijma'
hii kutokuwa hoja imara – kwa mujibu wa maelezo ya Abu Zuhra ni kule kupatikana
(ihtimaalat) tatanishi."
Shaykh Abu
Zuhra baada ya kutaja udhaifu huo aliendelea kusema:
“Kuwepo utata
mwingi ndani ya Ijma' hii Sukutiy inaifanya Ijma' hii kutozingatiwa kuwa ni
hoja.”
Kwa hivyo, Ijma' inayofaa kutangulizwa
katika mjadala wa kielimu ni Ijma' –Sariyhi na wala sio Ijma'–Sukutiy.
Ni vyema ieleweke pia, kwenda kinyume
(kuikhalifu) Ijma'-Sukutiy sio
makosa wala mtu haambiwi kuwa amefanya jambo la ufasiki kama alivyosema Shaykh
Saalimiy:
“Mwenye
kukhalifu (kwenda kinyume na) Ijma' – Sukutiy haiambiwi kuwa ametenda kosa la
ufasiki.”
Naye Shaykh Abu Zuhra katika kueleza
rai zilizopo juu ya Ijma'-Sukuty na kuonesha uzito wa hoja katika ljmai-Sariyhi
amesema ifuatavyo:
“Rai nyengine
inasema (hii Ijmai-Sukuty) nayo ni Ijma' lakini sio sawa (katika uzito wa hoja)
kama ilivyo Ijma'-Sariyhi.”
Kutokana na miongozo sahihi ya
Wanazuoni wa fani ya Usulul-Fiqhi
tumeelewa kuwa: Ijma'-Sariyhi
ndiyo yenye uzito wa hoja, na hakuna khitilafu juu ya jambo hilo. Pia
tumejifunza kuwa kwa upande wa Ijma'-Sukutiy
ni Ijma' yenye mzozo mbele ya Wanazuoni kutokana na kupatikana ndani
yake tatanishi (Ihtmaalaat).
Kwa maana hiyo hapawezi kutegemewa
Ijma'-Sukutiy kama ni hoja katika mjadala wa khitilafu za miandamo ya mwezi.
Miongoni mwa Wanavyuoni ambao hawakuzingatia Ijma' hii kuwa ni hoja; mmoja wao
ni Imam Shaffi (Radhiya Allaahu ‘Anhu) kama ilivyoelezwa katika kitabu cha Abu
Zuhra.
Neno 'Arafah au 'Arafah
ni jina linalotokana na uwanja au viwanja maalum vilioko nje kidogo ya
Mji Mtukufu wa Makkah. Mahujaji wote ambao wamehirimia kutekeleza Ibada ya
Hijja hukusanyika katika viwanja hivyo. Jambo hilo la kwenda kusimama kwenye
viwanja hivyo kwa kuomba dua na kumtaja Allaah ni katika nguzo kubwa ya ibada
hiyo ya Hijja. Inampasa kila Hajji kusimama au kushiriki hata kwa muda mdogo
katika mchana huo.
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi
wa sallam) amebainisha hayo kwa kusema:
Jambo hilo linathibitisha kwamba mtu
yeyote asiyetekeleza ibada ya kusimama 'Arafah anapokuwa Makkah, atakuwa
hakuipata ibada hiyo ya Hijja.
Watu humiminika na kusimama kwenye
uwanja wa 'Arafah siku ya tarehe 9 -
Dhul-Hijjah ya kila mwaka. Ikumbukwe kwamba tarehe 9 hiyo ni ya huko
Makkah pahala ambapo inafanyika ibada ya Hijja wala siyo ya pahala pengine
popote duniani.
Ni vyema kuzingatia kwamba funga hii ya
'Arafah pamoja na 'Iyd yake ni vitu ambavyo havina mahusiano na kuandama kwa
mwezi kutokana na kila nchi inavyoona mwezi wake. Chanzo cha funga hii ya
'Arafah ni ule uhusiano wa ile siku ambayo Mahujjaji wanaposimama katika uwanja
wa 'Arafah. Ambapo jambo la kusimama 'Arafah linapatikana sehemu moja tu
ulimwenguni ambayo ni siku inayosadifu tarehe 9 - Dhul-Hijjah huko mji wa Makkah, sio tarehe 9 ya nchi nyengine
yoyote ile.
Kwa maneno mengine ni kuwa
tutakapotofautiana katika kufunga Siku
ya 'Arafah na 'Iydul–Hajj
itakuwa kama kwamba kila nchi ina uwanja wake wa 'Arafah na Makkah yake. Kwa
uthibitisho zaidi wa funga ya siku ya 'Arafah tunajifunza kuwa Mtume (Swalla
Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kila alipokuwa akieleza umuhimu wa siku
hii alitumia neno “siku” wala
hakutamka neno “tarehe.”:
Ama kwa mujibu wa maelezo ya ndugu yetu
Juma, kama kawaida yake yeye anaona kuitwa “Siku ya 'Arafah” haina maana kuwa lazima tufunge sawa na Saudia,
bali anaona kuwa hiyo ni “Idhaafatu-Tashriif”
(yaani kuitengeneza siku hiyo kwa ajili ya utukufu wa pahala hapo au kwa ajili
ya utukufu wa tokeo lenyewe).
Sisi kwa upande wetu tunamuuliza ndugu
Juma, Je yapo maandiko yoyote ya kilugha au ya kisheria yanayotufunza kuwa
pahala pakitumika “Idhaafatu-Tashriif”
huwa haparuhusiki tena kutoa mafunzo mengine yaliyomo ndani ya “idhaafa” hiyo? Tujuavyo sisi zipo Aya
nyingi za Qur-aan ambazo zimetumika ndani yake hiyo “Idhaafatu-Tashriif” lakini utakuta wanavyuoni wa tafsiri wametoa
mafunzo mengine yapatikanayo katika “idhaafa”
hizo.
Akaendelea ndugu Juma kutoa kikwazo
ambacho anaona kuwa haiwezekani kufunga siku ya 'Arafah sawa na tokeo lenyewe
huko Makkah kwa kisingizio cha kuwa kuna nchi zinazotofautiana kwa masaa mengi.
Kisha akasema:
((Na (kama) inavyojulikana kwamba
tafauti za kisiku zina athari zake kwa makubaliano ya Waislamu. Waliyo upande
wa mashariki, hakika wao wanaanza kufunga kabla ya waliyo upande wa magharibi
na wanafuturu kabla yao.))
Kama ni hivyo tofauti ni nchi zilizo
Magharibi kwa nchi zilizo za Mashariki zinatofautiana, sisi tunamuuliza ndugu
Juma vipi tena kwa nchi zilizo jirani kama vile Omani na Dubai, au Omani ya
Yemeni, Je! Kuna suala la Mashariki na Magharibi hapa? Au kama ni hivyo basi
mbona Juma hakubali uwezekano wa kufunga pamoja nchi zote za Mashariki kwa
wakati mmoja na zote za Magharibi kwa wakati mwengine?
Ndugu Juma ni vyema aelewe kwamba upo
uwezekano wa kufunga 'Arafah siku moja dunia nzima kama tulivyoelezea katika
kurasa za nyuma za kitabu hichi kwamba dunia nzima inashirikiana katika mchana
mmoja na inashirikiana katika usiku mmoja ingawaje kuna nchi zinazotanguliza na
nyengine zinazofuatia. Mfano nchi zote za Afrika zinaweza kushirikiana kufunga
siku moja kwani baadhi ya nchi za Afrika zinatofuatiana kwa masaa machache tu
sio usiku mzima wala mchana mzima.
Katika kitabu cha Shaykh Naaswir Bachuu
imeandikwa kwamba tofauti iliyopo kwa nchi za Kiislamu zilizo Mashariki ya
mbali kama Phillipines na Indonesia na zile zilizo Magharibi ya mbali kama
Al-Maghrib yaani Morocco ni tofauti ya masaa 9 tu. Kwa hivyo upo uwezekano wa
kitaalamu (Kijiografia) wa kuweza kufunga kwa pamoja katika siku hiyo hiyo
moja. Tofauti iliyopo ni ya masaa tu. Tunafunga siku moja sio wakati mmoja wala
sio dakika moja. Msisitizo upo katika kufunga siku moja sio kuanza wakati mmoja.
Ndugu Juma anasema: ((Utapolifahamu hili, utakuwa umefahamu
kwamba, siku ya kufunga ni tarehe tisa mfunguo tatu, sawa siku hio imeafikiana
na Arafa au imetafautiana,....))
[uk. 141]
Sisi tunamjibu kwamba: Sasa kama
anaruhusu kutafautiana, tena kwanini imeitwa ((Funga ya 'Arafah)) isiitwe “Funga ya tarehe 9”?
Kisha ndugu Juma anaamini kwamba: ((Arafa ni tokeo ambalo linatokea Makka tu, wakati Ramadhani ni
tokeo la dunia nzima.))
Kama kawaida yake ndugu Juma
anajikanganya kila mara, kama kweli anaamini kila nchi ifunge kwa muandamo wake
na 'Arafah, kila nchi ifunge kivyake, inakuaje tena Ramadhaan iwe ni ya dunia
nzima, 'Arafah iwe kila mtu na yake?
Hebu tuangalie hoja nyengine ya ndugu
Juma katika uk. 142 wa kitabu chake anapodai kunukuu maneno ya Shaykh
Al-'Uthayminiy, anaposema:
(("Na wakati wa mwezi (التَّوْقِيْتُ الشَّهْرِيُّ ) ni kama wakati
wa siku (التَّوْقِيْتُ الْيَوْمِيُّ).
Kama vile ambavyo miji inatafautiana katika kuanza kujizuia (na kula na
kunywa na jimai: yaani kuanza kufunga) na (inavyotafautiana katika) kufuturu
kwa siku (daily au يَوْمِيًّا),
basi vivyo hivyo inawapasa watafautiane katika kujizuia na kufuturu kwa
mwezi (monthly au شَهْرِيًّا).))
a) Suala
linakuja: Je! Kama anavyosema miji inatafautiana kufuturu kwa mwezi kama inavyotafautiana kwa siku. Sasa vipi katika nchi moja iliyo
kubwa kama Tanzania ambayo ina mikoa inayotafautiana kuanza kula na kunywa kama
Dar es Salaam na Kigoma? Je! Mbona haitafautiani kwa mwezi? Inafunga kwa
muandamo mmoja lakini Dar es Salaam na Kigoma zinatafautiana katika kuanza kula
na kunywa (kufuturu) kwa zaidi ya dakika 45?
b) Kwa
nini basi nchi kama Omani na Dubai zinatafautishwa katika kuangalia mwezi
wakati ambapo nchi hizo hazina tofauti kubwa katika kuanza kula na kunywa? Wala
hazina tofauti ya matlai wala masaa ya kuanza na kuingia kwa siku?
c) Tujuavyo
sisi nchi zote za Uarabuni zinapata usiku wao mmoja na mchana wao mmoja, kwa
hivyo hakuna shida yoyote katika kufunga 'Arafah siku moja kwa wote.
Shaykh Naaswir Khamiis 'Abdur-Rahmaan wa Mombasa Kenya ameandika kitabu
chake “Mwezi Ko-Ongo” na amethibitisha tofauti ya masaa baina ya nchi mbali
mbali mfano: "tofauti ya mji wa Mombasa na nchi ya magharibi ya mbali mwa Afrika
kama Algeria ni masaa mawili na dakika ishirini na nane (2:28)" - uk. 22.
Katika jambo la kuonesha ufinyu
aliokuwanao ndugu yetu Juma, ule wa kutokufanya uchunguzi wa kina katika
mas-ala haya, yeye anaamini kwamba jambo hili limeanzishwa na Shaykh Naaswir
Bachuu na wala halikuwepo ulimwenguni kama anavyodai mwenyewe kwa kauli yake
ifuatayo:
((Ninasema: Enyi walimwengu wenzangu tazameni
hoja za kielimu hizo!!!!!!! Kwani nyinyi Wazanzibari kabla ya kuja fikra hio ya
Sheikh Nassor Bachoo ya kufunga kwa muandamo mmoja…))
Sasa sisi tunataka kumtihibitishia
ndugu Juma kuwa wapo watu wengi ambao pengine hawakuwafikiana na Shaykh Naaswir
Bachuu katika baadhi ya mambo au misimamo lakini kwa bakhti nzuri katika hili
suala la kufunga 'Arafah na kusali siku ya 'Iydul-Adh-ha wanafuata Makkah na wanaungana na ulimwengu mzima.
Mfano mzuri kabisa ni ndugu zetu wa Tarika ya Kadiria, takriban wote wanafunga
'Arafah kwa kufuata tarehe 9 - Dhul-hijjah ya Saudia (Makkah). Hayo
yanathibitishwa na aliyekuwa kiongozi wao Mkuu wa Tarika hiyo mwanachuoni
maarufu Al-Marhuum Shaykh Muhammad Naaswir Abdulla Al-Qaadiry ambaye aliandika
kitabu alichokiita: “Kitabu 'Arafah”
na kuandika kwenye gamba la kitabu hicho kwamba:
“Nguzo Kubwa
Ya Hijjah Ni 'Arafah Tarehe Tisa Mfunguo Tatu Na Kuswali 'Iydul-Hajj Sawa Na
Makkah.”
Katika uk. 22 wa kitabu chake hicho pia
ameandika kama ifuatavyo:
“Waislamu wote ulimwenguni wafunge
Sunnah ya 'Arafah sawa na 'Arafah ya Makkah.”
Kisha katika uk. 74 ameandika Fatwa zifuatazo:
“'Arafah ya
Makkah tarehe 9 mwezi wa Mfunguo Tatu (Dhul-Hajj) ndiyo 'Arafah ya Mwenyezi
Mungu (Subhaanahu wa Ta’ala) na ndiyo 'Arafah ya Waislamu wote popote walipo ulimwenguni.”
“Wananaokwenda
Hijja, kwao ni haramu kufunga siku hiyo ya 'Arafah huko 'Arafaati (Makkah) na
waliobaki majumbani, kwao ni Sunnah kubwa kufunga siku hiyo hiyo ya 'Arafah ya
Makkah kokote waliko ulimwenguni.”
“Tarehe 10
Mfunguo Tatu (Dhul-Hajj) ndiyo siku ya 'Iyd ya Mwenyezi Mungu (Subhaanahu
wa Ta’ala) na 'Iyd ya dunia nzima kwa Waislamu wote. Kufunga
siku hiyo yote kamili ni haramu. Anayeswali 'Iyd tarehe 10 ya Makkah
amefanikiwa na ole wake yule anayeswali 'Iyd siku atakayo mwenyewe. Kwa ujumla
kufunga tarehe 9 Mfunguo Tatu kwa Mahujaji 'Arafah ni Haramu. Na kufunga kwa
Waislamu wote ulimwenguni tarehe 10, 11, 12 na 13 Mfunguo Tatu ni Haramu.”
“Hivyo ni
jambo baya kabisa na lenye kutia huzuni sana kuwaona baadhi ya ndugu zetu
Waislamu wanaacha kufunga siku ya 'Arafah Aliyoiteua Mwenyezi Mungu (Subhaanahu
wa Ta’ala) na badala yake wanafunga siku ya kuchinja tarehe 10
(ya Makkah) wakisingizia kuwa ndiyo siku yao ya 'Arafah waitakayo wao
waliyoichagua wao wenyewe ambayo kufunga siku hiyo ni haramu.”
Ni vyema kujikumbusha kwamba maelezo ya
kisayansi yaliyopatikana kwenye Qur-aan Tukufu yanazingatia kwamba “Nyakati” hupatikana kutokana na
mipinduko ya jua, mwezi na dunia. Hapana shaka yoyote dunia ina mizunguko yake
miwili. Kwanza kuna ule mzunguko wa dunia kulizunguka jua, ambapo mzunguko huo
husababisha mabadiliko ya miongo (seasons) mbali mbali kama vile mchoo, vuli,
kipupwe au kiangazi. Pili ni ule mzunguko wa dunia kujizunguka yenyewe katika
mhimili wake, mzunguko huu wa pili ndio unaosababisha kupatikana usiku na
mchana. Kwa kawaida dunia hujizunguka yenyewe kamili kwa muda wa masaa 24
ambayo hupatikana siku moja yenye usiku mmoja na mchana mmoja.
Ni vyema ikumbukwe kwamba hakuna nchi
yoyote duniani iliyotafautiana na nchi nyengine katika kupata usiku kwa masaa
24. Nchi zote duniani zinashirikiana katika usiku mmoja pia zinashirikiana
katika mchana mmoja huo huo. Isipokuwa nchi nyengine hutangulia na nyengine
zitafuatia nyuma.
Sasa tukirudi nyuma katika maelezo ya
ndugu Juma katika kuelezea Laylatul-Qadri kwa kupitia fani hii ya Jiografia
anaeleza kama ifuatavyo:
((Sasa nchi ambazo zimepishana na Makka
kwa masaa 12 au zaidi hazitopata nazo LAILATUL-QADRI, kwani LAILATUL-QADRI
mwisho wake ni kuchomoza Alfajiri kama Qur-an ilivyosema, na wakati huu kuna
nchi bado ni jioni. Sasa vipi hawa wao hawamo au na wao watapata zamu yao
baadae?))
Hayo tumeshayaeleza sana kwamba hakuna
nchi iliyopishana na nyengine kwa masaa zaidi ya 12. Wala hakuna nchi ya
Kiislamu iliyopishana na nchi nyengine ya Kiislamu kwa zaidi ya masaa 9.
Kama kweli ndugu Juma anaelewa mambo,
ingekuwa jambo la busara akaeleza kwa mfano nchi zote za Kiarabu zina tofauti
gani ya usiku au mchana? Au Ulaya (Europe) nzima ina tofauti gani katika kupata
usiku au mchana wao? Huku akizingatia kwamba kuna nchi moja kama Canada iliyo
na ukubwa kuliko bara zima la Ulaya.
Mara nyinyi tumekuwa tukimfahamisha
ndugu Juma kuwa anapojadili jambo lililoambatana na fani fulani basi alijadili
jambo hilo kwa kupitia njia sahihi zenye kukubalika kwa mujibu wa fani hiyo.
Hususan anapojadili mas-ala ambayo yanahitaji madondoo muhimu kuliko maneno
matupu. Kwa uchunguzi zaidi juu ya maelezo ya ndugu Juma tutakuta kuwa hakuweza
kutoa ushahidi wa kina hasa anapoelezea tofauti iliyopo katika kutofautiana na
baadhi ya nchi juu ya suala zima la
kuingia usiku na mchana.
Kuhusu Laylatul-Qadri: Bila shaka ni usiku mmoja unaotokea mara moja kila
mwaka katika mwezi wa Ramadhaan. Hayo yanathibitishwa na Mwenyewe Allaah (Subhaanahu
wa Ta’ala)
pale Anapoeleza asili ya siku yenyewe katika Qur-aan Tukufu pale aliposema:
{{Hakika tumeiteremsha (Qur-aan) katika
Laylatul-Qadri (usiku wenye heshima kubwa), (usiku wa mwezi wa Ramadhaan).}} (87: 1)
Katika kuifasiri Aya hii, Shaykh
Abdallah Al-Farsy ametoa maelezo yafuatayo:
“Qur-aan kama
ijulikanavyo ilikuwa ikiteremshwa kidogo kidogo, basi siku ile iliyoanza
kuteremshwa ilikuwa katika Laylatul-Qadri (usiku wenye heshima kubwa). Ndio
ikaambiwa kuwa Qur-aan imeteremshwa katika Laylatul-Qadri, ni usiku mmoja
mtukufu umo katika mwezi wa Ramadhaan, ambao umebarikiwa kuliko miezi alfu,
yaani mtu akifanya amali njema katika usiku huo hupata thawabu kama za mwenye
kufanya amali ile kwa zaidi ya miezi elfu, na mwenye kufanya maovu naye hupata
dhambi za mwenye kufanya maovu kama yale kwa zaidi ya miezi elfu. Na Mwenyezi
Mungu Ameuficha usiku huu haujulikani ni upi, ili watu wajitahidi kufanya Ibada
katika mwezi mzima wa Ramadhaan; lakini watarajiwa zaidi kuwa katika kumi la
mwisho na hasa usiku wa kuamkia mwezi 23, 25, 27 na 29. Basi atakaye kujua
yakini kuwa ameupata usiku huu, bila ya shaka, inamlazimu ajipinde na kufanya
ibada mwezi mzima. Wala si lazima kwa mwenye kuupata usiku huu kuona alama
yoyote.”
Kisha Shaykh Abdallah Al-Farsy
akabainisha maneno kama hayo alipokuwa akiifasiri Suratud-Dukhaan kama
ifuatavyo:
{{Kwa yakini tumeiteremsha (Qur-aan) katika usiku
uliobarikiwa… Katika (usiku) huu hubainishwa kila jambo la hikima.}} (44: 3, 4)
Shaykh anaendelea kusema:
“Hii ‘Laylatin Mubaarakatin ….. Fiyhaa
yufraqu Kullu amriin Hakym.” Dhahir Shahir hapa kuwa siku hii imo katika mwezi
wa Ramadhaan kama yalivyobainishwa haya na Mwenyewe Mwenyezi Mungu katika Aya
ya 185 ya Suratul-Baqarah.”
Ndugu yetu Juma yeye bado anahoji:
((Sasa nchi ambazo zimepishana na Makka
kwa masaa 12 au zaidi hazitopata nazo LAILATUL-QADRI, kwani LAILATUL-QADRI
mwisho wake ni kuchomoza Alfajiri kama Qur-an ilivyosema, na wakati huu kuna
nchi bado ni jioni. Sasa vipi hawa wao hawamo au na wao watapata zamu yao
baadae?))
Sisi tunapenda kumuelimisha ndugu Juma
kama ifuatavyo:
Tunajifunza katika Aya za Qur-aan
tulizozitaja kwamba Laylatul-Qadri ni
usiku mmoja tu kwa ulimwengu mzima.
Mwenyezi Mungu Mtukufu (Subhaanahu
wa Ta’ala)
Anauadhimisha usiku huo kila mwaka mara moja ndani ya usiku huo kwa amani na
baraka nyingi.
Hakuna aliyesema kuwa usiku huo hutokea
Makkah pekee au kwamba watu wote waitafute Laylatul-Qadri kwa usiku wa Makkah.
Kinachozungumzwa hapa ni kwamba usiku huu ni mmoja kwa dunia yote ingawaje kuna
nchi zenye kutangulia kabla ya nyengine. Labda ndugu Juma amechanganyikiwa
baina ya usiku wa Laylatul-Qadri na
'Arafah, ambayo ilizungumzwa
kwamba ibada ya funga ya 'Arafah ina uhusiano wa moja kwa moja na Uwanja wa
'Arafah ulioko Makkah.
Kila eneo lina kupambazukiwa kwake na
alfajiri kama ilivyo katika hukmu ya kula daku na kuanza kufuturu linapozama
jua. Na hayo tumeshayaeleza sana kwamba hata katika nchi moja kubwa kuna
kutafautiana alfajiri zao. Kama Dar es Salaam linazama na kuchomoza jua kwa
zaidi ya dakika 40 kabla ya Kigoma.
Katika kuutetea msimamo wake wa kufunga
kwa kuzingatia “matlai”, Ndugu
Juma amejaribu kutoa hoja ya kutumia “Qiyaas”
cha “Ibada ya Swala” kwa “Ibada ya Swaum.” Kulinganisha kwake
huko, Ndugu Juma anatoa taswira ya kuwa: “Kama ilivyokuwa hatuwezi kuswali kwa kufuata machweo ya jua ya nchi ya
mbali, vile vile hatuwezi kufunga kwa kufuata nchi nyengine yoyote ile.”
Sisi kwa upande wetu tunapenda
kumzindua ndugu Juma kwa haya yafuatayo:
i). Kwanza hakuna mwanachuoni
anayekubalika aliyewahi kutumia “Qiyaas”
cha wakati wa Swala kwa wakati wa Swaumu katika mas-ala haya
ya kuandama kwa mwezi.
ii).
Pili tunapenda kumfahamisha ndugu Juma kwamba ziko nchi nyingi
zinazofuata kama huo msimamo wake ambazo zinashirikiana kufunga siku moja,
lakini haziswali wakati mmoja wala hazili daku wakati mmoja. Mfano nchi za
Tanzania, Kenya na Uganda zinafunga siku moja lakini haziswali wakati mmoja.
Wakati wa Swala kama ya “Adhuhuri” ya Dar es Salaam ni tofauti kabisa na wakati
wa “Adhuhuri” ya Kampala.
iii).
Wanavyuoni wanakubaliana kwamba kila eneo lina wakati wake wa kuanza kufuturu (kufungua
Swaum) wakati wa magharibi linapozama jua, wakati wa kujizuilia kula daku
inapokaribia alfajiri na pia kila eneo litatekeleza ibada ya swala zake zote
tano kwa kuangalia mipinduko ya jua.
Na hata kama yupo mwanachuoni aliyesema
kuwa Hadiyth fulani inawaruhusu watu wa nchi fulani ambapo wengine haiwaruhusu,
maneno hayo pia hayawezi kuchukuliwa kama ni hoja sahihi na yenye mashiko madhubuti kwa sababu
zifuatazo:
Kwanza: Hadiyth zote zilizotaja wajibu
wa kufunga na kufungua zimekuja kwa matamko ya kujumuisha Waumini wote popote
walipo. Na kanuni ya Usulul-Fiqhi inatufahamisha tuendelee kushikamana na 'aam (عام)
mpaka
ipatikane Khaas (
خاص).
Pili: Kutegemea maneno, matupu ya
mwanachuoni kama ni Khaas (خاص) bila ya kuonyesha
dalili zenye kukubalika kifani, huo utakuwa ni udhaifu.
iv). Tunapenda kusisitiza maneno yetu
ya nyuma ya kwamba cha msingi ni kufunga Swaum na kufungua siku moja kwa Waislamu wote sio
kufunga au kufungua kwa saa au dakika
moja.
v). Haiwezekani kutumika “Qiyaas” cha Swala na Swaum katika
misingi ya Shari'ah kwani kwa hapa patakosekana nguzo za kufanyia “Qiyaas.” Ni vyema tuelewe kwamba “Qiyaas” hutumika pale tu ambapo
hakuna Aya wala Hadiyth juu ya jambo hilo. Shar'iah ya Usulul-Fiqhi inasema ifuatavyo:
1. لا قياس مع وجود النصوص الصرحية.
2. إذا وجد النص فلا للقياس.
Kanuni zote hizo mbili zina maana ya
kuwa: “Qiyaas” hakitumiki kwa
kuwepo dalili za uwazi (yaani: Qur-aan na Hadiyth). Na jambo hili la muandamo
wa mwezi limetajwa wazi katika Hadiyth nyingi za Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi
wa aalihi wa sallam).
Wala huwezi kusema kila nchi itaswali wakati mmoja kwani kuna baadhi ya
nchi moja kama ambayo ni kubwa sana, yenyewe ina tofauti ya masaa mengi kutoka
eneo moja kwenda jengine.
Katika kejeli zake ndugu Juma kwenye
hoja za Kidini, hata katika maneno ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi
wa sallam) anathubutu kuyaumbua kwa kusema kama ifuatavyo:
((Hoja nyengine – ya mitaani – inasema kwamba Ramadhani
inapoingia hupatikana rehema fulani. Miongoni mwa hizo ni kuwa mashetani wote
hufungwa kama Bwana Mtume (s.a.w.) alivyosema: "Ramadhani ikiingia,
milango ya mbingu (na katika riwaya ya pili) milango ya pepo hufunguliwa, na
milango ya jahannam hufungwa na
mashetani hutiwa minyororo." Na
Hadithi nyengine inasema: "Inapoingia siku ya kwanza ya Ramadhani upepo
hupiga chini ya Arshi kutoka katika majani ya pepo (kuwapiga upepo huo)
Mahuru-Al-ain."))
Maneno kama haya ya kuyakejeli na
kuyabeza maneno matukufu ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)
na kuyafanya kama kwamba ni maneno ya mitaani au kuifanya haki kuwa batil ni
katika mambo yanayompelekea mtu kuingia katika kufru.
Kitu cha msingi ni vyema kukumbuka
kwamba Shaykh Naaswir Bachuu hakuonesha lugha za kashfa na kejeli hata katika
yale maeneo ambayo hakukubaliana nayo basi pia alitumia lugha ya kistaarabu.
Tukirudi katika mafunzo ya Mtume
(Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) juu ya kufungwa kwa mashetani
tunazingatia juu ya kuingia kwa mwezi wa Ramadhaan, kwani maneno ya Mtume
(Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) yamekuja katika matamko yasemayo:
((Inapoingia
siku ya mwanzo ya Ramadhaan mashetani hufungwa…))
Ndugu Juma akiendelea kudai kwamba:
((Ikiingia Ramadhani" ni sawa sawa
na kusemwa: "Ikiingia J/tatu" au kusemwa "Ukiingia
usiku" na hii haina maana kwamba J/tatu ikianza kuingia sehemu moja
huwa imeingia dunia nzima: bali ikianza kuingia sehemu moja – yaani baada ya
kutua jua magharibi – sehemu nyengine bado ni J/pili asubuhi.))
Hayo ndio kama yale tunayomueleza ndugu
Juma kila mara kwamba Suala la kutangulia mchana au usiku sio hoja katika
mas-ala ya muandamo wa mwezi. Hilo ni jambo lisilowezekana kutumia “Qiyaas” cha mwezi na jua. Hapawezekani kutumiwa “Qiyaas”
cha Swala, kuanza kufutari wakati wa magharibi au nyakati za kula daku kabla ya
alfajiri hata katika nchi moja kuna kutafautiana katika kuingia mchana na usiku
pia kuna kutafautiana katika kuingia “siku.”
Tuchukulie mfano Dar es Salaam inaingia katika siku ya Jumapili pale jua
linapotua, wakati huo huo Kigoma bado iko katika siku ya Jumamosi jioni. Lakini
kumbuka kwamba wanafunga siku moja ya muandamo wa mwezi mmoja. Tukichukua mfano
mwengine wa nchi kubwa kama Canada au Urusi, ndani ya nchi hizo kuna tafauti ya
masaa mengi kutoka mashariki hadi magharibi zake.
Akiendelea kutoa hoja zake ndugu Juma
juu ya kufungwa kwa Mashetani anahoji: ((Na kipi kinatujuilisha sisi kwamba
mwezi ukiandama sehemu moja hufungwa mashetani wa dunia nzima au kila mahala
hufungwa mashetani kwa mujibu wa muandamo wa mwezi wa mahala hapo?)) Hapa Ndugu Juma amekuja na dhana
kwamba mashetani hufungwa pale tu ilipoingia Ramadhaan. Na sisi tunamuuliza ni
wapi ameona kuwa ikiingia Ramadhaan hufungwa mashetani wa sehemu hiyo tu
iliyoandama mwezi?
Tujuavyo sisi ni kuwa tamko la (الشياطين ) “Ashshayaattwiinu”
kwa hapa lina maana ya mashetani wote dunia nzima. Tamko lililokuja katika
Hadiyth ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuhusu kufungwa
kwa mashetani inapoingia siku ya mwanzo ya Ramadhaan yaani وصفدت الشياطين ,
lina “Alif na Laam” (ال) ambayo linaonesha ni
tamko la umumi ('aam) (
عام
). Neno الشياطين ni
اسم الجنس na kawaida ya neno “Ismul-jinsi” اسم الجنس linawakilisha maana ya ('aam) (عام) yaani linazungumzia
“ujumla” au “wote”.
Baadhi ya vitabu vilieleza kwamba
“Ismul–jinsi” اسم
الجنس kuwa ni ('aam) (عام) ni hivi vifuatavyo:
195-196
|
صفحة........
|
مذكرة
فى أصول الفقه – محمد الأمين
|
1)
|
82, 83, 84
|
صفحة........
|
كتاب
شرح طلعة الشمس على الأفية
|
2)
|
329
|
صفحة........
|
الإحكام
فى أصول الأحكام - الآمدى
- الجزء الثابى
|
3)
|
307
|
صفحة........
|
الوجيز
فى أصول الفقه - د – عبد الكريم زيدان
|
4)
|
148
|
صفحة........
|
أصول
الفقه - لشيخ محمد الحضر مى
|
5)
|
المفصل فى علوم البلأغة
|
6)
|
||
معارج
الأمال على مدارج الكمال - الجزء الأول
|
7)
|
||
165
|
صفحة........
|
أصول
الفقه - محمد أبوزهرة
|
8)
|
62
|
صفحة........
|
كتاب
أصول الفقه للسنوات المتوسطة - تاليف آدود ابرهيم
|
9)
|
207
|
صفحة........
|
علوم
الشريعة - السنة الثالثة
|
10)
|
Ni vyema kuelewa kuwa msimamo wa Shaykh
Naaswir Bachuu katika kitabu chake ni kuwataka Waumini wote wafunge na kufungua
kwa “Siku moja” na msimamo wake huo unatokana na Hadiyth sahihi ya Mtume
(Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) isemayo na watu wote kwamba: ((Fungeni
kwa kuonekana mwezi – muandamo.))
Maneno hayo ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi
wa aalihi wa sallam) yanawajumuisha Waumini wote, popote walipo kama
tulivyokwisha elezea hayo katika kurasa zilizopita. Kwa upande wa utekelezaji
wa kufunga na kufungua kwa dunia nzima siku moja, uwezekano huo pia upo kama
tulivyokwisha elezea kwa urefu.
Baada ya maelezo kama hayo: Ndugu Juma
anatoa hoja za kutokuwepo uwezekano huo kwa kutoa mifano tofauti kama ifuatayo:
((je mtu aliyepanda ndege siku ya
J/pili – mathalan – ikamkuta magharibi humo katika ndege katika sehemu fulani
ya anga ya dunia akafuturu, kisha baada ya saa moja au mbili akaingia katika
anga ya nchi nyengine bado ni saa 9 za jioni ya siku hio hio ya J/pili, funga
yake itakuwaje: je ataambiwa kafunga huyu siku ya J/pili au kafunga nusu ya
siku hio katika sehemu moja ya dunia na kala katika sehemu nyengine ya dunia? Tena
mara ya pili: je mtu aliyepanda ndege akaanza kusali Adhuhuri humo
katika sehemu ambayo jua tayari limetenguka au akasali magharibi katika sehemu
ambayo jua tayari limezama na kabla ya kumaliza ikawa ndege imeingia katika
sehemu ambayo jua bado halijatenguka au halijazama, je yule aliyesali
Adhuhuri ataambiwa kasali Adhuhuri au kasali nusu adhuhuri na nusu Dhuha?!))
Jawabu yetu kwa ndugu Juma ni pale pale
kwamba:
a). Hayo ni mas-ala ya Ijtihaad kama
alivyotaja mwenyewe ndugu Juma kwenye uk. 168 wa kitabu chake. Ndio maana
hakuna kauli moja ya Wanavyuoni katika mas-ala hayo.
b). Ndugu Juma anapenda kutumia
“Qiyaas” cha Sala na Funga (Swaum) ambapo tumeshaeleza kwamba ni jambo
lisilokubaliana kabisa. Hayo tumeyaeleza sana, tatizo sio muandamo mmoja au
mingi, hata katika nchi moja inatokea, unaweza kusafiri kwa ndege ukasali
katika anga la Dar-es-salaam Adhuhuri ukafika Kigoma bado haijaingia Adhuhuri.
Je utasema Dar-es-salaam na Kigoma kila moja iangalie mwezi wake? Au kama
utaondoka Dar es Salaam umeshafuturu ukafika Kigoma jua halijatua bado
utafanyaje?
Kabla ya kuendelea na ufafanuzi zaidi
ni vyema kumnukuu ndugu Juma katika maelezo yake anaposema:
((Sasa cha muhimu kujua ni kuwa Dini ya
Kiislamu imeyagawa mambo katika sehemu nne kuu. Moja ni kitu
ambacho kimeelezwa katika Qur-an kwa uwazi. Pili ni kitu ambacho
kimeelezwa katika Sunnah (Hadithi) kwa uwazi. Tatu ni kitu
ambacho Umma umekubaliana juu ya kitu hicho. Mambo matatu haya hayafai
kupingwa: ni lazima tufanye vile vile ilivyoelezwa kwa uwazi. Sasa mambo
mengine (ambayo ndio ya nne) ni yale ambayo hayakuelezwa kabisa
au hayakufafanuliwa))
Kwa maelezo hayo mazuri aliyoyaeleza
ndugu Juma tungependa kumuuliza:
Je suala la kufunga na kufungua kwa
muandamo mmoja ataliweka wapi katika mafungu hayo? Bila shaka suala hili
litawekwa katika kifungu cha pili. Yaani Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa
aalihi wa sallam) amelieleza jambo hili kwa uwazi. Riwaya zote zilizokuja
katika agizo hili ni sahihi na zenye kukubalika mbele ya Wanazuoni wote wa
Kiislamu. Na riwaya zote hizo zimekuja kwa Waumini wote popote walipo
watekeleze agizo hilo. Mwanachuoni maarufu Al-Jassas katika kitabu chake
Ahkamul-Qur-aan J. I uk. 305 katika kuielezea kauli hii ya Mtume (Swalla Allaahu
‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema hivi:-
“Ni jambo
linaloeleweka kuwa kauli ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)
isemayo: ((Fungeni kwa kuonekana mwezi na fungueni
kwa kuonekana mwezi)), ni ya jumla inawahusisha watu wa pande zote za
dunia na kwamba haihusu watu wa nchi moja peke yao pasi na wengine.”
Kuna milango katika kitabu alichoandika
ndugu Juma ambayo hatukupenda kuizungumza, kwani ukichunguza utakuta maneno
yake yote yamejengeka katika dhana mbili. Moja ni ile kauli aipendayo kuikariri
kwamba ((Penye andiko huwa hakuna ijtihadi:)) Bila shaka andiko alilokusudia ni ile
kauli ya Ibnu 'Abbas (Radhiya Allaahu ‘Anhu) alipokataa mwezi wa Sham kwa
kusema: ((La! Hivi ndivyo
alivyotuamuru Mjumbe wa Mwenyezi Mungu(Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa
sallam)….))
Kwa upande wetu tumejaribu kuilezea
kifani kauli hii na tumeonesha kwa kutumia ushahidi mbali mbali juu ya udhaifu
unaopatikana katika kuitegemea kauli hiyo katika mas-ala haya.
Dhana ya pili ya ndugu Juma imejengeka
katika msingi dhaifu wala haina nafasi katika uwanja wa fani (kitaalamu) nao ni
kule kusukuma kwake juu ya elimu ya Jiografia. Umeonekana udhaifu wake hasa
pale alipokuwa akijaribu kuelezea tofauti iliyopo baina ya nchi na nchi katika
suala zima la kutofautiana kwa masaa na kuingia kwa usiku na mchana kwa baadhi
ya nchi.
Kwa upande wa suala hilo pia
tumeshalieleza na kulitolea mifano mbali mbali.
Mwisho tunachukua fursa hii kumuonya
ndugu Juma kuwa amuogope Mwenyezi Mungu hususan katika mas-ala ya kielimu.
Akumbuke kuwa Mwenyezi Mungu Ameonya juu ya mtu kusema jambo au kufanya
asilolijua. Aelewe kwamba ataulizwa juu ya hilo.
Lingekuwa jambo la busara kama ndugu
Juma angalikubali kuuliza na kufanya utafiti zaidi juu ya mas-ala haya kama
agizo la Mwenyezi Mungu linavyotutaka.
{{وَلَا تَقْفُ مَا لَيْسَ لَكَ بِهِ
عِلْمٌ ۚ إِنَّ السَّمْعَ
وَالْبَصَرَ وَالْفُؤَادَ كُلُّ أُولَـٰئِكَ كَانَ عَنْهُ مَسْئُولًا.}}
{{Wala usifuate (ukipita ukiyasema au kuyafanya)
usiyo na ilimu (ujuzi) nayo. Hakika
masikio na macho na moyo, hivyo vyote vitaulizwa.}} (17: 36)
[1][1] Angalia Dar es
Salaam na Kigoma – Tanzania, wanafunga siku moja, wala Kigoma hawatizami mwezi
wao, wanafuata mwezi ulioonekana Dar es Salaam, lakini hawaswali kwa wakati wa
Dar es Salaam.
[2][2] Katika semina iliyofanyika Unguja juu ya
mjadala huu tarehe 22 - 23/5/1991, Mwanachuoni mmoja wa Kishia Sh. Ahmad Khatib
amethibitisha kutokuwepo kwa ‘Matlai–Qamar’
ndani ya Qur-aan.
[6][6] Angalia uk. 174 wa
kitabu chake: 'Ushahidi Uliowekwa Wazi Katika Suala La Miandamo', Chapa ya
kwanza.
[9][9] Kwa ufafanuzi zaidi, angalia kitabu cha
‘Kuandama Kwa Mwezi’ cha Shaykh Naaswir Bachuu uk. 9 - 13.
[11][11] Wanazuoni
wengi sana wameeleza sababu ya
kuteremshwa aya hiyo ni
kama tulivyoeleza hapo juu.
Lakini ndugu Juma anaona
riwaya hiyo siyo sahihi kwa
hivyo tunamuomba ndugu Juma atutajie
riwaya nyengine ambayo
yeye anaamini kuwa ni
sahihi.
No comments:
Post a Comment