Tuesday, June 24, 2014

FUNGA YA RAMADHAAN, HUKMU, FADHILA NA ADABU ZAKE







SAMMAHATU SHEIKH; IBRAHIM GHULAAM

بسم الله الرحمن الرحيم
الحمد لله رب العالمين   و الصلا ة  و السلا م  علي نبينا  محمد  وعلى آله  وصحبه,  و بعد:

UTANGULIZI.

Baada ya kumshukuru  Allah (Subhaanahu wa Ta'ala)  na kumtakia rehma na amani Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa sallam) pamoja na Ali zake na Maswahaba zake wote.

Basi kwa hakika Mwenyezi Mungu Mtukufu (Subhaanahu wa Ta'ala)  amejaalia kwa waja wake  miongo [misimu] ya kuzidisha ndani yake matendo mema  na Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Ta'ala)  huzidisha pia malipo ya matendo hayo kwa waja wake, na miongoni mwa miongo hiyo ni huu  mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Basi katika makala hii nitaelezea kwa ufupi  juu ya funga na yale yanayoambatana nayo ikiwa ni pamoja na  hukumu, fadhila na adabu zake.

Ninamuomba Allah (Subhaanahu wa Ta'ala)  awanufaishe waislamu kwa yale nitakayoyaelezea, na aturuzuku ikh-laswi [kutaka radhi zake pekee] katika matendo yetu yote,  amiiin.

Na kwake pekee ndio kwenye mafanikio ya dunia na akhera.

MAANA YA FUNGA

Neno swaumu ambalo ni funga katika lugha ya kiswahili,   kilugha lina maana ya  kujizuilia .
Ama katika sheria funga [swaumu] ni kumuabudu Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Ta'ala)  kwa kujizuilia na vyenye kufuturisha [kufunguza] kuanzia kudhihiri alfajiri  [ya pili] mpaka kuchwa [kuzama] kwa jua na kwa kunuilia kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Ta'ala) .

HISTORIA YA FUNGA

Kwa hakika funga si ibada ngeni, bali ni ibada iliyofaradhishwa kwa umati zilizotangulia na pia kufaradhishwa katika umati huu.
Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu: {{Enyi mlioamini! mmelazimishwa kufunga [saumu] kama walivyolazimishwa waliokuwa kabla yenu ili mpate kumcha Mungu}} (2:183).
Ama katika umati huu wa Muhammad (Swalla Allahu 'alayhi wa sallam) funga  ilifaradhishwa katika mwezi wa Shaabani mwaka wa pili baada ya hijrah (2H).

HUKUMU  YA FUNGA

Funga ya mwezi wa Ramadhani ni nguzo katika nguzo za Uislamu, nayo ni wajibu kwa dalili ya kitabu (Qur-aan), Sunnah na Ijmai (makubaliano) ya wanavyuoni wote wa Kiislamu.

1: Amesema Allah (Subhaanahu wa Ta'ala) : {{Enyi mlioamini mmelazimishwa kufunga (saumu) kama walivyolazimishwa waliokuwa kabla yenu ili mpate kumcha mungu.  Siku chache tu ( kufunga huko)...(Mwezi huo mlioambiwa mfunge) ni mwezi wa Ramadhani ambao imeteremshwa katika mwezi huo hii Qur-aani ili iwe uwongozi kwa watu, na hoja zilizo wazi wa uongozi na upambanuzi (wa baina ya haki na batili) Atakae kuwa katika mji  katika huu mwezi (wa Ramadhani)afunge. …}(2:183-185) .

2: Na imepokewa hadithi  kutoka kwa Abdullah ibn ‘Umar (radhiya Allahu 'anhuma)  amesema : Nimemsikia Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa sallam) akisema: “Umejengwa Uislamu juu ya nguzo tano; kushuhudia ya kwamba hakuna Mola anayestahiki kuabudiwa kwa haki isipokuwa Allah (Subhaanahu wa Ta'ala)  na kwamba hakika ya Muhammad (Swalla Allahu 'alayhi wa sallam) ni mtume wa Allah(Subhaanahu wa Ta'ala)  na usimamishaji Swalah na utoaji zakah na kuhiji katika nyumba (tukufu) ya alkaaba na funga ya ramadhani. (Al Bukhariy na Muslim).

Na kuna hadithi nyingine nyingi zinazojulisha wajibu huo, na  wanavyuoni wote wamewafikiana juu ya uwajibu huo.

INAE MUWAJIBIKIA FUNGA YA RAMADHANI

Funga ya Ramadhani inamuwajibikia kila Muislamu, baleghe, mwenye akili, alie katika mji wake (asiwe msafiri), mwenye siha (afya- asiwe mgonjwa), asiwe na mambo yanayozuia kusihi kwa funga (kama hedhi na nifasi kwa wanawake).
*Na inatakikana kwa wazazi kuwafundisha kufunga watoto wao wanapofikia umri wa miaka  saba (7) na kuwalazimisha hadi ikibidi kuwapiga wanapofikia umri wa mika kumi (10), na hili inabidi pia kuzingatia afya na ukuaji wa mtoto.

NYUDHURU ZA KUFUNGA

Nyudhuru za kuacha kufunga zinatofautiana na kila udhuru una hukumu yake, na hapa nitazielezea  nyudhuru hizo kwa ufupi.

1- Hedhi (damu ya mwezi) na nifasi (damu ya uzazi), huu ni udhuru ambao unamlazimisha mwanamke kuacha kufunga, na inakuwa haramu kwake funga na iwapo atafunga haitosihi    
(haitokubaliwa) funga yake, na ni wajibu kwake kulipa funga hiyo.

2- Maradhi au Safari. Na mwenye udhuru wa maradhi (yanayotibika kwa kawaida) pamoja na msafiri wanaruhusiwa kutokufunga na itawawajibikia kulipa. Amesema Allah (Subhaanahu wa Ta'ala) :{{Atakaye kuwa katika mji katika huu mwezi (wa Ramadhani) afunge. Na mwenye kuwa mgonjwa au safarini, basi (atimize) hisabu (ya siku alizoacha kufunga) katika siku nyingine. Mwenyezi Mungu anakutakieni yaliyo mepesi wala hakutakieni yaliyo mazito.. .}} (2:185).      Na kama maradhi yatazidi au kumletea madhara iwapo atafunga basi itakuwa lazima kwake kutokufunga.

*Ama safari ambayo inaruhusiwa kwa sababu yake kutokufunga wanachuoni wengi wemesema: Ni safari ya siku mbili kwa ngamia au kwa mwendo wa miguu (mar-hala mbili) ambayo ni sawa na umbali wa takiribani kilomita (85km). Na ruhusa hii inapatikana kwa msafiri anayesafiri kwa chombo cha aina yoyote atakachosafiria,ijapo kwa dhahiri safari hiyo haimpi uzito wowote.


3- Vizee (vikongwe) na wenye maradhi sugu (yasiotarajiwa kupoa). Na haya mawili iwapo yana msababishia madhara basi ni katika udhuru na ruhusa ya kuacha kufunga, na itamlazimikia atoe fidia kwa kumlisha masikini kibaba (mudi) cha chakula (ambacho ni sawa na na uzito wa gramu 600g takiribani)au chakula kinacho mshibisha masikini mmoja kwa kila siku aliyoacha kufunga.

4- Waja wazito na wanyonyeshaji.
Nao ni katika wenye ruhusa ya kutokufunga, na inawabidi kulipa siku walizoshindwa kufunga kwa sababu ya udhuru huo.

5:Iliemzidia njaa au kiu na akahofia kuangamia, huu pia ni katika udhuru wa kuacha kufunga, bali wamesema wanachuoni kwamba: yule mwenye kuhofia kuangamia inakuwa kwake ni wajibu kufungua, na itamuwajibikia kulipa kama mgonjwa.

NGUZO ZA FUNGA

1- Nia nayo ni kukusudia kufunga usiku wa kuamkia funga, kwa funga ya faradhi.
2- Kujizuilia na vyenye kufunguza (kufuturisha).
3- Muda wa kufunga (mchana kuanzia alfajiri mpaka kutwa (kuzama) kwa jua).

UNAVYOTHIBITI KUINGIA MWEZI WA RAMADHANI

1- Kwa kukamilika siku thelathini (30) za mwezi wa shaabani.
2- Kwa kuonekana mwezi mwandamo siku ya  29 ya mwezi wa Shaabani, imepokewa hadithi na Abu Hurayrah (radhiya Allahu 'anhu)  kwamba Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa sallam) amesema: {Fungeni kwa kuonekana kwake (mwezi mwandamo) na fungueni kwa kuonekana kwake} (Al Bukhariy na Muslim).
*Na mwezi wa kuingia Ramadhani inatosha kuonekana na Muislamu mmoja mwadilifu ama mwezi wa kumalizika Ramadhani ni lazima uonekane na Waislamu waadilifu wawili au  zaidi.

YANAYO BATILISHA (KUHARIBU) FUNGA

1- Kula au kunywa  kwa kukusudia.
2- Kila kinachoingia tumboni au kooni kwa kukusudia.
3- Kukutana kimwili (kuingiliana) kati ya mume na mke.
4- Kujitoa manii (mbegu za uzazi) au kusababisha kutokwa na manii (kwa kujichezea sehemu za siri, kukumbatiana au kupigana mabusu nakadhalika).
5- Kujitapisha kwa makusudi. Imepokewa hadithi kutoka kwa Abu Hurayrah (radhiya Allahu 'anhu)  amesema: amesema Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa sallam): {...na mwenye kujitapisha basi inamuwajibikia kulipa.}
(wameipokea maimamu watano).

6- Kutokwa na damu ya mwezi (hedhi) au damu ya uzazi (nifasi).

*Wakati wowote yanapomtokea mwanamke mawili hayo funga yake ya siku hio itakuwa imeharibika na itamlazimikia kuilipa siku hio baada ya mwezi wa Ramadhani.

YASIO FUNGUZA

1- Kula au kunywa kwa kusahau.Imepokewa hadithi kutoka kwa Abu Hurayrah amesema, amesema Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa sallam): {Mwenye kusahau nae amefunga, basi akala au akanywa na aikamilishe funga yake….} ( Al Bukhariy na Muslim ).

2- Kusukutua au kupandisha maji puani wakati wa udhu (bila ya kubalighisha).

3- Kuoga au kujiburudisha kwa kujimwagia maji katika kiwiliwili (hasa katika maeneo yenye joto kali).

4- Kuonja chakula kwa mpishi (kwa sharti ya kutokumeza alichokionja).

5- Kutokwa na mbegu za uzazi (manii) katika usingizi (ndoto) au bila ya kukusudia.

6- Kuamka na janaba. Imepokewa hadithi kutoka kwa Mamama `Aishah na Ummu Salamah (radhiya Allahu 'anhuma)  kwamba Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa sallam) alikuwa akiamka na janaba kutokana na kukutana kimwili na wake zake, kisha anaoga na kufunga (Al Bukhariy na Muslim).

7- Kupiga mswaki (wakati wowote).

8- Kuchoma sindano ya kawaida ya tiba.

9- Kung`oa jino na mfano wake.

10- Mwanamke kuamka kabla ya kuoga kwa hedhi au nifasi.

ADABU ZA FUNGA

BAADHI YANAYOSUNIWA KWA MFUNGAJI

1- Kula daku. Imepokewa hadithi kutoka kwa Anas ibn Maalik (radhiya Allahu 'anhu)  amesema: amesema Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa sallam):  {Kuleni daku kwani hakika  chakula cha daku kina baraka ndani yake} (Al Bukhariy na Muslim).       

 *Na inasuniwa kuchelewesha kula daku mpaka kukaribia alfajiri.

2-Kuharakisha kufutari (mara tu likizama jua). Imepokewa hadithi kutoka kwa Sahl ibn Saad (radhiya Allahu 'anhu) , Hakika Mjumbe wa Mungu (Swalla Allahu 'alayhi wa sallam) amesema: {Watu watakuwa bado wapo katika kheri muda wa kuwa wanaharakisha futari}.( Al Bukhariy na Muslim).

*Na inasuniwa (kuanza) kufutari kwa tende au maji. Imepokewa  hadithi kutoka kwa Salmaan ibn`Aamir (radhiya Allahu 'anhu)  kutoka kwa Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa sallam)amesema: {Anapofutari mmoja wenu basi na afuturu kwa tende na kama hakupata (tende) basi na afutari kwa maji kwani hakika ya maji ni kitoharisho (kisafisho) ( Wameipokea Maimamu watano).

*Na pia inasuniwa kwa mfungaji kuzidisha kuomba dua na hasa wakati wa kufutari, kwani dua ya mfungaji na hasa wakati wa kufutari ni katika dua zinazokubaliwa na Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Ta'ala) .

BAADHI YANAYOTAKIWA AYAKITHIRISHE MUISLAMU KATIKA MWEZI WA RAMADHANI

1- Kisimamo cha usiku (Swalah ya tarawehe), amesema Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa sallam): {Mwenye kusimama (kwa ibada) katika mwezi wa Ramadhani kwa imani (thabiti) na hali ya kutaraji malipo toka kwa Allah (Subhaanahu wa Ta'ala)  husamehewa yale aliyoyafanya katika madhambi yake}. (Al Bukhariy na Muslim).

*Na inafaa kwa wanawake kuhudhuria Swalah katika misikiti maadamu watachunga na kufuata taratibu za dini (sharia),  amesema Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa sallam): {Msivizuilie vijakazi vya Mwenyezi  Mungu (wanawake) (kuhudhuria ibada) katika misikiti ya Mungu}.(Al Bukhariy na Muslim).      Na haifai kwa wanaume kuwazuilia wanawake walio katika usimamizi wao kuhudhuria ibada hizo bila ya kuwa na sababu za kimsingi zinazo kubalika kisheria, amesema Mtume(Swalla Allahu 'alayhi wa sallam): {wakiwaombeni ruhusa wanawake zenu kwenda msikitini basi waruhusuni}. (Muslim).

2- Kuzidisha kusoma Qur-aan.

Mwezi wa Ramadhani ni mwezi wa Qur-aan na ndio mwezi ulioteremshwa ndani yake Qur-aan, Amesema Allah (Subhaanahu wa Ta'ala): {{Hakika tumeiteremsha (Qur-aani) katika laylatul-Qadr (usiku wenye heshima kubwa), (usiku wa mwezi wa ramadhani).}} (97:1). Na {{(Mwezi huo mlioambiwa mfunge) ni mwezi wa Ramadhani ambao imeteremshwa katika (mwezi) huo hii Qur-aani…}} (2:185).

3- Sadaka. Pamoja na fadhila zake katika masiku yote huzidi fadhila na thawabu zake katika mwezi wa Ramadhani. Amesema Ibn ‘Abbaas (radhiya Allahu 'anhuma) : Alikuwa Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa sallam) mkarimu (mtoaji) na alikuwa mkarimu zaidi katika mwezi wa Ramadhani wakati anapokutana na Jibriyl (a.s.) (Al Bukhariy na Muslim).

*Na katika sadaka zinazotiliwa mkazo katika mwezi wa Ramadhani ni kuwafuturisha waliofunga, amesema Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa sallam): {Mwenye kumfutarisha aliyefunga anakuwa na malipo mfano wa malipo ya aliyemfutarisha na hayapungui malipo ya aliyefunga kitu chochote}. (Ahmad na Annasaiy).

4- Kufanya Umrah, amesema Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa sallam): {Umrah katika mwezi wa Ramadhani una malipo sawa na Hijjah}. (Muslim).

5- Itikafu (nako ni kubaki msikitini bila ya kutoka ukijishughulisha na ibada mbalimbali), inasuniwa kufanya itikafu na hasa katika kumi la mwisho la mwezi wa Ramadhani. Imepokewa hadithi kutoka kwa Ibn ‘Umar (radhiya Allahu 'anhuma)  amesema: Alikuwa Mtume(Swalla Allahu 'alayhi wa sallam) akifanya itikafu siku kumi za mwisho za mwezi wa Ramadhani.(Al Bukhariy na Muslim).

6- Kuutafuta usiku wa cheo (laylatul-qadr), na zaidi katika kumi la mwisho la Ramadhani, imepokewa hadithi kutoka kwa Mama ‘Aishah (radhiya Allahu 'anha)  amesema: Amesema Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa sallam): {Utafuteni usiku wa cheo (laylatul-qadri) katika siku kumi za mwisho za Ramadhani}   (Al Bukhariy na Muslim)  

Na amepokea Abu Hurayrah (radhiya Allahu 'anhu)  kutoka kwa Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa sallam) amesema: {Mwenye kusimama katika usiku wa cheo (laylatul-qadri) kwa imani thabiti na kwa kutaraji malipo kutoka kwa Allah (Subhaanahu wa Ta'ala)  husamehewa madhambi alioyafanya (kabla ya hapo)} (AlBukhariy na Muslim).

7- Toba. Nako ni kurudi kwa Allah (Subhaanahu wa Ta'ala)  kutokana na makosa aliyoyatenda mja na kuomba msamaha kutoka kwake, kujuta na kuazimia kutokuyarudia tena makosa hayo).

*Tukumbuke ya kwamba Mwanaadamu si mkamilifu daima yupo katika hatari ya kufanya makosa, sawa makosa hayo ikiwa ni makosa ambayo ameyahisi au hakuyahisi wakati wa kuyafanya kwake, toba ndio njia ya kujikosha na madhambi ya makosa hayo,na kipindi cha mwezi wa Ramadhani ni fursa muhimu ya kutubia.                             
* Ikiwa katika makosa yake kuna haki za wanaadamu inamlazimu kuzirejesha kwa wenyewe haki hizo.

FADHILA ZA FUNGA

Zimepokewa Hadithi nyingi sana zinazoelezea fadhila za funga ya Ramadhani, miongoni mwa hadithi hizo ni hadithi zifuatazo:

1- Amesema Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa sallam): {Mwenye kufunga Ramadhani kwa imani na kutarajia malipo (toka kwa Allah (Subhaanahu wa Ta'ala) ) husamehewa madhambi aliyoyatanguliza}. (Al Bukhariy na Muslim).

2- Na amesema Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa sallam): {amesema Allah (Subhaanahu wa Ta'ala) : Kila amali ya mwanaadamu (aifanyayo) ni yake, wema (mmoja) hulipwa kwa  mfano wake mara kumi mpaka mara mia saba, isipokuwa funga, hakika ya funga ni Yangu mimi, na Mimi najua namna gani Nimlipe kwa funga hiyo, ameacha matamanio yake na chakula chake na kinywaji chake kwa ajili Yangu, mfungaji ana furaha mbili, furaha wakati wa kufutari kwake na furaha nyengine  pale atapokukutana na Mola wake. Harufu yakinywa cha mfungaji inapendeza zaidi kwa Mwenyezi M ungu kuliko harufu ya miski}. (Al Bukhariy na Muslim).

YANAYOPASWA KUJIEPUSHA NAYO MFUNGAJI.

1-  Tabia chafu na maneno maovu, kama kusengenya, kusema uongo, na kadhalika.
2- Kuzidisha usingizi (kulala kupita kiasi) ambao unampotezea Muislamu fursa ya kufanya ibada zaidi.
3- Kupoteza wakati mwingi katika michezo na maongezi yasiyo na faida, na kuacha kuutumia wakati huo katika kazi na ibada mbali mbali.
4- Kuacha kula daku au kuchelewa kufuturu baada ya kutwa kwa jua.
5- Kufanya israfu katika vyakula na vinywaji wakati wa kufutari.
6- Kufutari kwa vyakula vyenye harufu ya kuchukiza, kama: vitunguu thaumu,vitunguu maji, doriani, na kadhalika kwa kuhofia kuwaudhi Waislamu wakati mnapojumuika  kwa Swalah.
7- Kutokuswali tarawehe kwa utulivu na unyenyekevu.

YANAYOTAKIWA KWA KUMALIZIKA RAMADHANI.

1- Kutoa zakatul-fitri,nayo ni wajibu kwa kila Muislamu, (mwanamume, mwanamke, mkubwa, mdogo, muungwana (huru) au mtumwa).*Watoto wadogo,Watumwa na pia Wanawake waliochini ya usimamizi wa Wanaume itawalazimikia zakah hio wasimamizi wao, ama Wanawake wanaojitegemea itawalazimikia wao wenyewe.

*Na inatakikana itolewe zakatul-fitri kabla ya Swalah ya iddi.

Imepokewa hadithi kutoka kwa Ibn ‘Umar (radhiya Allahu 'anhuma)  amesema: Amefaradhisha Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa sallam) Zaka ya fitri (ya kumalizika Ramadhani) pishi ya tende au pishi ya shairi kwa mtumwa na huru (muungwana), mume na mke, mdogo na mkubwa katika waislamu, na akaamrisha (hiyo zakah ya fitri) itolewe kabla ya kutoka watu kuelekea katika Swalah (ya iddi). (Al Bukhariy na Muslim).

*Na wajibu ni kutoa pishi ya chakula maarufu katika mji uliopo (ambayo ni sawa na uzito wa kilo mbili na gramu mia nne (2.4 kg) takribani kwa nafaka kama mchele na mfano wake) (au thamani yake kwa baadhi ya wanachuoni).

2- Takbir, inasuniwa kuleta takbir baada ya kuandama (kuonekana) mwezi wa kumalizika Ramadhani, kuanzia kuchwa (kuzama) kwa jua mpaka wakati wa Swalah ya iddi. Na inasuniwa kunyanyua sauti kwa wanaume njiani, masokoni na hata majumbani.

3- Swalah ya iddi, kwa wanaume na wanawake.

*Na inasuniwa ifanyike katika viwanja, na hata akina mama walio katika siku zao (hedhi) inasuniwa na wao wahudhurie ingawa wao hawatoshiriki katika kuswali.

4- Na inasuniwa kula tende kwa idadi ya (witri) au chakula chengine hafifu kabla ya kutoka kwa ajili ya Swalah ya iddi al-fitri.

5- Pia inasuniwa kubadilisha njia wakati wa kwenda na kurudi kwenye Swalah ya iddi. Imepokewa hadithi kutoka kwa Jaabir (radhiya Allahu 'anhu)  amesema: Alikuwa Mjumbe wa Allah (Swalla Allahu 'alayhi wa sallam) inapokuwa siku ya iddi akibadilisha njia (ya kwenda na ya kurudia). (Al Bukhary).

6- Kuvaa mavazi bora zaidi anayoyamiliki Muislamu.            
*Na inatakikana kwa wale wenye familia kuwaandalia mavazi mazuri watu wa familia zao (bila ya kufanya israfu).

7- Na pia inasuniwa baada ya kumalizika Ramadhani kufunga siku sita katika mwezi wa mfunguo mosi (shawwali). Amesema Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa sallam): {Mwenye kufunga Ramadhani kisha akaifuatilizia siku sita katika mwezi wa shawwali (mfunguo mosi) inakuwa kama aliyefunga mwaka (mzima kamili).(Muslim).

8- Na tukumbuke ya kwamba siku hii ya iddi inakatazwa (ni haramu) kufunga ndani yake. Imepokewa hadithi kutoka kwa Abu Said Al khudriy (radhiya Allahu 'anhu) :( Hakika Mjumbe wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allahu 'alayhi wa sallam) amekataza kufunga katika siku mbili: Siku ya (iddi) alfitri na siku ya (iddi) ya kuchinja (iddi l-adh`ha)).(Al Bukhariy na Muslim).

CHANZO; alhidaaya.com

No comments:

Post a Comment