Serikali ya Bangladesh imeendelea kuyakandamiza makundi yenye
mielekeo ya Kiislamu nchini humo kwa kutoa hukumu ya kifo dhidi ya kiongozi wa
chama kikubwa zaidi cha Kiislamu nchini humo.
Mahakama ya kufuatilia jinai za kivita ya Bangladesh imemuhukumu
kifo Motiur Rahman Nizami, mkuu wa chama cha Jamaat-e-Islami mwenye umri wa
miaka 71 kwa tuhuma za kufanya magendo ya silaha, kuhusika katika mauaji ya
umati, jinai na machafuko nchini humo.
Baada ya kutolewa hukumu hiyo, jeshi la polisi la nchi hiyo
limeimarisha ulinzi katika maeneo yote muhimu ya Dhaka, mji mkuu wa Bangladesh.
Kwa mujibu wa kanali ya 24 ya televisheni ya Bangladesh, ulinzi
umeimarishwa pia katika miji mingine tofauti ya nchi hiyo.
Wafuasi wa Motiur Rahman wanaamini kuwa, kiongozi wao huyo hana
hatia na kwamba serikali ya Bi Sheikh Hasina Wajed, Waziri Mkuu wa Bangladesh
inatumia vibaya idara ya mahakama kuwakandamiza wapinzani hususan viongozi wa
makundi ya Kiislamu kwa kuwatuhumu kufanya jinai za kivita.
Kabla ya kutolewa hukumu hiyo dhidi ya mkuu wa chama cha
Jamaat-e-Islami, mahakama ya Bangladesh ilikuwa imewahukumu kifo pia watu
wengine wanane akiwemo Mufti Abdul Hannan, mkuu wa chama kilichopigwa marufuku
cha Harkatul Jihadil Islami.
Bi Sheikh Hasina Wajed na chama chake cha Awami League ameendelea
kung'ang'ania madaraka ya nchi hiyo baada ya kuitisha uchaguzi uliojaa utata
ambao ulisusiwa na vyama vya upinzani na hivi sasa anafanya kila njia
kuhakikisha anawamaliza wapinzani wake wa kisiasa na kidini.
Hii ni kwa sababu sambamba na kutolewa hukumu ya kifo kwa
wanaharakati wa Kiislamu, ndugu wa kiume wa mmoja wa mawaziri wa zamani wa nchi
hiyo katika serikali ya Khaleda Zia, Waziri Mkuu wa zamani wa Bangladesh naye
alihukumiwa adhabu ya kifo jambo ambalo linaonesha wazi kuwa idara ya mahakama
nchini Bangladesh imeazimia kuwanyamazisha kwa kila njia wapizani.
Katika hatua ya mwanzo kabisa ya kuyakandamiza makundi na vyama vya
Kiislamu nchini Bangdalesh, Waziri Mkuu wa nchi hiyo Bi Sheikh Hasina Wajed
aliamua kukipiga marufuku chama pekee cha Kiislamu nchini humo cha
Jamaat-e-Islami na hivyo kuwazuia wanachama wa chama hicho kushiriki katika
uchaguzi wa Bunge wa mwezi Januari mwaka huu.
Moazzam Husain, Jaji wa Mahakama Kuu ya Bangladesh alitangaza kuwa
chama cha Kiislamu cha Jamaat-e-Islami kinaendesha shughuli zake kinyume cha
sheria katika mfumo unaopinga dini wa 'kisekula' unaotawala nchini Bangladesh.
Baada ya hapo serikali ya nchi hiyo ikaanza kuwaandama viongozi wa
chama hicho na kuwahukumu adhabu za kifo licha ya kukumbwa na malalamiko makali
ndani na nje ya nchi hiyo.
Ali Ahsan Muhammad Mojahed, kiongozi mwingine mwandamizi wa chama
hicho cha Kiislamu naye amehukumiwa kifo huku kiongozi wa kidini na kimaanawi
wa chama hicho, Sheikh Ghulam Azam naye akihukumiwa kifungo cha miaka 90 jela.
Baada ya kutolewa hukumu hizo, maelfu ya wananchi wa Bangladesh
walimiminika mabarabarani, na tayari zaidi ya watu 100 wameshauawa katika
machafuko yaliyozuka baada ya kutolewa hukumu hizo.
Mashirika ya haki za binadamu nayo yamelaani hukumu hizo na kusema
zinakanyaga sheria za kimataifa.
Makundi ya Kiislamu nchini Bangladesh yanaamini kuwa serikali ya
nchi hiyo inashirikiana na Marekani kujaribu kuyadhoofisha makundi hayo ya
Kiislamu na kutia nguvu fikra za kisekula na kilaiki za kupinga dini nchini
humo sambamba na kuchochea ufuska miongoni mwa wananchi.
Makundi hayo yanasema, ni kwa sababu hiyo ndio maana serikali Bi
Sheikh Hasina Wajed ikatumia Mahakama Kuu ya nchi hiyo kuvipiga marufuku vyama
vya Kiislamu na kutoa hukumu za kifo kwa viongozi wa vyama hivyo.
No comments:
Post a Comment