FUNGA
YA RAMADHANI, HUKUMU, FADHILA, NA ADABU ZAKE
Utangulizi
Sifa zote njema zinamstahikia Allah (Subhaanahu
wa Ta'ala) na sala na salamu zimfikie Mtume wake (Swalla Allahu alayhi
Wasallam) pamoja na ndugu na maswahaba zake.
Baada ya kumshukuru Allah (Subhaanahu
Wata'ala) na kumtakia rehma na amani Mtume Muhammad (Swalla Allahu alayhi
Wasallam) pamoja na ndugu zake na maswahaba zake wote, basi kwa hakika Mwenyezi
Mungu Mtukufu (Subhaanahu Wata'ala) amejaalia kwa waja wake miongo
[misimu] ya kuzidisha ndani yake matendo mema na Mwenyezi Mungu
(Subhaanahu wa Ta'ala) huzidisha pia malipo ya matendo hayo kwa waja
wake, na miongoni mwa miongo hiyo ni huu mwezi mtukufu wa Ramadhani.
Basi katika makala haya nitaelezea kwa
ufupi juu ya funga na yale yanayoambatana nayo ikiwa ni pamoja na
hukumu, fadhila na adabu zake.
Ninamwomba Allah (Subhaanahu wa Ta'ala)
awanufaishe Waislamu kwa yale nitakayoyaelezea, na aturuzuku ikh-laswi [kutaka
radhi zake pekee] katika matendo yetu yote, amiiin. Kwake pekee
ndiyo kwenye mafanikio ya dunia na akhera.
Maana ya Funga
Neno swaumu ambalo ni funga katika lugha ya
Kiswahili, kilugha lina maana ya kujizuilia. Ama katika
sheria, funga [swaumu] ni kumuabudu Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Ta'ala)
kwa kujizuilia na vyenye kufuturisha [kufunguza] kuanzia kudhihiri
alfajiri [ya pili] mpaka kuchwa [kuzama] kwa jua na kwa kunuilia kujikurubisha
kwa Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Ta'ala).
Historia ya Funga
Kwa hakika funga si ibada ngeni, bali ni ibada
iliyofaradhishwa kwa umati zilizotangulia na pia kufaradhishwa katika umati
huu. Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu: {{Enyi mlioamini! mmelazimishwa kufunga [saumu] kama
walivyolazimishwa waliokuwa kabla yenu ili mpate kumcha Mungu}} (2:183).
Ama katika umati huu wa Muhammad (Swalla Allahu
'alayhi Wasallam) funga ilifaradhishwa katika mwezi wa Shaaban mwaka wa
pili baada ya Hijrah (2H).
Hukumu ya Funga
Funga ya mwezi wa Ramadhani ni nguzo katika
nguzo za Uislamu, nayo ni wajibu kwa dalili ya kitabu (Qur-aan), Sunnah na
Ijmai (makubaliano) ya wanavyuoni wote wa Kiislamu.
1: Amesema Allah (Subhaanahu wa
Ta'ala) : {{Enyi mlioamini mmelazimishwa
kufunga (saumu) kama walivyolazimishwa waliokuwa kabla yenu ili mpate kumcha
mungu. Siku chache tu ( kufunga huko)...(Mwezi huo mlioambiwa mfunge) ni
mwezi wa Ramadhani ambao imeteremshwa katika mwezi huo hii Qur-aani ili iwe
uwongozi kwa watu, na hoja zilizo wazi wa uongozi na upambanuzi (wa baina ya
haki na batili). Atakayekuwa katika mji katika huu mwezi (wa Ramadhani)
afunge. …}(2:183-185) .
2: Na imepokewa hadithi kutoka kwa
Abdullah ibn ‘Umar (Radhiya Allahu 'anhuma) amesema: Nimemsikia Mtume
(Swalla Allahu 'alayhi Wasallam) akisema: “Umejengwa Uislamu juu ya nguzo tano;
kushuhudia ya kwamba hakuna Mola anayestahiki kuabudiwa kwa haki isipokuwa
Allah (Subhaanahu wa Ta'ala) na kwamba hakika ya Muhammad (Swalla Allahu
'alayhi Wasallam) ni Mtume wa Allah (Subhaanahu wa Ta'ala) na
usimamishaji Swala na utoaji zakah na kuhiji katika nyumba (tukufu) ya Alkaaba
na funga ya Ramadhani. (Al Bukhariy na Muslim).
Na kuna hadithi nyingine nyingi zinazojulisha
wajibu huo, na wanavyuoni wote wamewafikiana juu ya uwajibu huo.
Inayemuwajibikia Funga ya Ramadhani
Funga ya Ramadhani inamuwajibikia kila
Mwislamu, baleghe, mwenye akili, aliye katika mji wake (asiwe msafiri), mwenye
siha (afya - asiwe mgonjwa), asiwe na mambo yanayozuia kuswihi kwa funga (kama
hedhi na nifasi kwa wanawake).
Na inatakikana kwa wazazi kuwafundisha kufunga
watoto wao wanapofikia umri wa miaka saba (7) na kuwalazimisha hadi
ikibidi kuwapiga wanapofikia umri wa mika kumi (10), na hili inabidi
pia kuzingatia afya na ukuaji wa mtoto.
Nyudhuru za Kufunga
Nyudhuru za kuacha kufunga zinatofautiana na
kila udhuru una hukumu yake, na hapa nitazielezea nyudhuru hizo kwa
ufupi.
1. Hedhi (damu ya mwezi) na nifasi (damu ya
uzazi). Huu ni udhuru ambao unamlazimisha mwanamke kuacha kufunga, na inakuwa
haramu kwake kufunga na iwapo atafunga haitosihi (haitokubaliwa) funga yake, na
ni wajibu kwake kulipa funga hiyo.
2. Maradhi au safari. Na mwenye udhuru wa
maradhi (yanayotibika kwa kawaida) pamoja na msafiri wanaruhusiwa kutokufunga
na itawawajibikia kulipa. Amesema Allah (Subhaanahu wa Ta'ala) :{{Atakayekuwa katika mji katika huu mwezi (wa Ramadhani)
afunge. Na mwenye kuwa mgonjwa au safarini, basi (atimize) hisabu (ya siku
alizoacha kufunga) katika siku nyingine. Mwenyezi Mungu anakutakieni yaliyo
mepesi wala hakutakieni yaliyo mazito.. .}} (2:185). Na kama
maradhi yatazidi au kumletea madhara iwapo atafunga basi itakuwa lazima kwake
kutokufunga.
Ama safari ambayo inaruhusiwa kwa sababu yake
kutokufunga, wanachuoni wengi wemesema: Ni safari ya siku mbili kwa ngamia au
kwa mwendo wa miguu (mar-hala mbili) ambayo ni sawa na umbali wa takribani
kilomita (85km). Na ruhusa hii inapatikana kwa msafiri anayesafiri kwa chombo
cha aina yoyote atakachosafiria, ijapo kwa dhahiri safari hiyo haimpi uzito
wowote.
3. Vizee (vikongwe) na wenye maradhi sugu
(yasiotarajiwa kupoa). Na haya mawili iwapo yanamsababishia madhara, basi ni
katika udhuru na ruhusa ya kuacha kufunga, na itamlazimikia atoe fidia kwa
kumlisha masikini kibaba (mudi) cha chakula (ambacho ni sawa na uzito wa gramu
600 takribani) au chakula kinachomshibisha masikini mmoja kwa kila siku
aliyoacha kufunga.
4. Waja wazito na wanaonyonyesha. Nao ni katika
wenye ruhusa ya kutokufunga, na inawabidi kulipa siku walizoshindwa kufunga kwa
sababu ya udhuru huo.
5. Iliyemzidia njaa au kiu na akahofia
kuangamia, huu pia ni katika udhuru wa kuacha kufunga, bali wamesema wanachuoni
kwamba yule mwenye kuhofia kuangamia inakuwa kwake ni wajibu kufungua, na
itamuwajibikia kulipa kama mgonjwa.
Nguzo za Kufunga
Nguzo za kufunga ni tatu:
1. Kwanza ni kunuia. Nia ni kukusudia kufunga
usiku wa kuamkia siku ya kufunga, kwa funga ya faradhi.
2. Kujizuilia na vyenye kufunguza
(kufuturisha).
3. Muda wa kufunga (mchana kuanzia alfajiri
mpaka kutwa (kuzama) kwa jua).
Unavyothibiti kuingia Mwezi wa Ramadhani
1. Kwa kukamilika siku thelathini (30) za mwezi
wa Shaaban.
2. Kwa kuonekana mwezi mwandamo siku ya
29 ya mwezi wa Shaaban. Imepokewa hadithi na Abu Hurayrah (Radhiya Allahu
'anhu) kwamba Mtume (Swalla Allahu 'alayhi Wasallam) amesema: {Fungeni
kwa kuonekana kwake (mwezi mwandamo) na fungueni kwa kuonekana kwake}. (Al
Bukhariy na Muslim).
Na mwezi wa kuingia Ramadhani inatosha
kuonekana na Muislamu mmoja mwadilifu ama mwezi wa kumalizika Ramadhani ni
lazima uonekane na Waislamu waadilifu wawili au zaidi.
Yanayobatilisha (kuharibu) Funga
Mambo yafuatayo hubatilisha (huharibu) funga.
Nayo ni:
1. Kula au kunywa kwa kukusudia.
2. Kila kinachoingia tumboni au kooni kwa
kukusudia.
3. Kukutana kimwili (kuingiliana) kati ya mume
na mke.
4. Kujitoa manii (mbegu za uzazi) au
kusababisha kutokwa na manii (kwa kujichezea sehemu za siri, kukumbatiana au
kupigana mabusu na kadhalika).
5. Kujitapisha kwa makusudi. Imepokewa hadithi
kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allahu 'anhu) amesema: Amesema Mtume
(Swalla Allahu 'alayhi Wasallam): {...na mwenye kujitapisha basi inamuwajibikia
kulipa}
(wameipokea maimamu watano).
6. Kutokwa na damu ya mwezi (hedhi) au damu ya
uzazi (nifasi).
Wakati wowote yanapomtokea mwanamke mawili
hayo, funga yake ya siku hiyo itakuwa imeharibika na itamlazimikia kuilipa siku
hiyo baada ya mwezi wa Ramadhani.
Yasiyofunguza
1. Kula au kunywa kwa kusahau. Imepokewa
hadithi kutoka kwa Abu Hurayrah amesema, {amesema Mtume (Swalla Allahu 'alayhi
Wasallam): {Mwenye kusahau naye amefunga, basi akila au akinywa na aikamilishe
funga yake….} ( Al Bukhariy na Muslim ).
2. Kusukutua au kupandisha maji puani wakati wa
udhu (bila ya kubalighisha).
3. Kuoga au kujiburudisha kwa kujimwagia maji
katika kiwiliwili (hasa katika maeneo yenye joto kali).
4. Kuonja chakula kwa mpishi (kwa sharti ya
kutokumeza alichokionja).
5. Kutokwa na mbegu za uzazi (manii) katika
usingizi (ndoto) au bila ya kukusudia.
6. Kuamka na janaba. Imepokewa hadithi kutoka
kwa Mamama Aishah na Ummu Salamah (Radhiya Allahu 'anhuma) kwamba
Mtume (Swalla Allahu 'alayhi Wasallam) alikuwa akiamka na janaba kutokana na
kukutana kimwili na wake zake, kisha anaoga na kufunga (Al Bukhariy na Muslim).
7. Kupiga mswaki (wakati wowote).
8. Kuchoma sindano ya kawaida ya tiba.
9. Kung'oa jino na mfano wake.
10. Mwanamke kuamka kabla ya kuoga kwa hedhi au
nifasi.
Itaendelea.
Mwandishi wa makaha haya, Dk. Ibrahim Ghulaam,
Katibu Mtendaji wa Umoja wa Wanazuoni wa Kiislamu Tanzania (Hay-atul Ulamaa).
Anapatikana kupitia:
Simu: 0777 306 307 / 0658 88 22 12/ 0785 031 024
Barua pepe: ibralhamd2000@yahoo.com
No comments:
Post a Comment