Monday, June 2, 2014

SHEIKH IBRAHIM GHULAM


FUNGA YA RAMADHAN, HUKMU YAKE, SHARTI ZAKE NA ADABU ZAKE SEHEMU YA TATU.

IMEANDIKWA NA SHEIKH DK. IBRAHIM GHULAAM
DAR ES SALAAM
Sheikh Dk. Ibrahim Ghulaam, katika sehemu ya tatu ya makala
haya ataelezea kwa kina kuhusu yasiyofunguza na adabu za funga. Sasa fuatana naye katika sehemu hii ya mwisho.
Fadhila za funga
Zimepokewa hadithi nyingi zinazoelezea fadhila za funga ya Ramadhani, miongoni mwa hizo ni zifuatazo:
1- Amesema Mtume (Swalla Allahu ‘alayhi wa sallam): {Mwenye kufunga Ramadhani kwa imani na kutarajia malipo (toka kwa Allah (Subhaanahu wa Ta’ala) husamehewa madhambi aliyoyatanguliza}. (Al Bukhariy na Muslim).
2- Na amesema Mtume (Swalla Allahu ‘alayhi wa sallam): {amesema Allah (Subhaanahu wa Ta’ala): Kila amali ya mwanadamu (aifanyayo) ni yake, wema (mmoja) hulipwa kwa mfano wake mara kumi mpaka mara mia saba, isipokuwa funga, hakika ya funga ni Yangu mimi, na Mimi najua namna gani Nimlipe kwa funga hiyo, ameacha matamanio yake na chakula chake na kinywaji chake kwa ajili Yangu, mfungaji ana furaha mbili, furaha wakati wa kufutari kwake na furaha nyengine  pale atapokukutana na Mola wake. Harufu ya kinywa cha mfungaji inapendeza zaidi kwa Mwenyezi Mungu kuliko harufu ya miski}. (Al Bukhariy na Muslim).
Mfungaji anayopaswa kujiepusha nayo:

1. Tabia chafu na maneno maovu, kama kusengenya, kusema uongo, na kadhalika. 2- Kuzidisha usingizi (kulala kupita kiasi) ambao unampotezea Muislamu fursa ya kufanya ibada zaidi.

3. Kupoteza wakati mwingi katika michezo na maongezi yasiyo na faida, na kuacha kuutumia wakati huo katika kazi na ibada mbalimbali. 4. Kuacha kula daku au kuchelewa kufuturu baada ya kutwa kwa jua.

5. Kufanya israfu katika vyakula na vinywaji wakati wa kufutari.

6. Kufutari kwa vyakula vyenye harufu ya kuchukiza, kama: vitunguu thaumu, vitunguu maji, doriani, na kadhalika kwa kuhofia kuwaudhi Waislamu wakati mnapojumuika kwa swala.

7. Kutokuswali tarawehe kwa utulivu na unyenyekevu.
Yanayotakiwa kwa kumalizika Ramadhani

1. Kutoa zakatul-fitri, nayo ni wajibu kwa kila Muislamu, (mwanamme, mwanamke, mkubwa, mdogo, muungwana (huru) au mtumwa). *Watoto wadogo, watumwa na pia wanawake waliochini ya usimamizi wa wanaume itawalazimikia zakah hiyo wasimamizi wao, ama wanawake wanaojitegemea itawalazimikia wao wenyewe. *Na inatakikana itolewe zakatul-fitri kabla ya swala ya Idd.
Imepokewa hadithi kutoka kwa Ibn ‘Umar (radhiya Allahu ‘anhuma)  amesema: Amefaradhisha Mtume (Swalla Allahu ‘alayhi wa sallam) Zaka ya fitri (ya kumalizika Ramadhani) pishi ya tende au pishi ya shairi kwa mtumwa na huru (muungwana), mume na mke, mdogo na mkubwa katika Waislamu, na akaamrisha (hiyo zakah ya fitri) itolewe kabla ya kutoka watu kuelekea katika Swalah (ya iddi). (Al Bukhariy na Muslim).
Ni wajibu ni kutoa pishi ya chakula maarufu katika mji uliopo (ambayo ni sawa na uzito wa kilo mbili na gramu mia nne (2.4 kg) takriban kwa nafaka kama mchele na mfano wake) (au thamani yake kwa baadhi ya wanachuoni).

2. Takbir: Inasuniwa kuleta takbir baada ya kuandama (kuonekana) mwezi wa kumalizika Ramadhani, kuanzia kuchwa (kuzama) kwa jua mpaka wakati wa swala ya Idd. Na inasuniwa kunyanyua sauti kwa wanaume njiani, sokoni na hata nyumbani.

3. Swala ya Idd kwa wanaume na wanawake.

Na inasuniwa ifanyike katika viwanja, na hata akina mama walio katika siku zao (hedhi) inasuniwa na wao wahudhurie ingawa wao hawatoshiriki katika kuswali.

4. Na inasuniwa kula tende kwa idadi ya (witri) au chakula chengine hafifu kabla ya kutoka kwa ajili ya Swala ya Iddi el-fitr.

5. Pia inasuniwa kubadilisha njia wakati wa kwenda na kurudi kwenye Swala ya Idd. Imepokewa hadithi kutoka kwa Jaabir (radhiya Allahu ‘anhu) amesema: Alikuwa Mjumbe wa Allah (Swalla Allahu ‘alayhi wa sallam) inapokuwa siku ya iddi akibadilisha njia (ya kwenda na ya kurudia). (Al Bukhary).

6. Kuvaa mavazi bora zaidi anayoyamiliki Muislamu. *Na inatakikana kwa wale wenye familia kuwaandalia mavazi mazuri watu wa familia zao (bila ya kufanya israfu).

7. Na pia inasuniwa baada ya kumalizika Ramadhani kufunga siku sita katika mwezi wa mfunguo mosi (shawwali). Amesema Mtume (Swalla Allahu ‘alayhi wa sallam): {Mwenye kufunga Ramadhani kisha akaifuatilizia siku sita katika mwezi wa shawwali (mfunguo mosi) inakuwa kama aliyefunga mwaka (mzima kamili). (Muslim).

8. Na tukumbuke ya kwamba siku hii ya iddi inakatazwa (ni haramu) kufunga ndani yake. Imepokewa hadithi kutoka kwa Abu Said Al khudriy (radhiya Allahu ‘anhu): (Hakika Mjumbe wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allahu ‘alayhi wa sallam) amekataza kufunga katika siku mbili: Siku ya (iddi) alfitri na siku ya (iddi) ya kuchinja (iddi l-adh`ha)). (Al Bukhariy na Muslim).

Namalizia makala hii kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Ta’ala) aliyeniwezesha kufanikisha lengo langu hili.

Kisha natoa shukurani zangu za dhati kwa wale wote waliochangia kwa njia moja au nyengine kuifikisha kwa jamii makala hii. Na ninamuomba Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Ta’ala) atupe kila la kheri hapa duniani na kesho akhera. Amiin.
Mwandishi wa makaha haya, Dk. Ibrahim Ghulaam, amejitambulisha kuwa ni Katibu Mtendaji wa Umoja wa Wanazuoni wa Kiislamu Tanzania (Hay-atul Ulamaa).
*Mwandishi amechukua:
1. Shahada ya kwanza katika fani ya sharia (Islamic law).
2. Shahada ya pili katika fani ya sharia (kitengo cha “usulul   fiqhi”).
3. Anamalizia shahada ya tatu katika fani ya sharia (kitengo cha fat`wah).
Anapatikana kupitia:
Simu: 0777306307/0658882212

No comments:

Post a Comment