Monday, June 9, 2014

JESHI LA POLISI LAINGIA KWENYE KASHFA DHIDI YA KUNDI LA BOKO HARAM, MAGAZETI YAFUNGIWA.






Wakurugenzi wa magazeti manne ya Nigeria wamedai kwamba, maafisa wa jeshi la Nigeria wamezuia kuchapishwa na kusambazwa magazeti yao.
Wakurugenzi hao wa magazeti ya Nation, Daily Trust, Leadership na Punch wamedai kwamba, nakala za magazeti hayo zimekusanywa na maafisa wa jeshi la Nigeria.
Mkurugenzi wa gazeti la Daily Trust pia amedai kwamba, askari jeshi wamevamia ofisi za gazeti hilo katika mji mkuu Abuja na kwenye mji wa kaskazini wa Kano.
Amesema kuwa, tukio hilo linakumbusha vitendo vya kufunika ukweli vya wakati wa kipindi cha utawala wa kijeshi nchini humo.
Hata hivyo Christ Olukolade Waziri wa Ulinzi wa Nigeria amekanusha madai hayo na kuzima sauti za wakosoaji.
Kuandikwa magazetini madai ya kushindwa jeshi la Nigeria kukabiliana na mashambulizi ya kila siku na mauaji ya Boko Haram, pengine ndio sababu kuu iliyopelekea kuzuiwa kusambazwa magazeti hayo na nakala zake kukusanywa.
Katika miezi ya hivi kaaribuni jeshi na serikali ya Nigeria imekuwa ikikosolewa sana na vyombo vya habari na fikra za walio wengi.
Ingawa hali ya hatari ilirefushwa katika majimbo manne ya kaskazini mashariki mwa nchi hiyo kwa muda wa mwaka zaidi, lakini mashambulizi ya kundi ya Boko Haram nayo pia yameongezeka. 
Karibu watu 500 wamepoteza maisha katika mashambulizi ya hivi karibuni yaliyofanywa na kundi hilo kwenye mkoa wa Borno.
Kutekwa nyara wasichana wa shule karibu 200 Aprili 14, kumeongeza malalamiko ndani ya Nigeria na kuitia wasiwasi jamii ya kimataifa.
Katika hali ambayo miezi miwili imepita huku watoto hao waliotekwa nyara wakiwa bado hawajakombolewa, wasichana wengine kadhaa nao wametekwa nyara na Boko Haram katika vijiji vya kaskazini mwa Nigeria hivi karibuni.
Ni kwa sababu hiyo ndio maana moja ya magazeti ya Nigeria liliandika makala iliyowatuhumu makamanda wa jeshi la nchi hiyo kwamba baadhi yao wanatumia kambi za jeshi za mjini Abuja kuwahifadhi jamaa zao.
Pia gazeti moja liliandika kwamba, majenerali 10 wa jeshi na makamu watano wa ngazi za juu wa serikali ndio wanaosababisha jeshi lishindwe katika mapambano dhidi ya kundi la Boko Haram.
Waziri wa Ulinzi wa Nigeria amesema kuwa, madai hayo yameratibiwa kwa lengo la kulichafulia jina jeshi na wanajeshi nchini humo na barani Afrika kwa ujumla.
Bila kuzingatia kuwa tuhuma walizoelekezewa majenerali na jeshi la Nigeria ni za kweli au la, kutolewa madai hayo katika wakati huu ambapo  wananchi Waislamu, Wakristo pamoja na jamii nyinginezo nchini humo wanaishi kwa hofu kubwa ya kushambuliwa na Boko Haram, kunaweza kuleta hasira na chuki katika jamii.
Nigeria ambayo ina jumla wa watu milioni 170 inahesabiwa kuwa nchi yenye watu wengi zaidi barani Afrika, na kwa miaka mitano sasa imekuwa ikishuhudia kushambuliwa misikiti, makanisa, Waislamu na pia Wakristo.
Inaaminika kuwa, kundi hilo lenye misimamo mikali limeundwa na linaendeshwa na baadhi ya nchi za Magharibi zinazofanya njama za kuwalazimisha walimwengu waamini kuwa dini ya Uislamu ni ya kikatili na isiyotumia akili.
Weledi wa mambo wanaamii kuwa, serikali na jeshi la Nigeria kwa kushirikiana na nchi jirani za magharibi mwa Afrika, litaweza kuimarisha nguvu zake za kijeshi na kijasusi katika kukabiliana na Boko Haram na hatimaye kulisambaratisha kundi hilo.
Wakati huo huo kukusanywa na kuzuia kuchapishwa na kusambazwa magazeti ni hatua zinazokinzana na haki ya uhuru wa vyombo vya habari suala ambalo pia linaweza kuwafanya wananchi wazidi kutilia shaka na kukosa imani na serikali.


No comments:

Post a Comment