Abdul-Fattah el Sisi ameapishwa kuwa rais wa
Misri hapo jana katika Mahakama ya Katiba mjini Cairo huku kukiwa na ulinzi
mkali.
Adli Mansour aliyekuwa rais wa muda Misri
alimkabidhi rasmi el Sisi hatamu za uongozi katika sherehe hiyo.
Vyombo vya habari vya Misri vimeripoti kuwa,
viongozi wasiopungua 45 wa Kiarabu na kimataifa walikuwepo kwenye sherehe hizo.
Katika hotuba yake el Sisi amesema atajitahidi
kuimarisha uchumi na misingi ya kijamii na kiusalama nchini humo. Aidha amewashukuru
wawakilishi wa nchi za kigeni walioshiriki katika sherehe za kuapishwa kwake na
kuongeza kuwa sambamba na ujenzi mpya wa Misri atahuisha nafasi na ushawishi wa
Cairo kieneo na kimataifa.
El Sisi ameongeza kuwa Misri mpya itashiriki
katika kurejesha amani na uthabiti wa kieneo.
Rais mpya wa Misri ameendelea kusema kuwa taifa
la Misri lichukue hatua za kuhakikisha lina mustakabali mwema wenye matumaini.
Wakati huo huo duru katika serikali ya Misri
zinadokeza kuwa Ibrahim Mahlab ambaye hivi sasa ni waziri mkuu wa nchi hiyo
ataendelea kushikilia nafasi yake hadi pale uchaguzi wa bunge utakapofanyika.
Uchaguzi wa bunge Misri unatazamiwa
kufanyika bada ya kuidhinishwa katiba mpya ya Misri.
Abdul Fattah El Sisi ameapishwa kuwa rais wa
Misri huku wafuasi wake wakiwa na matumaini mengi, huku kukiwa na wale wasemao
kuwa yamkini akawa na nafasi nzuri katika mustakabali wa Misri huku
wengine wakiamini kuwa jenerali huyo wa zamani jeshini atatumia mkono wa chuma
dhidi ya wananchi hasa wapinzani.
El Sisi amewaahidi wananchi kuwa ataboresha
maisha yao katika kipindi cha miaka miwili ijayo.
Aidha amesema atahakikisha kuwa wananchi
wanafikia malengo yao ya mapinduzi.
Haya ni mapinduzi ambayo miaka miwili iliyopita
yalianza katika Medani ya Tahrir mjini Cairo kwa shaari za uhuru, uadilifu wa
kijamii na heshima ya mwanaadamu.
Hivi sasa Wamisri wanatarajia kuwa el Sisi
atatekeleza shaari hizo la sivyo serikali yake itakabiliwa na hali mbaya siku
za usoni.
Inavyoelekea ni kuwa watu wa Misri hivi sasa
wako katika hali ya hofu na matumaini, wakisubiri kuona iwapo El Sisi
kama alivyoahidi ataipelekea Misri katika mkondo wa demokrasia au kama
wanavyosema wapinzani wake ataunda utawala wa kiimla wenye kutawala kwa mkono
wa chuma na kuwakandamiza wapinzani.
No comments:
Post a Comment