JE KUPINGA KIFO CHA YESU NI
KUMPINGA MUNGU?
MAHFUDHI M. MAHFUDHI
Naomba nafasi katika gazeti
lako ili niweze kumjibu Bw. Anthony Mtambo katika makala yake iliyochapishwa
katika gazeti la kidini toleo namba 022 la Agosti 2-8, 1998 iliyokuwa na
kichwa cha habari "Kupinga kifo cha Yesu ni kumpinga Mungu".
Baada ya kutoa
maelezo mengi ambayo nitayanukuu hapa amesema, "Wale wanaofanya juhudi
za kukanusha kifo (msalaba) cha Yesu Kristo, watambue kwamba wanapingana na
Mungu. Wanapingana na Mungu kwa sababu huu ni mpango wa Mungu…". Pia
nimenukuu sehemu ya hitimisho la makala yake: "Kwa wale walio na mapokeo
ya dini yoyote iliyotofauti na Ukristo, ambao wamefundishwa kinyume na
ilivyosema Biblia Takatifu, basi niko tayari kutoa msaada wa kuelimisha juu
ya suala la kifo cha Bwana Yesu kwa eneo lao".
Maelezo ya
mwandishi hayana nguvu, na lau angelikuwa na maarifa ya kuwaelimisha
"wale walio na mapokeo ya dini yoyote iliyo tofauti na Ukristo",
basi asingedai kwamba kukanusha kifo cha Yesu ni kumpinga Mungu. Hoja yake ya
Mungu kupingwa haina ushahidi ni jitihada yake kuwahofisha watu waamini tu,
pasipo kuhoji mantiki ya misingi ya imani yenyewe.
Kabla ya
kuonesha udhaifu wa maoni yake napenda kumfahamisha na kumuelimisha msimamo
wa dini ya Kiislamu juu ya anachodai kuwa ni "kifo cha Yesu
msalabani". Tunafahamishwa na Mwenyezi Mungu katika Qur’an Tukufu 4:157:
Na kwa (ajili
ya) kusema kwao: "Sisi tumemuua Masihi Isa, mwana wa Maryamu Mtume wa
Mungu", hali hawakumuua wala hawakumsulubu, bali walibabaishiwa mtu
mwingine wakadhani Nabii Isa). Na kwa hakika wale waliokhilitafiana katika
hakika hiyo (ya kumuua Nabii Isa) wamo katika shaka nalo (jambo hilo la kusema kauawa).
Wao (kabisa) hawana yakini juu ya (jambo) hili (ila kuwa kweli wamemuua Nabii
Isa), isipokuwa wanafuata dhana tu. Na kwa yakini hawakumuua. (Tafsiri ya
Kiswahili ya Qur’an ya Sheikh A. Farsy).
Kwa uchache ni
kwamba, Yesu hakusulubiwa wala hakuuawa na hivyo hakuna "kufufuka"
na wanaoamini kinyume na hivi wanafuata dhana tu. Kwani Biblia inasemaje?
Mathayo
anatufahamisha katika Injili yake:
"Hapo
baadhi ya waandishi na Mafarisayo wakamjibu, wakasema, Mwalimu, twataka kuona
ishara kwako. Akajibu, akawaambia, kizazi kibaya na cha zinaa chatafuta
ishara, wala hakitapewa ishara, ila ishara ya nabii Yona. Kwani kama vile
Yona alivyokuwa siku tatu mchana na usiku katika tumbo la nyangumi, hivyo ndivyo
mwana wa Adamu atakavyokuwa siku tatu mchana na usiku katika moyo wa nchi.
(Mt. 12:38-40) (Rejea Yona 1:15 –2:1).
Kwa maelezo haya
ya Yesu ni kwamba hatakufa kama vile ambavyo
Yona hakufa, ila atakaa kaburini siku tatu, mchana na usiku kwa kila siku, na
hivyo kusingekuwa na ufufuko. Lakini Mathayo anaeleza katika 27:45 – 28:1-6
kwamba Yesu alikufa, akazikwa kisha akafufuka. Kanisa nalo linafundisha
kwamba Yesu alikufa Ijumaa jioni na akafufuka Jumapili alfajiri, yaani kukaa
kaburini siku moja na nusu tu.
Bado kuna
hitilafu nyingi kuhusu mwisho wa Yesu baada ya kukamatwa. Kwa mfano, Marko
anasema Yesu alisulubiwa saa tatu asubuhi (Mk. 15:25) lakini Yohana anasema
alisulubiwa baada ya saa sita mchana (Yn. 19:14). Luka anapingana anaposema
kwamba Yesu alipaa siku ile ile aliyofufuka (Lk. 24:13-51). Lakini katika
kitabu chake cha Matendo ya Mitume akaeleza kuwa alipaa siku ya arobaini
baada ya kufufuka (Mdo 1:1-12).
Tatizo la Bw.
Anthony ni kwamba ameegemea zaidi kwenye itikadi ya Kanisa kuliko maandiko ya
Biblia na hivyo kulazimika kuchagua vifungu vya Biblia vinavyohami imani yake
tu kwa vile Kanisa haliifuati Biblia yote. Biblia ni bahari pana yenye
vifungu vingi vinavyopingana na visivyofahamika asili yake. Na Waislamu
hatutilii shaka maneno ya Mwenyezi Mungu katika Qur’an Tukufu anaposema
kwamba imani ya Yesu kusulubiwa msalabani na kufa ni dhana. Tunaposema
migongano kama nilivyoelezea juu kwa
uchache, tunazidi tu kukumuamini Mwenyezi Mungu. Kwani Bw, Anthony ana
uhakika gani kwamba Yesu alisulubiwa msalabani (saa tatu au sita?) na kukaa
kaburini siku moja na nusu tu na sio kwamba ni siku tatu mchana na usiku tena
akiwa hai kama alivyowaambia Waandishi na
Mafarisayo.
Licha ya hayo,
hakuna ushahidi wowote unaothibitisha kama
Waandishi wa Injili nne walikuwa watu wa kutumainiwa na walioongozwa na
Mungu. Kwa mfano, Biblia Takatifu, Agano Jipya, UBS 1990, inaeleza katika uk. 13
"utangulizi wa Injili kama
ilivyoandikwa na Mathayo":
Injili ya
Mathayo haisemi chochote kuhusu mtungaji wake. Kadiri ya mapokeo ya zamani,
Mathayo mtoza ushuru na mmoja wa Mitume kumi na wawili aliandika maneno ya
Yesu katika lugha ya Kiaramu. Bahati mbaya mtungaji wa Injili yetu ya sasa
aliyeandika katika lugha ya Kigiriki (ambaye habari zake maalum hatuna)
aliongozwa na mawaidha ya Mathayo, mfuasi wa Yesu).
Na kuhusu Injili
ya Luka tunaelezwa:
Kadiri ya
mapokeo ya zamani Injili ya tatu imeandikwa na Luka aliyezaliwa Antokia akawa
Daktari. Alikuwa mpagani (au wa asili ya mazingira ya Kigiriki) si Myahudi kama walivyokuwa akina Mathayo, Marko na Yohana (Uk. 84
wa Biblia hiyo hiyo).
Nayo Biblia
Takatifu T.M.P. Book Department Tabora, 1967, uk, 911 inaeleza kwamba Marko
hakuwa mwanafunzi wa Yesu, na Injili yake ni muhtasari wa mafundisho ya
Petro. Na ama Injili ya Yohana inajishuhudia yenyewe kwamba waandishi wake ni
wengi na wala hawafahamiki:
Huyu ndiye yule
mwanafunzi ayashuhudiaye haya, na aliyeyaandika haya; nasi twajua ya kuwa
ushuhuda wake ni kweli. (Yn. 21:24).
Na hii ikawa
ndio sababu ya wasomi wa juu wa Kikristo kusema kwamba mwandishi wa Injili
hii sio Yohana, huenda labda ni wanafunzi wake (Dictionery of the Bible, John
Mackenzie; 1981 maelezo kuhusu Injili ya Yohana).
Kwa hiyo, Bw.
Anthony anapodai kutaka kufundisha "eneo" la Waislamu juu ya kifo
cha Yesu inabidi ajiulize maswali kadhaa, kwamba, je, anaifahamu Biblia yake
vyema? Anatambua tofauti kati ya Ukristo na Biblia? Anaifahamu Qur’an
inavyotakiwa kuifahamu? Na zaidi ya yote anatakiwa kuacha fikra lemavu ya
kutaka kujaribu kulinganisha Ukristo na Uislamu.
Napenda kumfahamisha
kwamba Waislamu hatuna lolote la kujifunza kwake kuhusiana na somo hili, ila
tu atupe hoja kuthibitisha kwamba itikadi anayoitetea haikujengeka juu ya
dhana. Pia kwa Waislamu kupinga kifo cha Yesu sio kumpinga Mungu kwa sababu
Mwenyezi Mungu hajasema mahali popote kwamba Yesu kafa. Hayo ni madai ya watu
wasiofahamika (kwa wanahistoria wa Kikristo na Wakristo wenyewe) pamoja na
Wapagani.
Tuzingatie
tahadhari aliyoitoa Mwenyezi Mungu katika Qur’an Tukufu:
Basi adhabu kali
itawathibitikia wale wanaoandika kitabu kwa mikono yao, kisha wakasema, "hiki kimetoka
kwa Mwenyezi Mungu". (Wanasema uwongo huo) ili wachukue thamani ndogo ya
kilimwengu. Basi ole wao kwa yale walivyoyaandika kwa mikono yao (wakasingizia kuwa ya Mungu). Na ole
wao kwa yale wanayoyachuma. ( Qur’an Tukufu 2:79).
Kwa hiyo, Bw.
Antony azingatie onyo hili anaposema kwamba maneno fulani ni ya Mwenyezi
Mungu pasipo kuwa na elimu ya kina juu ya maneno yenyewe.
|
CHANZO:
AN-NUUR
Na.164 Jamada Awal 1419, Agosti 28 - Septemba 3, 1998
Na.164 Jamada Awal 1419, Agosti 28 - Septemba 3, 1998
No comments:
Post a Comment