UKWELI KUHUSU MAZISHI YA KIISLAMU
Bismillaahir Rahmaanir Rahiim
Kwa hakika kila sifa njema ni Zake Allaah, tunamtukuza Yeye, na
tunamtaka msaada Yeye na tunamuomba msamaha Yeye. Tunajilinda kwa Allaah
kutokana na maovu ya nafsi zetu na udhaifu wa vitendo vyetu. Aliyeongozwa na
Allaah hakuna wa kumpoteza na aliyepotezwa na Allaah hakuna wa kumuongoza.
Nashuhudia kuwa hapana apasaye kuabudiwa kwa haki ila Allaah na nashuhudia kuwa
Muhammad ni mja Wake na Mtume Wake.
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ
آمَنُوا اتَّقُوا اللَّـهَ حَقَّ تُقَاتِهِ وَلا تَمُوتُنَّ إِلا وَأَنتُم
مُّسْلِمُونَ
“Enyi mlioamini mcheni Allaah
(kwa kuyatekeleza yote Aliyowaamrisha na kujiepusha na yote Aliyowakataza) kama
ipasavyo kumcha wala msife ila mumekwisha kuwa Waislamu kamili” (Qur-aan 3: 102)
يَا أَيُّهَا النَّاسُ
اتَّقُوا رَبَّكُمُ الَّذِي خَلَقَكُم مِّن نَّفْسٍ وَاحِدَةٍ وَخَلَقَ مِنْهَا
زَوْجَهَا وَبَثَّ مِنْهُمَا رِجَالا كَثِيرًا وَنِسَاءً ۚ وَاتَّقُوا
اللَّـهَ الَّذِي تَسَاءَلُونَ بِهِ وَالأرْحَامَ ۚ إِنَّ اللَّـهَ كَانَ
عَلَيْكُمْ رَقِيبًا
“Enyi watu mcheni Mola wenu
ambaye Amekuumbeni kutokana na nafsi (asili - Adam) moja. Na akamuumba mkewe
katika nafsi ile ile. Na akaeneza wanaume wengi na wanawake kutokana na wawili
hao. Na mcheni Allaah ambaye kwaye mnaombana. Na (muwatazame) jamaa. Hakika
Allaah ni Mlinzi juu yenu (Anayajua mnayoyafanya).” (Qur-aan 4: 1)
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ
آمَنُوا اتَّقُوا اللَّـهَ وَقُولُوا قَوْلًا سَدِيدًا ﴿٧٠﴾ يُصْلِحْ لَكُمْ
أَعْمَالَكُمْ وَيَغْفِرْ لَكُمْ ذُنُوبَكُمْ ۗ وَمَن يُطِعِ اللَّـهَ
وَرَسُولَهُ فَقَدْ فَازَ فَوْزًا عَظِيمًا ﴿٧١﴾
“Enyi mlioamini
mcheni/muogopeni Allaah na mseme maneno yaliyo ya haki (maneno ya kweli).
(Allaah) Atakutengenezeeni vizuri vitendo vyenu, na Atakusameheni madhambi
yenu. Na mwenye kumtii Allaah na Mtume Wake bila shaka amefanikiwa mafanikio
makubwa.” (Qur-aan
33: 70-71)
Kwa hakika maneno ya kweli
kabisa ni yale ya Kitabu cha Allaah, na uongozi ulio bora zaidi ni uongozi wa
Muhammad (Rehma na amani ya Allaah ziwe
juu yake). Na maovu yaliyo mabaya zaidi ni mambo ya kuzua (yaliyo mageni katika mafundisho ya Uislamu), na kila lenye
kuzushwa katika dini ni bidaa (uzushi),
na kila bidaa ni upotofu na kila upotofu mwisho wake ni katika moto.
Ndugu msomaji, Allaah
Mtukufu Anasema:
تَبَارَكَ الَّذِي بِيَدِهِ
الْمُلْكُ وَهُوَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ ﴿١﴾ الَّذِي خَلَقَ الْمَوْتَ
وَالْحَيَاةَ لِيَبْلُوَكُمْ أَيُّكُمْ أَحْسَنُ عَمَلا ۚ وَهُوَ الْعَزِيزُ
الْغَفُورُ ﴿٢﴾
“Ametakasika (Ametukuka) Yule
ambaye mikononi Mwake upo ufalme na Yeye ni Muweza juu ya kila kitu. Yeye
(Allaah) ndiye Aliyeumba umauti na uhai ili apate kuwajaribu ni nani kati yenu
mwenye vitendo vizuri. Na Yeye (Allaah)
ni Mwenye nguvu na ni mwingi wa kusamehe.” (Qur-aan 67: 1-2)
Mtume Muhammad (Rehma na amani ya Allaah iwe juu yake)
amesema:
“Sikuwa mimi katika hii
dunia isipokuwa ni mfano wa msafiri jangwani aliyepumzika katika kivuli cha
mti, kisha akaondoka na kukiacha kivuli kile”. (Hadiyth sahihi: Al-Albaaniy, namba, 438).
Ndugu msomaji, fahamu kuwa
kwa mujibu wa mafundisho sahihi ya Uislamu, maiti ana haki nne anazopaswa
kutendewa, ambazo ni:
1. Kuoshwa,
2. Kuvishwa sanda,
3. Kuswaliwa, na
4. Kuzikwa.
Hii ina maana kuwa Waislamu
watawajibika kuyafanya haya kwa kila maiti Muislamu na si vinginevyo. Na
watakapoacha kumfanyia maiti mambo hayo watapata dhambi Waislamu wote wa sehemu
ile.
Ndugu msomaji, tunafahamu
kuwa una hamu kubwa ya kuyajua kiundani mambo manne tuliyoyataja hapo juu.
Shaka ondoa, makala hii iliyo mikononi mwako itakuonesha hayo kadiri
utakapozidi kufungua kurasa zake.
Awali ya yote tunapenda
kukujulisha itikadi ya Uislamu kuhusu maisha na uhai huu wa dunia.
Ndugu msomaji, Waislamu
wanaitakidi kuwa, kila kilichopo katika dunia kitaondoka (kitakufa). Na hii ni
kutokana na kauli ya Allaah Aliposema:
كُلُّ مَنْ عَلَيْهَا فَانٍ
“Kila
kilicho juu ya ardhi ni chenye kufa…” (Qur-aan 55: 26)
Kama ilivyozoeleka kuwa hakuna mwanzo usiokuwa na mwisho, wala
hakuna mchana usiokuwa na usiku, kadhalika hakuna uhai usiokuwa na mauti.
Allaah Anasema:
كُلُّ نَفْسٍ ذَائِقَةُ
الْمَوْتِ
“Kila nafsi
itaonja umauti (Itakufa)…” (Qur-aan 21: 35)
Na Mtume (Rehma na amani ya Allaah ziwe juu yake)
ameweka wazi katika Hadiyth tuliyoitanguliza hapo nyuma.
Ndugu msomaji, waweza
kujiuliza kuwa umauti ni nini?
Nasi kwa kulifahamu hilo
tuna haki ya kukufafanulia kama ifuatavyo:
Umauti ni mtengano au
mfarakano kati ya mwili na roho ya kila kiumbe hai, kama mwanadamu, wanyama,
majini n.k. Hapo huwa ndio mwisho wa kazi ya kila kiungo cha aliyekufa; macho,
mdomo, sikio, mikono, mguu na mfano wake.
Si kama wanavyodai baadhi
ya wasiokuwa na ufahamu sahihi na wasio na akili zenye kuwatosha kuwa eti kuna
baadhi ya watu ambao huwa wanakufa baadhi ya viungo na baadhi havifi. Huu ni
uongo wa wazi kabisa na kila mtu aliye na akili timamu atampa msemaji wa maneno
haya moja kati ya sifa tatu zifuatazo:
1. Mjinga,
2. Punguani, hajui alisemalo,
3. Ni mtu aliyeamua kuifanya
nafsi yake kuwa pumbavu, mfano wake ni
kama mtu anayedai mchana kuwa usiku na usiku kuwa mchana.
kama mtu anayedai mchana kuwa usiku na usiku kuwa mchana.
Haiingii
akilini kabisa kuwa mtu afe halafu mguu wake usife au mkono wake au macho yake
yasife au tupu yake isife. Hii haihitaji Aayah, Hadiyth, wala elimu kubwa wala
muujiza, kwani akili inamtosha mwenye nazo na akazitumia. Ama yule asiyekuwa na
akili basi Aayah, Hadiyth wala elimu yoyote pia haitamfaa.
Ndugu msomaji, katika hili
tunaomba mchango wako wa kiakili na kujiuliza kuwa, Je, inawezekana kweli mtu
afe baadhi na baadhi abaki kuwa hai halafu aitwe maiti? Jawabu liwe akilini
mwako.
Mpendwa msomaji, baada ya
kupata jawabu, sasa nikueleze yale mambo manne anayopaswa kufanyiwa maiti wa
Kiislamu.
Jambo
La Kwanza Ni Kuosha
Waislamu wanaosha maiti kwa
sababu hayo ni mafundisho ya dini, na ni shari’ah.
Mtume Muhammad (Rehma na amani ya Allaah ziwe juu yake)
ametufundisha hayo katika Hadiyth ya Swahaba (mfuasi wa karibu) mtukufu Ibnu
‘Abbaas (Radhi ya Allaah iwe juu yake) katika kitabu cha Imam Al-Bukhaariy na
Muslim kama alivyoeleza Shaykh Al-Albaaniy katika kitabu chake Ahkaamul
Janaaiz, na Abuu Nu’am katika al-Mustakhraj Hadiyth namba, 139-140:
Maana ya Hadiyth:
“Siku moja mtu mmoja alikuwa
amesimama ‘Arafah, ghafla mtu huyo akaanguka kutoka katika mnyama wake na yule
mnyama akamkanyaga na kufa papo hapo. Mtume (Rehma na amani ya Allaah ziwe juu yake) akasema: “Muosheni kwa maji
na majani ya mkunazi na mumvishe sanda…”
Hivyo basi kwa mujibu wa
mafundisho ya Mtume Muhammad (Rehma na
amani ya Allaah ziwe juu yake) Waislamu wanawajibika kuosha maiti yao pale
linapowezekana, kwa sababu hayo ndiyo mafundisho ya dini yao na si vinginevyo,
wala si kama wasemavyo wenye chuki dhidi ya Uislamu kuwa eti Waislamu wanaosha
maiti kwa sababu huenda ina janaba (yaani ilizini).
Swali la kujiuliza, Je ni
kitabu gani kinachozungumzia hayo? Jibu ni hakuna ushahidi juu ya hayo katika
kitabu chochote au mafunzo yoyote ya Uislamu wala hakuna ushahidi wowote wa
kimazingira. Unaweza kujiuliza, kwa nini basi wanasema wasiyo na ushahidi nayo?
Jibu linaloweza kupatikana ni moja tu, nalo ni chuki dhidi ya Uislamu.
Ndugu msomaji, ukweli ulio
wazi ni kuwa chuki dhidi ya Uislamu imewapelekea watu (maadui) kuuzungumzia
Uislamu na kuuzushia mambo ambayo hayapo na hayana ushahidi wowote. Muradi wao
ni kuupiga vita Uislamu katika hali yoyote ile iwayo, na hili Allaah Mtukufu
Amelitanabahisha katika Qur-aan, Aliposema:
ولا يَزَالُونَ
يُقَاتِلُونَكُمْ حَتَّىٰ يَرُدُّوكُمْ عَن دِينِكُمْ
“Hawataacha kukupigeni kwa
chuki walizo nazo mpaka wakutoeni katika dini yenu watakapoweza kufanya hivyo” (Qur-aan 2:217)
Ndugu msomaji, suala la
zinaa limekatazwa katika Qur-aan kuanzia katika hatua zake za mwanzo. Allaah
Mtukufu Amesema:
وَلَا تَقْرَبُوا
الزِّنَا ۖ إِنَّهُ كَانَ فَاحِشَةً وَسَاءَ سَبِيلًا
“Wala msikaribie zinaa kwani
huo ni uchafu na ni njia iliyo mbaya kabisa” (Qur-aan 17:32)
Haifai kumtazama mwanamke
kwa matamanio, imekatazwa pia kupeana mikono na mwanamke/mwanamume ambaye si
ndugu yako wa karibu, si hilo tu, Uislamu hauruhusu wanaume kuchanganyika na
wanawake katika hali yoyote ile. Kama hilo halitoshi, mwanamke katika Uislamu
anatakiwa avae hijabu, vazi lisilo bana mwili wala lisilovutia na linalofunika
mwili mzima. Katika hali hii na kwa mazingira haya, iweje Muislamu azini? Hapo
ndipo utagundua kuwa aliyesema haya ima alitoka usingizini au hatumii akili.
Ndugu msomaji, fahamu kuwa
hakuna mfumo au utaratibu wa maisha wenye kumuhimiza na kumuhitaji mtu kuwa
mbali na zinaa kama utaratibu wa Kiislamu. Ndio maana Uislamu ukahimiza kuoa na
ukakemea vikali uhuni na ukapera (kuto oa). Tunakushauri ndugu msomaji, uusome
Uislamu, na hii ndio njia pekee ya kuujua ukweli, badala ya kusikiliza maneno
ya watu wenye chuki na uadui dhidi ya Uislamu, ambao wengine wanadai kuujua
Uislamu lakini kiukweli ni kuwa wanachotafuta ni kuwadanganya wasiokuwa
Waislamu ili kupata muradi wao wa siku.
Namna
Ya Kuosha Maiti
Ni nani mwenye haki zaidi
ya kumuosha maiti? Kwa mujibu wa mafundisho ya Uislamu, mwenye haki zaidi ya
kumuosha maiti ni yule mwenye ufahamu sahihi juu ya utaratibu wa kuosha maiti
na Sunnah[1] zake, na hasa akiwa ni
katika jamaa zake kama vile, mkewe/mumewe, mwanawe n.k.
Waoshaji huwa ni wawili au watatu
kulingana na hali halisi. Watu hawa hawana majina maalum kishari’ah, kama
wanavyodai baadhi ya watu kuwa eti kuna kiguzo, kigingi, na mshika kata; huu ni
uzushi. Vitabu vinaonesha kuwa, Mtume (Rehma
na amani ya Allaah ziwe juu yake) alioshwa na ‘Aliy akisaidiwa na Al-Fadhlu
ibnu ‘Abbaas na Usaamah bin Zayd (Radhi
ya Allaah iwe juu yao), wala hawakupewa majina maalumu. Haya yameelezwa na
Abuu Daawuud kwa mapokezi sahihi juzuu ya pili (2) ukurasa wa 69.
Hatua
Ya Kwanza:
Maiti itavuliwa nguo kwa upole
na kufunikwa shuka ndefu baada ya kumfumba macho kama ilivyopokewa na Imaam
Muslim, Ahmad na Al-Bayhaqiy kitabu cha tatu (3) ukurasa wa 334 na kama
alivyoeleza Shaykh al-Albaaniy katika Ahkaamul Janaaiz ukurasa wa 12 katika
Hadiyth ya Ummu-Salamah amesema:
“Aliingia Mtume (Rehma na amani ya Allaah ziwe juu yake)
kwa Abu-Salama akamkuta macho yake yapo wazi akamfumba, kisha akasema “ hakika
roho inapotolewa macho huifuata iendapo…”
Huu ni uthibitisho wa
mwongozo sahihi wa Uislamu katika kumuosha maiti, si kama wanavyodai maadui wa
Uislamu.
Hatua
Ya Pili:
Baada ya kuvuliwa nguo,
haraka iwezekananvyo, maiti itaoshwa. Yataandaliwa maji ambayo yatakuwa
yamechanganywa na majani ya mkunazi[1][2] na kaafuur. Maji si lazima yawe ya moto, ila
ikiwa kuna baridi kali maji yawe ya uvuguvugu. Atakayesema kuwa maji lazima
yawe ya moto, huyo ni muongo kwani haya yameelezwa katika vitabu vya
kishaafi’iy kama kitabu cha shekhe ‘Abdullaah bin Abdir-Rahmaan al-Hadharamiy
(850-918) ukurasa wa 48 hadi 49, katika mlango wa Al-Janaaiz.
Maiti ataoshwa majosho
matatu au matano kulingana na hali halisi ya maiti huyo. Hii ni kutokana na
Hadiyth iliyosimuliwa na Ummu ‘Atwiyah kuwa:
“Aliingia Mtume (Rehma na amani ya Allaah ziwe juu yake)
wakati tukiwa tunamuosha binti yake, Zaynab, akasema: Muosheni mara tatu au
mara tano au mara saba au zaidi ya hapo ikiwa mtaona haja ya kufanya hivyo....”[1][3]
Ikiwa maiti ni wa kiume,
nywele zake zitaachwa kama zilivyo ila zitaoshwa vizuri na wala hakitakatwa
chochote kwenye mwili wake, si nywele wala kucha. Na ikiwa maiti ni wa kike,
nywele zake zitafumuliwa ikiwa zimesukwa, kisha zitaoshwa, halafu zitasukwa
tena njia tatu zikielekezwa kisogoni mwake. Na hii ni kutokana na Hadiyth
iliyosimuliwa na Ummu ‘Atwiyah.[1][4]
Hatua Ya Tatu:
Ndugu msomaji, muoshaji
atafunga kitambaa au atavaa kitu chochote mkononi mfano wa glovu, kisha ataosha
sehemu za siri za maiti, baada ya kumpapasa tumboni kwa taratibu, ili kuondoa
uchafu ulio karibu kutoka. Muoshaji atayafanya hayo bila kuangalia uchi wa
maiti. Ni uzushi na ni uongo mkubwa kudai kuwa maiti wa Kiislamu hukamuliwa kwa
Nguvu tumboni, kwani kufanya hivyo ni kinyume na mafundisho sahihi ya Uislamu.
Muoshaji atatupa kitambaa
cha kwanza, kisha atachukua kingine na kuanza kusafisha meno ya maiti, baada ya
kulowanisha kitambaa hicho kwa maji. Baada ya hapo, muoshaji na msaidizi wake
watamtawadhisha[1][5] maiti, Wudhuu kamili. Watayafanya hayo yote kwa
kuanzia kuliani kwa maiti na kumalizia kushotoni kwa maiti. Kwa mfano, wataosha
mkono wa kulia halafu wa kushoto na mfano wa hayo.
Ndugu msomaji, fahamu kuwa
maiti haitaingizwa maji mdomoni au masikioni au popote pale kwani hakuna
ushahidi wowote juu ya hilo katika mafundisho ya Uislamu. Yeyote atakayeleta
madai ya namna hii una haki ya kumtaka atoe ushahidi juu ya hilo.
Baada ya kutawadhishwa,
maiti ataoshwa mwili wote mara tatu, tano, saba au zaidi ya hapo, kama
tulivyoelezea hapo nyuma. Atamwagiwa maji upande wa kulia, kisha upande wa
kushoto na kuoshwa vizuri kabisa. Na iliyo bora ni kuchanganya maji ya kuoshea
kwa majani ya mkunazi kama tulivyokwisha elezea hapo awali katika Hadiyth ya
Ummu ‘Atwiyah. Lililo bora katika osho la mwisho ni kuchanganya maji na kaafuur.
Hii ni aina ya manukato yanayowekwa kwenye maji.
Kufikia hapa ndugu msomaji,
tunataraji utakuwa umefahamu usahihi wa kuosha maiti, japo kwa ufupi.
Pamoja na hayo, ndugu
msomaji, una haki ya kufahamu mambo yafuatayo:
Hataoshwa maiti aliyekufa
shahidi[1][6], bali atazikwa na nguo zake hizohizo. Hii ni
kutokana na dalili nyingi, miongoni mwazo ni ile Hadiyth ya Jaabir (Radhi za Allaah ziwe juu yake) pale
Mtume (Rehma na amani ya Allaah ziwe juu
yake) aliposema kuwaelekeza katika kuwazika Maswahaba[1][7] waliofariki katika vita ya Uhudi kuwa, “Wazikeni na damu zao…”[1][8]
Fahamu pia kuwa, aliyekufa
hali ya kuwa amehirimia (ameshakuwa tayari na amekusudia) kufanya hija, mtu
huyo naye hatapakwa manukato wala hatafunikwa kichwa chake.
Ikiwa maiti itaharabika
kutokana na namna ya kifo chake, kama vile kutokana na ajali ya gari, kuungua
moto, kuangukiwa na nyumba, n.k, basi maiti huyo atatayamamishwa (yaani badala
ya kutumika maji utatumika udongo ulio safi na twahara), na kama itashindikana
basi, uwajibu (ulazima) wa kufanya hivyo
utaondoka. Allaah, Mtukufu,
anasema katika Qur-aan 2:286:
لا يُكَلِّفُ اللَّـهُ
نَفْسًا إِلا وُسْعَهَا
“Allaah Haikalifishi
(hailazimishi) nafsi ila kwa yaliyo sawa na uwezo wake…”
Pia Wanachuoni wa kanuni za
Fiqh (Usuul al-Fiqhi) wana msemo usemao:
“Hakuna uwajibu endapo hauwezekani
(hautekelezeki)…” (La waajiba ma’al ‘ajzi). Na Allaah ni Mjuzi zaidi.
Hutokea baadhi ya nyakati
kuwa, mathalani, mtu kafariki na baadhi ya viungo vyake, kama mikono au mguu, vimekosekana.
Na maiti huyu ameoshwa, kaswaliwa, na hatimaye kuzikwa akiwa hana viungo vyote.
Mara tu baada ya kuzikwa kikaonekana kiungo au baadhi ya viungo
vilivyokosekana, Je, kiungo au viungo
hivyo vitaoshwa na kuswaliwa? Ndugu msomaji, suala hili aliwahi kuulizwa
Shaykh Muhammad bin Swaalih Al-‘Uthaymiyn[1][9] (Allaah Amrehemu),
akajibu:
“Viungo vidogo vidogo kama
mikono na miguu vitakapopatikana na maiti ameshaswaliwa, viungo hivi
havitaoshwa wala kuswaliwa kwa kuwa ameshaswaliwa.”
Akaendelea kusema:
“Ama itakapokuwa maiti
haikupatikana bali kimepatikana kiungo katika mwili wake kama vile kichwa au
mguu au mkono, basi kitaswaliwa na kuzikwa kilichopatikana baada ya kuoshwa
vizuri na kuvishwa sanda[1][10].
Mpaka hapa tuna imani kuwa
tumeondoa kiu yako juu ya moja kati ya mambo mane anayopaswa kufanyiwa maiti.
Hatua inayofuata baada ya hii ni kuvishwa sanda.
Kuvishwa
Sanda
Baada ya maiti kuoshwa
vizuri, hatua inayofuata ni kuvishwa sanda, nguo au shuka ndefu yenye uwezo wa
kufunika mwili wote wa maiti. Ni bora zaidi na inapendeza shuka hiyo ikiwa
nyeupe. Na hii ni kutokana na Hadiyth sahihi ya Mtume (Rehma na amani ya Allaah ziwe juu yake) aliposema:
”Pendeleeni kuvaa mavazi
meupe kwani hayo ni katika mavazi bora kwenu na mukafini (muwavishe) maiti wenu
kwa hizo sanda.”[1][11]
Sanda huwa ni shuka tatu
(3) tu, na si zaidi, kutokana na Hadiyth iliyosimuliwa na mama wa Waumini
‘Aaishah (Radhi ya Allaah iwe juu yake) aliyesema:
“Mtume (Rehma na amani ya Allaah ziwe juu yake) alikafiniwa (alivishwa
sanda) katika nguo tatu…”[1][12]
Ndugu msomaji, hakuna
tofauti kati ya sanda ya maiti mume na sanda ya maiti mke, na hii ni kutokana
na kukosekana ushahidi sahihi juu ya hilo, na kama upo, basi ni Hadiyth ambazo
hazikusihi upokezi (sanadi) wake. Mfano wa Hadiyth dhaifu inayotumiwa na baadhi
ya watu ni Hadiyth ya Layla bint Qaaif Ath-Thaqafiy inayoeleza kuwa sanda ya
kike ni nguo tano zikiwa shuka mbili, kikoi, kanzu, na kilemba. Hadiyth hii
upokezi (isnadi) yake ni dhaifu. Ndani ya msururu wa wapokezi (isnadi) kuna mtu
mmoja, anaitwa Nuuh bin Haakim Ath-Thaqafiy, ambaye hajulikani zaidi ya jina
lake tu, kama alivyoelezea al-Haafidh bin Hajar na wengineo[1][13].
Uandaaji
Wa Sanda
Shuka hizo kwa ajili ya
sanda zitatandikwa sehemu safi. Kisha zitafukizwa udi na manukato mazuri mara
tatu, kama alivyoelekeza Mtume (Rehma na
amani ya Allaah ziwe juu yake):
“Mtakapoweka manukato ya
maiti basi wekeni mara tatu.”[1][14] Isipokuwa sanda ya aliyehirimia kufanya hija
haitapakwa manukato wala haitafukizwa udi.”
Hii imeesimuliwa na Ibn
‘Abbaas (Radhi ya Allaah iwe juu yake)
kwamba Mtume (Rehma na amani ya Allaah
ziwe juu yake) amesema:
“…Msimpake manukato wala
msimfunike kichwa chake kwani huyo atafufuliwa siku ya kiama hali ya kuwa
analeta talbiya”[1][15] (Al-Bukhaariy na Muslim).
Baada ya kutandikwa sanda,
maiti atalazwa juu yake. Itachukuliwa ncha ya upande wa kulia na iletwe hadi
kifuani mwake, na ncha ya kushoto itafanywa hivyo hivyo. Utaratibu huo
utafuatwa kwa shuka ya pili na ya tatu. Kisha itachukuliwa kuanzia kichwani na
itafungwa na miguuni pia itafungwa. Pia itawekwa pamba iliyolowanishwa manukato
mazuri na itawekwa juu ya macho yake na mdomoni mwake kama alivyoelekeza Shaykh
Ibn ‘Uthaymiyn. Mpaka hapa, maiti itakuwa tayari kwa ajili ya kutekelezewa
jambo la tatu ambalo ni kuswaliwa.
Kumswalia
Maiti
Ndugu msomaji, ni wajibu
kumswalia kila maiti wa Kiislamu isipokuwa hawa wafuatao:
1. Mtoto mdogo ambaye
hajafikia kubalehe. Na hii tunaipata katika Hadiyth iliyosimuliwa na bi Aaisha
(radhi ya Allaah iwe juu yake) kuwa:
“Alikufa Ibraahim mtoto wa
Mtume wa Allaah na hali ya kuwa ana miezi minane na Mtume hakumswalia.”[1][16]
2. Mtu aliyekufa shahidi
(aliyekufa vitani) kwani Mtume (Rehma na
amani ya Allaah ziwe juu yake) hakuwaswalia waliokufa katika vita vya Uhud.
Ndugu msomaji, fahamu kuwa
tunaposema kuwa si wajibu kuwaswalia watu wa aina hii hatuna maana kuwa ni
haraam kuwaswalia, bali tunamaanisha kuwa hakuna ulazima au uwajibu wa hilo.
Lakini wakiswaliwa inafaa kwa kuwa kuna ushahidi juu ya hilo kama alivyosimulia
‘Aaishah, mama wa waumini, anayesimulia:
“Aliletwa mtoto kwa Mtume wa
Allaah (Rehma na amani ya Allaah ziwe juu
yake) miongoni mwa watoto wa answaar (watu wa Madiynah) na Mtume
akamswalia”.[1][17]
Ndugu msomaji, ni matarajio
yetu kuwa utangulizi huu utakuwa ni mwanzo wa kuifahamu vizuri Swalah ya
Jeneza.
Namna
Ya Kumswalia Maiti
Maiti huswaliwa kwa kufuata
utaratibu huu:
Atasimama Imaam (kiongozi
wa Swalah) upande wa kichwa, kama maiti ni mwanaume, na hii imethibiti katika
Hadiyth ya Abu Ghaalibi al-Khayyaat, amesema:
“Nimemshuhudia Anas bin
Maalik akiswalia maiti ya kiume akasimama usawa wa kichwa chake.”
Pia Imaam atasimama usawa
wa katikati wa ikiwa maiti ni mwanamke, kama ilivyothibiti katika Hadiyth ya
Samurah bin Jundub, anasema:
“Nimeswali nyuma ya Mtume (Rehma na amani ya Allaah ziwe juu yake)
naye akimswalia mama wa Ka’ab….akasimama katikati yake.”
Kisha, Imaam ataleta
takbira kwa kusema, ‘Allaahu Akbar’, (Allaah ni mkubwa) mara nne au tano au
tisa, kwani aina zote hizi zimethibiti kutoka kwa Mtume (Rehma na amani ya Allaah ziwe juu yake). Lakini mara nyingi Mtume (Rehma na amani ya Allaah ziwe juu yake)
alileta takbira nne (4).
Katika takbira ya kwanza,
itasomwa suratul-Faatihah, baada ya kumlaani Shaytwaan, bila kudhihirisha
sauti.
Katika takbira ya pili,
itasomwa Swalah ya Mtume kwa ukamilifu wake.
اَللّهُمَّ صَلِّ عَلَى مُحَمَّدٍ وَعَلَى آلِ مُحَمَّدٍ كَمَا
صَلَّيْتَ عَلَى اِبْرَاهِيمَ وَعَلَى آلِ اِبْرَاهِيمَ و بارك على محمدٍ وعلى آلِ
محمدٍ كما باركتَ على إِبراهيم وعلى آلِ إبراهيمَ إِنَّكَ حَميدٌ مَجيد
Katika takbira ya tatu
itasomwa du’aa ya kumuombea maiti, nazo ni nyingi zilizothibiti kutoka kwa
Mtume (Rehma na amani ya Allaah ziwe juu
yake).
Katika takbira ya nne,
ambayo ni ya mwisho, itasomwa du’aa yoyote au atanyamaza (anayeswali) na kisha
atatoa salamu. Namna zote hizi mbili zimethibiti.[1][18]
Ndugu msomaji, ni muhimu
ufahamu kuwa kuna nyakati tatu muhimu ambazo haifai kuswali ndani yake ila kwa
dharura. Nyakati hizo zimebainishwa katika Hadiyth ya ‘Uqbah bin ‘Aamir (Radhi ya Allaah iwe juu yake)
anayesimulia:
“Alikuwa Mtume (Rehma na
amani za Allaah iwe juu yake) anatukataza kuswalia au kuzika maiti katika
nyakati tatu:
Kwanza - wakati wa kuchomoza
jua mpaka linyanyuke juu,
Pili – wakati anaamka
aliyelala qayluulah (yaani saa 6:00 mchana wakati jua linapokuwa utosini au
katikati mpaka lihame kuelekea upande wa Magharibi).
Tatu – wakati jua
linapokaribia kuzama mpaka lizame kabisa.”[1][19]
NB: Suala hili lina
mitazamo tofauti miongoni mwa wanachuoni wa Ahlus Sunnah wal-Jama’ah[1][20] juu ya kufaa kuswalia jeneza na kuzika katika
nyakati hizi. Lakini wengi kati yao wanaliona hilo halipendezi kishari’ah
(makruhu) nao ni kama vile ‘Atwaa, An-Nakha’iy, Al-Awza’iy, Ahmad, Is-haaq, na
Ath-Thawriy. Ash-Shaafi’iy yeye anaona kuswalia wakati wowote na kuzikwa inafaa[1][21]. Kauli
ya jamaa (ya kwanza) ni bora kwa kuwa imeafikiana na Hadiyth.
Kuzikwa
Jambo la nne analopaswa
kutekelezewa maiti ni kuzikwa. Kaburi ni lazima liwe refu kwenda chini na liwe
pana. Kina cha kaburi kiwe sawa na kimo cha mtu mzima na kunyoosha mkono, na
litachimbwa kiasi maiti akilazwa kwa ubavu wa kulia atakuwa anaelekea Qiblah[1][22].
Kaburi likiwa tayari, maiti
atachukuliwa katika jeneza na kuwahishwa katika kaburi. Wakati wa kusindikiza
jeneza (kumpeleka maiti kaburini), mambo yafuatayo yanapaswa kuchungwa:
Kwanza, lisifuatwe jeneza kwa sauti wala kwa moto.
Mtume (Rehma na amani ya Allaah ziwe juu
yake) amesema katika Hadiyth iliyosimuliwa na Abu Hurayrah:
“Msifuate jeneza kwa sauti
wala kwa moto.”[1][23]
Hapa inamaanisha sauti
yoyote ya mwanadamu. Pia haifai kubeba chetezo cha ubani chenye moto wakati wa
kusindikiza jeneza.
Pili, jeneza lisifunikwe na chochote. Kufunika jeneza au kaburi wakati wa
kuzika ni miongoni mwa mambo yasiyokuwa na ushahidi[1][24]. Baada ya maiti
kuwasilishwa kaburini, watatakiwa watu baadhi washuke ndani ya kaburi, na iliyo
bora zaidi ni kuwa watakaoingia ndani ya kaburi wawe ndugu wa marehemu.
Allaah Mtukufu Anasema:
وَأُولُو الأرْحَامِ
بَعْضُهُمْ أَوْلَىٰ بِبَعْضٍ فِي كِتَابِ اللَّـهِ ۗ إِنَّ اللَّـهَ بِكُلِّ
شَيْءٍ عَلِيمٌ
“Na jamaa wa nasaba
wanastahikiana wenyewe kwa wenyewe zaidi (katika kurithiana na mambo mengineyo)
katika Kitabu cha Allaah. Hakika Allaah ni Mwenye kujua kila kitu”[1][25]
Maiti atalazwa kama
tulivyoelezea katika uandaaji wa kaburi, huku wakisema wanaomlaza maiti kwenye
mwana-ndani:
“Kwa jina la Allaah na juu
ya mila ya Mtume wa Allaah” au “Kwa jina la Allaah na juu ya Sunnah ya Mtume wa Allaah.” Haya yamethibiti kwa
riwaya zote.
Wanaotakiwa kuyasema maneno
haya ni wale wanaomuweka maiti katika mwanandani (sehemu ndogo inayochimbwa
ndani ya kaburi kwa ajili ya kumlaza maiti kwa ubavu wake wa kulia) na sio
walio juu ya kaburi. Haya yameelekezwa na Mtume (Rehma na amani ya Allaah ziwe juu yake) katika Hadiyth
iliyosimuliwa na Swahaba mtukufu Al-Bayadhi kuwa:
“Maiti anapolazwa katika
kaburi basi aseme yule anayemuweka katika kaburi wakati wa kumuingiza katika
mwanandani; Kwa jina la Allaah na kwa ajili ya Allaah na juu/kwa kufuata mila
ya Mtume wa Allaah.”[1][26]
Baada ya maiti kulazwa
katika mwanandani, kaburi litafukiwa na mwisho litainuliwa kiasi cha shibri[1][27] moja tu. Na hili linathibitika kutokana na
Hadiyth ya Jaabir (Radhi ya Allaah iwe
juu yake) amesema:
“Kwa hakika Mtume (Rehma na amani ya Allaah ziwe juu yake)
aliwekwa katika lahdi (mwanandani) na yakawekwa nyuma yake matofali na
likanyanyuliwa kaburi lake kiasi cha shibri moja.”[1][28]
Kujengea
Kaburi
Kwa taratibu na mafunzo
sahihi ya Kiislamu, kaburi halitajengewa. Haikupata kuonekana zama za Mtume (Rehma na amani ya Allaah iwe juu yake)
kaburi likajengewa na yeye akiwa hai, bali alionekana na kusikika kwa kinywa
chake akilikemea vikali suala hili. Dalili juu ya hili zipo nyingi, mojawapo ni
Hadiyth hii ambayo ameisimulia Abuu Ya’ala akisema,
“Amekataza Mtume wa Allaah
kujengwa juu ya kaburi na kukaa au kukanyaga juu yake na kuswali kwa kuyaelekea
makaburi.”[1][29]
Ndugu msomaji, jua ya
kwamba makaburi ya Baqiy (sehemu walikozikwa Waislamu wa mwanzo, Maswahaba)
mpaka sasa yapo na Waislamu wanaendelea kuzikwa katika eneo hilo. Waliojaaliwa
kwenda Hijja ni mashahidi kwani huwa wengi wanayazuru makaburi haya na hayajajengewa.
Suala la kujiuliza ni Je, kama makaburi hayo yangekuwa yanajengwa ingewezekana
leo kuwepo eneo la kuzikia hadi sasa? Hasa ukizingatia kuwa kutoka Mtume (Juu yake rehma na amani ya Allaah)
alipokufa mpaka sasa ni zaidi ya miaka 1400 imeshapita? Ni wazi kuwa
kusingekuwa na nafasi tena ya kuzikia.
Kwa msingi huu tunatumia
fursa hii kumuusia kila asomaye Makala haya kuwa maiti hanufaiki na na wala
hana haja na vitu vya duniani, si vigae, marumaru, wala jengo la aina yoyote
katika kaburi, bali anachohitaji zaidi maiti ni du’aa yako. Mkumbuke, kisha
muombee msamaha kwa Allaah Ampunguzie adhabu za kaburi bila kutumia utaratibu
maalum, hapo utakuwa umemfanyia jambo kubwa sana.
Kutokana na Hadiyth
tuliyoinukuu punde tunajifunza mambo kadhaa ambayo huwa tunayafanya bila kujua
ubaya wake. Mfano wa hayo ni kama kukalia na/au kukanyaga makaburi. Haya
tunayashuhudia wakati maiti anapofikishwa katika eneo la makaburi, watu
husimama juu ya makaburi na wengine huyakalia. Hili ni suala la kuwa makini
nalo na kujichunga wakati tukiingia makaburini tusiyakanyage wala kuyakalia.
Kuzika
Maiti Msikitini
Ndugu msomaji, miongoni mwa
makatazo ni kuzika maiti Misikitini. Imekuwa kasumba ya baadhi ya watu kuacha
wasia kuwa wakifa wazikwe Misikitini kwa kuwa pengine wao ndiwo waliotoa maeneo
yaliyojengwa Misikiti hiyo au vinginevyo. Hii inawapelekea watu kuswali kwa
kuyaelekea makaburi, jambo ambalo limekatazwa na shari’ah ya Kiislamu. Jambo
hili limekuwa ni fitna kubwa miongoni mwa Waislamu kwani miongoni mwa madhara
makubwa yatokanayo na jambo hili ni kwa watu kuanza kuomba na kufanya tawassul
(kumuomba Mola kupitia makaburi hayo) na hatimaye kuabudiwa kabisa makaburi
hayo. Haya ni masikitiko makubwa.
Aliulizwa mmoja wa
wanachuoni, Shaykh Ibn ‘Uthaymiyn kuwa ni ipi hukumu ya Swalah kwenye Msikiti
wenye kaburi?
Akajibu akasema,
“Ikiwa kaburi limeutangulia
Msikiti (yaani kaburi lilikuwepo kabla Msikiti haujajengwa) basi ni wajibu
kuuhama Msikiti huo na ubomolewe na liachwe kaburi. Na kama Msikiti
umelitangulia kaburi basi ni wajibu kufukuliwa (kuhamishwa) kaburi hilo na
maiti akazikwe makaburini.”
Pia Shaykhul Islaam
amesema,
“Wala haitaswihi (haitafaa)
Swalah kwenye makaburi au kwa kuyaelekea makaburi, na katazo hili ni kwa kuziba
mianya ya shirki”[1][30]
Kuhusu
Kaburi La Mtume (Rehma Na Amani Ya Allaah Ziwe Juu Yake)
Maswali huja kuwa mbona
kaburi la Mtume (Rehma na amani ya Allaah
ziwe juu yake) liko ndani ya Msikiti na limejengewa? Katika kulifafanua
hili inahitajika kwa wewe msomaji kuzingatia kwa umakini, kwani jambo hili
linatatiza wengi katika watu.
Historia inaonesha kuwa
Msikiti wa Madiynah haukujengwa juu ya kaburi lolote kwani Msikiti ulijengwa
mwaka wa kwanza wa Hijrah (mwaka wa Kiislamu) na wakati huo Mtume (Rehma na amani ya Allaah ziwe juu yake)
akiwa hai.
Pia haikushuhudiwa kuwa
Mtume (Rehma na amani ya Allaah ziwe juu
yake) aliwahi kumzika yeyote katika Maswahaba zake katika Msikiti.
Tatu, Mtume (Rehma na amani ya Allaah ziwe juu yake)
hakuzikwa ndani ya Msikiti, na yeye mwenyewe alikemea hilo la kuzika watu
Misikitini kwa kusema katika Hadiyth iliyosimuliwa na ibn Mas’uud (Allaah
amuwie radhi) kuwa,
“Hakika miongoni mwa viumbe
waovu ni wale ambao kitafika Qiyamah hali ya kuwa wapo hai na wale ambao wameyaweka
makaburi Misikitini (wamezika watu ndani ya Misikiti).”[1][31]
Maswahaba ni mfano bora wa
kuigwa kwani wao waliyazingatia vilivyo na kuyafanyia kazi maneno na mafunzo ya
Mtume (Rehma na amani ya Allaah ziwe juu
yake), kiasi waliweza kufikia kutoa mali zao na nafsi zao kwa ajili yake.
Unaweza kujiuliza, inawezekana kweli watu hawa (Maswahaba) wakakiuka maelekezo
ya Mtume (Rehma na amani ya Allaah ziwe
juu yake) na hatimaye wamzike Msikitini? Kama hawakumzika Msikitini, je ni
nani aliyeliingiza kaburi la Mtume (Rehma
na amani ya Allaah ziwe juu yake) Msikitini, na wapi lilikuwa kabla?
Jawabu ni kuwa
aliyeliingiza Msikitini kaburi la Mtume (Rehma
na amani ya Allaah ziwe juu yake) ni ‘Umar bin Abdil-‘Aziyz kwa amri ya
mtawala wa zama hizo aitwaye Al-Waliyd bin ‘Abdil-Malik katika mwaka wa 88 H.
Inafahamika kuwa nyumba ya
Mtume (Rehma na amani ya Allaah ziwe juu
yake) ilikuwa inapakana na Msikiti kwa kutengwa na ukuta mmoja upande wa
kushoto na hasa chumba cha Bibi ‘Aaishah (Allaah awe radhi naye) ambacho ndiko
alikozikwa Mtume (Rehma na amani ya
Allaah ziwe juu yake), pamoja na Maswahaba zake wawili, Abu Bakr na ‘Umar
(Allaah awawie radhi wote wawili). Baada ya Msikiti kupanuliwa, makaburi hayo
yakaingia/yakaingizwa Msikitini, na hii ni kwa sababu Al-Waliyd bin
‘Abd-l-Malik alikuwa hana elimu juu ya hilo. Baadhi ya wafuasi wa Maswahaba
(Taabi’iyn) walipojaribu kulipinga hilo walionekana hawana kauli. Miongoni mwao
ni Sa’iyd bin al-Musayyib, yeye alijaribu kushauri kuwa basi chumba cha Bibi
‘Aaishah (Allaah awe radhi naye) (mke wa Mtume), ambako alizikwa Mtume (Rehma na amani ya Allaah ziwe juu yake)
kisiingizwe ndani ya Msikiti, bila mafanikio. Kwa kuwa Al-Waliyd alikuwa ndiye
mwenye mamlaka, akamlazimisha ‘Umar bin ‘Abdil-Aziyz kubomoa ukuta uliokuwa
unatenganisha makaburi hayo na Msikiti na kwa hiyo makaburi yakajumuishwa ndani
ya Msikiti. Kwa ufafanuzi huu mfupi, ni wazi kuwa hakuna hoja ya kudai kuwa
inafaa kuzika au kujengea makaburi.[1][32]
Kuwekea
Alama Makaburi
Je, ni namna gani unaweza
kulitambua kaburi au kuliwekea alama kaburi? Hilo linajibiwa katika Hadiyth
iliyosimuliwa na Swahaba mtukufu Al-Muttwallib bin Abi Wadaa (Allaah amuwie
radhi) kuwa, pindi alipokufa ‘Uthmaan bin Madh’uun, ndugu wa Mtume (Rehma na amani ya Allaah ziwe juu yake)
kwa kunyonya ziwa moja, baada ya kumaliza kufukia kaburi, Mtume (Rehma na amani ya Allaah ziwe juu yake)
alibeba jiwe na akaliweka upande wa kichwani kisha akasema,
“Nimeliweka jiwe hili ili
nipate kulijua kaburi la ndugu yangu na nizike pembeni yake atakayekufa katika
jamaa zangu”[1][33]
Baada
Ya Kuzika
Ndugu msomaji,
kinachofuatia baada ya kufunika kaburi ni kukaa kwa ajili ya kuwakumbusha
waliohudhuria mazikoni, kama alivyofanya Mtume (Rehma na amani ya Allaah ziwe juu yake) katika Hadiyth ya Al-Baraa
bin ‘Aazib iliyopokelewa na Jama’ah.[1][34]
Fahamu kuwa hakuna kitu
kinachoitwa talaqini baada ya maziko, kwani mapokezi juu ya jambo hilo ni
dhaifu na hayakusihi kabisa. Hadiyth inayozungumzia talaqini ni dhaifu na
haifai kuitumia katika hoja, na yeyote anayefanya talaqini anahesabika kuwa ni
mzushi[1][35].
Mtume
(Rehma Na Amani Ya Allaah Ziwe Juu Yake)
Alikuwa Akifanya Nini Alipomaliza Kuzika?
Mtume (Rehma na amani ya Allaah ziwe juu yake) akishamaliza kuzika (yaani
baada ya kufukia kaburi) alikuwa akisimama na kisha husema maneno haya:
“Muombeeni msamaha ndugu
yenu na mumuombee uthabiti, kwani hakika sasa hivi anaulizwa maswali”[1][36] kama ilivyokuja katika
Hadiyth ya ‘Uthmaan bin ‘Affaan.
Pia ifahamike kuwa, haifai
kwa Muislamu kuzikwa katika makaburi ya wasiokuwa Waislamu, wala wasiokuwa
Waislamu kuzikwa katika makaburi ya Waislamu[1][37].
Kufikia hapa mpendwa
msomaji, tunataraji kuwa, kwa mapenzi ya Allaah, utakuwa umefahamu, japo kwa
ufupi, ukweli kuhusu mazishi sahihi ya Kiislamu.
Tunataraji pia kuwa,
utakuwa umebaini uzushi na uongo kuhusu mazishi ya Kiislamu. Utaufahamu uongo
huo pale utakapoona au kusikia watu wanasema au kufanya kinyume na haya
tuliyoeleza, halafu yakawa hayana ushahidi, au ushahidi upo lakini ni dhaifu.
Tukupe changamoto ndugu
msomaji, pindi ikitokea unahudhuria muhadhara wake, fanya kumuomba akupe
ushahidi kutoka katika Qur-aan au katika Hadiyth za Mtume, kama ambavyo
tumekuwa tukibainisha katika makala hii. Hapo ndipo utakapogundua hila yake
yeye pamoja na wengine wanoupaka matope Uislamu.
Fahamu pia kuwa, ibada
yoyote utakayoona inafanywa na Muislamu lazima iwe na uthibitisho kutoka kwa
Mtume (Rehma na amani ya Allaah ziwe juu
yake), kinyume chake huo utakuwa ni uzushi katika dini.
Tunamuomba Allaah Ajaalie
Makala hii iwe chachu ya Waislamu kuipenda dini yao na kujifunza na
kuyatekeleza yaliyo sahihi katika dini.
Tunamuomba Allaah Atusamehe
madhambi yetu na walio kufa kabla yetu katika Imani.
Na Allaah
Ndiye Mjuzi zaidi.
Imeandaliwa
Na Vijana Wa Kiislamu Musoma-Tanzania
[1][1] Sunnah ni matendo aliyoyafanya Mtume
Muhammad (Rehma na amani ya Allaah ziwe juu yake) au aliyoyashuhudia
yakifanywa.
[1][2] Aina ya majani yanayochanganywa katika maji…
[1][3] Al-Bukhaariy (3/99-104), Muslim (3/47-48), Abuu
Daawuud (2/60-61), An-Nasaaiy (1/266-267)
[1][4] Shaykh Al-Albaaniy katika Ahkaamul Janaaiz uk.
48, Shaykh Bin ‘Uthaymiyn katika Min Ahkaam Al-Fiqhiyah, uk. 68.
[1][5] Kutawadha (Wudhuu) ni utaratibu maalum wa kuosha
viungo vya mwili, viganja vya mikono, kusukutua, kusafisha pua, kuosha uso,
kuosha mikono miwili mpaka vifundoni, kupaka maji kichwani na kusafisha
masikio, kuosha miguu miwili mpaka kwenye kongo za miguu, pale Muislamu
anapotaka kutekeleza ibada yoyote maalum.
[1][6] Shahidi ni mtu aliyekufa katika Jihaad, vita
takatifu ya kuupigania Uislamu. Kujilipua kwa kujitoa muhanga haifai katika
Uislamu na anayekufa katika hali hii si shahidi, wala si katika Jihaad
kujihusisha na vitendo vya kigaidi.
[1][7] Maswahaba ni wafuasi wa mwanzo waliomkubali
Mtume na ni wa mwanzo kuukubali na kuueneza Uislamu.
[1][8] Al-Bukhaariy 3/165, An-Nasaaiy 1/277,
[1][9] Alizaliwa nchini Saudi Arabia sehemu iitwayo
‘Unayzah tar. 27 Ramadhaan 1347H na kufa 15 Shawwal 1421H.
[1][10] Fataawa Arkaanil Islaam uk. 406.
[1][11] Imepokelewa na Jamaa: Abuu Daawuud 2/176,
At-Tirmidhiy 2/132, na wengineo kama Bin Maajah, al-Al-Bayhaqiy na Al-Haakim.
[1][12] Imepokelewa na maimamu sita na Al-Bayhaqiy na
Ahmad katika Hadiyth namba, 93. Imesahihishwa na Al-Albaaniy.
[1][13] Nisbur Raayat 2/258
[1][14] Al-Albaaniy katika Ahkaamul Janaaiz uk 64 chapa
ya Beirut ya mwaka 1406H sawa na 1966AD.
[1][15] Talbiyah ni matamshi maalum ayasemayo anayehiji
wakati wa kuhiji.
[1][16] Abuu Daawuud 2/166, Bin Hazm 5/158, Ahmad 6/267
na wengineo.
[1][17] Muslim 9/55, An-Nasaaiy 1/476, Tazama pia
kitabu Ahkaamul-Janaaiz uk. 80 – 82.
[1][18] Ahkaamul Janaaiz Uk. 123.
[1][19] Muslim 2/208, Abu ‘Awaanah ameisahihisha,
1/396.
[1][20] Ahlus Sunnah: Waislamu wenye kufuata mafundisho
ya Uislamu kulingana na Qur-aan, Sunnah, na (wakafuata njia ya) ufahamu na
walivyouelewa Maswahaba na wafuasi wao kutoka katika watangulizi wetu wema.
[1][21] Ahkaam uk. 131 katika maandishi madogo chini ya
ukurasa.
[1][22] Qiblah ni muelekeo ambao Waislamu huelekea
wanapokuwa wanaswali au kuchinja, nao ni mwelekeo ulipo mji mtukufu wa Makkah.
[1][23] Ahmad 2/427,528,532
[1][24] Abu Shaamah katika kitabu Al-Baa’ithu ‘alaa
inkaari al-Bid’ah uk. 67
[1][25] Qur-aan 8:75
[1][26] Al-Haakim na ameipa daraja ya Hasan katika
Ahkaam uk 152.
[1][27] Shibri ni kipimo cha kiganja kimoja…
[1][28] Ibn Hibbaan katika sahifa yake uk.2160,
Al-Bayhaqiy 3/410, na isnadi ya Hadiyth ni hasan (nzuri).
[1][29] Amepokea Imam Al-Haythamiy katika Majmu’
Az-Zawaaid 3/61 na amesema wapokezi wa Hadiyth hii ni waadilifu.
[1][30] Ikhtiyaarat al-‘Ilmiyya uk. 25
[1][31] Ibn ‘Uthaymiyn katika Fataawa uk. 302. Ahmad
1/405-435.
[1][32] Fataawa uk. 301
[1][33] Abu Daawuud 2/69, Al-Bayhaqiyy 3/412, Ahkaam
uk. 155.
[1][34] Ahkaam uk. 156 - 159
[1][35] Tazama kitabu Zaadul-Ma’aad cha bin-al-Qayyim
1/206, tazama pia kitabu Subulus Salaam cha Imaam Asw-Swana’aniy 2/161.
[1][36] Abu Daawuud 2/70, Al-Haakim 1/370, na
Adh-Dhahabiy ameikubali.
[1][37] Ahkaam uk. 136
No comments:
Post a Comment