Tuesday, June 17, 2014

WANAUME WANAOWEKA SIMU MFUKONI HATARINI KUPOTEZA KIZAZI






Tathmini ya utafiti kutoka chuo kikuu cha Exeter nchini Uingereza, inaonyesha kuwa kiwango cha mbegu za uzazi za wanaume huathiriwa kwa kuweka simu za mkononi kwenye mifuko ya suruali.

Hata hivyo, mwanasayansi wa maswala ya uzazi na shahawa, anasema kuwa ushahidi huo bado hauna uhakika wowote mpaka sasa

Uchunguzi huo uliochapishwa katika jarida la 'Environment International' umeonesha kuwa mnunurisho (radiation) wa kielectromagnetiki kuwa ndio chanzo kikuu kinachoathiri mbegu za wanaume.

Wataalamu walichanganua utafiti tofauti kuonyesha ubora wa shahawa wakihusisha wanaume 1,492.

Hii ilijumuisha kupimwa kwa shahawa zilizowekwa wazi kwa mnunurisho wa simu za rununu, kwa maabara na udadisi wa wanaume katika kliniki za uzazi

Kiongozi wa uchunguzi huo Dkt.Fiona Mathews amesema kuwa kutokana na uchunguzi huo,mmoja tu ndio ulionyesha uhusiano kati ya utumizi wa simu na kudidimia kwa ubora wa shahawa.

"Nafikiri kwa mwanamume wa makamu hakuna haja ya kuingiwa na hofu,iwapo unajua una uwezekano wa kuwa na shida ya kizazi basi itakuwa jambo la busara kutoweka simu mfukoni, pia kugeuza mtindo wako wa kula."

Aidha, amekubali kukosolewa na wanasayansi wengine huku akiunga mkono kuwa kuna umuhimu wa kufanya uchunguzi zaidi.

Dkt,Mathews amemaliza kwa kusema"hili ni jambo la kusisimua lakini hatusemi kwa uhakika kuwa kila anayebeba simu mfukoni atakuwa na shida ya kizazi."

Nae, Dkt.Allan Pacey kutoka chuo kikuu cha Sheffield amesema kuwa wazo hilo la kudidimia kwa shahawa na kuharibu "DNA" linatokana na mnunurisho wa kielectromagnetiki zinazopatikana kwenye simu na pengine joto aidha moja kwa moja kutoka kwenye simu au mnunurisho.

Dkt huyo anayefanya uchunguzi wa shahawa bado hajashawishika akisema ushahidi huo hauna msingi na ataendelea kuweka simu mfukoni.

Amedokeza kuwa "kumekuwa na shauku kwa mda kama kuweka rununu mfukoni kunaweza changia kudidimia kwa ubora wa shahawa na nguvu za kiume kivyovyote.

Ameongeza kwa kusema kuwa “hadi pale tutakapo tafakari hayo, nitaendelea kuweka simu yangu katika mfuko wa mkono wa kulia wa suruali yangu!"

No comments:

Post a Comment