NA MOHAMMED SAID
Hayo si maneno yangu. Ni maneno yaliyotoka kinywani mwa mmoja wa rafiki zangu wa kambi ya ''walioufyata'' ndani ya Bunge Maalumu la Katiba Dodoma. Nilimuuliza sahibu yangu huyu: ''Ilikuwaje nyinyi mliokuwa mkitoa cheche za moto vinywani na kunguruma kama Simba hapa Zanzibar kulalamikia mfumo uliopo wa Muungano, lakini mara mlipofika Dodoma mkageuka vipanya vilivyojikunyata kwa hofu ya mlio tu wa paka?''
Jibu
alilonipa ni hili: ''Sikiliza bwana, sisi hatuko tayari
kurudia kosa lililofanywa na waliotutangulia.'' Nikamuuliza kwa udadisi
mkubwa: ''Kosa gani hilo?'' Akasema: ''Ni kosa la kuchonga mdomo mbele
ya Watanganyika kwa
kujifanya watetezi wa Zanzibar na wapinzani wa Muungano uliopo.Umesahau
wewe yaliyomfika Aboud Jumbe mwaka 1984 na
waliomuunga mkono akina Brigedia Ramadhan Haji, Aboud Talib na Hafidh
Suleiman (Sancho) ambao wote walilazimika kujiuzulu baada ya yeye
kupelekwa machinjioni
na kusulubiwa Dodoma? Umeyasahau yaliyomfika huyo Seif Sharif mwaka 1988
huko
huko Dodoma na wenzake kadhaa, akiwemo marehemu Shaaban Khamis Mloo, Ali
Haji
Pandu, Hamad Rashid Mohammed, marehemu Sudi Yusuf Mgeni, marehemu Maulid
Makame
na wengineo? Ya karibuni tena ya kina UAMSHO na Mansour nadhani umeyaona
mwenyewe,'' aliendelea sahibu yangu huyo na kumalizia kwa kunambia:
''Kwa hivyo
sisi hatuko tayari kupoteza ulua wetu.''
Nikamwambia: ''Ina maana nyinyi mko radhi muendelee kuwa
watumwa wa Tanganyika na kuiacha Zanzibar iendelee kuwa koloni lake?'' Akacheka
na kusema: ''Watumwa tu? Haidhuru na tuwe hata watwana kwa Watanganyika, la
muhimu kwetu ni kuendelea kuwa mabwana kwa Wazanzibari. Tukiwaridhisha hao
unaosema mabwana zetu wa Tanganyika na kuendelea kuwa hewalla bwana kwao,
tutaendelea milele kutawala na kubaki madarakani Zanzibar na kuwa mabwana kwa
Wazanzibari. Na tukiondoka sisi watarithi watoto wetu, na ndio maana hatuko
tayari kuukubali mfumo wa serikali tatu kwa sababu ingawa ni kweli utakuwa na
maslahi kwa Zanzibar, lakini unahatarisha ulua wetu.''
Mimi
sikukomea hapo nikaendelea kumhoji: ''Sasa huku kuitwa
wasaliti wa Zanzibar, wasakatonge na vibaraka wa Tanganyika hakuziumizi
wala
kuzisononesha nyoyo zenu?'' Akaniambia:''Wacha watuite watakavyo, ni
maneno tu
hayo, sawa na kelele za mlango.'' Nikajaribu kumbana zaidi kwa
kumwambia: ''Lakini hata wanaokuungeni mkono nao pia wamejua kuwa
mnachojali zaidi ni
matumbo yenu, kwa hivyo na wao pia washaamka, mnaweza mkapoteza nafasi
zenu au
hata kushindwa katika uchaguzi wa mwakani.''
Nilitarajia hilo litamgusa na kumshtusha, lakini badala yake alicheka sana na kunambia: ''Watu wetu sisi wanahitaji dozi ndogo tu kuwaweka sawa na kuwarejesha kwenye msimamo. Nikamhoji: ''Dozi gani hiyo?'' Sahibu yangu akanambia: ''Ni ileile ya kasumba ya ''Usultani wa Waarabu utarudi na Mpemba hatawali. Tukishawapa dozi hiyo hawaelewi chochote, watakuwa radhi sisi tuendelee kuvimbisha matumbo yetu na wao waendelee kula dongo. Isitoshe madamu tumewatii hao unaosema mabwana zetu wa Tanganyika, hatuna hofu tena kwa ajili ya uchaguzi wa mwakani. Wewe mwenyewe si unajua, wakati ukiwadia, mbali na Polisi ya Muungano, ikilazimu hata jeshi la JWTZ litatinga hapa Zanzibar kuja kulinda ushindi wetu.'' Kwa kweli jibu lake liliniacha kinywa wazi nikabaki nayatafakari na kuyawaza yote aliyonieleza.
No comments:
Post a Comment