Makala haya yana jadili fasili ya
neno kwa mujibu wa wataalamu mbalimbali, ugumu wa fasili ya neno na kiini cha
utata huo. Katika kujadili hayo makala yatagawanywa katika sehemu tatu, sehemu
ya kwanza itaelezea maana ya neno kwa mujibu wa wataalamu mbalimbali, Sehemu ya
pili tutaelezea kiini cha ugumu huo, na sehemu ya tatu tutatoa hitimisho.
Mdee (2010:5) hueleza kwamba dhana
ya neno ina utata, kwani ni umbo lenye sura nyingi, utata huo hutokana na mitazamo
tofauti ya wanaisimu, kuhusu kipashio hiki kitahajia (jinsi linavyo andikwa),
kimatamshi na kimaana.
TUKI (2009) Hueleza kuwa neno ni
kipashio cha usemaji ambacho hujengwa na mwandamano au mkuroro wa sauti
zilizopangika kisilabi na ambazo hutambuliwa na wasemaji wa lugha inayohusika,
kuwa kitu kimoja chenye maana mahususi.
TUKI (2010) Huelezea kuwa neno ni
sauti au mkusanyiko wa sauti zinazotamkwa au kuandikwa pamoja na kuleta maana
Kwa mujibu wa Mdee (ameshatajwa) hueleza kuwa neno ni mfululizo wa herufi zilizo fungamana pamoja na kuzungukwa na nafasi tupu. (Mdee, amekwishatajwa)
Kwa upande wake Cruse (1986:3) kama
alivyo nukuliwa na Mdee, husema kuwa neno ni kipengele kidogo kabisa cha
sentensi ambacho kinaweza kuhamishwa kutoka nafasi moja kwenda nyingine bila
kuathiri sarufi ya lugha katika sentensi hiyo.
Vilevile neno huweza kuelezewa kama
kipashio cha lugha,kinachowakilisha taarifa kama vile , matamshi, maana, tabia
za kimaumbo na za kimuundo (Spencer, 1991)
Kiini cha ugumu wa kufasili neno
Zipo njia kadha za kisarufi ambazo
zinaweza kutumika katika kuelezea dhana ya neno na katika kugawa mipaka ya
maneno, miongoni mwa njia hizo ni, neno kama kipashio cha maana, neno kama
kipashio cha kifonetiki au kifonolojia na neno kama kipashio huru na kisicho
gawanyika (Rubanza, 2010). Ni vigumu kuwa na fasili toshelevu ya neno, sababu
kubwa au kiini cha....
ugumu huo ni kutokana na vigezo tofauti vinavyo tumika katika kulifasili neno ambavyo hutupa maana tofautitofauti, vigezo hivyo ni kama ifuatavyo;
ugumu huo ni kutokana na vigezo tofauti vinavyo tumika katika kulifasili neno ambavyo hutupa maana tofautitofauti, vigezo hivyo ni kama ifuatavyo;
Maana ya neno kiothografia, kigezo hiki huchukulia neno kuwa ni maandishi yanayo acha nafasi mwishoni, neno hudhihirika linapokuwa katika maandishi tu na lisiwe na nafasi katikati, kwa mfano, meneno ambatano kama vile; bwana-misitu, bata mzinga, tahajia kama hiyo huchukulia kuwa ni maneno mawili bila kuangalia kuwa maneno haya yana dhana moja. Rubanza (ameshatajwa) hueleza kwamba neno kiothografia ni mfuatano wa maandishi ambao huacha nafasi tupu mwishoni bila uwepo wa nafasi tupu katikati
Matatizo ya kigezo hiki
Hushidwa kuelezea maneno ambatani,
kwao uandikaji wa neno ambatani kwa kutenga au kuacha nafasi katikati
huchukulia kuwa ni maneno mawili. Hii sio sahihi kwani maneno ambatani huwa na
dhana moja hivyo hutakiwa kuchukuliwa kama neno moja.
Kigezo hiki kina dhima ndogo katika
uchambuzi wa kisarufi, hujihusisha tu zaidi katika namna ya kujifunza kuandika
lugha(Rubanza, ameshatajwa) T.Y. Kigezo hiki hakijihusishi na lugha ya maongezi
ambayo ndiyo inayotupa lugha ya maandishi.
Tatizo lingine ni kwamba zipo lugha
ambazo hazitengi maneno yake katika uandishi wake, swali ni kwamba hapa
utafasili je neno? Kwa mfano lugha kama Kigreenland “uluminippuq” maana yake,
yumo (mwanaume) ndani ya nyumba yake, haya ni maneno mengi yaliyowekwa pamoja.
Hapa kigezo hiki ni vigumu kufanya kazi.
Dhana ya nafasi tupu huonekana
katika maandishi tu, tunapozungumza nafasi hizo tupu hazionekani au
kujidhihirisha, sasa je neno liko kimaandishi tu?
Neno kifonolojia, huchukulia kwamba neno ni kipande cha lugha kinachotokana
au kujengwa na kipashio kidogo cha kimatamshi, kufuatana na vigezo fulani
vilivyo wekwa ambavyo hutofautiana kutoka lugha moja na nyingine. Rubanza
(ameshatajwa) hueleza kwamba zipo lugha ambazo upo uwezekano wa kulitambua neno
kwa kutumia sifa za kimatamshi. Lugha kama hizi ni zile ambazo zina utaratibu
wa kuweka mkazo mahali fulani maalumu katika maneno wakati wote. Hueleza zaidi
kwamba sehemu hiyo inaweza kuwa mwanzoni mwa kila silabi ya kwanza ya neno, ua
silabi ya pili toka mwisho kwa baadhi ya lugha. Kwa mfano katika lugha ya
Kingereza;
“The rest of the books’ll have to go
there,” mgawanyo wa maneno ni kama ifuatavyo; [the rest] [of the books’ll]
[have to] [go] [there]. Hapo tuna mikazo mitano, inayoangukia katika; rest,
boks, have, go na there, kwahiyo hapa tuna maneno matano ya kifonolojia.
Katika lugha ya Kiswahili mkazo huwa
katika silabi ya pili kutoka mwisho, kwa mfano; anacheza, mkazo upo
kwenye “che”.
Matatizo ya kigezo hiki
Kwa baadhi ya lugha, hasa Kiswahili
na lugha nyingine za Kibantu mkazo huhama kadri maneno yanavyoongezeka kwenda
kulia katika tungo. Kwa mfano;
(a) Baba
(b) Baba analima
(c) Babaanalima shambani
Neno la kwanza mkazo msingi upo
kwenye “ba” ya kwanza , neno la pili
mkazo msingi umehamia kwenye “li” na
neno la tatu mkazo msingi umehamia kwenye “mba”
Swali ni je kama neno katika kigezo hiki
cha kifonolojia tunaangalia mkazo msingi , haya maneno ambayo mkazo wake huhama
sio maneno tena?
Tatizo lingine ni katika lugha ya
Kingereza ambapo utengaji wa maneno kifonoloja huonekana kuwa mgumu, kwani neno
moja kifonolojia kimaandishi huweza kuonekana kama maneno mawili au zaidi.
Vilevile maneno mengine yenye dhima za
kisarufi hayapewi mkazo, bali hutegemea maneno yanayo ambatana nayo, kwa mfano
maneno kama vile; her, it, that,
yakisimama yenyewe hayapewi mkazo.
Kigezo cha kilekisika, hiki ni kiini kingine cha ugumu wa kufasili neno, katika
kigezo hiki wataalamu wake hueleza kuwa neno ni kipashio dhahania cha
kilekisika ambacho huweza kudhihirika kimaana na kikazi. Kipashio hicho huweza
kuwakilishwa kimaandishi au kimatamshi. Cystal (1980) kama alivyo nukuliwa na
Mdee anaelezea kuwa leksimu ni kipashio dhahania kinacho wakilisha maumbo
kadhaa yanayotokana nacho. Kwa mfano;
refu – ndefu, mrefu, kirefu
baya- baya, mbaya, wabaya
Japokuwa leksimu inaweza kuwa neno
si kila leksimu ni neno wala kila neno sio leksimu
Mapungufu ya kigezo hiki,
Swali je, maumbo yanayotokana na
leksimu moja kama ilivyo mfano hapo juu ni maneno tofauti au neno moja? Pia
kuna maumbo yenye umbo moja lakini maana tofauti, je haya nayo yatakuwa neno
moja au maneno zaidi ya moja, kwa mfano;
1. Paa – mnyama
2. Paa – enda angani enda juu
3. Paa – sehemu ya juu ya nyumba
Kigezo cha kisarufi,
Kufasili
neno kwa kutumia kigezo hiki nayo ni mojawapo ya kiini cha ugumu wa kufasili
neno, kigezo hiki hueleza kwamba neno ni kipashio cha lugha kisicho na maana
kubwa lakini huwa na dhima kisarufi. Kazi kubwa ya maneno haya ni kukamilisha
maana kisarufi katika tungo. Mfano
katika lugha ya Kiswahili;
a)
Juma ni hodari wa
kucheza mpira wa gofu
Hapa maneno “ni”
na “wa”, yana maana kisarufi. Mfano
Katika lugha ya Kingereza;
b) A pen, an egg, with spoon, na by bicycle,
hapa napo maneno “a” “an” “with” na “by”
yana dhima kisarufi.
Upungufu wa kigezo hiki
Kigezo hiki huzingatia dhima zaidi
kuliko maana, pia ili neno lijidhihirishe vizuri kidhima ni lazima liwe katika
tungo/sentensi.
Kigezo cha maana,
Kwa mujibu wa Mdee (ameshatajwa)
hueleza kwamba neno ni kipashio kidogo cha lugha chenye maana, hueleza zaidi
kwamba neno ni lazima liwe na maana. Mfano;
baba – mzazi wa kiume, mama –
mzazi wa kike. Kwa hiyo kwa kutumia kigezo hiki neno hutambuliwa kuwa ni
kipashio cha kiisimu chenye maana
Mapunufu ya kigezo hiki
Je, maneno yote ya luha yana maana
ya kisemantiki? Pia kuna maneno mawili au zaidi yenye maana moja, Kwa mfano;
mkono wa birika, maana yake mchoyo. Yapo maneno mengine yenye maana zaidi ya
moja, mfano; kaa, paa, na kata, maneno haya yakisimama yenyewe huwezi kupata
maana moja mpaka yawe katika mahusiano
na maneno mengine kwenye sentensi.
Pamoja na vigezo mbalimbali
vinavyotumika kufasili neno kuonekana ndicho kiini cha ugumu wa fasili ya neno
lakini pia tofauti za lugha nazo huchangia kufanya fasili ya neno kuwa ngumu.
Hii ni kwa sababu tabia za lugha hutofautiana. Pia mitazamo tofautitofauti ya
wataalamu nayo ni sababu nyingine ya ugumu huo.
Hitimisho
Kutokana na uwepo wa vigezo vingi
vitumikavyo kuainisha maneno, mitazamo tofauti ya wataalamu na kutofautiana kwa
tabia ya lugha moja na nyingine, ni vigumu mtu yeyote kutoa maana itakayo
kubalika kwa watu wote. Hivyo ili kutoa utata huu ni muhimu vigezo hivi
vichanganywe ili kuwa na kigezo kimoja jumui kitakachotumika kutoa fasili ya
neno iliyo kamilifu. Vitu hivi
vikizingatiwa vinaweza kupunguza ua kuondoa ugumu wa kufasili neno.
MATEJEO
Katamba, F. (1993) Morphology. Mac Millan Press Ltd, L
ondon
Mdee, S. (2010) Nadharia na Historia ya Leksikografia. TUKI, Dar es Salaam
Rubanza. (2010) basic Reading.
Yaliyoandailwa na Rubanza.
Spencer, A. (1991) Morhological Theory in Generative Grammar.
Congress cataloging, London
TUKI (209). Kamusi ya Kiswahili Sanifu. TUKI, Dar es Salaam
TUKI (2010). Kamusi ya Kiswahili Sanifu. TUKI, Dar es Salaam
CHANZO: CHOMBOZ
No comments:
Post a Comment