Thursday, July 10, 2014

SHEIKH SULEIMAN KILEMILE AWAASA WAISLAMU KUWA KITU KIMOJA




 

Waislamu nchini Tanzania wametakiwa kudumisha umoja, mapenzi na mshikamano na kuweka kando tofauti zao ili kuipa nguvu dini ya Allah (SW)
 
Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa Jumuia ya Umoja wa Wanazuoni nchini Tanzania HAYYIATUL-ULAMAA, Samahatu Sheikh Suleiman Kilemile wakati akitoa nasaha fupi kufuatia hafla ya futari ya pamoja iliyoandaliwa na Umoja wa wafanyabiashara wa Tanzania na Uturuki (ABITAT) wakishirikian ana taasisi ya Camel Foundation, iliyofanyika katika ofisi za ABITAT jijini Dar  es Salaam

Sheikh Kilemile akizungumza mbele ya jopo la maulamaa kutoka taasisi mbalimbali za kiislamu nchini Tanzania amesema, lengo la futari ya pamoja ni kutoa fundisho kwa viongozi wa dini hiyo kusimama imara katika umoja na mshikamano kwani hayo ndiyo mafundisho sahihi ya Quran na Sunna ya Mtume Muhammad (SAW)

Amesema waislamu sasa hivi wapo katika kipindi kigumu ambapo maadui wa uislamu wamefanikiwa katika kuwagawa, jambo ambalo imekuwa ni vigumu kurejesha nguvu na heshima yao.

Amesema inapaswa ifahamike kuwa bila kuwa na umoja dhabiti miongoni mwa waislamu itakuwa ni vigumu katika kufikia malengo yao kwani msaada wa Allah (SW) upo tu kwa wale walio katika kamba moja ya Allah (SW) na sio walio katika mifarakano.


Awali akifungua mazungumzo hayo mwenyekiti wa Taasisi ya Camel Foundation, Sheikh Bekir Atasoy amesema Umoja huo umeweza kujivunia mafanikio makubwa kwa kipindi kifupi, ikiwa ni pamoja na kuanzisha shule ya Shamsiya ambayo imekua ni chachu ya kufaulisha wanafunzi jijini Dar es Salaam pamoja na kuwasaidia watu wasiojiweza katika kuwapatia futari na mavazi hususan katika mwezi mtukufu wa ramadhan.

 

No comments:

Post a Comment