Tuesday, July 22, 2014

WANAFUNZI WAASWA MASOMO YA SAYANSI



Wanafunzi wa shule mbalimbali nchini wametakiwa kujifunza masomo ya sayansi kutokana na umuhimu wake katika ugunduzi wa vitu ili kusaidia taifa kimaendeleo.

Imeelezwa kuwa idadi kubwa ya wanafunzi na walimu hukimbia masomo hayo na kusababisha watu kuamini ni magumu hasa kwa jinsi yanavyofundishwa.

Akitoa rai hiyo jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Shirikisho la Wanasayansi Chipukizi (YS), Dk. Gozibert Kamugisha, ameeleza kuwa taifa linakabiliwa na changamoto ya wataalamu wa masomo hayo, hivyo kusababisha kutofikia hatua ya kugundua vitu kama ilivyo kwa nchi nyingine.

Kamugisha amesema kuwa idadi kubwa ya wanafunzi na walimu wanashindwa kujua jinsi ya kujifunza masomo hayo hatimaye kuchangia ongezeko kubwa la upungufu wa wasomi kwenye sekta ya sayansi.

Amesema kuwa miongoni mwa masomo ambayo yanakimbiwa ni Hesabu, Fizikia, Biolojia, Kemia na Sayansi ya Jamii, hivyo kupunguza idadi ya ugunduzi wa vitu mbalimbali vinavyofanywa na watu wengine duniani.

Hata hivyo, Kamugisha amefafanua kwamba, katika kutumia njia za kuwavutia wanafunzi na walimu kupenda masomo hayo, shirikisho hilo limekuwa likiandaa mashindano kila baada ya mwaka, lengo likiwa kushindanisha shule mbalimbali ili kujifunza masomo hayo kwa njia ya vitendo.

No comments:

Post a Comment