Thursday, October 2, 2014

ABOUT HIJJA



FIQHI ILIYOWEPESISHWA: HIJJA
FAROUK ABDALLA AL-BARWANI

Hijja, kilugha ni kukusudia; kisharia ni kukusudia kwenda Makka kutekeleza nguzo za Hija, tangu 'tawaf, sa'i (Safa na Marwa), kuhudhuria 'Arafa, na nguzo nyengine za Hija. Hutenda haya kutekeleza amri ya Mwenyezi Mungu Mtukufu na kutafuta ridhaa zake.

Hija ni fardhi kwa kila mwenye uwezo, ni nguzo ya tano miongoni mwa nguzo tano za Uislam. Hija imekuja kwa Qauli ya wenyezi Mungu Mtukufu, qauli ya Mtume wetu Mpenzi s.a.w. na itifaqi ya Umma. Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

    "............Na kwa ajili ya Mwenyezi Mungu imewajibikia watu wahiji kwenye Nyumba hiyo, kwa yule awezae njia ya kwendea……". (Al 'Imraan : 97).

Na amesema Mtume wetu Mpenzi s.a.w.:   "Umejengwa Uislam juu ya (Nguzo) tano", (mpaka mwisho wa Hadithi).
Na amesema Mtume wetu Mpenzi s.a.w.:   "Hijini kabla hamjakuwa hamuwezi kuhiji". (Imehadithiwa na Al Bayhaqy).
Mwenye kukanya kuwajibika Hija huwa amekufuru.

Wamekubaliana wanazuoni kuwa Hija ni fardhi mara moja katika umri. Al Aqra'i alimuuliza Mtume wetu Mpenzi s.a.w. kama Hijja ni kila mwaka? Mtume s.a.w. akasema:   " "Ni mara moja, mwenye kuongeza ni sunna".  (Imehadithiwa na Ahmad).


'Umra ni fardhi kama ilivyo Hija, ni fardhi kwa Qauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Na timizeni Hija na 'Umra kwa ajili ya Mwenyezi Mungu……". (Al Baqara : 196).

Imepokewa kutoka kwa Sayyidah 'Aisha r.a. kwamba alimuuliza Mtume wetu Mpenzi s.a.w. kama wanawake wanalazimika na Jihadi, akasema s.a.w.:   "Naam, Jihadi isiyo na vita ndani yake, Hijja na 'Umra".

Ameeleza Imam Al Tirmidhy r.a. kwamba Jaabir r.a. alimuuliza Mtume wetu Mpenzi s.a.w. kama 'Umra ni waajb, Mtume wetu Mpenzi s.a.w. akajibu:     yaani, si waajibu, lakini ukifanya 'Umra ni kheri. Yenye kufanywa katika ibada ya 'Umra ni kama yale yenye kufanywa katika ibada ya Hija, lakini kwenye 'Umra hamna nguzo ya 'Arafa wala kulala Muzdalifa wala nguzo ya kulembea vijiwe (mawe), wala kuchija.

Inampasa mwenye kutaka kwenda kuhiji ajifunze hukmu zote za Hija, yale ya waajibu, ya sunna, yenye kuruhusiwa na yale yenye kukatazwa na yale yenye kuba'tilisha Hija. Kujifunza ni waajibu, kwa sababu lenye kulazim kulifanya ni lazima kujuwa namna ya kulifanya. Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu: Basi waulizeni wenye ukumbusho kama nyinyi hamjui…". (Annahl : 43).
Na amesema Mtume wetu Mpenzi s.a.w.:   "Kutafuta elimu ni fardhi (waajibu) juu ya kila Muislam mwanamume” (Imehadithiwa na Al Bayhaqy)
Na katika riwaya nyengine: "Na Muislam mwanamke".

La mwanzo lenye kupasa kujifunza ni kujuwa baina ya halali na haraam. Hivi ni kwa vile halali inasaidia katika kufanya mema na kujiepusha na maovu. Mwenyezi Mungu Mtukufu ni mwema, hapendi isipokuwa vyema. Mwenyezi Mungu Mtukufu amewaamrisha Waumini yale yale aliowaamrisha Mitume a.s., amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu kuwaambia Mitume a.s.w.:
 "Enyi Mitume! Kuleni vyakula vizuri na tendeni mema. ……". (Muuminun : 51).
Na amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu kuwaambia Waumini:
 "Enyi mlio amini! Kuleni vizuri tulivyo kuruzukuni, ....". ( Al Baqara : 172)

Mwenye chumo la halali, hutakasika vitendo vyake; na asiekuwa na chumo la halali, inakhofiwa kuwa vitendo vyake huenda visikubaliwe.
Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu: "…Hakika Mwenyezi Mungu huwapokelea wachamngu". (Al Maidah: 27).
Amesema mshairi:

"Ukenda kuhiji kwa mali asili yake haraam, basi hukuhiji; amehiji mnyama (kipando chako)".
Hija ni miongoni mwa bora mno za a'amali, hivi ni kwa qauli ya Mtume wetu Mpenzi s.a.w.:   

  "Bora mno ya a'amali kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu ni imani isiokuwa na shaka, na kupigana Jihadi kwa ajili ya Mwenyezi Mungu Mtukufu, na Hijja iliofanywa kwa ukamilifu na haikuingia ndani yake lolote lile lililokatazwa". (Imehadithiwa na Jama'a Wapokeaji Hadithi).

Na amesema Mtume wetu Mpenzi s.a.w.:    "Mwenye kuhiji asiseme maneno machafu, atarejea kama alivyokuwa siku aliozaliwa na mama yake". (Imehadithiwa na Jama'a Wapokeaji Hadithi).
Hijja ni waajibu wenye kutekelezwa penye wasaa, lakini ni bora kufanya hima na haraka kuutekeleza mara ukipata uwezo, hivi ni kwa qauli ya Mtume wetu Mpenzi s.a.w.:

"Mwenye kumiliki mali na kipando cha kumfikisha kwenye Nyumba ya Mwenyezi Mungu Mtukufu - Makka - na akawa asende kuhiji, basi hakuna juu yake isipokuwa kufa katika mila ya Kiyahudi au ya Kinasara". (Imehadithiwa na Al Tirmidhy).
Na amesema Mtume wetu Mpenzi s.a.w.:

"Asiezuilika kutokana na maradhi, au haja ya hakika, au kuzuilika kutokana na mwenye madaraka (sultani, raisi, mfalme, n.k.) muovu; na akawa mtu huyo hakuhiji, basi akitaka naafe katika mila ya Kiyahudi au mila ya Kinasara". (Imehadithiwa na Ahmad).
Kuwajibika Hijja kuna shuruti tano:
Ya Kwanza, kuwa ni Muislam, kwani Hija ni ibada sawa na ibada nyengine kama vile, Sala, Saumu, Zaka. Na kwa qauli ya Mtume wetu Mpenzi s.a.w. kwa Mu'adh r.a. alipompeleka Yaman:

"Waite washuhudie kwamba hakuna wakuabudiwa kwa Haqi isipokuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu, wakiku'tii; basi waelimishe kwamba wanawajibika na kadha (hili na hili)". Ikatajwa Hija kuwa ni miongoni mwa hayo wanayowajibika nayo kuyatekeleza.
Kama ilivyo hukmu kukhusu ibada nyengine, Hija nayo haiwajibiki juu ya kafiri wa asili. Ama mwenye kurtadi, yaani mwenye kutoka kwenye Uislam; yeye - kama ilivyo hukmu kukhusu ibada nyengine - itaendelea juu yake hukmu ya Hija. Ikiwa alipokuwa kwenye Uislam alikuwa na uwezo wa kuhiji, lakini hakuhiji; basi itabakia juu yake dhima ya nguzo hii ya Hija na kulazimika juu yake kuitekeleza ikiwa atarejea kwenye Uislam. Dhima ya kuitekeleza hii nguzo ya Hija itabakia juu yake ikiwa ana uwezo wa kuhiji au hana uwezo wa kuhiji, hivi ni kwa vile pale alipokuwa kwenye Uislam alikuwa na uwezo wa kuhiji; lakini hakuhiji.
Ikiwa ataporejea kwenye Uislam akawa na uwezo wa kuhiji, lakini asiwahi kuhiji mpaka akafikwa na mauti; basi atahijiwa kutoka katika mali yake kabla ya kugaiwa mirathi.
Ya Pili, kuwa ni balegh, mtoto mdogo kabla ya balegh halazimiki na Hija; sawa na ibada nyengine. Hivi ni kwa qauli ya Mtume wetu Mpenzi s.a.w.:  
   (imetangulia kutajwa Hadithi hii), yaani watu watatu imeondoshwa kuhisabiwa juu yao; miongoni mwao ni mtoto mdogo kabla ya balegh.
Ya Tatu, awe ni mwenye akili timam; mgonjwa wa akili haimlazim Hija, sawa na ibada nyengine. Hivi ni kwa qauli ya Mtume wetu Mpenzi s.a.w. katika Hadithi hii hii ambayo imetajwa kabla,    , yaani watu watatu imeondoshwa kuhisabiwa juu yao; miongoni mwao ni mgonjwa wa akili, mpaka apowe.
Ya Nne, kuwa huru, asie kuwa huru hawajibikiwi na Hija, huwajibikiwa na Hija pale anapokuwa huru. Hivi ni kwa qauli ya Mtume wetu Mpenzi s.a.w.:  

    "Mtumwa yeyote yule akihiji kisha akapewa uhuru, itamlazim ahiji tena".
Kutowajibikiwa mmilikiwa na Hija ni kwa hoja ya vile kutowajibikiwa na Sala ya Ijumaa, ambayo aghlab ya hali huwa karibu zaidi na makaazi yake, tafauti na Hija ambayo huwa mbali zaidi na huchukuwa muda zaidi kutekelezwa. Hivi ni katika kuhifadhi haki ya mmiliki.
Ya Tano, uwezo. Hivi ni kwa Qauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu.:
  
 "........Na kwa ajili ya Mwenyezi Mungu imewajibikia watu wahiji kwenye Nyumba hiyo, kwa yule awezae njia ya kwendea……". (Al 'Imraan : 97).
Uwezo huwa ni kwa mawili, uwezo unaokhusiana na yeye mwenyewe; na uwezo usiokhusiana na yeye mwenyewe.
Uwezo unaokhusiana na yeye mwenyewe umo katika mambo matano:
Kwanza, awe na kipando cha kumfikisha Hija, kipando chake mwenyewe au cha kuajiri; hivi ni kwa yule ambae yuko kwenye masafa yenye kujuzisha kupunguza Sala au zaidi kwa kipimo cha mwendo wa kawaida (mwendo wa miguu). Ikiwa yuko kwenye masafa mafupi na mwenye uwezo wa kufika Hija bila ya kipando, sharti ya kipando haitakuwepo juu yake; na itamlazim Hija kwa kutimia shuruti nyengine.

Ama akiwa mgonjwa hawezi kufika ila kwa kipando, basi sharti ya kipando itakuwepo kwake hata kama yuko kwenye masafa mafupi.
Pili, awe na uwezo wa cha kumpeleka na kumrudisha Hija, shuruti ya kipando na uwezo iwe anacho cha kumtosheleza yeye mwenyewe na wale wanaomlazim yeye kuwaqim, tangu kwa chakula, mavazi, na kila la haja ya dharura; tangu kuondoka mpaka kurejea kwake. Ikiwa atakuwa na uwezo wa kutekeleza fardhi ya Hija, lakini ikawa ni mwenye kuhitajia zaidi kuowa kwa kukhofia kuingia katika uzinzi; basi kuowa ni bora kwake katika hali hio kabla ya kuhiji. Hivi ni kwa vile juu yake yeye kuowa kushakuwa ni kwenye kuhitajika upesi, wakati Hija ni ibada yenye uwezekano wa kungojeka; ama akiwa hana khofu ya kuingia kwenye uzinzi, basi kutanguliza kutekeleza Hija ni afadhali.
Tatu, amani ya njiani; ikiwa atakhofia madhara yoyote kwa nafsi yake, au kitu chake, au hishima yake kutokana na ukosefu wa salama njiani, basi haitamlazim Hija katika hali hio.
Nne, wakati wa kutosha; yaani uwepo wakati wa kutosha kumfikisha na kuwahi kutekeleza ibada za Hija kwa ukamilifu, pamoja na nguzo ya 'Arafa.
Uwezo usiokhusiana na yeye mwenyewe, ni vile kuwajibika yeye ikiwa ni mwenye dhima hiyo; kumuwakilisha wa kumtekelezea mtu aliekufa na ana dhima ya Hija atekelezewe kutokana na mali yake kabla ya kugaiwa mirathi, au mtu ambae hawezi kuhiji yeye mwenyewe kwa sababu ya uzee au sababu nyengine, kama vile kutoweza zahma na mashaka ya safari na kutekeleza nguzo za Hija.

Nguzo za Hijja ni tano:

Ya Kwanza, kuhirimia, kuhirimia ni kutia nia ya kuingia katika a'amaali (nguzo) za Hija au 'Umra. Imeitwa iharaam kwa vile imo ndani yake maamrisho ya kujizuia na yale yaliokatazwa wakati wa kutekeleza hii nguzo ya Hija. Kuwajibika kwa huku kuhirimia, yaani kutia nia kumekuja kwa qauli ile ile ya Mtume wetu Mpenzi s.a.w. kukhusu kusihi ibada yoyote ile, nayo ni: , yaani "hakika ya kusihi a'amaali ni kulingana na nia".
Katika kutekeleza nguzo za Hijja/'Umra kuna mifumo (mipango) ya aina tatu:
Wa Kwanza, () "Al-Ifraad". Hivi huwa kwa kuhirimia katika mipaka ", ya nchi yake (nchi anayotoka), kwa nia ya kutekeleza nguzo za Hijja (pekee). Baada ya kutekeleza nguzo za Hijja, atatoka katika ihraam; atahirimia (katika mipaka iliowekwa), kwa nia ya kutekeleza nguzo za 'Umra (pekee). Kwa mfumo huu, yaani mfumo wa "Hijja Al-Ifraad"; inakuwa kwa kutangulizwa Hijja, kisha ndio 'Umra.
Wa Pili, ()"At-tamatu'i". Hivi huwa kwa kuhirimia katika mipaka  , ya nchi yake (nchi anayotoka), kwa nia ya kutekeleza nguzo za 'Umra (pekee). Baada ya kutekeleza nguzo za 'Umra, atatoka katika ihraam; atahirimia (nae yupo hapo hapo Makka), kwa nia ya kutekeleza nguzo za Hijja (pekee). Kwa mfumo huu, yaani mfumo wa "Hijja Attamatu'i"; inakuwa kutangulizwa 'Umra, kisha ndio Hijja. Huu mfumo wa "Hijja At-tamatu'i" ndio waliokubaliana wanazuoni kupendekezwa kuutumia. Umeitwa mfumo huu "At-tamatu'i" kwa vile kutoka katika ihraam moja, yaani ihraam ya 'Umra (akapumzika), kisha akaingia katika ihraam ya pili, yaani ihraam ya Hijja.
Wa Tatu, () ''Al-Qiraan". Imeitwa "qiraan", kutokana na neno , yaani kaunganisha. Hivi huwa kwa kuhirimia katika mipaka " ya nchi yake (nchi anayotoka), kwa nia ya kutekeleza nguzo za Hijja na 'Umra kwa ihram moja (kwa pamoja). Kwa mfumo huu nguzo za 'Umra hufidiwa na zile nguzo za Hijja, kwahivyo basi, akikamilisha Hijja yake atakuwa kakamilisha 'Umra yake vile vile; hapo tena ndipo atakapotoka katika ihraam. Mfumo wowote kati ya mifumo mitatu hii unajuzu, wanazuoni wao basi wamekhitalifiana rai juu ya upi miongoni mwa mifumo mitatu hii ni bora; hawakukhitalifiana rai kwa kujuzu huu na kutojuzu mwengine. Imam Shafi'ii r.a. yeye amefadhilisha kwa ubora, mfumo wa "Al-Ifraad", kisha "At-tamatu'i; kisha "Al-Qiraan", yaani katika mpango uliokuja hapo juu.
Dalili ya kujuzu wowote miongoni mwa mifumo mitatu hii ni haya alioyaeleza Mama wa Waumini, Sayyidah 'Aisha r.a.:

"Tulikwenda pamoja na Mtume wetu Mpenzi s.a.w. kwenye "Hijja ya Kuaga", katika sisi wako walio hirimia 'Umra, na wako walio hirimia Hijja na 'Umra, na wako walio hirimia Hijja. Mtume wetu Mpenzi s.a.w. yeye alihirimia Hijja". (Imehadithiwa na Ahmad na Al Sheikhan na Maalik).
Nguzo ya Pili, kusimama (kushinda) 'Arafa; hivi ni kwa vile Mtume wetu Mpenzi s.a.w. aliamrisha mtu anadie: ", yaani Hijja ni kuhudhuria 'Arafa kwa kutekeleza a'amali za 'Arafa. Huhisabika kuwa umetekeleza nguzo hii ya kuhudhuria 'Arafa kwa kuhudhuria hapo 'Arafa na kutekeleza japo sehemu tu ya a'amali za 'Arafa, hata ikiwa kama kwa kupita kutafuta (mnyama) aliekimbia au aliepotea. Pia huhisabiwa kuipata 'Arafat hata lau kama atafika huko na akalala mpaka wakati wa kuondoka, hivi ni kwa kubakia juu yake kuhisabika na Sharia. Shuruti ya kujuzu "", yaani kushinda hapo 'Arafa na kutekeleza a'amali zake; ni kuwa yeye ni mtu mwenye kujuzu kisharia kufanya ibada. Na popote pale ataposimama Hujaj (mwenye kuhiji) katika 'Arafa, itajuzu kwa a'amali za 'Arafa. Wakati wa kusimama (kushinda 'Arafa na a'amali zake) ni tangu kutenguka jua siku ya 'Arafa, yaani taarikh tisa ya mfunguo tatu, mpaka kuchomoza jua siku ya pili yake, yaani taarikh kumi ya mfunguo tatu; wala haishurutishwi kukutana usiku na mchana, lakini ni afadhali.

Ya Tatu, ku'tufu katika Nyumba Kongwe - Msikiti wa Makka, yaani 'tawaaf Al-Ifaadha; hivi ni kwa walivyokubaliana wanazuoni kuwa ku'tufu huku ndiko kulikokusudiwa kwa Qauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu:
   "……, na waizunguke Nyumba ya Kale". (Al Hajj : 29).
Miongoni mwa waajibu za 'tawaaf ni ku'tahirika na hadathi kubwa na ndogo, yaani awe na udhu na asiwe na janaba, hedhi wala nifasi; vilevile ni ku'tahirika na najsi mwilini, nguoni na mahala anapo'tufu. Vilevile miongoni mwa waajibu za 'tawaf ni kujisitiri kwa nguo ilio 'taahir, hivi ni kwa qauli ya Mtume wetu Mpenzi s.a.w.:
"Ku'tufu kwenye Nyumba Tukufu ni Sala, isipokuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu ameruhusu kuseme kwenye ku'tufu, basi asiseme mtu isipokuwa la kheri".
Na kwa qauli ya Mtume wetu Mpenzi s.a.w. kumwambia Asma binti 'Umais - nae amepatwa na hedhi wakati huo:   "Fanya wanayofanya, isipokuwa usi'tufu Nyumba Tukufu".
Ikiwa atatokwa na udhu katika 'tawaafi, itamlazim atie udhu na aendeleze 'tawaaf yake. Wanazuoni wengine wanasema aanze upya 'tawaaf yake. Na katika waajibu za 'tawaf ni kufanya kwa mpango.
Mahala pa kuanzia ku'tufu pamebainishwa kwa alama yenye kuonekana wazi kabisa, hapapotezi wala hapababaishi. Na katika waajibu za 'tawaf ni kuhakikisha kuwa una'tufu mara saba, yaani unazunguka mizunguko saba kaamili, si lazima kufululiza; lakini ni afadhali kufululiza mpaka kukamilisha mizunguko saba.
Inasuniwa kuomba du'a wakati umo kwenye 'tawaafi, ameeleza Bwana Abdulla bin Assaib r.a. kwamba amemsikia Mtume wetu Mpenzi s.a.w. akisema wakati yupo baina ya   (rukni yamani na hajari-l-aswad  "Mwenyezi Mungu Mtukufu tupe hapa duniani mema na Kesho Akhera utupe mema na utukinge na adhabu ya Moto". (Imehadithiwa na Ahmad, na Abu Daud, na Al Nissaai, na Ibnu Hibaan na Al Haakim wameipa darja ya Hadith sahih).
Na amesema Abu Huraira r.a.:

"Mwenye ku'tufu Nyumba Tukufu mara saba na hasemi isipokua: "Ametakasika Mwenyezi Mungu Mtukufu, na hapana afaae kuabudiwa kwa haqi isipokuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu, na ni Mkubwa Mwenyezi Mungu Mtukufu, na hapana hila wala nguvu isipokuwa ni kutokana na Yeye; atafutiwa makosa yake kumi, na ataandikiwa ujira wa mema kumi, na atapandishiwa kwa haya daraja kumi". (Imehadithiwa na Ibnu Maajah).
Na amesema Sayyidah 'Aisha r.a. kwamba Mtume wetu Mpenzi s.a.w. amesema:  "Hakika imejaaliwa ku'tufu Nyumba Tukufu na kwenda 'Safaa na Marwa kwa ajili ya kusimamisha (kuendeleza) kumtaja Mwenyezi Mungu Mtukufu". (Imehadithiwa na Abu Daud na Al Haakim).
Ya Nne, "", yaani kwenda mara saba baina ya 'Safaa na Marwa. Hivi ni kwa vile yeye Mtume wetu Mpenzi s.a.w. kufanya hivi, na kwa qauli yake s.a.w. wakati yumo katika kwenda baina ya 'Safa na Marwa:  "Nendeni (kwa kuchapuka, harakaharaka), kwani Mwenyezi Mungu Mtukufu ameandika (amewajibisha) juu yenu kwenda hivi".
Imeshurutishwa kufanya hii kwenda baina ya 'Safaa na Marwa baada ya kumaliza 'tawaaf, ikiwa ni 'tawaaf ifaadha au 'taawaf quduum. Vilevile katika kutekeleza hii Sa'ai imeshurutishwa kuanzia 'Safa, ('Safa ni kilimani kwenye jabali ambalo watu hukaa kupumzika, kwa hapa unaaiona Al Kaaba kwa uwazi kabisa, upande wa pili ndio Marwa) na kumalizia Marwa. Akianza kutoka 'Safa mpaka akafika Marwa, huwa ni (shoti) mara ya kwanza; ya pili huwa kwa kutoka Marwa mpaka 'Safa, akifika 'Safa huwa ni shoti ya pili; hufanya hivi mpaka kutimiza shoti saba baina ya 'Safa na Marwa. Hivi ndiyo alivyofanya Mtume wetu Mpenzi s.a.w. Tafauti na 'tawafi, hii "sa'ai", yaani mwendo wa 'Safa na Marwa haishurutishwi kuwa na udhu wala shuruti nyengine za Sala.
Lakini haijuzu kuwacha kufanya waajibu huu, wala hailipiwi kwa kuchinja, wala hawezi mtu kutoka kwenye ihraam mpaka atekeleze na nguzo hii. Lakini inajuzu hata kama atachukuliwa juu ya kigari au juu ya kitanda, muhimu zipatikane kuhudhuria yeye mwenyewe shoti saba za baina ya 'Safa na Marwa.
Ya Tano, kunyowa au kupunguza nywele baada ya kukamilisha shoti saba za sa'ai; hivi ni kwa Qauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu:   "....... na hali mmenyoa vichwa vyenu na mmepunguza nywele…". (Al Fathi : 27).
Na amesema Mtume wetu Mpenzi s.a.w.:

"Mwenyezi Mungu Mtukufu amewarehemu wenye kunyowa". Wakasema Masahaba r.a.: "Na wenye kupunguza (nywele) Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu Mtukufu". Akasema s.a.w.: "Na wenye kupunguza". (Imehadithiwa na`Al Sheikhan).
Yote mawili, yaani kunyowa nywele zote au kupunguza nywele, inajuzu kwa mwanamume na kwa mwanamke; lakini kwa wanaume ni bora kunyowa na kwa wanawake ni bora kupunguza. Kwa mwenye kuhiji - isipokuwa Hija tamatu'i - yeye atanyowa baada ya kulembea vijiwe kwenye " (jamratu-l-al'aqaba), na mwenye kufanya 'Umra na mwenye kufanya Hija tamatu'i, (kupumzika), wao kunyowa au kupunguza huwa baada ya kukamilisha " mwendo wa 'Safa na Marwa. Na mwenye kalazimika kuchinja yeye hunyowa au hupunguza nywele baada ya kuchinja. Na inapendekezwa kwa asiekuwa na nywele (kipara) kupitisha kiwembe kichwani.

Tumetangulia kutaja nguzo za Hija, sasa Inshaallah tutataja waajibu za Hija; na kueleza tafauti baina ya nguzo na waajibu. Nguzo ya Hija, inalazimika kutimia nguzo ili itimie Hija, wala haiwezi kuungika (kufidiika) kwa (damu) kuchinja. Waajibu ya Hija, hailazimiki kutimia waajibu ili itimie Hija, ikikosekana kutimizwa la waajibu kwa udhru; huungika (hufidiika) kwa (damu) kuchinja.
Wa Kwanza, iwe kuhirimia kwenye " (miiqaat) mipaka, ikiwa ataipita miiqaat yake bila ya kuhirimia; itamlazim arejee kabla hajaingia katika ibada aliokusudia, ikiwa ni 'Umra au Hija hata ikiwa kesha hirimia (kahirimia nje ya mpaka); arejee ili ahirimie kwenye miiqaat yake. Asiporejea, au akirejea baada ya kuingia katika ibada alizokusudia; itamlazim achinje, hata ikiwa amefanya hivi kwa kusahau au kutojuwa, lakini hatopata dhambi kwa vile kusahau au kwa kutojuwa. Aghlab ilivyo kila nchi ina miiqaat yake. Katika kila msafara huelezwa qabla mahala pakuhirimia, yaani ndani ya miiqaat yao. Ni afadhali kuhirimia kwenye msikiti aliohirimia hapo Mtume wetu Mpenzi s.a.w.
Hii miiqaat iko namna mbili, miiqaat ya zama/wakati na miiqaat ya mahala/mtaa. Miiqaat ya zama/wakati kwa Hija ni mfunguo mosi, mfunguo pili, na siku tisa za mfunguo tatu, na mwisho wake ni usiku wa kuamkia siku ya kuchinja. Hivi ni kufuatana na Qauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Hija ni miezi maalumu…………". (Al Baqara : 197).
Na Qauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu:
      "Wanakuuliza khabari ya miezi. Sema: Hiyo ni vipimo vya nyakati kwa ajili ya watu na Hija………". (Al Baqara : 189).
Ama miiqaat ya zama/wakati kukhusu kufanya 'Umra, wamekubaliana wanazuoni kuwa mwaka mzima inajuzu kufanya 'Umra.
Miiqaat ya mahala, kwa mkaazi wa Makka; miiqaat yake ni Makka yenyewe, imesemwa pia kuwa Makka yenyewe na sehemu yote ya Haram. Mkaazi wa Makka yeye atatia nia ya ihraam mlangoni pa nyumbani kwake. Ikiwa si mkaazi wa Makka, ikiwa nyumba yake ni baina ya Makka na miiqaat; basi yeye miiqaat yake ni ule mtaa anaoishi au kijiji wanachofikia Mabedui. Ikiwa nyumba yake iko nyuma ya miiqaat, yaani baada ya miiqaat; basi miiqaat yake ni ile atakayoipita.
Miiqaat wa Kwanza: " " (Dhu Hulaifah), huu ni (mpaka) miiqaat kwa wenye kutokea Madina.
Miiqaat wa Pili: "" (Jahfa), huu ni (mpaka) miiqaat kwa wenye kutokea sehemu za Sham, Misri, Moroco na sehemu zilizo sehemu hizo. Huu umebadilishwa hivi sasa kwa miiqat ya (mpaka wa) Buraghi.
Miiqaat wa Tatu: " " (Yalamlam), huu ni (mpaka) miiqaat kwa wenye kutokea Yaman na sehemu zilizo sehemu hio.
Miqaat wa Nne: " " (Qarni), huu ni (mpaka) miiqaat kwa wenye kutokea Najdi.
Hii (mipaka) miiqaat minne tulioitaja hapo juu, imetajwa katika Hadithi ya Mtume wetu Mpenzi s.a.w., mwisho wa qauli yake katika Hadithi hio ni hivi:  "Hio (mipaka) miiqaat, yao wao na wenye kuipita humo kati ya wasiokuwa wao, miongoni mwa wenye kuiendea Hija au 'Umra".
Miiqaat wa Tano: " " (Dhatu 'Irqi), huu ni (mpaka) miiqaat kwa wenye kutokea Iraq na Kharsaan. Wanazuoni wengi wanasema kuwa na huu vilevile umetajwa na Mtume wetu Mpenzi s.a.w., wanazuoni wengine wanasema kuwa huu ni kutokana na jitihada ya Sayyidna 'Umar r.a.

Ikiwa mtu anaekusudia kwenda kutekeleza ibada ya Hija au ya 'Umra au zote mbili na akaupita (mpaka) miiqaat yake bila ya kuhirimia, ni haraam kwake kufanya hivyo; akifanya hivyo, itamlazim kuchinja; achinje ama kondoo wa miaka miwili kuingia mwaka wa tatu, au mbuzi wa miaka mitatu. Hivi ni kwa qauli ya Mtume wetu Mpenzi s.a.w.:  "Mwenye kuwacha la waajibu katika waajibu za Hija, itamlazim kuchinja". (Imehadithiwa na Ibnu 'Abbaas).
Ikiwa atarejea kwenye miiqaat yake ili akatie nia ya ihraam, katika hali ya kabla ya kuingia kwenye ibada alioikusudia kuifanya; hapo hatalazimika kuchinja. Ikiwa atarejea kwenye miiqaat yake ili akatie nia ya ihraam, katika hali ya baada ya kuwa keshaingia kwenye ibada alioikusudia kuifanya; itakuwa anaendelea kulazimika na kuchinja, kwa hivyo itamlazim achinje.
Hivi ni kwa sababu ameingia kwenye ibada kwa ihraam iliopungua shuruti zake, hapa sharti ni vile kuwajibika kutia nia ya ihraam kwenye miiqaat yake kabla ya kuingia kwenye ibada alioikusudia kuifanya, kitu ambacho yeye hakukifanya. Haya ni sawa ikiwa ibada hio ni ya fardhi au ya sunna.
Waajibu wa Pili, Kulembea Vijiwe 
Ukamilifu wa kulembea ni kulembea vijiwe sabiini, kwenye maguzo manne katika siku nne. Mpango wa kulembea huku ni hivi: " .
1.      " (Siku ya Kuchinja) yaani taarikh kumi ya mfunguo tatu, atalembea "" (Guzo Al 'Aqaba) kwa vijiwe saba. Baada ya kulembea hapa ndio atakwenda kuchinja, kisha atanyoa au atapunguza nywele. Hapa ndio atatoka kwenye ihraam.
2.      Taarikh kumi na moja ya mfunguo tatu, atalembea vijiwe ishirini na moja kwenye maguzo matatu (si Guzo Al 'Aqaba), kila guzo vijiwe saba.
3.      Taarikh kumi na mbili ya mfunguo tatu, atalembea vijiwe ishirini na moja kwenye maguzo matatu (si Guzo Al 'Aqaba), kila guzo vijiwe saba.
4.      Taarikh kumi na tatu ya mfunguo tatu, atalembea vijiwe ishirini na moja kwenye maguzo matatu (si Guzo Al 'Aqaba), kila guzo vijiwe saba.
Kama ilivyo hapo juu, itakuwa amelembea vijiwe sabiini; kwenye maguzo manne katika siku nne. Huo ndio ukamilifu wa kulembea.

Uchache wa kulembea ni vile kulembea vijiwe arubaini na tisa, kwenye maguzo manne katika siku tatu za mwanzo. Hali hii huwa kwa yule atakaekuwa hataweza kulembea siku ya nne, yaani siku ya taarikh kumi na tatu kwa udhuru wa kuharakisha safari yake. Yeye hujuzu kwake kulembea katika siku tatu za mwanzo tu. Kujuzu huku kumekuja kwa Qauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu:
  "Na mtajeni Mwenyezi Mungu katika zile siku zinazo hisabiwa. Lakini mwenye kufanya haraka katika siku mbili (akarejea) si dhambi juu yake; na mwenye kukawia pia si dhambi juu yake, kwa mwenye kumchamngu……… ..." (Al Baqara : 203).
Kulembea () hutimia kwa kufanya hivyo kwa njia yenye kujuulikana ni kulembea kwa kawaida. Ikiwa atalembea kwa panda, au kwa cha mfano wa hivyo; haitajuzu. Katika hivi kulembea inashurutishwa iwe analembea kwa nia ya kutekeleza waajibu wa ibada ya Hijja. Ikiwa atalembea kijiwe chake juu, kikaangukia juu ya guzo lenye kulembewa, hivyo haitajuzu. Vilevile inashurutishwa alembee vijiwe saba mara saba, ikiwa atalembea vijiwe viwili kwa mara moja, hivyo huhisabiwa kuwa ni  kijiwe kimoja; hata kama atalembea vyote vijiwe saba kwa mara moja basi itahisabiwa kuwa ni kijiwe kimoja tu. Ikiwa mtu kwa udhru kashindwa kwenda kulembea yeye mwenyewe, inajuzu kumuwakilisha mtu amlembelee, lakini sharti huyu anaewakilishwa awe yeye mwenyewe keshalembea vijiwe vyake; kama sio hivyo haitajuzu

Waajibu wa Tatu, kunyowa au kupunguza nywele. Hivi ni kwa Hadithi ya kwamba Mtume wetu Mpenzi s.a.w. aliwaamrisha Masahaba zake, r.a., kunyowa au kupunguza. Kwa wanaume afadhali kunyowa, kwani hivi ndivyo alivyofanya Mtume wetu Mpenzi s.a.w. katika Hijja ya kuaga. (Imehadithiwa na Muslim).
Vilevile ni kwa qauli yake Mtume wetu Mpenzi s.a.w.: , yaani Mwenyezi Mungu Mtukufu waghufirie wenye kunyowa, na katika mara ya tatu ndio akasema s.a.w.: " " yaani, "na wenye kupunguza".

Mwanamke sawa na mwanamume inamuwajibikia Hija zikitimia shuruti za Hijja, kwa mwanamke inaongezeka shuruti ya kuwa iwe afatane na mumewe au mahaarim wake; mahaarim ni yule ambae hawezi kumuowa kwa sababu ya nasab, au ukwe (kuowana,) au kwa kunyonya. Kutokana na Ibni 'Abbaas r.a. amesema kuwa kamsikia Mtume wetu Mpenzi s.a.w. akisema:

"Mwanamume asiwe peke yake na mwanamke isipokuwa awe na maharim wake, wala asisafiri mwanamke ila iwe pamoja na maharim wake. Akasema mtu: “Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu Mtukufu!” "Mke wangu kenda kuhiji na mimi nimejitolea kwenda kwenye vita vya jihadi". Akasema (Mtume wetu Mpenzi s.a.w.): "Nenda ukahiji pamoja na mke wako".  (Imehadithiwa na Al Bukhary na Muslim).
Na ameeleza Yahya bin 'Abaad kwamba: "Mwanamke katika watu wa Ariy alimuandikia Ibrahim Al Nakhi'i akisema kuwa yeye (huyo mwanamke) haja Hiji, hija ya Muislam na anao uwezo wa mali, lakini hana mahaarim. Ibrahim Al Nakhi'i akamuandikia huyu mwanamke: "Hakika yako wewe ni miongoni mwa ambao Mwenyezi Mungu Mtukufu hajawajaalia njia". Wanazuoni wamekubaliana kuwa wanawake waaminifu hutosha kuwa wao ni mahaarim baina yao wenyewe.

Sunna za Hijja ni saba:
Ya Kwanza, kuhiji Hijja Al-Ifraad " yaani Hijja ya bila ya kuchanganya na 'Umra, yaani si Hija Al-Qiraani yaani Hijja ya kuchanganya na 'Umra, wala si Hijja At-tamatu'i " yaani Hijja ya kupumzika. Ishatangulia kutajwa kukhusu aina tatu hizi za Hija.
Ya Pili, "
Namna ya kulabbi ni hivi

Maneno haya tunaweza kujitahidi kuyatarjumu kama hivi: "Tunakuitikia Mwenyezi Mungu Mtukufu, tunakuitikia. Tunakuitikia, hakuna mshirika Nawe, tunakuitikia. Hakika shukrani na ne'ema ni zako Wewe, na Ufalme ni wako Wewe hakuna mshirika nawe".
Inapendekezwa kufanya mno katika hivi kulabbi, kila wakati, ikiwa kwenye kipando, ikiwa kwenye kitako, ikiwa umo njiani kwa miguu. Hii kulabbi inajuzu hata kwa aliomo kwenye hedhi au janaba. Kulabbi hupendekezwa zaidi katika kila kupanda au kuteremka kwenye sehemu ilioinuka au ilioshuka, na ikitokea lolote lile la kutanabahisha. Pia inapendekezwa kulabbi kila wanapokutana watu, unapoingia usiku, kunapokucha, kwenye msikiti Al Khaif, kwenye Msikiti Mtakatifu. Talbia haipendekezwi kwenye 'tawaaf quduum ('tawaf ya kuamkia Msikiti), wala kwenye kwenda baina ya 'Safaa na Marwa, kwani humu zimo du'a zake khaasa. Wala halabbi kwenye 'tawafi-l-ifaadha, wala kwenye 'tawafi-lwida'i ('tawafi ya kuaga), hivi ni kwa vile wakati wa kulabbi humalizika baada ya kumaliza kulembea vijiwe kwenye guzo la 'aqaba, yaani taarikh kumi ya mfunguo tatu na kabla ya kuchinja. Katika kulabbi inapendekezwa kwa wanaume kuinua sauti, wanawake hawatakiwi kuinua sauti. Inapendekezwa mwisho wa kila talbia kumsalia Mtume wetu Mpenzi s.a.w. na kumuomba Mwenyezi Mungu Mtukufu radhi zake na kuomba Pepo na kuomba kuepukana na Moto, pia aombe kila la kheri analolitaka, wala asizungumze wakati wa kulabbi. Ni makruuh kumtolea salaam mtu aliomo kwenye talbia, lakini akitolewa salam anatakiwa ajibu salaam.
Ya Tatu, 'tawaaf quduum (tawaaf ya kuamkia Msikiti), 'tawaf hii ni kuamkia Msikiti Mtukufu, kwenye kitabu cha Hadithi cha Imam Muslim r.a. amesema kuwa Mtume wetu Mpenzi s.a.w. ali'tufu alipoingia Makka.
Ikiwa mtu yumo kwenye 'Umra, aka'tufu kwa 'Umra hutosheleza hio 'tawaaf ya 'Umra kuwa ni 'tawaaf quduum. Hivi ni sawa na vile kuingia msikitini ukusali fardhi moja kwa moja bila ya kusali sunna ya tahiyatu-lmasjid, hii Sala ya fardhi itafidia sunna ya tahiyatu-l-masjid.
Ya Nne, kulala Muzdalifa; hupatikana hii kulala Muzdalifa japo kwa kupitisha sehemu kubwa ya usiku hapo Muzdalifa. Wanazuoni wengine wamesema hupatikana hii kulala Muzdalifa japo kwa kupitisha sehemu tu ya baada ya nusu ya pili ya usiku. Hulala hapa Muzdalifa wakati wa kurejea kutoka 'Arafa. Hapa Muzdalifa aghlab ndipo watu wanapo okota vijiwe vya kulembelea maguzo yaani,  
  .
Ya Tano, kusali raka'a mbili baada 'tawaaf ya fardhi, hivi ni kwa qauli ya Mtume wetu Mpenzi s.a.w, yaani Sala tano mchana na usiku. Mtu kumuuliza Mtume wetu Mpenzi s.a.w.: "Je, ninalazimika na zaidi ya hizo"? Akasema Mtume wetu Mpenzi s.a.w.: "" , yaani hulazimiki zaidi ya hizo Sala tano, isipokuwa ukisali za sunna.
Ya Sita, kulala Mina usiku wa kuamkia siku ya 'Arafa; yaani taarikh nane ya mfunguo tatu, kuamkia taarikh tisa ya mfunguo tatu. Hupatikana huku kulala Mina kwa kupitisha sehemu kubwa ya usiku hapo Mina.

Ya Saba, 'tawaafu-l-widaa'i, 'tawaafu ya kuaga. Hili ndilo la mwisho analofanya mwenye kuhiji kwa kutimiza a'amali zake za Hija. Hivi ndivyo ilivyopokewa kuwa Sayyidna 'Umar r.a. amesema: ", yaani mwisho wa a'amali za Hija ni 'tawaaf ya kuaga Nyumba Tukufu. (Imeelezwa na Imam Maalik).

Haijuzu kwa kwa aliomo kwenye ihraam, ikiwa ni ya 'Umra au ni ya Hija; kuvaa nguo ilioshonwa au viatu vilivyoshonwa. Mwenye kuhirimia inapendekezwa avae shuka nyupe na guo jeupe la kujitupia mabegani na viatu vya kanda mbili (vya mpira). Amesema Ibnu Al Mundhir r.a. kwamba imethibiti kuwa Mtume wetu Mpenzi s.a.w. amesema:  "Naahirimie mmoja wenu hali amevaa shuka nyeupe na guo jeupe na viatu (vya kanda mbili)".
Na ameeleza Imam Bukhary r.a. kutokana na Ibni 'Abbaas r.a.:  "Amehirimia Mtume wetu Mpenzi s.a.w. nae amevaa shuka nyeupe na guo jeupe, na hivyo ndivyo walivyofanya Masahaba wake r.a.". (Imehadithiwa na Muslim).
Kukhusu kuvaa shuka nyeupe na guo jeupe, hivi pia ni kwa qauli yake Mtume wetu Mpenzi s.a.w. (iliyotangulia kutajwa):    "Vaeni nguo nyeupe kwani hizo ni bora ya nguo zenu na wakafinini maiti wenu kwa nguo nyeupe". (Imehadithiwa na Abu Daud na Al Tirmidhy).
Ni makruuh kuvaa nguo ya rangi. Inapendekezwa asali raka'a mbili kabla ya kuhirimia, asome kwenye raka'a ya kwanza  raka'a ya pili asome "  " 

 ". Ikiwa atasali Sala ya fardhi itatosheleza hizi raka'a mbili za sunna ya kuhirimia, yaani Sala ya fardhi itakuwa mahala pa hizi raka'a mbili za sunna.

Inaharamishwa (inakatazwa) kwa aliomo kwenye ihraam mambo kumi:
La Kwanza, mwanamume kuvaa nguo iliyoshonwa.
La Pili, mwanamume kufunika kichwa.
La Tatu, mwanamke kufunika uso. Mwanamume akisha hirimia inakatazwa kuvaa mwilini mwake - tangu miguuni mpaka kichwani - nguo iliyoshonwa; ikiwa ni kanzu, shuka, suruwali, kofia, au kilemba. Hivi kwa qauli ya Mtume wetu Mpenzi s.a.w. pale alipoulizwa nini avae mtu aliomo kwenye ihraam, akasema s.a.w.:

"Msivae kanzu, wala kilemba, wala suruwali, wala barnisi*, wala khufaaf**, ila ikiwa hamkupata viatu (ndaara), basi vaaeni hizo hizo khufaini, lakini zikateni chini kwenye visigino, wala msivae nguo iliyotiwa (ya) rangi au za'afarani".
Imesemwa kuwa mwenye kukosa viatu inajuzu kuvaa khufaini, bila ya kuzikata visiginoni. Hadithi ya kukata khufaini visiginoni imefutwa kwa Hadithi yake yeye Mtume wetu Mpenzi s.a.w. ambayo haikutaja kuzikata visiginoni hizo khufaini: ".  

  "Mwenye kukosa viatu naavae khufain, na mwenye kukosa shuka naavae suruwali". (Imehadithiwa na Al Sheikhan na Ibnu 'Abbaas).
Kukhusu kukatazwa mwanamume kufunika kichwa akiwa katika ihraam imekuja kwa qauli ya Mtume wetu Mpenzi s.a.w. kukhusu mtu aliekuwemo kwenye ihraam akaanguka kutoka kwenye ngamia wake akafa.
.Amesema Mtume wetu Mpenzi s.a.w.:  

  "Musimfunike kichwa, kwani atafufuliwa Siku ya Qiyama nae analabbi". (Imehadithiwa na Al Sheikhan).
* Guo lenye kofia iliounganishwa pamoja na hilo guo.
** Wingi wa khuffu mbili - imetangulia kutajwa hizi khuafain
Shuka inajuzu kuifunga kwa uzi, na inajuzu kuipiga fundo kwa wepesi na kunusuru isije ikamvuka. Kukhusu guo analojizongeresha kupitia mabegani, hili haijuzu kulifunga kwa uzi, au kulifunga kwa ncha yake.
Hivi ni kukhusu mwanamume, ama kwa mwanamke; uso wake ni sawa na kichwa kwa mwanamume - asijifunike uso. Mwanamke ajisitiri mwili wake wote pamoja na kichwa chake kwa nguo ya kushonwa.
Mwanamke anaweza kufunika uso wake kwa nguo au kitambaa lakini kwa sharti kisiguse uso wake, hujuzu hivi kwa haja au bila ya haja, kama vile kujihifadhi na joto au baridi, au akichelea fitna na hali kama hio.
La Nne, kuchana nywele au kujikuna kichwa hali akijua kuwa kuzichana au kujikuna kichwa zitatoka nywele zake kwa kupukutika au kwa mfano wa hivyo.
La Tano, kuondoa nywele, kwa kunyowa; hivi ni kwa Qauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu 

  "…… Wala msinyoe vichwa vyenu mpaka wanyama hao wafike machinjoni mwao………". (Al Baqara : 196).
Huku kukatazwa kuondoa nywele ni kwa njia yoyote ile na nywele zozote zile za mwili. Kuondoa ikiwa kwa kunyoa, au kupunguza, au kunyonyoa, au kuziunguza au kwa kutumia dawa ya kutoa nywele, au kwa njia yoyote ile.

La Sita, kukata kucha au kupunguza; kwa njia yoyote ile, ikiwa kwa kukata au kwa kutafuna, au kwa kuzivuta kwa mkono na kuzinyofuwa, au kwa njia yoyote ile.
La Saba, kujitia manukato kwenye nguo na/au kwenye mwili; kwani kitendo hiki ni kitendo cha pambo na raha; na mwenye kuhiji ni mtu aliejaa mavumbi, na machofu, hivi kama ilivyokuja kwa qauli ya Mtume wetu Mpenzi s.a.w.:  

  "Ama manukato uliyonayo (unayonukia), jikoshe (kuondoa harufu yake) mara tatu". Na manukato ni chochote kile kinachotumika kwa makusudio ya kunukia, kama vile mawaridi, asumini, mafuta mazuri; vitu ambavyo hutumiwa kwa ada ya kunukia. Ikiwa atachukua miski, au udi, au chochote kile kwenye kitu kilichofungiwa uzuri na bila ya makusudio ya kunukia yeye, hivyo haikatazwi.
La Nane, kuwinda, na kuwinda ni njia ya kumpata mnyama wa mwitu kwa njia ya hila; sawa ikiwa yeye atafanya hivyo kwa furaha yake au kwa haja. Huku kuwinda kunakokatazwa ni sawa ikiwa kwa mnyama au ndege, muhim ni kuwinda - kusaka. Na kama inavyo haramishwa kuuwa wanyama na ndege kwa njia ya kuwinda, inaharamishwa pia kuwinda kwa kuwaweka pambo na kadhaalika. Hivi ni kwa Qauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu:  

  "………Na mmeharimishiwa mawindo ya wanyama wa bara maadamu mmeharimia Hija………". (Al Maida : 96).
Kuharamishwa kuwinda na kuuwa vinyama na vidudu ni kwa wanyama wenye kuliwa na wasiodhuru wala kuudhi. Ama wanyama wenye kudhuru na/au kuudhi, kama vile nyoka, nnge, kunguru, mbwa mwenye kutafuna, chui, bweha, panya, viroboto, mbu, chawa na wengineo miongoni mwa wanyama na vidudu vyenye kudhuru/kuudhi; hivi inajuzu kuviuwa hata wakati umo kwenye ihraam.
La Tisa, kufunga ndoa na yenye kuambatana na ndoa; kuingiliana mwanamume na mwanamke, kuchezeana kwa matamanio, na ya mfano wake. Muhrim anakatazwa kufunga ndoa yeye mwenyewe, au kwa niaba ya mwengine au kutoa idhini ya walii, kama inavyo katazwa kwa mwanamume inakatazwa kwa mwanamke kuolewa; hivi ni kwa qauli ya Mtume wetu Mpenzi s.a.w.:  

    "Asiowe muhrim wala asiolewe".
Na katika Hadithi nyengine, " , yaani asiposhe. (Imehadithiwa na Muslim).
Na katika Hadithi aliopokea Darqu'tny r.a.:  

   "Asiowe muhrim wala asiozeshe".
Akiowa basi ndoa haisihi, kwa sababu hivi kukatazwa inaingia kutosihi kitendo hicho. Kuingiliana mwanamume na mwanamke kumekatazwa kwa Qauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu: "…., basi asiseme maneno machafu wala asifanye vitendo vichafu wala asibishane katika Hija………". (Al Baqara : 197).
", ni kitendo cha kuingiliana mwanamke na mwanamume, ambacho ndicho kilichokatazwa. Vilevile imekatazwa kuchezeana kwa matamanio, na kujichezea mwenyewe, na kujitoa manii na yote yalio mfano wa haya.

Yote haya yaliokatazwa, tangu kutia manukato na mengineo; mwenye kufanya lolote miongoni mwa haya itamlazim atoe fidia, hivi ni kwa vile amejitia katika yale yaliokatazwa. Katika kuchezeana au kujichezea, fidia huwajibika juu yake ikiwa itafika kutokwa na manii.
Kufunga ndoa hakuwajibikii fidia, kwa sababu hio ndoa yenyewe asili yake haikusihi. Ama kuingiliana mwanamume na mwanamke hili halina fidia, kwa sababu kwa kitendo hiki Hija huba'tilika, kama inavyo haribika Hija kwa kitendo hiki ndivyo huharibika 'Umra vilevile. Lakini basi, hata hivi kuba'tilika Hija yake, itamlazim aendelee nayo kwa a'amali zake zote za Hija - wala asiikate - mpaka amalize a'amali zote; hivi ni kwa Qauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu:  

  "Na timizeni Hija na Umra kwa ajili ya Mwenyezi Mungu……". (Al Baqar : 196).
Kwa hivi kufisidika hii Hija yake itamlazim ailipe kwa haraka bila ya kuchelewa, sawa sawa ikiwa ni Hija ya fardhi au ya sunna. Ni deni ambalo haifai kuakhirishwa kulipwa. Kukhusu mwanamke, ikiwa ameingiliwa na mume wake bila ya ridhaa yake yeye mwanamke, au akiingiliwa usingizini bila ya kujuwa, yeye Hija yake haitaba'tilika; lakini ikiwa wameingiliana kwa ridhaa zao wote wawili, basi na yeye mwanamke Hija yake itaba'tilika vile vile, na hukmu yake ni sawa na mumewe; kukhusu kuendelea na Hija na kuilipa hio Hija kwa haraka.
Mwenye kukosa kushinda Arafa, kwa kuchomozewa na jua siku ya kuchinja, yaani taarikh kumi ya mfunguo tatu, na hakuwahi usiku wake, yaani usiku wa taarikh tisa mfunguo tatu kuamkia taarikh kumi ya mfunguo tatu kuwa 'Arafa; basi ameikosa Hija; hivi ni kwa qauli ya Mtume wetu Mpenzi s.a.w.:

"Mwenye kuwahi (kuwepo/kufika) 'Arafa usiku (wa kuamkia siku ya kuchinja) ameipata Hijja, na mwenye kukosa (kuwepo/kufika) 'Arafa usiku (wa kuamkia siku ya kuchinja) ameikosa Hija; basi naainuwie kuwa 'Umra na juu yake (ailipe kwa) Hijja inayokuja". (Imehadithiwa na Darqu'tny).
Kama ilivyo tangulia kuelezwa kwa qauli ya Mtume wetu Mpenzi s.a.w. kwamba: " 

 ", yaani Hija ni kutekeleza nguzo ya 'Arafa", na vile hii 'Arafa ni ibada yenye wakati maalum, basi haiwi kutekelezwa nje ya wakati wake, kama vile Sala ya Ijumaa, ukipita wakati wake haiwi kusaliwa baadae. Inatakiwa kwa mwenye kuikosa 'Arafa, kwa kuba'tilika Hija yake afanye haraka kutoka kwenye ihraam ya Hijja kwa kunuilia na kutekeleza 'Umra, nayo ni kwa kufanya 'tawaaf na sa'ai (mwendo wa baina ya 'Safaa na Marwa), kisha anyowe na kutoka kwenye ihraam. Ikiwa alipoingia Makka alifanya 'tawaaf ya kuamkia Msikiti Mtukufu " 

 " , basi haitamlazim ku'tufu tena, atafanya sa'ai, (mwendo wa 'Safaa na Marwa) kisha atanyoa na kutoka kwenye ihraam. Yeye haitamlazim kulembea wala kulala Muzdalifa hata kama bado wakati ungalipo.
Kama inavyomlazim kuilipa hii Hija yake ilioba'tilika kwa vile kukosa kutekeleza nguzo ya 'Arafa, inamlazim vilevile kutoa fidia, yaani kuchija. Alikwenda Bwana Habbaar bin Al Aswadi r.a. kwa Sayyidna 'Umar r.a. siku ya kuchinja, akasema: "Ewe Amir-l-Muuminiin!" "Tumekosea hisabu" (Imeelekea ni hisabu ya taarikh ya mwezi mwandamo). Sayyidna 'Umar r.a. akamwambia: "Nenda Makka ka'tufu weye na walio pamoja na wewe, na fanyeni sa'ai na chinjeni, ikiwa mnacho cha kuchinja, kisha nyoweni au punguzeni kisha rejeeni. Mwaka ujao, fanyeni Hija na chinjeni, asiekuwa nacho cha kuchinja, afunge siku tatu katika Hijja na siku saba akirejea (kwake). (Imehadithiwa na Imam Malik r.a.). Ilienea hukmu hii, kwa hivyo ikakubalika na wanazuoni wote.

Mwenye kuwacha/kukosa kutekeleza nguzo yoyote ile ya Hijja hatoki kwenye ihraam mpaka aitekeleze hio nguzo, wala haiungwi (haifidiwi) hio nguzo alioiwacha/alioikosa kuitekeleza kwa kuchinja, lakini hubakia dhima juu ya yake; kwa sababu kukamilika Hijja ni kwa kukamilika nguzo zote za Hijja; sawa na Sala, haikamiliki Sala wala haindoki dhima yake mpaka ikamilike kwa nguzo zake zote.

Damu (kuchinja) yenye kuwajibika katika utekelezaji wa Hijja, ikiwa ni kwa kuwacha/kukosa kutekeleza la waajibu au kwa kufanya lililoharamishwa, inawajibika kuchinja kondoo au mbuzi. Ama kwa kuingiliana na mwanamke, hukmu yake ishatangulia kuelezwa. Ama kukhusu fidiya kwa kufanya kosa la kuwinda au kuuwa mnyama kama ilivyokatazwa, hivyo inalazim kulipa fidiya kwa kuchinja mnyama wa mfano wa kilicho windwa au kuuliwa, ikiwa kikubwa, basi alipe kwa kuchinja mnyama mkubwa, ikiwa kidogo, alipe kwa kuchinja mnyama mdogo.

Kuwajibika kuchinja huwa kwa sababu tano:

Ya Kwanza, kwa kuwacha/kukosa kutekeleza la waajibu, kama vile kukosa kuhirimia kwenye (mipaka) miiqaat yake, au kukosa kulembea "jamaarik" maguzo. Kwa haya itamlazim achinje kondoo au mbuzi, akikosa kupata cha kuchinja atanunua chakula cha thamani hii atoe sadaqa, akishindwa kufanya hivi atafunga siku moja kwa kila kibaba cha chakula ambacho ilikuwa akitoe sadaqa.

Ya Pili, kunyowa/kupunguza nywele au kufanya lolote lile la raha, kama vile kukata kucha, kutia manukato au lolote lililoharamishwa katika sehemu hii. Mwenye kunyowa au kukata nywele tatu au kucha, itamlazim kutoa fidiya. Huyu yeye amepewa khiyari, baina ya kuchinja au kutoa sadaqa ya pishi tatu kuwapa masikini sita - kila masikini ampe nusu pishi - ya chakula cha kawaida cha mji, au kufunga siku tatu. Asili ya huku kupewa khiyari kumekuja kwa Qauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu:

   "... Na atakaye kuwa mgonjwa au ana vya kumuudhi kichwani mwake basi atoe fidiya kwa kufunga au kwa kutoa sadaka au kuchinja wanyama………". (Al Baqara : 196).
Imekadiriwa ya kwamba kunyowa wakati kumekatazwa kwenye ihraam inalazim kutoa fidiya, na amebainisha haya Mtume wetu Mpenzi s.a.w.:

"Je, zinakuudhi mvi za kichwani mwako"? Akajibu: "Naam". Akasema s.a.w.: "Chinja kondoo au mbuzi, au funga siku tatu, au walishe masikini sita chakula cha pishi tatu". (Imehadithiwa na Al Sheikhan).

   (faraq) moja ni pishi tatu. Na katika kunyowa inaingia na kukata kucha, kutia manukato na kila la raha ambalo limekatazwa katika sehemu hii.

Ya Tatu, kuzuilika kukamilisha Hijja au 'Umra. Ikiwa mwenye kuhiji au kufanya 'Umra amezuilika kwa sababu yoyote ile kukamilisha a'amali zake za Hijja au 'Umra, kuzuilika huku sawa sawa ikiwa yeye yumo kwenye ihraam au hayumo kwenye ihraam na asipate njia nyengine ya kuendeleza na kukamilisha a'amali zake hizo za Hijja/'Umra basi atatoka kwenye ihraam, (ikiwa alikuwa bado yumo kwenye ihraam) na atachinja kutoa sadaqa. Atachinja kwa uchache kondoo au mbuzi kama vile inavyofaa katika kulazimika kuchinja kwa sababu nyengine katika utekelezaji wa ibada hii, na muhim katika hali hio atie nia ya kutoka kwenye ihraam - ikiwa yumo kwenye ihraam. Haya ni kwa Qauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu:  
   "…………Na ikiwa mkizuiwa, basi (chinjeni) wanyama walio wepesi kupatikana………". ( Al Baqara : 196 ).
Na kwa kukadiria makusudio ya Aya hii ni kwamba mnapozuilika, basi tokeni kwenye ihraam na juu yenu kuchinja mnachokiweza katika wanyama. Na imekuja kwenye Hadithi ya kwamba Mtume wetu Mpenzi s.a.w. alikuwa kwenye ihraam kwa ibada ya 'Umra, alipofika Hudaibiya Makafiri wakamzuilia kuinigia Makka kutekeleza 'Umra; s.a.w. alitoka kwenye ihraam. Ni lazima kutanguliza kuchinja kabla ya kunyowa, hivi ni kwa Qauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu  

 "……… Wala msinyoe vichwa vyenu mpaka wanyama hao wafike machinjoni mwao………". (Al Baqara : 196 ).
Ya Nne, kuuwa mnyama. Aliomo kwenye ihraam, ikiwa atauwa kwa makusudi mnyama ambae ana mfano wake mnyama huyo; basi amepewa khiyari baina ya kuchinja mnyama wa mfano wa huyo mnyama aliemuuwa na kuitoa nyama hiyo sadaqa kwa masikini waliomo katika sehemu ya Haram ya Al Ka'aba, na baina ya kutoa thamani ya mnyama alielazimika kumchinja na kuwapa thamani hio masikini sadaqa ya chakula cha kawaida, au afunge siku moja kwa kila kibaba ya chakula cha kawaida kinacho nunulika kwa thamani hio. Hivi ni kwa Qauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu:

"Enyi mlio amini! Msiue wanyama wa kuwinda nanyi mmehirimia katika Hija. Na miongoni mwenu atakaye muuwa makusudi, basi malipo yake yatakuwa kwa kuchinja kilicho sawa na alicho kiuwa, katika mifugo, kama wanavyo hukumu waadilifu wawili miongoni mwenu. Mnyama huyo apelekwe Al Kaaba, au kutoa kafara kwa kuwalisha masikini; au badala ya hayo ni kufunga, ili aonje ubaya wa jambo lake hili. ..............". (Al Maaidah : 95).
Na ikiwa mnyama aliemuuwa hakuna mfano wake, basi anapewa khiyari baina ya kutoa sadaqa thamani ya mnyama huyo au kufunga siku moja kwa kila kibaba cha chakula cha kawaida kinacho nunulika kwa thamani hio. Hikma ya kulipishwa hivi ni kwa khasara alioitia. Na inaposemwa mnyama aliefanana na yule alieuliwa, inakusudiwa kufanana kwa kukaribiana, si kufanana kwa kila kitu, au kuwa iwe wa jinsi moja.
Miongoni mwa wanazuoni Masahaba wamehukumu zaidi ya mara moja kwa mwenye kuuwa mbuni kuchinja ngamia, na kwa mwenye kuuwa punda-milia au n'gombe, kwa kuchinja n'gombe, na kwa mwenye kuuwa bweha kwa kuchinja kondoo, pia wamehukumu kwa mwenye kuuwa paa kwa kuchinja mbuzi jike. Na hivi hivi amehukumu Mtume wetu Mpenzi s.a.w. na Masahaba zake r.a. Na kwa kuuwa mnyama mkubwa achinjwe mnyama mkubwa vilevile, na ikiwa ameuliwa mnyama jike, achinjwe mnyama jike vilevile. Na ikiwa alieuliwa ni mnyama kiguru, basi na kujicha achinjwe mnyama kiguru vilevile; hivi yote ni kujitahidi kupata ile kufanana alioitaja Mwenyezi Mungu Mtukufu kwenye hii Aya ya 95 ya Surat Al Maaidah.

Ya Tano, kuingiliana mwanamume na mwanamke. Kuchinja (damu) kwenye kuwajibika kwa kuingilia mwanamke huwa kwa kufuatilia kiwango baada ya kiwango. Kiwango cha mwanzo hutakiwa achinje ngamia, akikosa ngamia achinje n'gombe, akikosa n'gombe achinje kondoo/mbuzi saba, akikosa kondoo/mbuzi saba, itathaminiwa bei ya ngamia na kwa thamani hio atanunulia chakula cha kawaida akitoe sadaqa kwa masikini wa hapo kwenye haram ya Al Kaaba. Akishindwa kufanya lolote kati ya haya, atafunga siku moja kwa kila kibaba cha chakula ambacho kinanunulika kwa hii thamani ya ngamia. Kukhusu kuwajibika kuchinja ngamia ndivyo walivyotoa fatwa juu yake Sayyidna 'Umar r.a. na mwanawe; Sayyidna Abdulla bin 'Umar r.a. na hivyo hivyo ndivyo walivyotoa fatwa Sayyidna Ibnu 'Abbaas r.a. na Sayyidna Abu Huraira r.a. Ama kukhusu kuingizwa kuchinja n'gombe au mbuzi/kondoo saba hii imechukuliwa kutokana na hukmu ya kuchinja kwenye kuwajibika. Ama kukhusu kulisha masikini kwa thamani ya huyo ngamia ambae ndio asili ya kuchinja kwenye kuwajibika, hii imechukuliwa kutokana na hukmu ya kuchinja kwa mwenye kuuwa au kuwinda wakati yumo kwenye ihraam. Hivi kuthaminiwa ngamia huwa kwa bei ya Makka, na wanazuoni wengine wamesema kuwa ni kwa bei ya Mina, na wengine wamesema kuwa ni kwa bei ya pale pahala kilipotokea hicho kitendo cha kuingiliana.

Kuwajibika kuchinja huweza ikawa kwa sababu ya kuzuilika kukamilisha kutekeleza a'amali za Hija au 'Umra, au kwa kufanya lile lililoharamishwa kwa aliomo katika ihraam au kuwacha lile lililotakiwa kufanywa katika kutekeleza a'amali za Hija au 'Umra. Ikiwa kuchinja ni kwa sababu ya kuzuilika, basi atachinja pale pahala alipozuilika, hivi ni kwa vile Mtume wetu Mpenzi s.a.w. alizuilika alipokuwa Hudaibiya na akachinja wakati yupo hapo Hudaibiya. Kukhusu kuchinja kwa sababu ya kufanya lililokatazwa au kuwacha lililoamrishwa kufanywa, kuchinja kwa katika hali hizi inalazim kufanywa kwenye Haram ya Al Ka'aba; hivi ni kulingana na Qauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu:  

 , " yaani "Mnyama huyo apelekwe Al Kaaba". Na inapasa nyama hio igawiwe kupewa masikini waliomo humo, yaani katika Haram ya Al Ka'aba, kwani hii ndio dhamiri ya huko kuhukumiwa kuchinja. Kukhusu hawa masikini wa kupewa hii sadaqa, hapana tafauti ikiwa ni masikini wenye kuishi hapo Makka au wamepita tu; muhim ni kwamba wakati huo wapo hapo katika Haram ya Al Ka'aba. Vilevile ikiwa atatoa sadaqa chakula badala ya kuchinja, itawajibika kupewa msikini wa hapo Haram ya Al Ka'aba kama vile ilivyowajibika kupewa sadaqa ya hio nyama.
Ama kukhusu kufunga, anaweza kufunga popote pale, si lazima kwenye Haram ya Al Ka'aba. Uchache wa kuondosha waajibu katika kuwalisha masikini iwe amewalisha masikini watatu. Si lazima kila mmoja ampe sawa na mwengine, hujuzu kumpa mmoja zaidi kuliko mwengine, hutegemea hali yao baina ya hao maskini.

Kuwinda kwenye Haram ya Makka ni haraam kwa mwenye kuhirimia Hija/'Umra na asie hirimia, yaani ni haraam kwa kila mtu kuwinda katika Haram ya Makka. Vilevile ni haraam kukata mti au mmea wowote ule kwenye Haram ya Makka, madam mnyama au mti/mmea huo hauna madhara. Ama mti/mmea mkavu au mnyama mwenye kuudhi au madhara, si haraam kukatwa/kuuliwa. Hivi ni kwa qauli ya Mtume wetu Mpenzi s.a.w. Siku ya Ufunguzi wa Makka

"Hakika ya mji huu ni mtukufu kwa Utukufu wake Mwenyezi Mungu Mtukufu, haukatwi mti wake, wala hatishwi/hafurushwi mnyama wake, wala hakiokotwi kilichomuanguka mwenyewe mpaka ajuulikane mwenyewe; wala hayan'golewi majani yake mabichi. Akasema Al 'Abbaas r.a.: "Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu Mtukufu! Isipokuwa majani makavu, kwani hayo hutumiwa na wahunzi na wenye kututia dari za nyumba zao". Akasema Mtume wetu Mpenzi s.a.w.: "Isipokuwa majani makavu". (Imehadithiwa na Al Sheikhan).
Inajuzu kuchukuwa (kukata, kuchuma au kupurura) majani ya mti lakini asiugonge huo mti kuchelea kuuchuna magome yake. Kama inavyoharamishwa kukata mti katika eneo la Haram ya Makka, vilevile inaharamishwa kukata mimea ilioota wenyewe katika eneo la Haram ya Makka, yaani mimea ambayo haikupandwa. Hivi kuharamishwa kukata hii mimea ilioota wenyewe kunahukumiwa kwa kulinganishwa na kule kukatazwa kukata miti kulikotajwa kwenye hii Hadithi ya Mtume wetu Mpenzi s.a.w., kwa qauli yake s.a.w.:  

 , yaani "haukatwi mti wake". Imehukumiwa kwamba, madhali imeharamishwa kukata mti, basi kun'gowa mti ni haraam zaidi, na hii mimea ni miongoni mwa aina za miti. Ama kuchunga wanyama kwenye Haram ya Makka inajuzu. Vilevile inajuzu kun'gowa majani kwa ajili ya kulishia wanyama, wanazuoni wengine wanasema kuwa kun'gowa majani haijuzu. Ama kuchukuwa (kukata, kuchuma au kupurura) majani kwa ajili ya dawa, hili linajuzu na halina khilaf za wanazuoni, hivi ni kwa vile matumizi ya majani kwa haja ya dawa (aghlab ya hali) ni muhim kuliko maumizi ya majani kwa kututilia dari za nyumba.

Ikiwa mtu atakuwa ana uwezo wa kuhiji, asihiji, kisha akashindwa kuhiji, kwa sababu ya ugonjwa usiotarajiwa kupowa au kafikwa na uzee; inamlazim kwa hisab yake amteuwe mtu ende kumuhijia. Dalili ya haya ni Hadithi ya Ibni 'Abbaas r.a. kwamba mwanamke katika watu wa Khath'am alisema:

"Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Hakika kufaridhisha Mwenyezi Mungu Mtukufu juu ya waja wake kuhiji kumemfika baba yangu naye ni mzee hawezi kuthibiti nafsi yake juu ya kipando, je nimuhijie"? Mtume wetu Mpenzi s.a.w. akasema: "Naam". (Imehadithiwa na Maalik na Al Shafi'ii na Al Sheikhan na Abu Daud na Al Nissaai).

Amesema Imam Al Tirmidhy r.a. kwamba imethibiti kutokana na Mtume wetu Mpenzi s.a.w. zaidi ya Hadithi moja kukhusu suala hili la mtu kulazimika kuhijiwa katika hali hii iliotajwa hapo juu, yaani alikuwa na uwezo lakini hakuhiji. Mwenye kufa na ana waajibu wa Hija juu yake, inalazim kwa walii (mtu wake/wao) amuhijie maiti wake/wao au aandae/waandae mtu kumuhijia maiti wake/wao; hivi ni kwa ilivyohadithiwa kwamba mwanamke katika banu (watu wa) Juhainah alikwenda kwa Mtume wetu Mpenzi s.a.w. akasema: "Hakika ya mama yangu aliweka nadhiri kuhiji, lakini hakuhiji mpaka amekufa. Jee, nimuhijie? Mtume wetu Mpenzi s.a.w. akasema: "Naam, muhijie". Inashurutishwa kwa mwenye kumuhijia mtu mwengine iwe yeye mwenyewe amekwisha Hiji, na awe ni mtu mwaminifu na mwenye kufahamu vyema hukmu zote za Hija. Na inapendekezwa wakati wa kulabbi aseme," , yaani nina labbi (naitikia mwito Wako) kwa niyaba ya fulani.

  

No comments:

Post a Comment