DAR ES SALAAM
MBUNGE wa Kawe, Halima Mdee (35) na wanachama
wenzake wanane wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wamepelekwa
rumande baada ya kushindwa kukamilisha taratibu za dhamana katika kesi
inayowakabili ya kutotii amri halali ya Polisi na kufanya mkusanyiko bila
kibali.
Mdee ambaye ni Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake
Chadema (Bawacha) pamoja na wanachama hao, wamepandishwa kizimbani katika
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam.
Wengine ambao wameosomewa mashitaka mbele ya
Hakimu Mkazi, Janeth Kaluyenda ni Rose Moshi Mkazi wa Kinondoni B, Renina Peter
maarufu kama Lufyagila mkazi wa Kinondoni Mkwajuni, Anna Linjewile mkazi wa
Mbezi Luis na Mwanne Kassim mkazi wa Pugu Kajiungeni.
Mawakili wa Serikali, Bernard Kongola, Salum
Mohamed na Hellen Mushi wakisaidiana kusoma mashitaka, wamedai Oktoba 4, mwaka
huu, katika mtaa wa Ufipa, bila kuwa na uhalali washitakiwa hao walikiuka amri
halali ya kutawanyika iliyotolewa na Mrakibu wa Polisi (SP) Emmanuel Tillf kwa
niaba ya Jeshi la Polisi.
Katika mashitaka mengine inadaiwa siku hiyo
katika eneo hilo, kwa pamoja, walifanya mkusanyiko usio halali kwa lengo la
kutembea kwenda Ofisi ya Rais.
Hata hivyo, washitakiwa wamekana mashitaka hayo
na kesi hiyo imeahirishwa hadi Oktoba 21 mwaka huu itakapotajwa kwa ajili ya
usikilizwaji wa awali.
No comments:
Post a Comment