Friday, October 17, 2014

MUUNGANO WA ASASI ZA KIJINSIA "KATIBA INAYOPENDEKEZWA IPO POA"



Muungano wa Asasi za Kiraia Juu ya Jinsia na Katiba (GFC), umesema Katiba Inayopendekezwa imezingatia mapendekezo yao kwa zaidi ya asilimia 90, hasa katika usawa wa kijinsia na haki za watoto.

Aidha, umewataka wananchi kuacha ushabiki wa kisiasa na kufuata mkumbo wa kuipinga badala yake waisome na kuichambua kila kipengele ili waielewe.

Akizungumza jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa GFC, Victoria Mandari amesema wanaamini mafanikio yaliyofikiwa katika suala la kijinsia pia limetokana na juhudi za muungano huo unaoundwa na asasi saba za kiraia zikiwemo Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania (TAWLA) na Wanawake na Sheria Afrika Mashariki (WLEA).

Amesema kwa sasa kuna kesi nyingi mahakamani za migogoro ya ardhi na mali kutokana na utamaduni uliojengeka kwamba mwanamke hawezi kumiliki mali na mirathi lakini kwa sasa haki sawa itakuwapo kwa sababu Katiba hii ikipitishwa, inatamka wazi kuhusu usawa wa kijinsia.

Kwa upande wake, Mkurugenzi TAWLA, Tike Mwambipile amesema ni vyema kila mwananchi akaisoma katiba hiyo inayopendekezwa na kuielewa badala ya kufuata mkumbo ili muda wa kupiga kura ukifika aweze kujua nini kinapendekezwa.

No comments:

Post a Comment