Saturday, October 4, 2014

SIKU ZILIZOBARIKIWA ZA DHUL-HIJJAH





NA: QUR'AN WA SUNNAH SOCIETY
 Kutokamana na Ukarimu wake mkubwa usio na kifani, Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Ta’ala) amewajaalia waja wake, walio mahujaji na wakaazi (wasiokuwa mahujaji), idadi ya masiku yaliyobarikiwa.

Masiku hayo ni yale kumi na tatu ya mwanzo ya mwezi wa kiislamu ya Dhul-Hijja. Katika yafuatayo tutagusia baadhi za Sunnah kuhusu siku hizo tukitarajia kwa hayo kujiandaa na kuwa na hima ili tufanye yalio bora.

SIKU KUMI ZA MWANZO WA DHUL-HIJJA

Fadhila Zake:

Siku kumi za mwanzo wa Dhul-Hijja zina fadhila maalumu na umuhimu katika Uislamu. Nayo ni masiku yaliyo bora katika mwaka mzima. Amali njema zinapendwa zaidi na Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Ta’ala) na kwahivyo zina malipo makubwa zaidi kwenye siku hizo.

Jabir Bin 'Abdillah  (Radhiya Llahu anhu) akapokea kutoka kwa Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) kuwa amesema:
"Siku zilotukufu ulimwenguni ni siku kumi."[1]

Na akapokea Ibn Abbas  (Radhiya Llahu anhu) kwamba Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) amesema:
"Hakuna masiku ambayo amali njema zinapendwa zaidi na Mwenyezi Mungu kama masiku haya (kumi)."[2]

Kisha nae Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) akaulizwa: "Hata pia Jihad kwa njia ya Mwenyezi Mungu?" akajibu:

"Hata pia Jihad kwa njia ya Mwenyezi Mungu isipokuwa kwa yule alokwenda (Jihad) kwa nafsi yake na mali yake na asirudi na kitu (akapoteza hayo yote) kwa ajili ya Mwenyezi Mungu."[3]

Tufanyeje Katika Siku Hizi

Kama ilivyo-onyesha kwenye Hadithi hiyo ya mwisho, amali zote njema ni zenye kupendwa na Mwenyezi Mungu katika siku hizo.

Ma-Salaf wameifahamu vizuri sana; ikapokewa yakwamba wakati mmoja katika siku hizi kumi zilipoanza, Sa'id Bin Jubayr alijitahidi kupita kiasi (kufanya Ibada) mpaka akafika kiwango cha kujikalifisha.

Hasa zaidi, kufunga na kufanya dhikr (kumtaja na kumkumbuka Mwenyezi Mungu) yanatakikaniwa kufanywa zaidi katika siku hizi

Dhikr:
Ibn Umar na Abu Huraira  (Radhiya Llahu anhu) walikuwa wakienda sokoni kwenye hizi siku kumi wakifanya takbir. Na watu walikuwa wakifuata mfano wao nao wakisema takbir pia.[4]

Hii yaonyesha utwiifu wao kwa amri ya Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) kama ilivyopokewa na Ibn Umar  (Radhiya Llahu anhu):

"Hakuna masiku yaliyo matukufu mbele ya Mwenyezi Mungu, na ambayo amali njema zinapendwa zaidi na Yeye, zaidi ya hizi siku kumi, kwahivyo sema (wakati huo) kwa wingi, tahlil (La ilaha illallah – hapana Mola apasae kuabudiwa kwa haki illa Mwenyezi Mungu), takbir (Allahu Akbar – Mwenyezi Mungu ni Mkubwa) na tahmid (Al-hamdu lillah – Sifa zote na shukurani ni za Mwenyezi Mungu).[5]

Na katika tafsir (ufafanuzi) ya Aya "... na kulitaja jina la Mwenyezi Mungu (kwa wingi) katika siku zinazojulikana",[6] Ibn Abbas akasema:

"Siku hizi zinazojulikana ni siku kumi (za Dhul-Hijjah)."[7]

KUFUNGA:
Mmoja katika wake za Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) amesema: "Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w) alikuwa akifunga siku tisa za mwanzo za Dhul-Hijjah, siku ya Ashura na siku tatu za killa mwezi."[8]

Walaakin kufunga siku zote hizo sio wajib wala sio sunnah iliyo thabiti ambayo Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) hakuwahi kuikosa.

Akasema Aisha  (Radhiya Llahu anhaa), "Sikuwahi kumuona Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) akifunga hizo siku kumi."[9]

SIKU YA ARAFA

Siku ya tisa ya mwezi wa Dhul-Hijjah inaitwa siku ya Arafa kwa sababu Mahujaji huja kusimama kwa ibada kwenye mlima wa Arafa siku hiyo. Hiyo ni siku bora ya masiku yote ya mwaka mzima.

Abu Qataada akapokea Hadithi kutoka kwa Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) kuwa amesema:

"Saumu ya siku ya Arafa hufidia madhambi ya miaka miwili: mwaka ulopita na mwaka ujao. Na saumu ya siku ya 'Ashura hufidia dhambi za mwaka ulopita."[10]

Na Aisha  (Radhiya Llahu anhaa) akatuahadithia kuwa Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) amesema:

"Hakuna siku ambayo Mwenyezi Mungu huwaacha watu huru na moto (huwaokoa na moto) kama siku ya Arafa. Huja karibu (ya wale waliosimama Arafa) na kisha Akanadi mbele ya malaika Wake Akisema: 'Ni kitu gani wanachotaka hawa watu.'"[11]

SIKU YA ADH-HA:
Tarehe ya kumi ya Dhul-Hijja ndiyo 'Idd ul-Adh-ha au siku ya An-Nahr (kuchinja). Siku hii inaashiria kukamilika kwa kanuni za ibada za mahujaji na kuadhimisha Ukarimu wa Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Ta’ala) juu ya Mtume wake Ibrahim (a.s.) alipomruzuku kondoo dume amchinje kama kikombozi cha mwanae Ismail (a.s.).

Siku hii ni mojawapo ya siku kuu mbili kubwa ambazo Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Ta’ala) amewaridhia waislamu.

Anas  (Radhiya Llahu anhu) akatuhadithia yakwamba siku moja Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) aliwaona watu wa Ansar wakisherehekea siku fulani.

Akaiulizia siku hiyo na akaelezewa, "Hii ni mojawapo ya siku mbili ambazo tulizokuwa tukisherehekea wakati wa jaahiliyya na mpaka leo twaendelea nayo." Nae akawajibu:

"Kwa hakika Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Ta’ala) amewabadilishia nyinyi siku mbili bora: Siku ya Al-fitr na siku ya Al-adh-ha."[12]

Vile vile, Swahaba 'Uqbah Bin 'Amir  (Radhiya Llahu anhu) akaipokea Hadith kutoka kwa Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) kuwa amesema:

"Siku ya Al-Fitr, siku ya an-Nahr na siku ya Tashriq ni siku zetu za 'Idd sisi waislamu. Hizo ni siku za kula na kunywa."[13][14]

Siku ya an-Nahr ni siku tukufu baada ya Arafa. 'Abdullah Bin Qart  (Radhiya Llahu anhu) amepokea kutoka kwa Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) kwamba amesema:
"Siku zilotukufu mbele ya Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Ta’ala) ni siku ya an-Nahr, kisha siku ya al-Qarr(makao)"[15][16]

Hiyo ndiyo siku kuu ya Hajj iliyotajwa kwenye Qur'an[17] Ikathibitishwa siku hiyo na Hadith ilopokewa na 'Ali  (Radhiya Llahu anhu):

"Siku kuu ya Hajj ni ile siku ya kuchinja."[18]

SIKU TATU ZA TASHRIQ:

Siku za tashriq (kukausha nyama)[19] ni zile siku tatu zinazofuata 'Idd-ul-Adh-ha. Katika siku hizo mahujaji hukamilisha nguzo zao za hijja. Waislamu wakaendelea na sherehe zao za 'Idd na wamekatazwa kufunga.

Kwenye riwaya nyengine ya Hadith ya 'Uqbah Bin 'Amir  (Radhiya Llahu anhu) iliyopita, ameeleza kuwa Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) amesema:

"Siku ya Arafa, siku ya Kuchinja na siku ya Tashriq ndiyo 'Idd yetu (waislamu). Nazo ni siku za kula na kunywa."[20]

Akasema 'Amr Bin al-'As  (Radhiya Llahu anhu) kuhusu siku za Tashriq: "Hizi ni siku ambazo Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) alizotuamrisha tule na akatukataza kufunga."[21]

Nubayshah al-Huthali  (Radhiya Llahu anhu) akapokea kutoka kwa Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) kuwa amesema:

"Siku za Tashriq ni siku za kula, kunywa na kumtaja Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Ta’ala)."[22]

Na Abu Huraira  (Radhiya Llahu anhu) akapokea kutoka kwa Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) kuwa amesema:

"Siku za Mina[23] ni siku za kula na kunywa."[24]

[1] Imepokewa na Ibn Hibbaan na al-Bazzaar; Ikasahihishwa na al-Albaani (Sahih ul-Jaami' #1133).
[2] al-Bukhari, at-Tirmidhi na wengineo.
[3] At-Tirmidhi; imesahihishwa na al-Albaani (Irwa' ul-Ghalil #953).
[4] Al-Bukhari.
[5] Imepokewa na Ahmad na at-Tabaraani; Sahih. Vile-vile imepokewa na wapokezi wa kutegemewa kutoka kwa Ibn 'Abbas  (Radhiya Llahu anhu) kama ilivyo katika Majma' uz-Zawai'd ya al-Haythami.
[6] Al-Hajj 22:28.
[7] Tafsiri ya Ibn Kathir.
[8] Imepokewa na Abu Dawud; Imesahihishwa na al-Albaani (Sahih Abu Dawud #2129).
[9] Muslim.
[10] Muslim na wengineo.
[11] Muslim.
[12] Imepokewa na Ahmad, an-Nasa'i na wengineo. Imesahihishwa na al-Albaani (Sahih Abu Dawud #1004).
[13] Hapana shaka hapo imekusudiwa vinywaji vya halali. Hata katika sherehe na siku kuu zao, waislamu hawaruhusiwi hata kuonja vinywaji vya haramu wala kufanya vitendo vinavyofanana na makafiri.
[14] Imepokewa na Ahmad, an-Nasa'i na wengineo; Imesahihishwa na al-Albaani (Sahih ul-Jami' #8192).
[15] Hii ni siku ya kumi na moja ya Dhul-Hijja, ambayo mahujaji huweko kwenye "makao" hapo Mina.
[16] Imepokewa na Ahmad, Abu Dawud na wengineo; Imesahihishwa na al-Albaani (Irwa' ul-Ghalil #2018).
[17] At-Tawba 9:3.
[18] Imepokewa na at-Tirmidhi; Imesahihishwa na al-Albaani (Irwa' ul Ghalil #1101).
[19] Maana ya Tashriq ni kukausha nyama, na siku hizo tatu zikaitwa hivyo kwa sababu, hapo watu kawaida hukata nyama za vichinjo vyao na kuzikausha kwenye jua.
[20] Imepokewa na Abu Dawud. Imesahihishwa na al-Albaani (Sahih Abu Dawud #2114).
[21] Abu Dawud; Imesahihishwa na al-Albaani (Sahih Abu Dawud # 2113).
[22] Muslim na Ahmad.
[23] Zimeitwa siku hizo kwa jina la Mina kwa sababu mahujaji hukaa hapo Mina.
[24] Imepokewa na at-Tahaawi na Ahmad; Imesahihishwa na al-Albaani (As-Sahiha #1282).

 IMEFASIRIWA NA:ABUFARIDA MUHAMMAD A. BASAWAD

No comments:

Post a Comment