Sunday, June 1, 2014

UTARATIBU SAHIHI WA KUFANYA RUQYAH KWA NJIA YA QURAN NA SUNNA



UTARATIBU SAHIHI WA KUFANYA RUQYAH - TIBA KWA NJIA YA QUR-AAN NA SUNNAH

Kutafuta tiba kwa njia ya Ruqyah na Qur-aan ni suala zito linalohitaji ufafanuzi na mjadala wa wazi kutokana na ukweli kuwa yamezuka mambo mengi ya uzushi na ushirikina ambayo hayana ushahidi wa Qur-aan, Sunna wala vielelezo kutoka kwa Maswahaba wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam).
Mambo haya yamekuwa yakifanywa kwa jina la Ruqyah au ponyo la Qur-aan. Ingawaje Ruqyah hutafsiriwa kama “uganga,” au “uganga wa kitabu” lakini ainisho hili, kwa kiasi fulani, ni potofu na linabeba maana mbaya sana katika lugha ya Kiswahili.

Wakati neno uganga huhusishwa na mambo ya kishirikina (uchawi na mauzauza), Ruqyah maana yake ni usomaji wa Qur-aan na uombaji wa dua kwa Allah (Subhaanahu wa Ta’ala) ili kupata msaada wake katika tiba ya ugonjwa na matatizo mengine na haihusiani kabisa na mambo ya uganga.
Ibn Hajr Al-Asqalanii kasema kuwa ainisho la Ruqyah linajumuisha ta’awwuth ambayo maana yake ni kuomba ulinzi. Kwa maneno yake kasema hivi:
“Hakuna khitilafu yoyote miongoni mwa wanazuoni kuhusiana na suala la kumuelekea MwenyeziMungu kumuomba msaada na ulinzi kwa hali yoyote itokeayo au inayotarajiwa kutokea. (Fath Al-Barii)
Suala la Ruqyah huendana na Aqida na Akhlaq za Kiislamu na ni sehemu ya utekelezaji wa agizo la MwenyeziMungu kuwa Waislamu wamtegemee MwenyeziMungu tu katika mambo au matatizo yao yote.
Jambo la kusikitisha ni kwamba umezuka mtindo wa kufanya ‘tiba’ kwa Ruqyah kinyume na maana na lengo la Ruqyah. Hali hii imepelekea watu kupata “ajira isiyo rasmi” ya kufanya’uganga’ kwa maslahi binafsi huku wakijihami kwa kisingizio cha Ruqyah.

Sio siri hata kidogo kuwa kuna watu wamejipa uwezo wa “kuwatibu’ au’kuwaombea dua’ wengine ilihali hao wanaotibiwa au kuombewa dua hawana hata dalili moja ya imani juu ya MwenyeziMungu. Matokeo yake, “wateja” humtegemea zaidi “mganga” kuliko MwenyeziMungu
‘Tiba’ kwa kisingizio cha Ruqyah sio tu imekuwa “kitega uchumi” bali pia kumekuwepo na ukiukaji wa maadili kwa baadhi ya wale wanaosemekana kuwa ni “wataalamu wa tiba ya Ruqyah”.

Kama ilivyokwishaelezwa kuwa Ruqyah sahihi huendana na Aqida na Akhlaq au maadili ya Kiislamu, lakini baadhi ya waganga magirini wamekuwa wakilitumia jambo hili kama mtego wa kunasia “akina dada na akina mama”.
Wateja hawa wa kike sio tu hutoa “ada” au “malipo” ya pesa kwa ajili ya ‘kufanyiwa Ruqyah’ bali wakati mwingine huwa wahanga wa maumbile yao.
Hushikwashikwa miili yao, hupapaswa maungo ya siri, huchojolewa nguo, hukogeshwa maji ya ‘dawa’ uchi’ au humwagiwa maji juu ya kanga ili igandamane na mwili mganga apate kukidhi matamanio yake, na wengine hufanyiwa kabisa uchafu wa zinaa!
Utafiti unaonesha kuwa wateja wengi wa “Matabibu hawa wa Ruqyah” huwa ni akina dada na akina mama, baadhi yao wakiwa ni wake za watu. Tamaa ya ngono kwa “tabibu wa Ruqyah”, mara nyingine huchochewa na “shida za akinadada” wanaotaka “kuombewa ili wapate waume!”
Kwa kweli kuna mambo ya ajabu sana ambayo japo yanafanyika chini ya mwamvuli wa Ruqyah lakini yanakiuka kabisa msingi, maana na lengo la Ruqyah!
Yawezekana makala hii ikawaudhi wahusika lakini lazima waukubali ukweli kuwa hii wanayofanya siyo Ruqyah iliyofundishwa na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam). Hayo wanayoyanya wao ni kwa ajili ya matamanio ya nafsi zao na maslahi yao tu.
Kwa ajili hiyo, lazima wakubali kuwa, shughuli wanayofanya inawajengea ushirikiano wa karibu na shetani badala ya kuwakurubisha kwa MwenyeziMungu.
Lengo la Ruqyah sahihi ni kuwakurubisha waja kwa Mola wao. Na lengo la makala hii ni kuonesha tofauti kati ya Ruqyah inayoruhusiwa katika Uislamu na ‘Ruqyah feki’ inayofanywa na waganga magirini wanaohaha kuganga njaa zao.
Kwa minajili hiyo, makala hii, kwanza kabisa, inawahadharisha watu juu ya mambo ya uzushi yanayofanyika kwa jina la Ruqyah. Njia sahihi ya kuepukana na ghiliba zozote zile za ‘waganga’ ni kutafuta elimu sahihi ya Uislamu, kumuamini Allah na kumtegemea Yeye pekee
Moyo Wa Mwanaadamu
Moyo wa mwanadamu, kwa kawaida, hujaa mambo fulani na huwa hauruhusu kitu chochote kuingia mpaka kwanza kingine kilichomo ndani yake kitoke nje.
Ibnul-Qayyim kasema “ili mahali paweze kuruhusu kitu fulani kukaa basi ni shurti kuondosha kitu kingine kilichopo hapo. Hii ndiyo kanuni ya kimaada na ndiyo kanuni ya imani na nafsi pia. (Taz. Al-Fawa’id)”
Mja muumini humjuwa ipasavyo Muumba wake, anajuwa kwa nini yeye ameumbwa na anajuwa mwisho wa safari yake
Pia mja anayemuamini Allah anajuwa kuwa wanadamu na majini hawana uwezo wa kuwadhuru wala kuwanufaisha viumbe. Na wala hawana mamlaka juu ya maisha ya uhai wao, mauti yao au kufufuka kwao bila ya idhini ya MwenyeziMungu.
Kwa hali hiyo, Muumini mwenye tauhiid huishi maisha ya utulivu kwani anajuwa fika kuwa hakuna mwenye uwezo juu yake isipokuwa MwenyeziMungu kama Anavyosema katika Qur-aan:

“Hakika waja wangu wewe hutakuwa na mamlaka juu yao isipokuwa wale wenye kukufuata katika hao wapotevu”. (15:42).
“Na kama MwenyeziMungu akikugusisha madhara basi hakuna yeyote awezaye kuyaondoa ila Yeye; na kama akikugusisha kheri, Yeye ndiye Muweza juu ya kila kitu”. (6:17).

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) alimwambia Abdullah ibn Abbaas, “Ewe Kijana! Jichunge na MwenyeziMungu, Naye Atakuchunga. Chunga Haki Zake, Naye daima atakuwa pamoja nawe, ukilazimika kuomba basi muombe Yeye pekee; na ukihitaji msaada, Muombe msaada Allah pekee. Na kumbuka kuwa kama watu wote wakitaka kukunufaisha, hawataweza kukupa chochote isipokuwa kile tu alichokukadiria MwenyeziMungu na ikiwa wote wanataka kukudhuru basi hawataweza kukudhuru isipokuwa kile tu alichokupangia MwenyeziMungu. Kalamu zishasimamishwa na kuwekwa kando na wino wa (kuandikia) Kitabu (kadari) ushakauka”. (Ahmad na At-Tirmidhiy).
Kinyume cha hivyo, imani dhaifu katika kumpwekesha Allah, ulegevu wa imani katika kumtegemea MwenyeziMungu na ukosefu wa elimu sahihi huufanya moyo uwe kichaka cha kufichia mambo ya kishetani, mambo ya udanganyifu na mambo ya kipuuzi.

Kuhusiana na hali hii ya hatari ya moyo, Ibnul Qayyim kaandika hivi: Mashetani, mara nyingi, huwachezea wale wenye uelekeo hafifu wa dini yao, na wale ambao nyoyo na ndimi zao zimekimbiwa na imani-hawa ni watu ambao hawamkumbuki MwenyeziMungu na hawana njia ya kuimarisha imani yao. Pale mashetani wanapokutana na mtu dhaifu, asiye na silaha, na mtupu, huweza kumuandama na kumshinda (Attib An-Nabawii).

Aidha Ibn Qayyim kasema: “Uchawi wa wachawi huwadhuru watu wenye nyoyo dhaifu na watu waliogandamana na hadaa na tamaa za dunia...na wasioshughulika kusoma Qur-aan na nyiradi alizofundisha Mtume kila siku).
Wanazuoni wamesema: ‘wanaorogeka (wanaopatwa na uchawi) ni wale wanaoruhusu wenyewe kurogwa, kwani mara zote unakuta nyoyo zao zimekamatana na kushughulishwa na jambo hilo; na hivyo, nyoyo zao hizo hutetereshwa na jambo hili kulingana na kiwango ambacho zimeshikamana nalo, Allah ndiye Ajuwaye zaidi.” (Al-Fawa’id).
Ufumbuzi wa tatizo hilo ni kuujaza moyo na kukijaza kichwa mambo ya kumuabudia, kumfikiria na kumkumbuka Allah. Maisha yote ya mtu yatawaliwe na mambo haya. Kwa njiya hii imani hugeuka kuwa silaha kubwa ya kupambana na wale wanaotafuta uchawi na kiini macho ili kupata maslahi fulani.
Uhalali Wa Kutafuta Tiba
Hapana shaka kuwa Uislamu ulikuja na nguvu ya kutibu moyo na kiwiliwili. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) aliitafuta tiba na pia aliwahimiza Maswahaba zake kufanya hivyo. Jabir kasimulia kuwa Mtume(Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:
kuna dawa kwa kila ugonjwa na dawa hiyo inapotumika kutibu ugonjwa, ugonjwa hutibika kwa idhini ya MwenyeziMungu Sunhaanahu wataala.” (Muslim).
Akisherehesha Hadith hii; Ibn Qayyim kaandika hivi: “Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) aliamrisha tiba kwa kutumia dawa inayowiyana na ugonjwa. Kila ugonjwa una dawa. Kupona ugonjwa shurti kuendane na dawa inayowiana na ugonjwa huo.

Hivyo dawa ikizidi mno kiasi, itasababisha ugonjwa mwingine. Kinyume chake, dawa ikitumika chini ya kiasi kinachohitajika itashindwa kupambana na ugonjwa na kwa hali hiyo itaonekana kutofaa.

Hivyo basi, daktari asipogundua tiba halisi au iwapo tiba haihusiani na ugonjwa, suala la kupona huwa ni muhali. Zaidi ya hivyo ikiwa tiba inatolewa katika muda usiofaa, dawa haitasaidia kitu, au kama mwili haukubali dawa au mwili hauna nguvu kabisa ya kumudu dawa hiyo, au kuna kitu fulani kinachozuwia isifanye kazi, dawa haitasaidia. Lakini kinyume cha hivyo kama dawa inawiana na ugonjwa, tiba itafanya kazi kwa idhini ya Allah.” (Attib An-Nabawii).

Jambo la ajabu ni kwamba, kuna baadhi ya watu wanaopuuzia njia za kisasa za tiba na badala yake husingizia kukumbwa na majini, kurogwa au kutazamwa kwa jicho baya. Ujinga huu huweza hata kusababisha kifo kwa mgonjwa wakati watu wakipoteza muda kumtowa majini mgonjwa.
Hivyo, ni muhimu kwanza kugundua aina ya ugonjwa na kisha kujaribu kutafuta dawa sahihi inayoweza kutibu ugonjwa huo. Kwani kama mtu hana uhakika na aina ya ugonjwa, anawezaje kutoa tiba ya kufaa?
Baadhi ya watu wanaweza kuuliza je kutafuta tiba kunapingana na imani ya kumtegemea MwenyeziMungu (tawakkul). Kwa hakika Hadith chungutele za Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) ikiwemomoja iliyokwishatajwa hapo juu zinaunga mkono mtazamo huu kuwa kutafuta tiba ya dawa ni jambo linalokubalika kabisa, na limehimizwa katika Uislamu. Upo muafaka wa pamoja wa wanachuoni wa Kiislamu juu ya jambo hili.
Muungozo Wa Mtume Kuhusiana Na Kinga Na Tiba
Muongozo bora kabisa wa maisha yetu unapatikana kwa kuyasoma maisha ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) ambaye alituonesha namna ya kufanya mambo yetu katika mazingira yoyote yale.
MwenyeziMungu anamzungumzia Mtume hivi: “yanamuhuzunisha yanayokutaabisheni, anakuhangaikieni. (Na) kwa walioamini ni mpole na mwenye huruma.” (9:128).
Kwa hakika Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) katuongoza katika mema yote na kutuonya dhidi maovu yote. Muongozo wake unajumuisha na kinga dhidi ya aina zote za maradhi pamoja na njia za kupambana nayo pale yanapotokea.
Hapa tutaziangalia njia za kujikinga na maradhi alizofundisha Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) pamoja na tiba mbalimbali za kutibu madhara ya kijicho na uchawi.
Kinga dhidi uovu kwa ujumla hupatikana kwa nguvu ya tauhiid (imani ya kumpwekesha MwenyeziMungu), kumsabihi kwa Majina na Sifa Zake tukufu, kufanya Ibada Zake kwa ikhilasi, kutii amri Zake, kumtegemea yeye tu,kumpenda na kumkumbuka mara kwa mara.
Hii ndiyo njiya ya kutafuta ulinzi wa jumla wa MwenyeziMungu. Aidha kuna maelezo kuhusu namna ya kutafuta ulinzi wake kwa njia mahususi, kama vile kuomba dua kabla ya kufanya tendo la ndoa ili kumkinga mtoto atakayezaliwa, kusoma Surati Baqara nyumbani, na kusoma Ayatu Kursiyu pamoja na sura tatu za mwisho za Qur-aan, Ikhilas (QulhuAllahuAhadu), Falaq (Qulaudhubirabilifalaq) na Surat n-Nasi (Qulaudhubirabinnas). Sura hizi hujulikana kama Al-Muawwithat
Hata hivyo, ni muhimu kubainisha kuwa kuna tofauti kubwa kati ya maneno yanayotamkwa kwa ikhilasi kutoka ndani kabisa ya moyo na maneno yanayotokea mdomoni tu.
Kinachohitajika hapa ni dhikri inayohusisha moyo na ulimi. Ibnul-Qayyim kailezea hali hii kama ni “aina ya mapambano”, akisema: “Mpiganaji huweza kumshinda aduwi yake iwapo silaha anayotumia ni madhubuti na ikiwa yeye mwenyewe ni mkakamavu (shupavu) katika kutumia silaha hiyo.
Endapo moja kati ya masharti haya mawili halitimizwi, basi silaha haitakuwa na maana. Na mambo yatakuwa mabaya zaidi kama masharti yote mawili hayatimizwi” (Attib An-Nabawii).
Utaratibu Sahihi Wa Kufanya Ruqyah - 2 Tiba Ya Jicho la Husda Na Uchawi


Tiba Ya Jicho La Husda
Uwezo wa kuwadhuru wengine kwa kuwatazama au kuonea kijicho ambao hujulikana kama “kijicho” kweli upo. Ibn Abbas kasimulia kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam)kasema: “madhara ya Kijicho (al-ayn) kweli yapo. Kwani kama kungelikuwa na jambo la kuitangulia kadari basi lingekuwa ni dhara la kijicho” (Muslim).

Ili kuzuwia madhara ya kijicho, mtu akiona mtu au jambo la kumpendeza machoni na akachelea atashidwa kuizuwia nafsi kulihusudu au kulionea kijicho, basi aseme “maa shaa-Allaah (akitakacho MwenyeziMungu kiwe ndicho huwa!) na kisha amuombe MwenyeziMungu amjaalie kheri mtu huyo aliyemtazama au akijaalie kheri kitu alichokitazama.
Tiba ya kijicho yaweza kufanyika bila kujali kama mtu aliyemtazama mwenziwe kwa kijicho kajulikana au hakujulikana. Ikiwa mtu aliyemuonea mwenziwe kijicho kajulikana basi ushahidi wa jinsi ya kufanya tiba unapatikana katika Hadith ifuatayo:
Abu Umamah ibn Sahl ibn Hunayf kasimulia hivi: “Baba yangu, Sahl ibn Hunayf, alifanya josho (ghusl) pale al-Kharrar. Akavua juba alilokuwa amelivaa huku Amir ibn Rabia akimtazama, na Sahl alikuwa na ngozi nyororo nyeupe.
Amir akasema: “Sijapata kuona (ngozi)
mfano wa hii ambayo nimeiona leo, haifanani hata na ngozi ya mwanamwali.” Papo hapo Sahl akawa mgonjwa na hali yake ikawa mbaya sana.
Mtu mmoja akaenda kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam)na kumwambia kuwa Sahl ni mgonjwa na asingeweza kujimudu kuja pale kwa Mtume. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam)akaja pale alipokuwa Sahl. Sahl akamsimulia kilichotokea wakati alipokuwa na Amir.
Mtume wa Allaah akasema, “kwa nini mmoja wenu anamuua nduguye? Kwa nini (wewe Amir) hukusema ‘Tabarak-Allaah’ (MwenyeziMungu Akujaalie kheri)? Kijicho kipo kweli.”
Kisha Mtume akamwambia Amir, ‘tia udhu kwa ajili ya mwenzio’. Amir akatia udhu. Baada ya Amir kutia udhu, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam)akanyunyiza maji ya udhu ya Amir kichwani na mwilini mwa Sahl. Halafu Sahl akaondoka pamoja na Mtume na hakuwa na ugonjwa tena”. (Ahmad).
Endapo mtu aliyemuonea kijicho mwenziwe hajulikani, basi tiba inaweza kufanywa kwa Ruqyahh, duwa zinazoswihi za Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) zikiambatana na unyenyekevu uliojaa ikhilasi kwa Allaah.
MwenyeziMungu daima huitikia maombi ya wenye shida.kama isemavyo Qur-aan, “Au yule anayemjibu anayedhikika amwombapo na kuondoa dhiki (yake)..?” (27:62).

Ibn Qayyim kasema: “miongoni mwa njia za kuomba ulinzi wa MwenyeziMungu na zile zinazojumuisha Ruqyah ni: usomaji wa mara kwa mara wa Surat al-Falaq, surati An-Nasi, surati Al-Fatiha na Ayatul Kursiyu.
Mtu pia asome dua za Mtume kama hizi:
*Kwa maneno haya thabiti ya Allaah, najikinga Kwake na shari aliyoiumba.

*Kwa maneno thabiti ya Allaah, naomba Ulinzi Kwake dhidi ya kila shetani, kila mnyama hatari na kila jicho baya.
*Kwa maneno thabiti ya Allaah ambayo si Muumini wala si muovu anayeweza kuyakhalifu, najikinga Kwake na shari ya alivyoviumba, akavipa uhai na akavizalisha.
*Allaah Anatutosheleza na ndiye Mlinzi bora kabisa. Allaah Ananitosha. Hakuna mungu isipokuwa Yeye. Kwake Yeye nategemeza imani yangu, Naye ndiye Mola wa Arshi kuu.

Watu ambao wamejitahidi kuomba dua hizi kwa hakika wamepata manufaa makubwa na kukidhiwa haja shida zao kubwa kubwa kwani duwa hizi zinazuwia na kuondosha madhara ya kijicho kutegemeana na imani ya mtu anayezisoma.
Kadri imani yake inavyokuwa na nguvu ndivyo utegemezi wake kwa MwenyeziMungu unavyokuwa mkubwa. Kwa hakika hii ndizo silaha (za kupambana na uovu)” (Attib An-Nabawii).
Tiba Ya Uchawi
Huwa inasemwa kuwa Kinga ni bora kuliko Tiba. Kwa hiyo basi, mtu ajikinge na madhara ya uchawi kabla haujatokea. Pamoja na mambo mengine, kinga hii hupatikana kwa kumtii na kumuabudia Allaah pekee, kuamini Qudra na Qadari Yake, kuomba ulinzi Wake kwa kumdhukuru mara kwa mara na kusoma dua za Mtume katika nyakati zinazofaa.
Kula tende Ajwah ni njia nyingine ya kuzuia madhara ya uchawi kama ilivyobainishwa katika Hadith iliyosimuliwa na Sa’ad ambapo Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam)kasema, “mtu akila tende Ajwah kila asubuhi, hatadhurika kwa sumu au uchawi kwa siku hiyo.” (Al-Bukhaariy na Muslim).
Ni muhimu kutambua kuwa wale wanaostahili kunufaika na Hadith hii ni wale tu wanaoamini kikwelikweli haya aliyoyasema mtume na wanaoamini kwa dhati kabisa kuwa kila alichosema ni ukweli, ama wathibishe ukweli wake au la. Na kuhusu tiba ya uchawi, mtu aliyerogwa aoneshe subira na airidhie kudra ya Allaah. Pia ni jambo la msingi kwake kujirudi kwa dhambi yoyote ambayo ameitenda na afanye toba ya kweli kwa dhambi hiyo

Anapotafuta tiba, aepuke kabisa tiba za “kitekero” au”kisangoma” zinazotolewa na waganga magirini. Kama ikibidi, basi anaweza kushirikiana na watu wachaMungu kumuomba msaada Allaah kwa utaratibu anaouridhia Allaah.
Utaratibu Sahihi Wa Kufanya Ruqyah - 3 - Tiba Enzi Za Ujahili
 KUNA ina Mbili Za Ruqyah
Tiba Enzi Za Ujahili
Yafahamika kuwa watu katika zama za ujahiliya walikuwa wakitamka maneno mengi ya uganga katika mazingira mbalimbali.
Jabir kasimulia kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) aliharamisha uganga wa kienyeji. Ndipo familia ya Amr ibn Hazm ikaja kwa Mtume wa Allaah na kusema: “Sisi tunayajua maneno ambayo tunayatumia kuponeshea maumivu ya kung’atwa na n’nge, lakini wewe umeyakataza.” Wakatamka maneno hayo ya tiba mbele yake, naye akasema, “sioni ubaya wowote wa jambo hili. Yeyote kati yenu anayeweza kumsaidia nduguye afanye hivyo.” (Muslim)
Auf ibn Malik Al-shja’ii naye kasimulia hivi: “Tulifanya tiba katika zama za ujahili na tukasema, “Ewe Mtume wa Allaah! Nini rai yako kuhusu jambo hili?” Akasema, ‘hebu nifahamisheni tiba yenu’ Na kisha akasema, ‘hapana ubaya katika tiba ambayo haihusishi shirki (ushirikina).” (Muslim).
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) hakuzikataa Aina za tiba zilizokwishakuwepo katika zama za ujahili wala hakuwaamuru Masahaba wake kuacha kuzitumia. Badala yake upo ushahidi wa kutosha wa Hadith unaoonesha kuwa aliwaruhusu Waislamu kuchambua aina mbalimbali za tiba zilizokuwepo na kisha kuzikubali zile zisizohusisha mambo ya ushirikina au mambo yaliyoharamishwa ambayo yanaweza kusababisha jambo jingine la haramu.


Ruqyahh Na Du’aa
Ruqyah ni sawa tu na dua. Wakati ambapo inapendelewa kutumia dua alizotufundisha Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam), Wanazuoni wa Kiislamu wanakubaliana kuwa pia inajuzu kutumia dua ambazo hakutufundisha.
Sharti la kufanya hivyo ni kuwa dua hizo zisiwe na maneno ya haramu na wala zenyewe zisiwe dua za haramu au zinazokusudia jambo la haramu kama ilivyobainishwa na Hadith za Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam). Anas kasimulia, “Mtu mmoja alikuja huku akihema na akaingia katika safu ya waumini na kusema, ‘Sifa njema ni za Allaah, Ahimidiwe na atukuzwe kwa wingi.’ Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) alipomaliza Swala akauliza, ‘ni nani miongoni mwenu aliyetamka maneno haya?’ Watu wakanyamaza kimya. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akauliza tena, ‘nani kati yenu aliyetamka maneno haya?’ Mtu huyo akasema, ‘hakuna ubaya’. Halafu akasema, ‘nilikuja huku nikiwa na tatizo la kupumua, kwa hiyo nikatamka maneno hayo.’ Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akajibu, ‘niliona Malaika kumi na wawili wakiangaliana kuwa nani kati yao ayachukue maneno hayo kuyapeleka kwa MwenyeziMungu.’ (Muslim)
Ule ukweli kuwa jamaa aliyetamka maneno hayo alinyamaza pale Mtume alipouliza swali mara ya kwanza, unaonesha kuwa alidhani kafanya kosa katika dua yake na akachelea kuwa huenda Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) asingeyaridhia yale aliyoyasema. Kwa hakika maneno haya ya mtu huyo yakaja kuwa mfano wa dua zinazokubalika ambazo zinampendeza Allaah Taala.

Ingawaje inajuzu kuomba dua za aina hii ambazo hazikutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam), lakini kama ilivyoelezwa, zisiwe na maneno ya haramu, zisisababishe jambo la haramu, kama vile kuacha kabisa dua ambazo zimetoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam). Ni bora zaidi kufuatisha dua alizotufundisha Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam)]. Itazame Hadith hii ambayo inalibainisha jambo hili barabara.

Abu Hurayrah kasimulia kuwa Bedui mmoja aliingia msikitini wakati Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) alipokuwa amekaa. Kisha Bedui huyo akaswali rakaa mbili za Sala na kusema, ‘Ewe MwenyeziMungu, Mrehemu Muhammad na Unirehemu mimi na Usimrehemu mwingine yeyote pamoja nasi’. Mtume (SalAllaahu alaihi wasalam ) akasema, “umelifinya jambo hilo (yaani umezifinya Rehema za Allaah) ambazo ni pana (nyingi) zaidi. (Ahmad na Abu Daawuud).
Aina Mbili Za Ruqyah
1. Ruqyah halali: Hii ni aina ya Ruqyah aliyoitumia Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam). Ruqyah hii inajumuisha yafuatayo; kuomba dua zinazojuzu na kupuliza mikono na kuiparazia (kuipitisha) katika sehemu ya mwili iliyodhurika kama ilivyobainishwa na aya za Qur-aan na Hadith Sahihi lakini pasina kutia nyongeza yoyote na bila kufanya jambo hilo kiajabu-ajabu (kiuganga-uganga).

2. Ruqyah haramu: Hii ni Ruqyah inayojumuisha maneno ya kishirikina, mauzauza (mayakayaka), au jambo lolote lilliloharamishwa katika Uislamu.
Ruqyah Halali
Ibn Hajar kasema, “Wanachuoni wa Kiislamu wanaafikiana kuwa Ruqyah ni halali maadam itimize masharti matatu:
Mosi, yatumike maneno ya MwenyeziMungu (yaani Qur-aan) ikiwa ni pamoja na Majina au Sifa Zake
Pili, Ruqyah ifanywe kwa Kiarabu kinachoeleweka au hata kwa maneno ya lugha nyingine yanayoeleweka.
Tatu, wale wanaofanya Ruqyah lazima wawe waumini wenye yakini kuwa si ponyo linayoponya bali Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) ndiye anayesababisha ponyo kuponya. (Taz. Fath Al-Barii).

Na kuhusu dua au maombi, nayo ni halali maadam tu yasikiuke au kupingana na mafundisho ya Uislamu wala yasipelekee katika shirki. Kama ni kufanya Ruqyah kwa dua ambazo hakufundisha Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam), basi pasiwe na maneno ya ajabu-ajabu, wala isifanyike kiuganga-uganga kama wafanyavyo wanamazingaombwe au waganga wa kienyeji.
Ruqyah ya maneno yasiyoeleweka, (maneno ya kupandisha mzuka) haifai kwani inaleta mambo ya bidaa na inaweza kuhalalisha kazi ya waganga matapeli wa kienyeji. Kwa sababu hizi, kuelewa maana ya Ruqyah ni sharti la lazima katika kuitumia. Ikiwa ni hatua ya tahadhari, Ruqyah ya maneno yasiyoeleweka imeharamishwa.

Ibn Qudaamah kasema, “Imam Ahmad alifahamishwa na mtu mmoja kuhusu mtu mmoja aliyedai kupoza uchawi kwa kuweka maji kwenye chungu na kusema maneno yasiyoeleweka pamoja na mambo mengine. Ndipo Imam Ahmad, kwa kutoliridhia jambo hili, akamshika mkono mtu huyo na kusema, “mimi silijui jambo hili (la kipuuzi)” (Al-Kafii).
Al-Bajii kasema, Imam Malik aliona kuwa kutumia kifimbo cha chuma na chumvi wakati wa kufanya Ruqyah ni jambo la kuchukiza (makruhu) na kutumia vifundo na nyuzi ni jambo la kuchukiza zaidi.” (AlMuntaqa, Sharh Al-Muwatta).

Wanazuoni wengine wamekataa matumizi ya hirizi na visu na mambo mambo mengine kama vile kuuchanja chale mwili wa mgonjwa, hayo ni mambo yaliyoigwa kwa wachawi.
Muislamu lazima awe makini mno juu ya mambo haya na mara zote arejee katika Qur-aan na Sunnah pale anapokutana na jambo geni ili aone kama jambo hilo ni halali kabla hajalifanya.

Mambo tata ambayo hayana ushahidi wa Qur-aan na Sunnah yakataliwe, la sivyo yanaweza kuwapelekea baadhi ya watu kuingia katika uchawi na uganga mbali ya kuwachanganya wale wasio na elimu ya kutosha.
Kuhusiana na uchawi MwenyeziMungu Anasema,
“Wakafuata yale waliyoyafuata mashetani katika ufalme wa Suleiman; na Suleiman hakukufuru bali mashetani ndio waliokufuru, wakiwafundisha watu uchawi ulioteremshwa kwa Malaika wawili, Haruta na Maruta katika (mji wa) Babil. Wala (Malaika hao) hawakumfundisha yoyote mpaka wamwambie: “Hakika sisi ni mtihani basi msikufuru.” Wakajifunza kwao ambayo kwa mambo hayo walimfarakanisha mtu na mkewe. Wala hawakuwa wenye kumdhuru yeyote kwa hayo ila kwa idhini ya MwenyeziMungu. Na wanajifunza ambayo yatawadhuru wala hayatawafaa. Na kwa yakini wanajuwa kwamba aliyekhiyari haya hatakuwa na sehemu yoyote Akhera. Na bila shaka ni kibaya kabisa walichouzia nafsi zao laiti wangelijua (2:102).

Kuhusiana na aya hii, Ibn Taymiyya anasema, “Wale (wanaofanya uchawi) wanajuwa fika kuwa hautakuwa na manufaa Akhera na kwamba wale wanaoufanya watakuwa miongoni mwa watakaopata hasara, lakini bado wanavutwa na maslahi yake katika dunia hii.
(Iqtidhaa’ Assirat Al-Mustaqiim).
Ar-Rabii naye kasema, ‘nilimuuliza Imam Shafii kuhusu Ruqyah naye akasema, “Hakuna ubaya kufanya Ruqyah kwa kusoma Kitabu cha MwenyeziMungu na (kwa kutumia) aina zozote za dua anazozijua mtu...’ (Irshad As-Sarii).
Kwa hiyo mtu ajiepushe na utatanishi na badala yake aende kwenye msingi wa Ruqyah, ili kujua Ruqyah ni nini hasa. Kwamba Ruqyah ni njia ya kumuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) kwa utaratibu sahihi wenye ikhilasi na Imani thabiti kwa Allaah.

CHANZO: Na Fathi Al-Jundiy)
Imefasiriwa na Ummu Ashraf. Allah amzidishie.

2 comments:

  1. Ahsante kwa elimu. Binafsi nimeelimika sana kwa andiko hili

    ReplyDelete
  2. Subhanallah ametakasika yule aliyeziumba mbingu na ardhi. Asante kwa elimu ndugu yangu nimepata ilmu juu ya andiko hili na natamani ukaweka maandiko mengine zaid yatayotujenga kiimani zaid na kufikia lengo la kuumbwa kwetu. Allah akulipe kheri

    ReplyDelete