Friday, October 17, 2014

MUUNGANO WA ASASI ZA KIJINSIA "KATIBA INAYOPENDEKEZWA IPO POA"



Muungano wa Asasi za Kiraia Juu ya Jinsia na Katiba (GFC), umesema Katiba Inayopendekezwa imezingatia mapendekezo yao kwa zaidi ya asilimia 90, hasa katika usawa wa kijinsia na haki za watoto.

Aidha, umewataka wananchi kuacha ushabiki wa kisiasa na kufuata mkumbo wa kuipinga badala yake waisome na kuichambua kila kipengele ili waielewe.

Akizungumza jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa GFC, Victoria Mandari amesema wanaamini mafanikio yaliyofikiwa katika suala la kijinsia pia limetokana na juhudi za muungano huo unaoundwa na asasi saba za kiraia zikiwemo Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania (TAWLA) na Wanawake na Sheria Afrika Mashariki (WLEA).

Amesema kwa sasa kuna kesi nyingi mahakamani za migogoro ya ardhi na mali kutokana na utamaduni uliojengeka kwamba mwanamke hawezi kumiliki mali na mirathi lakini kwa sasa haki sawa itakuwapo kwa sababu Katiba hii ikipitishwa, inatamka wazi kuhusu usawa wa kijinsia.

Kwa upande wake, Mkurugenzi TAWLA, Tike Mwambipile amesema ni vyema kila mwananchi akaisoma katiba hiyo inayopendekezwa na kuielewa badala ya kufuata mkumbo ili muda wa kupiga kura ukifika aweze kujua nini kinapendekezwa.

MAAMBUKIZI YA VVU KUTOKA KWA MAMA KWENDA KWA MTOTO YAPUNGUA TABORA



Maambukizi ya virusi vya Ukimwi (VVU), kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto yamepungua kwa asilimia 90.

Hayo yamesemwa na Meneja wa shirika la EGPAF Mkoa wa Tabora, Dk. Alphaxard Lwitakubi, mara baada ya Rais Jakaya Kikwete kukagua banda la shirika hilo katika maonyesho ya wiki ya vijana.

Lwitakubi, amesema lengo la EGPAF ni kufikia asilimia 98 ifikapo mwishoni mwa mwaka 2015.

Amesema hatua hiyo itafikiwa endapo wanaume wataambatana na wake zao kwenda kwenye vituo vya afya kama inavyotakiwa, kwani hadi sasa zimefikiwa asilimia 48 kwa mwaka 2014 kutoka asilimia 5 mwaka 2010.

Dk. Lwitakubi, amesema Shirika la EGPAF limekuwa likijihusisha na kazi za kuzuia na kutokomeza maambukizi ya virusi vya Ukimwi (VVU), kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.

Kwa upande wake, Mratibu wa Mawasiliano na Utetezi wa EGPAF, Mercy Nyanda, amesema katika huduma zao kumekuwa na mafanikio, kwani kwa sasa wajawazito wengi wanajifungulia vituoni tofauti hapo mwanzo.

MRADI MKUBWA WA KUBORESHA UMEME DAR KUKAMILIKA AGUST MWAKANI!



Mradi mkubwa wa megawati 80 kwa ajili ya kuboresha umeme katikati ya Jiji la Dar es Salaam unatarajia kukamilika Agosti mwakani.

Hayo yamesemwa na Kamishna Msaidizi wa Umeme, Innocent Luoga kwenye kikao kilichokutanisha Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, Balozi wa Finland nchini, Sinikka Antila na ujumbe wake pamoja na wataalamu kutoka Wizara ya Nishati na Madini na taasisi zake.

Amesema mradi huo wenye thamani ya Sh bilioni 56 utaunganisha vituo vya kusambaza umeme katikati ya Jiji la Dar es Salaam ili kuhakikisha kuwa umeme haukatiki kabisa.

Ametaja vituo hivyo kuwa ni pamoja na Ilala, Kariakoo, Kituo cha Reli, Sokoine na Makumbusho na kuongeza kuwa mradi huo upo katika hatua ya utekelezwaji ambapo vifaa vya mradi vimeshapatikana pamoja na wataalamu kutoka Shirika la Umeme (Tanesco) kupatiwa mafunzo ndani ya nchi na nchini Finland.

Hata hivyo amesisitiza kuwa tayari wameshaanza kuzifanyia kazi changamoto hizo ikiwa ni pamoja na kuwakutanisha wadau wote wa mradi hususan Tanesco na Wakala wa Taifa wa Barabara Nchini (Tanroads).

SHILLING BILIONI 18 KUTUMIKA CHANJO YA SURUA



Serikali inatarajia kutumia kiasi cha shilingi bilioni 18 kwa ajili ya chanjo ya surua na ribela inayotarajiwa kutolewa Oktoba 18 mwaka huu nchini kote.

Hayo yamesemwa na Ofisa mafunzo na mawasiliano wa idara ya kinga na chanjo wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Ibrahim Maduhu wakati wa mkutano wa kamati ya huduma ya afya ya msingi wa jiji la Tanga.

Amesema kuwa uwekezaji huo ni mkubwa kufanywa na serikali kwa wananchi wake kwa lengo la kuwapatia afya bora.

Dk Maduhu amesema, kuwa ni jukumu la kamati za afya nchini nzima
kuhakikisha wanaelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa chanjo hiyo.

Naye mganga mkuu wa jiji hilo, Dk Asha Mahita amesema, kuwa asilimia 15 ya watoto waliopatiwa chanjo ya surua katika jiji hilo hawajajenga kinga kamili.

JAMII ZA WAFUGAJI ZAKABILIWA NA TATIZO LA KUZAA WATOTO WENYE VICHA VIKUBWA



Jamii za wafugaji zinadaiwa kukabiliwa na kiwango kikubwa cha tatizo la kuzaa watoto wenye vichwa vikubwa na mgongo wazi unaochangiwa na wajawazito kukosa vitamini itokanayo na mboga za majani kutokana na kitoweo chao kikubwa kuwa nyama.

Katika hatua nyingine imeshauriwa miezi miwili au mitatu kabla ya kubeba ujauzito, mwanamke awe amepata vitamini aina ya follic acid ama kupitia ulaji wa mboga na matunda au kwa kupata vidonge maalumu kwa ajili ya kukabili tatizo hilo.

Hayo yameelezwa na Mwenyekiti wa Chama cha Wazazi wa Watoto wenye Matatizo ya Mgongo Wazi na Kichwa Kikubwa (ASBAHT), Abdulhakim Bayakub katika mkutano na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari jijini Dar es Salaam.

Bayakub pamoja na tatizo hilo, amezungumzia Maadhimisho ya Siku ya kupunguza uzao wa watoto wenye ulemavu huo amesema yatafanyika Oktoba 25 katika Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI) jijini Dar es Salaam.

Amesema watoto wengi wamekuwa wakicheleweshwa kufikishwa hospitalini kutokana na sababu mbalimbali miongoni mwake ikiwa ni imani za kishirikina wakiamini kwamba tatizo hilo limetokana na uchawi.