Sunday, June 15, 2014

MAMBO (10) KATIKA MAANDALIZI YA MWEZI MTUKUFU WA RAMADHANI







Ikiwa ni siku chache mno zimebakia kuelekea katika mwezi mtukufu, mwezi wa rehma, mwezi wa maghfira na mwezi wa kuachwa mbali na moto wa Jahannama, mwezi mtukufu wa RAMADHANI ni vyema muislamu aingie katika mwezi huu mtukufu akiwa amekwisha elewa na amefanya maandalizi, huku akijua nini anatakiwa akifanye ili kujivunia zawadi ya TAQWA aliyoiahidi Allah (‘Azza wa Jalla) ndani ya kitabu chake kitukufu (QURAN). Utukufu wa mwezi huu na utukufu wa ibada iliyofungamana na mwezi huu, Bwana Mtume (SAW) anasema:

عنْ أَبِي هُرَيْرَةَ رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُ قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ: "كُلُّ عَمَلِ ابْنِ آدَمَ يُضَاعَفُ الْحَسَنَةُ عَشْرُ أَمْثَالِهَا إِلَى سَبْعمِائَة ضِعْفٍ قَالَ اللَّهُ عَزَّ وَجَلَّ إِلَّا الصَّوْمَ فَإِنَّهُ لِي وَأَنَا أَجْزِي بِهِ يَدَعُ شَهْوَتَهُ وَطَعَامَهُ مِنْ أَجْلِي لِلصَّائِمِ فَرْحَتَانِ فَرْحَةٌ عِنْدَ فِطْرِهِ وَفَرْحَةٌ عِنْدَ لِقَاءِ رَبِّهِ وَلَخُلُوفُ فِيهِ أَطْيَبُ عِنْدَ اللَّهِ مِنْ رِيحِ الْمِسْكِ"

Imepokewa kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘anhu): amesema, amesema mjumbe wa Mwenyezi Mungu (Rehma na amani ziwe juu yake) ((Kila amali njema ya mwanaadamu inalipwa mara kumi na inaongezewa thawabu kutoka kumi hadi mia saba, na Allaah (‘Azza wa Jalla) Anasema: Isipokuwa Swawm, kwani hiyo ni kwa ajili Yangu na Mimi Ndiye Nitakayemlipa.  Ameacha matamanio yake na chakula chake kwa ajili Yangu. Kwa aliyefunga swawm atapata furaha mbili; furaha anapofuturu na furaha atakapoonana na Mola wake, harufu inayotoka kinywani mwa aliyefunga ni nzuri mbele ya Allaah kuliko harufu ya misk)) [Muslim na Ahmad]

MAMBO YA KUZINGATIA.
1.     NIA
Jambo la msingi kabla ya yote ni kuziandaa nafsi zetu kwa kuboresha nia zetu tukifahamu ya kwamba nia ndio msingi mkuu wa ibada ya Muislamu, na bila ya nia zetu kuwa njema hata ibada zetu pia hazitokubalika kwa Allaah (‘Azza wa Jalla)  Allah (‘Azza wa Jalla) anasema katika suuratul-Al-Bayyinah:

وَمَا أُمِرُوا إِلَّا لِيَعْبُدُوا اللَّهَ مُخْلِصِينَ لَهُ الدِّينَ حُنَفَاء وَيُقِيمُوا الصَّلَاةَ وَيُؤْتُوا الزَّكَاةَ وَذَلِكَ دِينُ الْقَيِّمَة
Na hawakuamrishwa (chochote kile) isipokuwa wamwabudu Allaah mukhliswiyn (wenye kumtakasia) Dini, hunafaa[1] na wasimamishe Swalaah na watoe Zakaah; na hiyo ndiyo Dini iliyosimama imara.  [Al-Bayyinah:5]
 Aidha, Bwana Mtume Muhammad (SAW) amesema:  
  
 عن أَمِيرِ المُؤمِنِينَ أَبي حَفْصٍ عُمَرَ بنِ الخطَّابِ رَضِيَ اللهُ عَنْهُ قَالَ : سَمِعْتُ رَسُولَ اللهِ صلى الله عليه وسلم يَقُولُ:   ((إِنَّما الأَعْمَالُ بالنِّيَّاتِ وإنَّما لكُلِّ امْرِىءٍ ما نَوَى، فَمَنْ كانَتْ هِجْرَتُهُ إلى اللهِ ورَسُولِهِ فَهِجْرَتُهُ إلى اللهِ ورَسُولِهِ، ومَنْ كانَتْ هِجْرَتُهُ لِدُنْيا يُصِيبُها أو امْرأةٍ يَنْكِحُها فَهِجْرَتُهُ إلى ما هَاجَرَ إليه)).

رَوَاهُ إِمَامَا الْمُحَدِّثِينَ أَبُو عَبْدِ اللهِ مُحَمَّدُ بنُ إِسْمَاعِيل بن إِبْرَاهِيم بن الْمُغِيرَة بن بَرْدِزبَه الْبُخَارِيُّ     وَأَبُو الْحُسَيْنِ مُسْلِمٌ بنُ الْحَجَّاج بن مُسْلِم الْقُشَيْرِيُّ النَّيْسَابُورِيُّ   رَضِيَ اللهُ عَنْهُمَا فِي “صَحِيحَيْهِمَا

Kutoka kwa Amiri wa Waumuni, Abu Hafs ‘Umar Ibn Al Khattaab (radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake) amesema : Nilimsikia Mjumbe wa Mwenyeezi  Mungu, Muhammad (SAW) amesema:
 Vitendo vinategemea (vinalipwa kwa) nia na kila mtu atapata kwa mujibu wa kile alichokusudia.  Kwa hivyo yule aliyehama  kwa ajili ya Allaah na Mtume wake, uhamaji wake ni kwa ajili ya Allaah na Mtume wake, na  yule ambae uhamaji wake ulikuwa ni kwa ajili ya manufaa ya kidunia au kwa ajili ya kumuoa mwanamke (fulani)  uhamaji wake ulikuwa kwa kile kilichomuhamisha.
Imesimuliwa na Maimam wawili mabingwa wa hadithi Abu Abdalla Muhammad  Ibn Ismail Ibn Ibrahim Ibn Mughiyra Ibn Bardizbah Al Bukhari na Abu Al Husayn Muslim Ibn Al-Hajjaj Ibn Muslim Al Qushayri An-Naysaburi, katika sahihi zao mbili 

2.     IKHLAASW.
Ni kitendo cha kumkabidhi Allah (SW) amali zako huku ukitaraji malipo kutoka kwake yeye pekeyake. Hujumuisha kufunga Swawm kwa iymaan na matarajio kwa yale aliyo yaahidi Allah (‘Azza wa Jalla)
 قال صلى الله عليه وسلم: (( من صام رمضان إيماناً و احتساباً غفر له ما تقدم من ذنبه ))  أخرجه البخاري ومسلم
Amesema Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): ((Atakayefunga Ramadhaan kwa iymaan na kutaraji malipo ataghufuriwa madhambi yake yaliyotangulia )) Al Bukhaariy na Muslim.

3.     KUKITHIRISHA KUSOMA QUR-AAN.
 Mwezi wa Ramadhaan ni mwezi wa Qur-an, ni mwezi ambao   ndani yake ndi hasa  kimeteremshwa kitabu huki kitukufu (Qur-aan), Allaah (‘Azza wa Jalla) anasema katika Suuratul-Baqara:
شَهْرُرَمَضَانَ الَّذِيَ أُنزِلَ فِيهِ الْقُرْآنُ هُدًى لِّلنَّاسِ وَبَيِّنَاتٍ مِّنَ الْهُدَى وَالْفُرْقَان
 Mwezi wa Ramadhaan ambao imeteremshwa humo Qur-aan ili iwe Hidaaya kwa watu na hoja bayana za Hidaaya na Al-Furqaan (Upambanuzi). [Al-Baqarah: 185]

Ni vyema muislamu kuzidisha jitihada zake katika kukisoma  kitabu hiki kitukufu (Qur-aan) angalau kila muislamu aweze kukihitimisha japo mara moja katika mwezi huu. Kwani ilikuwa kawaida ya Jibriyl (‘alayhis-salaam) akimfikia Mtume (SAW) kwa ajili ya kumsikiliza na kumfundisha Qur-aan katika mwezi wa Ramadhaan.
Aidha ndiyo iliyokua desturi ya maswahaba waongofu kushindana katika kukisoma kitabu cha mwenyezi Mungu (‘Azza wa Jalla) 'Uthmaan bin 'Affaan (Radhiya Allaahu ‘anhu) alikuwa akihitimisha Qur-aan kila siku moja. 

4.     QIYAAMUL-LAYL (KISIMAMO CHA  USIKU)
 
Mtume (SAW) anasema:
   ((من قام رمضان إيماناً واحتساباً، غفر له ما تقدم من ذنبه))  أخرجه البخاري ومسلم
  ((Atakayesimama [kwa Swalah ya usiku] kwa iymaan na kutaraji malipo, ataghufuriwa madhambi yake yaliyotangulia)) [Al-Bukhaariy na Muslim] 

5.     KUWAKUMBUKA MAFUKARA, MASIKINI, WAJANE NA MAYATIMA.

Allah ((‘Azza wa Jalla) anasema:

 وَيُطْعِمُونَ الطَّعَامَ عَلَىٰ حُبِّهِ مِسْكِينًا وَيَتِيمًا وَأَسِيرًا ﴿٨﴾ إِنَّمَا نُطْعِمُكُمْ لِوَجْهِ اللَّـهِ لَا نُرِيدُ مِنكُمْ جَزَاءً وَلَا شُكُورًا ﴿٩﴾ إِنَّا نَخَافُ مِن رَّبِّنَا يَوْمًا عَبُوسًا قَمْطَرِيرًا ﴿١٠﴾  
 Na wanalisha chakula juu ya mapenzi yao (kwa hicho wanacholisha) masikini na mayatima na mateka. “Hakika sisi tunakulisheni kwa (ajili ya) Wajihi wa Allaah, hatutaki kwenu jazaa na wala shukurani. “Hakika sisi tunakhofu kwa Mola wetu siku inayokunjisha uso ngumu nzito.  [Al-Insaan: 8-10]
 
6.     KUTOA SADAKA
Mtume (SAW) anasema:
 قال صلى الله عليه وسلم: ((أفضل الصدقة صدقة في رمضان)) أخرجه الترمذي عن أنس
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallaam) amesema:   ((Sadaqah bora kabisa ni ile inayotolewa katika mwezi wa Ramadhaan)) [At-Tirmidhiy kutoka kwa Anas]
7.     KUMFUTURISHA ALIYEFUNGA SWAWM:

Mtume (SAW) anasema: Ramadhani kama tulivyokwisha tangulia kuelezana, ni mwezi wa kuhurumiana, ni vyema muislamu kumuangalia ndugu yake mwengine ambaye Allah (‘Azza wa Jalla) huenda akawa hakumjaalia nay eye kupata cha kufungulia kinywa chake baada ya kumuelekea Allah ((‘Azza wa Jalla) kwa mchana mzima. Mtume (SAW) anasema:
 قال صلى الله عليه وسلم: ((من فطر صائماً كان له مثل أجره غير أنه لا ينقص من أجر الصائم شيء)) أخرجه أحمد والنسائي وصححه الألبان
 Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallaam) amesema: ((Atakayemfuturisha aliyefunga Swawm, atapata ujira kama ujira wake bila ya kupungua chochote katika ujira wa yule aliyefunga)) [Ahmad, An-Nasaaiy –Ameipa daraja ya Swahiyh Shaykh Al-Albaaniy]

8.     ITIKAAF
Na nivyema kukithirisha itikaaf katika masiku ya mwisho (kumi la mwisho) kama ilivyokuwa kwa Mbwana Mtume (SAW). Imesimuliwa kutoka kwa mama Aisha, Mtume (SAW) amesema:
عن عائشة – رضي الله عنها- قالت "كان النبي يعتكف في كل رمضان عشرة أيام؛ فلما كان العام الذي قبض فيه اعتكف عشرين يوماً -   أخرجه البخاري  
 Kutoka kwa 'Aashah (Radhiya Allaahu 'anhaa) kwamba: "Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akikaa I'itikaaf kila Ramadhaan katika siku kumi za mwisho, na mwaka ambao aliondoka duniani alikaa I'itikaaf siku ishirini. [Al- Bukhaariy]

9.     KULA DAKU
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
 (( تسحروا فإن في السحور بركة ))   رواه البخاري ومسلم  
((Kuleni daku kwani katika huko kula daku, kuna  baraka)) [Al-Bukhaariy na Muslim]
Na inasuniwa daku iliwe icheleweshwe kama alivyokuwa akifanya Bwana Mtume (SAW), sambamba na kukimbilia kufuturu.

10.             WINGI WA KUOMBA DU'AA
 
Ramadhaan ni mwezi wa maghfira ni vyema muislamu ajikurubishe mno kwa allah (Subhaanahu wa Ta’ala) kwa Du'aa na Istighfaar mbalimbali. Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) anasema:
  وَإِذَا سَأَلَكَ عِبَادِي عَنِّي فَإِنِّي قَرِيبٌ أُجِيبُ دَعْوَةَ الدَّاعِ إِذَا دَعَانِ فَلْيَسْتَجِيبُواْ لِي وَلْيُؤْمِنُواْ بِي لَعَلَّهُمْ يَرْشُدُونَ   
Na watakapokuuliza (Ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) waja Wangu kuhusu Mimi, basi Mimi ni Qariyb (Yu karibu daima kwa elimu Yake); Naitikia maombi ya muombaji anaponiomba. Basi waniitikie Mimi na waniamini Mimi, wapate kuongoka.  [Al-Baqarah:186]  

    MUBARAKA ALI HAMAD


2 comments:

  1. Maa shaa ALLAH ,Jazakallahu kheir

    ReplyDelete
  2. Mashaallah.... Shukrani kwa somo zuri Allah awalipe kila la kheri inshaallah

    ReplyDelete