Sunday, June 15, 2014

WASOMI WA VYUO VIKUU WAHAHA NA AJIRA, ZAIDI YA 10,000 WAWANIA NAFASI 70 TU, WIZARA YATOA TAMKO!




Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi imebaini taarifa mbalimbali zinazozungumzwa na ambazo zimetolewa katika baadhi ya vyombo vya habari kuhusu zoezi la usaili wa nafasi ya Mkaguzi Msaidizi wa Uhamiaji lililofanywa na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi tarehe 13 katika Uwanja mpya wa Taifa, Dar es Salaam

Wizara ingependa kutoa ufafanuzi kuhusu baadhi ya tuhuma zilizotolewa na baadhi ya wadau kama ifuatavyo:

1.     RUSHWA
Tuhuma za rushwa zinazoambatanishwa na zoezi hili ni hisia tu za wahusika kwani, kwanza hazina ushahidi, na pia usaili ulifanywa kufuatana na kanuni na sheria zinazosimamia ajira za watumishi wa Umma.

2.     ULINZI
Katika Uwanja wa Taifa kulikuwa na Maafisa mbalimbali toka Taasisi za Wizara ya Mambo ya Ndani ya nchi ambao walikuwepo kuhakikisha kuwa zoezi hilo linafanyika kwa usalama.

3.     WINGI WA WASAILIWA
Nafasi za Mkaguzi Msaidizi wa Uhamiaji zilitangazwa katika magazeti na Tovuti ya Wizara na Idara ya Uhamiaji kufuatana na taratibu Serikali zinazosimamia ujazaji wa nafasi za kazi katika utumishi wa umma kwa lengo la kuiweka wazi kwa umma wa Watanzania na matokeo yake wahitimu zaidi ya 20,000 walitumia haki yao ya msingi kuomba nafasi hizo.

Kufuatana na wingi wa waombaji, Wizara ilifanya zoezi la mchujo wa awali ambao hatimaye ulibakiza kiasi cha maombi 10,000 yenye waombaji wenye sifa zinazohitajika.
Aidha kutokana na wingi huo, na haki ya kila muombaji ya kupatiwa nafasi ya kushindania nafasi hizo, ilibidi Wizara ifanye utaratibu wa kutafuta eneo lenye nafasi ya kutosha ya kuweza kuwapokea wasailiwa, ambalo hatimaye ilionekana iwe Uwanja mpya wa Taifa.

Wingi wa wasailiwa ni matokeo ya kidemokrasia ya kutoa nafasi kwa kila raia kushindania nafasi za ajira zinazotolewa nchini ili mradi awe na sifa.

4.     BAADHI YA WASAILIWA KUTOKUWA NA KALAMU
Maandalizi ya usaili ni pamoja na kuwa na vifaa vya kawaida vya kushiriki usaili hivyo msailiwa aliyefika katika eneo la usaili akiwa mikono mitupu ni yule ambaye hakujiandaa, wala kuwa na kalamu haihitaji kutangaziwa.

5.     UFINYU WA ENEO
Uwanja mpya wa Taifa Dar es Salaam una uwezo wa kukaliwa na watu 60,000 hivyo idadi ya wasailiwa 10,000 waliokuwapo uwanjani hapo haikuwa tishio kwa usalama wao.

MWISHO
Nia ya Wizara haikuwa kuleta usumbufu kwa mtu yeyote ila kutoa nafasi sawa kwa walioleta maombi kushindania nafasi zilizotangazwa.

Imetolewa na:
Sgn Isaac J. Nantanga
MSEMAJI WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI

No comments:

Post a Comment