Tuesday, June 24, 2014

WAFUASI WA MOHAMMED MORSI AMBAO TAYARI WAMESHAHUKUMIWA KIFO WAFIKIA 1,263 NCHINI MISRI.






Taasisi moja ya haki za binaadamu katika nchi za Kiarabu, imetangaza kuwa majaji wa Misri wamewahukumu adhabu ya kifo watu 1,263 katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita. 

Taasisi hiyo ya kujitegemea ya ‘Majaji na Mawakili’ imewataka viongozi wa Misri kukomesha kasi ya kutoa adhabu ya kifo nchini humo. 

Taasisi hiyo imetangaza kwamba, watu 1,264 wamekwishahukumiwa adhabu hiyo tangu alipong’olewa madarakani Mohammad Morsi aliyekuwa rais wa nchi hiyo. 

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, kiwango cha hukumu ya adhabu ya kifo nchini Misri kimeongezeka mara dufu ikilinganishwa na miaka kadhaa iliyopita ambapo mwaka 2009 watu 136 ndio waliohukumiwa adhabu hiyo, huku mwaka 2010 na 2011 idadi ya watu hao ikiwa ni 134 na 115 pekee. 

Aidha ripoti hiyo imesisitiza kwamba, kiwango cha hukumu ya adhabu ya kifo imeongezeka zaidi katika hali ambayo tuhuma za wahanga hazioani na makosa yanayohalalisha adhabu hiyo. 

Siku chache zilizopita Mahakama ya Jinai ya al Minya nchini Misri ilithibitisha hukumu ya adhabu ya kifo iliyotolewa kwa wafuasi 183 wa harakati ya Ikhwanul Muslimin akiwemo kiongozi mkuu wa harakati hiyo Mohammed Badie.

No comments:

Post a Comment