Monday, June 2, 2014

SHEIKH ABDIRASHID MOHAMMAD AUAWA GARISSA KENYA; MPAKA LINI WAHADHIRI WATAENDELEA KUUWAWA?



SHEIKH ABDIRASHID MOHAMMAD AUAWA GARISSA KENYA
 
Mhubiri maarufu Mwislamu ameuawa katika mji wa Garissa kaskazini mashariki mwa Kenya.
Duru zinaarifu kuwa Sheikh Abdirashid Mohammad amepigwa risasi na kuuawa na watu wasiojulikana Jumapili usiku mjini Garissa.
Mkuu wa Polisi katika kaunti ya Garissa Charles Kinyua amesema mhubiri huyo alipigwa risasi mara kadhaa kwa karibu mita chache tu kutoka Msikiti wa Khalifa karibu na Hospitali Kuu ya Garissa.
Hata hivyo afisa huyo wa polisi amesema lengo la waliomuua bado mpaka sasa halijulikana
Aidha amedai kuwa mhubiri huyo alikuwa na wapinzani ambao hawakutaka ahubiri katika baadhi ya misikiti.
Duru mjini Garissa zinadokeza kuwa Sheikh Abdirashid Mohammad aliwahi kunusurika na shambulizi kama hilo wakati alipoviziwa katika hoteli moja mjini humo.
Katika miaka ya hivi karibuni wahubiri kadhaa Waislamu wameuawa nchini Kenya hasa katika mji wa Mombasa.
Sheikh Abdirashid Mohamed Jelani amepigwa risasi mara kadhaa kwa karibu baada ya kuondoka Msikiti Khalifa mnamo saa 20:45, Kamanda wa Polisi wa kaunti ya Garissa Charles Kinyua alisema kwa mujibu wa gazeti la The Standard la Kenya.
"Pamoja na kwamba tukio hili lilitokea usiku tu na maafisa wetu wakiongozwa na [mkuu wa kitengo cha jeshi la polisi] bado wanafanya uchunguzi zaidi, mazingira ambayo kiongozi wa dini alipigwa risasi na washambuliaji wake ni tofauti na kawaida ya mashambulizi ya al-Shabaab ambayo kwa kawaida hulenga maeneo yenye msongamano wa watu," Kinyua alisema.
Pia amesema, siku ya Jumapili polisi iliwapiga risasi na kuwauwa watuhumiwa wawili wa ugaidi katika kitongoji cha Shafshafey cha mji Mandera, Kamanda wa Polisi wa Kaunti ya Nuhu Mwivanda  .
Amesema mtuhumiwa mmoja alifanikiwa kutoroka wakati wa tukio la saa 11:00, na mabomu manane yalipatikana katika gari la watuhumiwa'.
"Tumepokea dokezo kutoka kwa wakazi na polisi walilisimamisha gari lao katika eneo la ukaguzi wa usalama," alisema. "Watuhumiwa walirusha mabomu tatu kwa maafisa wa polisi na polisi walijibu kwa kupiga risasi za moto, na kuua wawili.
Tunaamini walikuwa wanaelekea kutekeleza mashambulizi katika eneo ambalo bado walikuwa hawajaweka lengo."
Nae, mmoja wa wakazi wa Mandera Abdalla Sambul amesema kuwa wakazi walikuwa wanafanya maandamano ya amani juu ya mauaji hayo.
"Watu waliouawa ni watu maarufu huko Mandera na kitongoji cha Metameta. Wao ni viongozi wa dini ambao walikuwa wanarudi kutoka Rhamu kwa misheni ya amani kati ya koo za Degodia na Gare ambazo zinapigana," Sambul alisema.
Wakati huo huo siku ya Jumamosi, wauaji wasiojulikana walirusha vifaa vya kulipuka katika karakana moja huko Garissa, na kuua fundi moja na kujeruhi wengine wanne, Mkurugenzi wa Idara ya Uchunguzi wa Makosa ya Jinai ya Garissa Musa Yego aliiambia Sabahi.
Mafundi hao walikuwa wakitengeneza gari katika gereji hiyo mnamo saa 2 usiku wakati mlipuko huo ulipotokezea.


No comments:

Post a Comment