Thursday, June 5, 2014

UKAWA WAZIDI KUITAFUNA SERIKALI



KILA MTANZANIA ANADAIWA SHILING LAKI SITA (600,000)

Vyama vya upinzani nchini Tanzania vimezidi kuisakama Serikali vikisema kuwa hivi sasa kila mtanzania ana deni la Shilingi 600,000 kutokana na fedha zilizokopwa kuendeshea warsha, semina, safari, mafunzo na matengenezo ya magari.
Vyombo vya habari nchini Tanzania vimemnukuu Waziri Kivuli wa Fedha, James Mbatia akiwasilisha taarifa ya kambi ya Upinzani bungeni na kusema kuwa, deni la taifa limeongezeka kwa Shilingi trilioni 8.2 kwa kipindi cha miezi saba tu na kwamba ukiligawanya deni hilo kwa idadi ya Watanzania milioni 45, kila mwananchi atakuwa anadaiwa Shilingi laki sita (600,000).
Vyombo hivyo vimeongeza kuwa, karibu fedha zote zilizotengwa na Wizara ya Fedha kwa mwaka wa fedha wa 2014/15, zitatumika katika kulipia Deni la Taifa.
Aidha vimesema, kati ya Shilingi trilioni 5.8 za bajeti ya Wizara ya Fedha mwaka 2014/15, Shilingi trilioni 4.3 zimetengwa kwa ajili ya kulipia Deni la Taifa.
Wapinzani hao pia wamesema, ingawa serikali ya Tanzania inasema kuwa deni hilo linavumilika, lakini linaonekana kuwaelemea Watanzania kwani hata mapato ya ndani yamezidiwa na matumizi ya kawaida hivyo kuifanya Serikali kukopa hata kwa ajili ya warsha, semina, safari, mafunzo na matengenezo ya magari.



No comments:

Post a Comment