DHANA YA LUGHA KIENZO NA UMUHIMU WAKE KATIKA
UTENGENEZAJI WA KAMUSI
Katika
kujadili mada hii tutaangalia dhana ya lugha kienzo kama ilivyojadiliwa na
wataalamu mbalimbali, mifano ya lugha kienzo kutoka katika kamusi, umuhimu wa lugha
kienzo na mwisho tutatoa hitimisho juu mada hii.
Dhana
ya lugha kienzo imejadiliwa na wataalamu mbalimbali, miongoni mwa wataalamu hao
ni pamoja na:
Bwenge
(1995) kama alivyonukuliwa na Mdee (1997) wanasema kuwa lugha kienzo ni lugha
au ni mtindo utumikao kufasili au kueleza leksimu za lugha. Kwa kifupi lugha
kienzo ni lugha itumikayo kuifafanua au kuifasili lugha. Anaendelea kusema
dhima ya lugha za lugha kienzo ni: kueleza lugha kwa ufasaha, utoshelevu , kwa
muhtasari na uwazi ili kumwezesha mtumiaji
kupata na kuelewa mara moja kile anachokitafuta bila kumchosha akili.
Fasili
hii inaelezea dhana ya lugha kienzo kwa ujumla katika lugha, lakini hata hivyo kamusi nayo ina lugha
inayotumiwa kuelezea taarifa mbalimbali zinazohusu kidahizo ambazo huingizwa
katika kamusi. Lugha hii ndio huitwa lugha kienzo ya kamusi.
Lugha
kienzo ya kamusi kwa mujibu wa Mdee (1992) akinukuliwa na Mdee (1997) ni lugha
ya mjazo au msimbo inayotumiwa kueleza vidahizo katika kamusi. Lugha hii ndio
anayoitumia mtunga kamusi kutoa maelezo ya kisarufi, ya kimaana ya kidahizo,
maelezo amabayo mtumiaji wa kamusi huyatafuta anaporejelea kamusi. Anaendelea
kufafanua kuwa lugha kienzo ya kamusi hujengwa kwa maneno, vifupisho vya
maneno, alama za vituo, na alama mabalimbali kadri ya mahitaji ya kamusi,
tarakimu , herufi n.k amabazo zimesimbwa dhana za kilekskografia.
Kulingana
nafasili hii lugha kienzo ya kamusi huchukuliwa kama msimbo, kwa maana kwamba
lugha kienzo ya kikamusi haiwezi kueleweka kwa mtu wa kawaida hadi asimbuliwe
maana za lugha kienzo zilizotumika katika kamusi husika. Na hii ndio sababu
kamusi nyingi hufafanua kwanza lugha kienzo ilyotumika katika ukurasa wa jinsi
ya kutumia kamusi.
Baada
ya kuangalia fasili ya lugha kienzo sasa tuangalie mifano ya lugha kienzo
inayotumika katika kamusi. Tutaangalia mifano ya lugha kienzo katika kamusi ya
TUKI (2004) na Mdee na wenzake (2011). Baadhi ya mifano ya lugha kienzo kutoka
katika kamusi hizi ni pamoja na hii
ifuatayo:
Vifupisho
agh.
– aghalabu
kd
– kidini
ms/(mse) /– msemo,
nh
– nahau,
sie/<sie>
– sielekezi.
Tarakimu
1,2,3. Zimetumika kutenga maana za maneno.
Tarakimu zilizo kwenye mabano ya mduara
(1), (2), (3), zimetumika kutenga misemo na nahau. Tarakimu za kipeo
kama vile paa1, paa2,
paa3, paa4 zimetumika
kuonesha maana mbalimbali za hiponimia.
Alama
, alama ya mkato inatenga orodha ya sinonimu na
mfuatano wa vinyambuo.
; alama nuktamkato inatenganisha fasili moja
na nyingine ya kidahizo zinazoachana kidogo, fasili na sinonimu ya kidahizo,
misemo, methali au nahau na fasili, mfano mmoja wa matumizi na mwingine,
kategoria moja na nyingine.
~ inaashiria nafasi ambayo inatakiwa kukaliwa na kidahizo
katika fungu la maneno au sentensi bila ya kurudia kukiandika. Mfano pig.a
~ana, ~iana.
Alama ya mshale huashiria vibadala
[
] kuonesha upatanisho wa kisarufi: [a-/wa-] au
uelekezi wa kitenzi [ele].
<
> kuonesha uamilifu wa vitenzi, katika Mdee na
wenzake, mfano; <ele>, <sie>
(
) kuonesha muktadha wa matumizi, mfano; dini
(din), ubaharia (bah), ushairi (ush), tarakimu za orodha ya misemo.
/
/ kuonesha
asili ya neno, mfno; /Kar/, /Kng/, /Kih/
kuonesha mnyambuliko wa neno unapoanza
baada ya maelezo ya neno kutolewa.
Pia
namna ya kufasili kidahizo katika kamusi zote hizi mbili imetokea katika
mitindo tofauti. Kwa mfano katika kamusi ya Mdee na wenzake (wameshatajwa),
mtindo wao katika kufasili kidahizo unaweza kuonekana katika mifano ifuatayo:
jaala nm
[i-] mambo yafanyikayo kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu; majaliwa.
alama nm [i-/zi-] 1mchoro unaoonesha alama 2 maksi
moja au zaidi anazotuzwa mtahiniwa baada ya
jaribio au shindano.
fundisha kt
<ele> 1 –pa mtu maarifa
fulani; elimisha 2 –pa mtu au mnyama
maelekezo au mazoezi ya kufanya kitu fulani.
tibua kt
<ele> fanya kitu kilichotulia au kutwama kivurugike kichanganyike na
uchafu k.m maji kwenye ndoo, bwawa au kisima.
Vidahizo hivihivi katika TUKI (wameshatajwa) vimefasiliwa
kwa mtindo tofauti kama ifuatavyo:
jaala nm mambo mtu afanyayo kwa uweza wake
Mungu; majaliwa
alama nm 1 mchoro au kitu cha kutambulisha kitu; ishara, athari 2 maksi.
fundish.a kt
[ele] 1 toa mafunzo; elimisha 2 wezesha mtu au mnyama kutenda kitu
fulani kwa
kumpa mafunzo au mazoezi.
tibu.a kt
[ele] vuruga kitu kilichotulia k.v maji katika kisima na kufanya yawe na
topetope.
Mtindo wa kufasili vidahizo kama inavyoonekana
umetofautiana, fasilinyingine zimefafanuliwa sana na nyingine zimeelezwa
kwaufupitu. Kwa hiyo utofauti huu wa kufasili kidahizo pia ni moja ya lugha
kienzo iliyotumika kwa mtindo tofauti katika kausi hizi mbili.
Baada
ya kuangalia mifano ya lugha kienzo inayotumika katika kamusi sasa tunaweza
kuangalia umuhimu wa lugha kienzo katika utungaji wa kamusi. Lugha kienzo
inachukua nafasi muhimu sana katika kamusi, umuhimu wa lugha kienzo ni kama
ifuatavyo:
Lugha
kienzo husaidia kuleta uwekevu katika utengenezaji wa kamusi, yaani kufupisha
maelezo yasiwe marefu. Kwa mfano matumizi ya alama na vifupisho mbalimbali kama
vile bugia kt <ele>, buluu, /King/. Hapa badala ya kusema hiki ni kitenzi
elekezi ametumia alama na vifupisho ili kuweka uwekevu, na badala ya kusema
neno buluu linaasili ya lugha ya kiingereza ametumia ufupisho ili kuweka
uwekevu, au katika neno kanisa
[li-/ya-] badala ya kusema neno hili lipo katika geli ya li-/ya emetumia
kifupisho li kuweka uwekevu.
Husaidia
kutolea taarifa mbalimbali za kikamusi kikamilifu. Kwa mfano fasili na matumizi
yake kama vile kambarau nm [i-/zi-] 1 winchi ya kuinulia vitu vizito, kali –enye ubapa
ulionolewa na unaoweza kukata kitu, -iliyochongoka: shoka limenolewa na sasa ni kali. Kwa hiyo taarifa hizi humsaidia
mtunga kamusi kuelezea kidahizo kwa ukamilifu na kieleweke vizuri kwa mtumiaji
wa kamusi, kwa kutumia vifupsho, na maelzo mafupi ya fasili na mifano ya
matumizi ya kidahizo hicho.
Huwasaidia
watengenezaji wa kamusi kutofautisha taarifa moja na nyingine kwa kutumia
mabano na alama za uelekezi. Mfano;
alama < > huonesha uamilifu wa vitenzi ambao ni <ele> na <sie>, [ ] huonesha upatanisho wa kisarufi [a-/wa-],
( ) huonesha muktadha wa matumizi,
mfano; kidini (dn), kibaharia (bah), kishairi (ush), / / huonesha asili ya neno, mfano; /Kar/,
/Kng/, /Kih/.
Husaidia
kukamilisha maelezo ya fasili hasa pale inapobainika kuwa maelezo ya fasili
bado hayatoshelezi katika kuelezea maana ya neno husika. Mfano, Balbu kitufe cha kioo kinachotoa mwanga
wa umeme; . Picha hii inafanya fasili ya
kidahizo kuwa dhahiri zaidi na hivyo ni rahisi kwa mtumiaji kujenga dhana ya
kitajwa hicho.
Lugha
kienzo humsaidia mtungaji kamusi kuitofautisha kamusi yake na kamusi nyingine.
Hii ina maana kwamba katika kufasili vidahizo mtungaji kamusi yuko huru kutumia
mtindo wake ambao utamwezesha kufasili kidahizo kwa ufasaha, uwazi na ufupi
bila kuacha uvulivuli wa maana ya kidahizo hicho. Na mtindo huu wa kufasili kidahizo ndio utamfanya kamusi
yake ionekane bora au isiyokuwa na ubora.
Pia
lugha kienzo husaidia kupamba kamusi na kuifanya iwe na mvuto kwa wasomaji. Kwa
mfano picha na michoro mbalimbali katika kamusi ya Mdee na wenzake
(wameshatajwa) imefanya kamusi hii iwe
na mvuto.
Pamoja
na umuhimu wa lugha kienzo katika utungaji wa kamusi lakini pia lugha kienzo
ina umuhimu kwa mtumiaji wa kamusi. Umuhimu wa lugha kienzo kwa mtumiaji wa
kamusi ni pamoja na:
Kumsaidia
mtumiaji wa kamusi kujua asili ya kidahizo husika hasa vile vyenye asili ya
kigeni, kwa mfano Ilani /Kar/. Kwa
hiyo mtumiaji wa kamusi ataelewa kuwa neno ilani lina asili ya kiarabu.
Kumsaidia
mtumiaji kamusi kuelewa taarifa za kidahizo kwa urahisi kama vile kategoria.
Taarifa mbalimbali za kidahizo humsaidia mtumiaji kuelewa maana ya
kidahizo kwa hurahisi.
Vilevile
lugha kienzo humsaidia mtumiaji wa kamusi kujua mipaka ya matumizi ya neno
husika. Mfano neno linatumika katika mazingira ya kidini, sheria au neno ni la
kilahaja.
Pia
humsaidia mtumiaji wa kamusi kujua kategoria mbalimbali za maneno kwa mfano. kambarau nm, bugia kt. Kwa hiyo mtumiaji anapoona maneno
haya atajua ni ya kategoria gani ya maneno.
Kwa
ujumla hakuna kamusi isiyokuwa na lugha kienzo na kila kamusi ina lugha kienzo
yake ingawaje hutofautiana kwa kiasi kidogo sana hasa katika matumizi ya alama,
vifupisho na mtindo wa kufasili kidahizo, kwa mfano alama [] katika kamusi ya
Mdee na wenzake (wameshatajwa) imetumika kuonesha upatanisho wa kisarufi
ilihali katika kamusi ya TUKI (wameshatajwa) imetumika kuonesha uelekezi wa
kitenzi. Kwa hiyo kutokana na tulivyokwisha jadili lugha kienzo ni muhimu sana
katika kamusi kwani husaidia ufafanuzi wa kidahizo ambacho ndio msingi wa kamusi
na pasipo lugha kienzo itakuwa vigumu sana kuelewa taarifa mbalimbali za
vidahizo.
MAREJEO
Mdee, J.S.
(1997). Naadharia na Historia ya
Leksikografia. Dar es Salaam: TUKI.
Mdee, J. S. na wenzake. (2011). Kamusi ya Karne ya 21. Nairobi: Longhorn
Publishers (K) Ltd.
TUKI (2004).
Kamusi ya Kiswahili Sanifu. Nairobi:
Oxford University Press
CHANZO:NENO THABITI; KISIMA CHA MAARIFA.
No comments:
Post a Comment