RAMADHANI NI MWEZI WA TOBA, JEE TUMETUBIA TOBA YA KWELI?
WASWAHILI HUSEMA “KUTANGULIA SI KUFIKA”
Sifa njema zinamstahiki Allah (SW) ambaye amenichagua mimi na wewe msomaji wa makala hii kuzaliwa ilhali tukiwa na shahada kamili ya kukubalika kuwa waislamu, na rehma na amani zimshukie mtukufu wa darja Mtume (SAW) ambaye ameletwa kuwa mkombozi wa haki, usawa na uadilifu.
Awali ya yote, tumshukuru Allah
(SW) kutujaalia kuweza kuudiriki mwezi mtukufu wa ramadhani hadi kufikia
kuukamilisha kwake. Tumuombe Allah (SW) atutaqabalie swaumu zetu, visimamo
vyetu, na ibada zetu kwa ujumla.
Allah
(SW) ametuletea mwezi mtukufu wa ramadhani, ambao umesifika kwa sifa kumtu,
kama vile; ramadhani kuwa ni mwezi wa rehma, mwezi wa maghfra (toba) au
msamaha, na nimwezi ambao waja wa Allah (SW) huachwa huru na moto.
Ni jambo
la kawaida kwa mswahili kusikika akisema “kutangulia si kufika” vivyo hivyo,
nachelea kusema kuwa tumefika safari yetu lakini huenda ikawa tumekwama sehemu fulani
au tumetangulia bila kufika safari yetu.
Tunapozungumzia “toba” tunamaanisha
kukusudia kurejea kwa Mola mlezi kwa kujiepusha
na madhambi au maasi ya aina zote huku
mja akijutia kwa yale aliyoyafanya na
kuazimia kutokurudia tena katika madhambi au maasi hayo na akitaraji msamaha wa
Allah (SW).
Kimsingi
hii ndio maana ya tauba(toba), ambayo ingembidi kila muislamu aipupie na kudumu
nayo katika maisha yake ya kila siku akitambua kuwa, suala la tauba (mja
kurejea kwa mola wake) ni suala la lazima.
Kurejea
kwa Allah (SW) ni jambo la lazima na lililogogotezwa katika kitabu kitukufu cha
Quran na Sunna ya Mtume Muhammad (SAW), kama Quran inavyothibitisha katika
(sura ya 66:8), pale Mola mlezi anaposema:
“ Enyi mlio amini! tubuni kwa Mwenyezi Mungu
toba iliyo ya kweli! asaa Mola wenu Mlezi akakufutieni maovu yenu na
akakuingizeni katika pepo zipitazo mito kati yake, siku ambayo Mwenyezi Mungu hatamdhalilisha
Nabii na walio amini pamoja naye. Nuru yao inakwenda mbele yao na pande zao za
kulia, na huku wanasema: Mola wetu Mlezi! tutimilizie nuru yetu, na
utughufirie! hakika Wewe ni mwenye uweza juu ya kila kitu. (Surat Attah'riim,
66:8)
Pia Allah mlezi amesema:
“…Na tubuni nyote kwa Mwenyezi Mungu, enyi waumini,
ili mpate kufanikiwa. (Suratun nur, 24:31)
Aidha, imegogotezwa na Mtukufu wa
darja, Bwana Mtume (SAW), pale aliposema:
“Mwenye
kutubia ni kipenzi cha Allah (S W)”
Tukiangalia maana ya toba kama ilivyofafanuliwa
hapo juu, huenda tukarejea katika msemo uleule wa waswahili usemao, kutangulia
si kufika.
Hii ni kutokana na kuwa msingi wa kimaana wa
tauba umebeba mihimili imara inayoshikilia maana hiyo, jambo linalojidhihirisha
kuwa masharti ya kukubalika kwa tauba hiyo.
Masharti hayo ni pamoja na kujuta kwa sababu ya
kufanya dhambi, Kuacha kwa haraka dhambi
yenyewe, kuazimia kutokurejea tena dhambi
hiyo baada ya kutubia na ikiwa dhambi ni katika haki ya mja, inabidi kwanza
irudishwe haki hio kwa mwenyewe au umuombe msamaha kwanza ndio utakubaliwa toba
yako na Allah (S.W)
Hapa ndipo ninapata
wasiwasi juu ya safari yetu hii ya kukamilika kwa mwezi mtukufu wa ramadhani
ambayo tayari tumetia nanga. Sijui kama kweli tumefikia kwenye toba hii ya
kweli aliyoilingania Allah Mlezi.
Katika hili, nimeona kuwa
tumeweza kugawanyika katika makundi takriban matatu. Kundi la kwanza ni kundi
la waja waliotubia tauba ya kweli, ambalo kiukweli kundi hili ni wachache
katika wengi tulioingia katika ibada hii tukufu ya Allah (SW).
Pia, wapo waliotubia ndani
ya mwezi wa ramadhani, lakini wakarejea katika maaswi baada tu ya kuindama
mwezi huu wa Shawwal, kisha wakajuta na kuzilaumu nafsi zao na kutamani
kutokurejea tena katika maaswi hayo.
Aidha, wapo wale waliomlilia
Allah (SW) ndani ya mwezi mtukufu wa ramadhani ukweli wa kumlilia, lakini wamezibatwilisha
toba zao ndani ya usiku mmoja tu wa Eidilfitri, na kurejea katika maaswi yao
kama walivyokuwa kabla ya mwezi wa ramadhani. Hawa wamekula hasara duniani na
akhera, wala haikuwa na tija biashara yao hiyo.
Ndugu yangu msomaji wa makala hii, kiuhakika
kila mmoja ni mjuzi juu ya nafsi yake, hebu nisaidie jibu la swali hili, Jee
tumefika safari yetu au kutangulia si kufika? Jibu unalokichwani mwako.
Ninamuomba Mola Mlezi atutaqabalie tauba zetu,
azithibitishe imani zetu, na atujaalie katika wale waliotubia tauba ya kweli. Ya
Allah ! badilisha maovu yetu kuwa mema, zifanye nafsi zetu kuwa ni nafsu l
mutwmainna zitakazonadiwa siku ya hukumu na mola zikiambiwa rejeeni kwa Mola
mlezi hali ya kuwa mumeridhika na kuridhiwa.
Makala hii imetayarishwa
na Muhitimu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Kitivo cha lugha za kigeni na
sayansi ya lugha.
Mubaraka Ghulaam.
Sim no.
0777663795 au0717169464
SIKILIZA
RADIO KHERI 104.1FM
“ NI FARAJA KWA UMMA FARAJA KWA WAISLAMU!”
No comments:
Post a Comment