Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim
Seif Sharif Hamad, ameonya hujuma zinazofanywa dhidi ya watalii wanaofika
visiwani humo kuwa vinaweza kuathiri uchumi wa nchi.
Amesema Zanzibar inategemea utalii kuendeleza
uchumi wake na kukuza pato la taifa, hivyo sekta hiyo ikiguswa kwa matukio ya
hujuma, itaathiri uchumi, ustawi wa jamii na sifa za ukarimu wa Wazanzibar.
Maalim Seif amesema wakati wa mahojiano na
waandishi wa habari, huku akisema kuwa kukabiliana na hujuma hizo, Serikali ya
Zanzibar inakusudia kuweka kamera za CCTV kwenye maeneo muhimu ya utalii, hasa
Mji Mkongwe ili kuwabaini wahusika wa hujuma hizo.
Kuhusu karafuu kwa maendeleo ya uchumi wa
Zanzibar, Maalim Seif amesema serikali imedhibiti magendo ya zao hilo baada ya
kuongeza bei na kuwashinda wanunuzi wengine Afrika Mashariki.
Amesema katika kuhakikisha ubora wa karafuu za
Zanzibar unalindwa na kudhibiti wauzaji wengine, serikali kupitia Wizara ya
Biashara, Viwanda na Masoko, itaweka nembo maalumu kuzitofautisha na karafuu za
maeneo mengine.
Makamu huyo wa rais ambaye pia ni Katibu Mkuu
wa Chama cha Wananchi (CUF), amesema kuhusu serikali ya umoja wa kitaifa kuwa itaendelea
kuwepo hata baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 kwa vile suala hilo ni la
kikatiba na lenye misingi maalumu.
No comments:
Post a Comment