Mikoa nchini bado inakabiliwa na changamoto ya
usimamizi kwenye mamlaka za serikali za mitaa ambazo ndizo msingi wa kutoa
huduma kwa wananchi.
Kauli hiyo imetolewa na Makamu wa Pili wa Rais
wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, wakati akifungua mafunzo ya siku tatu kuhusu
mawasiliano na uhusiano kwa wakuu wa mikoa na makatibu tawala iliyoandaliwa na
Taasisi ya Uongozi (Uongozi Institute) jijini Dar es Salaam.
Balozi Iddi, amesema wananchi bado wanalalamika
kuhusu huduma zisizoridhisha sekta ya umma na kuwapo kwa rushwa, ucheleweshaji
wa uamuzi, ubabaishaji, kukiuka maadili na kutojiamini kwa baadhi ya watumishi
wa umma, hivyo kusababisha ucheleweshaji wa maendeleo.
Amesema hayo yanatokana na kutoheshimiana na
kushirikiana baina ya viongozi na watumishi hata kusababisha misuguano ya
kiutendaji kati yao na kutia dosari katika ofisi zao.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uongozi,
Profesa Joseph Semboja, amesema mafunzo hayo ya kuimarisha mawasiliano na
uhusiano, yatafanyika pia kwa viongozi hao visiwani Zanzibar na kufuatiwa kwa
wakuu wa wilaya na makatibu tawala wao endapo bajeti ya serikali itaruhusu.
Kwa upande wake, Waziri katika Ofisi ya Waziri
Mkuu, Tamisemi, Hawa Ghasia, amesema mafunzo hayo ni kwa ajili ya mikoa yote
nchini, lakini ni mikoa 20 pekee hadi sasa ndiyo iliyothibitisha kuwapo, huku
mingine ikitoa udhuru kujumuishwa katika mafunzo yatakayofanyika Zanzibar.
No comments:
Post a Comment