Thursday, July 17, 2014

ZANZIBAR KILIO MATOKEO YA FORM SIX




Wakati watahiniwa 38,905 sawa na asilimia 95.98 ya waliofanya mtihani wa kidato cha sita 2014 wakifaulu, Zanzibar imeanguka kwa kutoingiza shule hata moja kumi bora, badala yake shule zake nne zimekuwa kati ya kumi za mwisho.

Kati ya watahiniwa waliofaulu, wasichana ni 12,080 sawa na asilimia 97.66 na wavulana 26,825 sawa na asilimia 95.25.

Kwa mujibu wa matokeo yaliyotangazwa na Baraza la Mitihani Tanzania (Necta), watahiniwa 41,968 waliandikishwa kufanya mtihani huo, lakini waliofanya ni 40,695, kati yao wa shule ni 35,418 na wa kujitegemea ni 5,277.

Akitangaza matokeo hayo, Kaimu Katibu Mtendaji wa Necta, Dk. Charles Msonde, amesema kuwa watahiniwa wa shule waliofaulu ni 34,645 wakati idadi ya watahiniwa wa kujitegemea waliofaulu ni 4,260.

Kuhusu ubora wa ufaulu kwa kuangalia madaraja ya watahiniwa wa shule, amesema inaonyesha kuwa 30,225 wamefaulu katika madaraja I-III, wakiwemo wasichana 9,954 na wavulana 20,271.

Katika mtiririko huo, daraja la kwanza, wavulana ni 2,232, wasichana 1,541. Daraja la pili, wavulana ni 6,179, wasichana 3,452 wakati daraja la tatu, wavulana ni 11,860 na wasichana 16,821.

No comments:

Post a Comment