Tuesday, July 22, 2014

TANZANIA NA JUMUIA YA KIMATAIFA KEMEENI UNYAMA WA ISRAEL



Balozi wa Palestina nchini, Nasri Abu Jaish, ameiomba Tanzania na jumuiya ya kimataifa kuikemea Israel iache kufanya mauaji ya kinyama kwa Wapalestina.

Akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari jijini Dar es Salaam kuelezea hali ilivyo nchini Palestina sasa, balozi huyo amesema kuwa mgogoro uliopo kati ya mataifa hayo si wa kidini kama unavyoelezwa, bali ni uvamizi wa Israel na kupora ardhi ya Wapalestina.

Balozi Jaish amesema inashangaza kuona Waisraeli wanavamia ardhi ya Palestina na kuwaua watu kinyama, halafu jumuiya ya kimataifa ikiwemo Marekani inawaunga mkono ikidai wana haki ya kujilinda dhidi ya maadui.

Mhadhiri mstaafu, Prof. Abdul Shariff, katika mada yake ya historia ya mgogoro huo na mazingira ya Tanzania, amesema kuwa Mwalimu Julius Nyerere aliwahi kuvunja uhusiano na Israel katika hatua ya kupinga ukatili wanaofanyiwa Wapalestina ambao wamegeuka wakimbizi katika taifa lao.

Prof. Shariff amesema kuwa inashangaza kuona mwaka 1995 kwa shinikizo la kupewa misaada na Marekani, Tanzania ilirejesha uhusiano na Israel ikidai haina tatizo na taifa hilo.

Naye Shaykh Jakala akizungumzia jukumu la ubinadamu, amesema kuwa kinachofanywa na Israel katika taifa la Palestina ni zaidi ya unyama.


No comments:

Post a Comment