Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mwantumu Mahiza, amewataka
wakazi wa Mkoa wa huo kujitokeza kwa wingi kwenye usajili na utambuzi wa watu
kwa ajili ya vitambulisho vya taifa.
Zoezi hilo ambalo linatarajiwa kuanza leo
katika maeneo ya mkoa huo, linatarajiwa kufanywa na Mamlaka ya Vitambulisho vya
Taifa (NIDA), ambapo viongozi kuanzia ngazi ya wilaya wametakiwa kutoa
ushirikiano, ili kufanikisha zoezi hilo.
Mahiza amesema atahakikisha analisimamia vizuri
zoezi hilo, ili liweze kufanikiwa, hivyo kuwaomba wakuu wa wilaya na
wakurugenzi kuhakikisha zoezi hilo linafanikiwa kama serikali ilivyoagiza.
Mkurugenzi wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa,
Dickson Maimu, amesema zoezi hilo linaingia Mkoa wa Pwani baada ya usajili
Zanzibar na Mkoa wa Dar es Salaam.
Maimu amesema mbali ya usaili, muda mwingi
utatumiwa na watendaji kuhakiki taarifa za waombaji wa vitambulisho vya taifa,
ili kuwa na taarifa sahihi za watu.
Aidha, Mkurugenzi huyo ameishukuru serikali kwa
kuwapatia fedha za kuendesha zoezi hilo, na kwamba watakapomaliza Mkoa wa Pwani
watahamia katika mikoa ya Lindi, Mtwara, Morogoro, Tanga na Kilimanjaro.
No comments:
Post a Comment