Wednesday, August 20, 2014

IDADI YA WALIOFARIKI DUNIA KUTOKANA NA EBOLA WAFIKIA 1229



GENEVA

Shirika la Afya Duniani (WHO) limetangaza kuwa idadi ya watu waliofariki dunia kutokana na maradhi hatari ya Ebola katika nchi nne za magharibi mwa Afrika imefikia 1229.

WHO limesema kuwa idadi hiyo ya vifo imeongezeka kati ya Agosti 14 hadi 16 mwaka huu, muda ambao shirika hilo limesajili kesi mpya 113 za ugonjwa huo hatari wa Ebola.

Jumuiya ya Madaktari Wasio na Mipaka (MSF) imesema kuwa mripuko wa homa ya ebola unaenea kwa kasi kuliko vile serikali zinavyoweza kukabiliana na maradhi hayo na kwamba itachukua muda wa miezi sita kuudhibiti ugonjwa huo.

Shirika la Afya Duniani limezitaka nchi zilizoathiriwa na maambukizo ya homa hatari ya Ebola kuwachunguza wasafiri wote  katika viwanja vya ndege, bandari na vivuko vya nchi kavu wanaosafiri nje ya nchi.

Hadi sasa hakuna tiba ya ugonjwa wa Ebola, homa ambayo huambatana na dalili za mtu kuhara, kutapika na kutokwa na damu.

Guinea, Liberia na Sierra Leone zimeathiriwa vibaya na homa ya Ebola ambayo sasa hivi pia imeingia huko nchini Nigeria.  

No comments:

Post a Comment