Jeshi la Polisi Zanzibar limesema linaendelea
kuishikilia kompyuta ndogo (laptop) ya waziri wa zamani wa Serikali ya
Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Mansour Yussuf Himid kwa uchunguzi zaidi wa kipolisi.
Naibu Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya
Jinai Zanzibar, Salum Msangi amesema laptop hiyo iko mikononi mwa polisi tangu
ilipokamatwa Agosti 2, mwaka huu baada ya Mansoor kukamatwa na kufunguliwa
mashtaka ya kupatikana na bunduki na risasi 407 kinyume na sheria.
Msangi amesema polisi inaendelea kuifanyia
upekuzi ili kujua yaliyomo ndani yake na imehifadhi vitu vya aina gani na iwapo
hakutakuwa na vitu vya uvunjifu wa sheria itarejeshwa kwa mhusika.
Amesema endapo watabaini kuwapo kwa vitu
vyovyote vya uvunjifu wa sheria itatumika kama kielelezo na kwamba kazi ya
kuipekua inaendelea.
Hata hivyo, amesema hatua za awali za uchunguzi
zimeonyesha kuna mambo alikuwa akiyatuma kwenye mitandao ya kijamii na
kushiriki hatua mbalimbali za mijadala inayohusu siasa na maendeleo ya jamii.
Amesema siyo kosa mtu kushiriki na kutoa maoni
katika mitandao ya kijamii lakini kuna mambo zaidi ya hapo yanahitaji
kuchunguzwa.
No comments:
Post a Comment