Mafanikio ya Mja duniani na akhera pia, yatafikiwa tu endapo
mwanadamu atajitambua kuwa yeye ni nani,
anahitaji nini, muda gani, na kwa namna gani.
Haya ni maswali muhimu ambayo mwanadamu analazimika kujiuliza kabla
ya kufanya chochote ambacho angedhamiria kukifanya. Hapa ndipo wanadamu wengi
wanapofeli katika maisha yao ya dunia na akhera pia.
Uislamu ni mfumo sahihi wa maisha ambao katu hautofanana na mfumo
mwengine wowote ulimwenguni ingawa wapo wanadamu wanatia pamba katika masikio
yao, na kuweka vizuizi katika macho yao ili wasiweze kuona ukweli wa hili. Mwenyezi
Mungu anasema katika maandiko matakatifu ya Quran, sura 41. surat fuss'ilat
(au h'a mim sajdah)
“Tutawaonyesha ishara zetu katika upeo wa mbali na katika nafsi zao
wenyewe mpaka iwabainikie kwamba haya ni kweli. Je! haikutoshi kwamba
mola wako mlezi
kuwa yeye ni shahidi wa kila kitu? (41:53)
Hii inamaana kuwa uislamu ni mfumo sahihi wa maisha ambao hauwezi
kuepukika katika maisha ya mwanadamu, vyovyote atakavyoishi na popote
atakapoishi, hata kama mwenyewe anaweza kujifanya kutokuukubali uislamu kiulimi
lakini ataukubali uislamu kiakili.
Kama tulivyokwishatangulia kueleza. juu ya maswali ya msingi katika
mafanikio ya mwanadamu, swali la mwanzo na lamsingi ni kujiuliza sisi ni nani?
Jibu la swali hili ni rahisi tu na halihitaji majibu ya kupindapinda, bali ni
kusema tu kuwa sisi ni viumbe kama walivyoviumbe wengine wa Mola mlezi, wenye
asili ya udongo na waliotokana na baba yetu Adam na mama yetu Hawwaa na
wenyekuzalikana kutokana na mchanganyiko wa maji ya uzazi ya viumbe viwili baba
na mama.
Maana hii inatufahamisha vitu muhimu vitatu, yaani; sisi ni viumbe
wa Allah, ni vizazi vya Adam na Hawaa, na tunazalika kwa njia ya mchanganyiko
wa maji ya uzazi kutoka kwa baba na mama. Maana hii inatosha kumfanya mwanadamu
kujitambua kuwa yeye ni kiumbe dhaifu na anaestahiki kumnyenyekea Allah kwa
masaa yote 24. Allah katika hili anasema:
“Enyi watu! Hakika Sisi tumekuumbeni kutokana na mwanamume na
mwanamke. Na tumekujaalieni kuwa ni mataifa na makabila ili mjuane. Hakika
aliye mtukufu zaidi kati yenu kwa Mwenyezi Mungu ni huyo aliye mchamngu zaidi
katika nyinyi. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua, Mwenye khabari” sura
ya (49:13)
Vivyo hivyo, inapaswa ifahamike kuwa lengo au kusudio la mwanadamu
hapa duniani si jengine zaidi ya lile la kumuambudu Allah (SW). mwenyezi mungu
anasema:
“Nami sikuwaumba majini na
watu ila waniabudu Mimi. Sura ya (51:56)
Falsafa hii hii ndiyo ingeweza kutumika kumfikisha mfungaji katika
lengo la ibada tukufu ya swaumu ya mwezi wa ramadhani. Swali la msingi ni lile
lile jee sisi ni nani? Jee ni wale wale waliokusudiwa kufaradhishiwa ibada hiyo
tukufu, lipi hasa lengo la ibada hiyo, na jee tumelifikia? Mola Mlezi amesema:
Enyi mlio amini!
Mmefaradhishiwa Saumu, kama
walivyofaradhishiwa walio kuwa kabla yenu
ili mpate kuchamngu. Sura ya (2:183)
Katika kauli hii ya Allah (SW) ni
wazi kuwa faradhi hii ya Swaumu imeletwa kwa watu maalumu, wenyesifa maalumu, na
kwa lengo maalumu. Hivyo, kabla ya kuangalia kufikia lengo hilo maalumu ni
vyema kujiuliza jee sisi ni katika hao watu maalumu, jee tunazo hizo sifa
maalumu, na mwisho jee hadi hivi sasa tumeonesha ishara ya kufikia hilo lengo
maalumu?
Waliostahiki kuingia katika ibada
hii ni wale walioamini, kwani hao ndio watakaofikia lengo la ramadhani ambalo
ni la uchamungu. Uchamungu ni imani ya mja iliyo moyoni mwake, juu ya utukufu
wa Allah (SW) kwa kufuata maamrisho yake na kuwacha makatazo yake sawa na
kuchunga mipaka ya Mola mlezi.
Wakati tunatathimini kufikia lengo hili la ramadhani ambalo ni
uchamungu, ni vyema kutambua kuwa ramadhani ni chuo cha mafunzo ya Umoja na
Mshikamano, Ukarimu, Upendo, Huruma, Utiifu pamoja na Unyenyekevu
kwa mola mlezi.
Haya yote ndiyo yanayomfanya mja kufikia lengo la kufaradhishwa kwa
ibada hii tukufu ya swaumu (funga).
Hapa ndio tungeweza kujitathmini juu ya lengo la ramadhani.
Kutambua kuwa mja ameweza kulifikia lengo hili inambidi ajiangalie nafasi yake
wakati alipokuwa nje ya ramadhani, ndani ya ramadhani na pia hata baada ya
ramadhani.
Ramadhani ni mwezi wa umoja, upendo na mshikamano. Ni kwa miaka mingi sasa waislamu tumeshindwa kufikia malengo yetu
kutokana na kukosekana kwa umoja thabiti kati ya waislamu wenyewe. Huu ndio
muda muafaka kwa waislamu kutokurejea tena katika mizozo, na mifarakano isiyoyalazima, ikiwa kweli tumelifikia hilo
lengo la ramadhani.
Ramadhani ni mwezi wa kuhurumiana.
Waislamu wanapaswa ndani ya ramadhani kuinamisha mioyo yao chini na kukunjua mikono
yao katika kuwaelekea wazazi na walezi, wanyonge, mayatima,
wajane, wenye madeni, pamoja na walimu wa madaarisu
mbalimbali. Mfungaji inampasa ajiangalie ni kwa kiwango gani ameweza
kuyaangalia makundi hayo kwa kadri ya uwezo wake. Kwa muislamu hili si jambo tu
katika mwezi mtukufu wa ramadhani, bali hata miezi mingine iliyosalia.
Imani yangu kwa wafungaji wote, wametambua lengo la Allah (SW) kuwafaradhishia mwezi mtukufu wa
ramadhani. Kama ndio hivyo, itakua ni jambo la ajabu kwa waislamu kupoteza nguvu
yao kwa kujinyima kula, kunywa, kustarehe na wake au waume wao wa halali,
kukesa usiku kumuelekea Alla (SW) kisha kutokuthamini nguvu yao hiyo kwa ajili
ya siku ya Iddi kugeuka siku ya maaswi.
Ninamuomba Allah (SW) atujaalie kulifikia lengo la mwezi mtukufu wa
ramadhani, azikubali ibada zetu, na atusamehe sisi na wazazi wetu.
Makala hii imetayarishwa na Muhitimu wa Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam, Kitivo cha lugha za kigeni na sayansi ya lugha.
Mubaraka Ali Hamad
Sim no. 0777663795 au 0717169464
Email: mubahamad@gmail.com
.
No comments:
Post a Comment