Friday, October 17, 2014

UMOJA WA MATAIFA (UN) WAMPONGEZA RAISI KIKWETE



Umoja wa Mataifa (UN) umempongeza Rais Jakaya Kikwete kwa uamuzi wake wa kutoa uraia wa Tanzania kwa waliokuwa wakimbizi 162,156 wa Burundi.

Pongezi hizo za UN zimetolewa na Mjumbe Maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Eneo la Maziwa Makuu, Balozi Said Djinnit wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Rais Kikwete katika Ikulu Ndogo, mjini Dodoma.

Balozi Djinnit amesema uamuzi huo wa Rais Kikwete kutoa uraia kwa  wakimbizi hao wa Burundi unathibitisha na kudumisha tunu za kihistoria ya ukarimu za Tanzania ambazo zimethibitisha mara kwa mara tangu Uhuru mwaka 1961.

Ameongeza Balozi Djinnit, kuwa“Uamuzi huo wa Mheshimiwa Rais ambao ni uamuzi wa Tanzania na unakwenda sambamba na tunu za nchi hii ya Tanzania na pia tunu za Umoja wa Afrika (AU).”

Balozi Djinnit pia amempongeza Rais Kikwete na uongozi wote wa Tanzania kwa uamuzi wake wa kupeleka askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kujiunga na Jeshi la Umoja wa Mataifa la Force Intervention Brigade (FIB) la Kulinda Amani Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Naye, Rais Kikwete amemwambia Balozi Djinnit kuwa Tanzania imeamua kutoa uraia kwa waliokuwa wakimbizi wa Burundi kwa sababu wametimiza masharti ya kuweza kuwa raia wa Tanzania, ukiwemo ukweli kuwa wakimbizi hao wamekuwa wakiishi Tanzania kwa miaka 42.

No comments:

Post a Comment