Friday, August 8, 2014

ARUSHA KICHEFUCHEFUUU!



Jiji la Arusha limekumbwa na taharuki baada ya kuibuka kwa matukio ya wanawake wanaoendesha magari kuvamiwa na kupigwa risasi na watu wasiofahamika ambao hutoweka bila kuchukua chochote.

Vyanzo vya habari mjini humo vimeeleza kuwa, hadi sasa, wanawake watatu wamekumbwa na kadhia hiyo huku mmoja akifariki.

Aidha, Jeshi la Polisi linaangalia uwezekano wa kufunga kamera ili kukabiliana na matukio ya uhalifu yanayolikumba Jiji, na kwa sasa wanaendelea na majadiliano na wadau mbalimbali ili kufanikisha hilo.

Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Liberatus Sabas, jamethibitisha kutokea kwa matukio hayo, ambayo amesema kuwa mawili yametokea eneo la Sakina kwa Iddi na moja Mbauda.

Amesema hadi sasa hawajajua sababu ya matukio hayo, ambayo walengwa wakuu wamekuwa ni wanawake wanaoendesha magari, hivyo kuiomba jamii kutoa taarifa zitakazowezesha kukamatwa kwa wahalifu hao.

Sabas, amemtaja aliyefariki kuwa ni Shamim Yulu, (30), ambaye  alipigwa risasi shingoni juzi majira ya saa 3.30 usiku wakati akikaribia kufika kwenye lango la nyumba yake maeneo ya Sakina kwa Iddi.


TANZANIA NA MALAWI SASA ZITAKUTANA MSUMBIJI






Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, amesema Tanzania na Malawi zinasubiri kuitwa kwenda Maputo nchini Msumbiji kwa ajili ya kuendelea na hatua nyingine ya usuluhishi wa mgogoro wa mpaka wa Ziwa Nyasa baina ya pande mbili hizo.

Waziri Membe amesema hayoa katika ujumbe wake mfupi kwa waandishi wa habari uliolenga  kujua ratiba ya usuluhishi huo kwa sasa baada ya Malawi kumaliza uchaguzi mkuu wake Mei mwaka huu.

 Ameongeza kuwa “Makubaliano ya mwezi Machi, mwaka huu, yalikuwa ni kuwataka wazee hao kuitisha kikao mara baada ya Malawi kumaliza uchaguzi wake

Mchakato wa kuendelea na usuluhishi wa mgogoro huo, ulisitishwa kwa muda baada ya Serikali ya Malawi kuliomba jopo la usuluhishi, lisubiri kumalizika kwa uchaguzi mkuu nchini humo ambao ulifanyika Mei mwaka huu.

Mgogoro wa mpaka wa Ziwa Nyasa uliibuliwa na aliyekuwa Rais wa Malawi, Joyce Julai mwaka juzi, kwa madai ya kwamba, eneo lote la ziwa hilo lipo upande wa nchi hiyo kinyume cha sheria za kimataifa zinazotaka kila upande kumiliki sehemu ya maji kwa asilimia 50 kama ilivyokuwa kabla ya hapo kwa miaka mingi.

 

Tuesday, August 5, 2014

SERIKALI SASA YAJIPANGA KUKABILIANA NA UPUNGUFU WA MAJI



Serikali imelenga  kuongeza upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama katika vijiji kufikia asalimia 75

Hayo yamesemwa na Waziri mkuu mheshimiwa Mizengo Pinda wakati akifungua mkutano mkuu wa kujadili utekelezaji wa miradi ya maji  vijijini uliyofanyika jijini Dar-es-salaam.

Amesema Serikali imeweka sekta ya maji katika mpango wa matokeo makubwa sasa (BRN) na kuongezea zaidi ya shilling billion 184 katika bajet ya wizara ya maji mwaka huu wa fedha na kuboresha huduma nyingine za maji vijijijni kutoka asilimia  40 hadi kufikia asilimia 51.

Pinda ameongeza kuwa tathmini ya BRN juu ya hali  ya huduma   ya maji vijijini iliyofanyika mwaka jana  ilibaini kushuka kwa hali ya upatikanaji  wa maji kutoka asilimia 57.8.hadi kufikia asilimia 40  kutokana na kuharibika kwa miundo mbinu ya maji.

Naye waziri wa maji, Profesa Jumanne Maghembe amesema kuwa, idadi ya watu waliokuwa wakipata maji zamani imeongezeka ikilinganisha na miaka ya nyuma, ambapo zaidi ya watu laki mbili walikuwa wakipata maji safi na salama lakini kwa sasa imefikia milioni mbili.

NYUMBA YA KATIBU WA BAKWATA MWANZA YANUSURIKA KUCHOMWA MOTO



Watu wasiojulikana wamechoma moto nyumba ya Katibu wa Baraza la Waislamu Tanzania (BAKWATA), Juma Mugoma mkaazi wa waliya ya Ilemela mkoani Mwanza.

Watu hao wasiojulikana wamefanya tukio hilo, kwa kuimwagia mafuta ya petrol na kuwasha moto nyumba hiyo iliyopo mtaa wa Mviringo Kitangiri mjini hapo.

Akielezea kutokea kwa tukio hilo, Mugoma amesema wakiwa wamelala na familia yake usiku wa manene alisikia kelele kutoka kwa mtoto wa ndugu yake akilalamika kwamba kuna moto unawaka sebuleni .

Mara baada ya kelele hizo alikwenda sebuleni na kukuta moto uliokuwa ukiunguza makochi, kabati na vyombo vingine, kwa kusaidiana na wasamaria wema.

Aidha, Mugoma ameongezea kuwa, anahisi tukio hilo limetokana na mgogoro wa kidini uliopo baina ya bakwata na uongozi wa muda wa msikiti wa taqwa  uliopo kata ya Nyamanoro, Wilaya ya Ilemela.

Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Kaimu kamanda wa Polisi mkoa wa Mwanza, Christopher Fuime, amekiri kutokea kwa tukio hilo na kusema kwamba bado wanaendelea na uchunguzi, na endapo utakamilika watatoa taarifa rasmi

BUNGE LA KATIBA KIZUNGUMKUTI LEO!




Bunge maalumu la katiba linatarajiwa kuanza leo njini Dodoma ikiwa ni sehemu ya pili baada ya kuahirishwa kwa muda kufuatia kupisha Bunge la Bajeti ya Serikali.

Wakati watanzania wakisubiri kwa hamu juu ya mustakbali wa mchakato wa katiba mpya, wananchi, wadau, na taasisi mbalimbali za dini na za kiserikali zimekuwa na mitazamo tofauti tofauti hasa kutokana na mwenendo wa mchakato huo.

Wakizungumza na Radio Kheri kwa nyakati tofauti na katika mikutano ya wazi na  ya siri, wadau hao kutoka bara na visiwani, wameendelea kuliombea bunge hilo, huku wakiwasihi wajumbe hao kuangalia zaidi mustakbali wa taifa badala ya kuangalia maslahi ya makundi yao.

Kwa upande wake aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya katiba, Jaji Joseph  Warioba amewataka wajumbe wa bunge hilo kuacha malumbano badala yake wajadili rasimu ya katiba ambayo mwisho wake itakuwa ni kupigiwa kura na wananchi.

Nae Mwenyekiti wa wa kamati iliyoundwa na wananchi waliohudhuria midahalo ya wazi kuhusu mchakato wa katiba mpya iliyoandaliwa na Taasisi ya utafiti na sera za Umma Zanzibar(ZIRPP), Bwana Ali Abdulla Salum amemuomba Raisi Kikwete akishirikiana na Drt. Shein kutumia hekima kuunusuru mchakato huo, kwani kama katiba mpya itakosekana Tanzania itaingia katika giza la kisiasa.