Thursday, July 31, 2014

RAISI KIKWETE KWA MARA NYINGINE TENA ATUNUKIWA TUZO YA KIMATAIFA YA NYOTA WA DEMOCRASIA AFRIKA MWAKA 2014




Rais Jakaya Kikwete kwa mara nyingine ametunukiwa tuzo ya kimataifa ya Nyota wa Demokrasia Afrika kwa mwaka huu.

Kwa mujibu wa barua aliyoandikiwa Rais Kikwete na kupokelewa Ikulu, Dar es Salaam, Rais Kikwete, amekuwa mshindi wa kwanza na kuwaacha wenzake mbali katika mchuano na marais watatu wa Afrika ambao walifikia mwisho mchuano wa kuwania tuzo hiyo.

Katika barua iliyochapishwa na  Mchapishaji na Mhariri Mkuu wa Jarida la The Voice, Pastor Elvis Iruh, akizungumza kwa niaba ya Kamati ya Tuzo 2014, amesema uongozi wa Rais Kikwete umekuwa ni hadithi ya kusifiwa ya mafanikio katika Bara la Afrika ambako hadithi za namna hiyo siyo nyingi.

Tuzo hiyo hutolewa na Jarida la The Voice na mwaka jana mshindi alikuwa ni Rais Bai Koroma wa Sierra Leone ambaye alikuwa ni mshindi wa pili wa tuzo hiyo, iliyotolewa kwa mara ya kwanza kwa Rais wa Kwanza wa Zambia, Mzee Kenneth Kaunda.

Miongoni mwa sifa zilizopelekea Rais Kikwete kutunukiwa tuzo hiyo ni kuwa msimamizi mzuri wa demokrasia, kuendelea kuhakikisha kuwa amani, utulivu na maendeleo vinaendelea kupatikana katika eneo la Afrika ambalo limepitia vipindi vingi vya migogoro na matatizo.

No comments:

Post a Comment