AL-AKHY MUBARAKA GHULAAM
01. MAANA YA FUNGA
Funga (Saum) kilugha maana yake ni ni kujizuilia.
Kisheria funga (Saumu) ni ibada ya kujizuilia kula, kunywa, na vyote
vinavyo funguzisha kama vile kuvuta sigara, kujamii, kujitoa manii, kujitapisha na mengineyo, kwa kipindi cha kati ya Al-fajri
ya kweli mpaka kuingia magharibi kwa kunuilia kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Ta’ala).
Ili saumu ya mfungaji iwe na maana na yenye
kufikia lengo, hana budi mfungaji kukizuilia (kukifungisha) kila kiungo chake
cha mwili - macho, ulimi, masikio, mikono, miguu, pamoja na fikra na hisia zake
na matendo yote aliyokataza Allah (Subhaanahu wa Ta’ala).
a)
Funga ya macho ni kujizuilia na
kuangalia aliyoyakataza Allah (Subhaanahu wa Ta’ala);
b)
Funga ya ulimi ni kujizuilia na
mazungumzo yote aliyoyakataza Allah (Subhaanahu wa Ta’ala) kama vile
kusengenya, kusema uwongo au kugombana.
c)
Funga ya masikio ni kujizuia
kusikiliza yale yote aliyoyaharamisha Allah (S.W).
d)
Funga ya miguu ni kujizuilia na kuyaendea
yale yote aliyoyakataza Allah (Subhaanahu wa Ta’ala)
e)
Funga ya fikra na hisia ni kujizuia na
fikra na dhana mbaya ambazo zinampelekea kuvunja amri na makatazo ya Allah (Subhaanahu wa Ta’ala).
Mtume (Swalla Allaahu ‘alahyi wa aalihi wa sallam) anasema:
من لم يدع قول الزور والعمل به فليس
لله حاجة في أن يدع طعامه وشرابه
“Yule ambaye haachi kusema uwongo na haachi
kufanya vitendo viovu, Allah hana haja na kuona kuwa anaacha chakula chake na
kinywaji chake’’ yaani Allah (Subhaanahu wa Ta’ala) hana haja na funga yake.
02. NAFASI YA FUNGA YA RAMADHANI KATIKA UISLAMU
Funga ya Ramadhani ni miongoni mwa nguzo za
Uislamu na ni faradhi kwa Waislamu kama inavyobainika katika aya ifuatayo:
أَيُّهَا الَّذِينَ ءَامَنُواْ
كُتِبَ عَلَيْكُمُ الصِّيَامُ كَمَا كُتِبَ عَلَى الَّذِينَ مِن قَبْلِكُمْ
لَعَلَّكُمْ تَتَّقُونَ
‘’Enyi mlioamini!
Mmefaradhishiwa kufunga (saumu) kama walivyofaradhishwa waliokuwa kabla yenu
ili mpate kumcha Mungu’’ (2:183)
Kama ilivyo katika nguzo nyingine za Uislamu,
mtu atakapoivunja makusudi nguzo hii hatabakia kuwa Muislamu japo atajiita
Muislamu na watu wakaendelea kumwita hivyo.
03. kuTHIBITI KUINGIA MWEZI WA RAMADHANI
kuthibiti
kuingia mwezi Mtukufu wa Ramadhani kutategemea moja ya mawili yafuatayo:
a) Kukamilika siku thelathini (30) za mwezi wa Shaabani.
b) Kuonekana mwezi mwandamo siku ya 29 ya mwezi wa Shaabani.
Angalizo;
Mwezi wa kuingia Ramadhani inatosha kuonwa na Muislamu mmoja mwadilifu
ama mwezi wa kumalizika Ramadhani ni lazima uonwe na Waislamu waadilifu wawili
au zaidi.
04. NANI iNAmuWAJIBIKiA FUNGA YA RAMADHANI?
Funga ya
Ramadhani inamuwajibikia kila Muislamu, ambaye ni:
i)
Baleghe
ii)
Mwenye akili
iii)
Alie katika mji wake (asiwe msafiri)
iv)
Mwenye siha (afya- asiwe mgonjwa)
v)
Asiwe na mambo yanayozuia kusihi kwa funga
(kama hedhi na nifasi kwa wanawake).
Zingatio.
Inatakikana kwa wazazi kuwafundisha kufunga watoto wao wanapofikia umri
wa miaka saba (7) na kuwalazimisha hadi ikibidi kuwapiga wanapofikia umri
wa mika kumi (10).
05. Ni akina nani WALIORUHUSIWA KUTOFUNGA
i.
Walio katika safari na wagonjwa wa kawaida.
Hawa ni wale ambao kufunga kwao kutawafanya wawe
wagonjwa zaidi. Haipendezwi kwa watu hao kufunga badala yake itawawajibikia
kuja kulipa siku hizo wasizofunga baada ya Ramadhaan.
Ama kwa upande wa Msafiri, ni safari ya siku mbili kwa
kutumia kipando cha ngamia yaani (mar-hala mbili) kwa lugha ya kitaalamu,
ambayo ni sawa na umbali wa takribani kilomita (85km).
ii.
Wanawake walio katika hedhi na Nifaas. Hawaruhusiwi kufunga, na wakifunga katika
hali hio, basi Swawm yao haitokubaliwa. Nao
pia ni lazima walipe kila siku walizoacha baada ya Ramadhaan.
iii.
Wanawake wajawazito
na wanaonyonyesha (ikiwa
watakhofu kuwa Swawm itawadhuru watoto wao au wenyewe). Na ni lazima wafunge baada ya Ramadhaan kulipa siku zao. Na
ikiwa waliacha kufunga kwa sababu tu ya kukhofia afya ya watoto wao, basi
wanapaswa kulipa na kumlisha maskini mmoja kwa kila siku moja iliyowapita
katika Ramadhaan.
iv.
Vikongwe (Vizee) na wenye
maradhi sugu (yasiyotarajiwa kupona). Kwa
wao inawatosheleza kulisha maskini mmoja kwa kila siku moja wanayoshindwa
kufunga.
v.
Iliyemzidi njaa na
akahofia kuangamia. Huyu pia ni mwenye
udhuru katika nyudhuru za kuruhusiwa kuacha kufunga, na itamuwajibikia kuja
kulipa kama kundi la kwanza la wagonjwa wa kawaida.
06. YANAYOBATILISHA (YANAYOHARIBU) SWAWM
i.
Kula na kunywa kwa makusudi. Na sio kwa
kusahau wala kwa bahati mbaya au kwa kulazimishwa, katika mchana wa ramadhani.
ii.
Kujitapisha kwa makusudi.
iii.
Mume kumuingilia Mke wake. Na pia
kumkumbatia au kumchezea hadi yakamtoka manii.
iv.
Kujitoa manii kwa makusudi kwa njia yoyote
ile. .
v.
Kupatwa na Hedhi au Nifasi kwa Mwanamke.
Hata kukiwa kutokea huko kuwa ni wakati wa kukaribia kufuturu/kufutari.
vi.
Mwenye kutia Nia ya kula wakati amefunga,
kwa sharti kuwa kaazimia tendo hilo hata kama hakulitekeleza
07. YASIYOBATILISHA (YASIYOHARIBU) SWAWM
i. Kula au kunywa kwa kusahau, kimakosa au kulazimishwa.
ii. Kuingia maji ndani ya matundu ya mwili bila kukusudia, kwa mfano wakati wa kuoga.
iii. Kudungwa sindano mwilini wakati wa maradhi.
iv. Dawa ya maji idondoshewayo machoni.
v. Kuoga na kujimwagia maji mwilini wakati wa joto kali.
vi. Kuonja chakula kwa mpishi kwa sharti asimeze kile akionjacho.
vii. Kumbusu au kumkumbatia mkeo, kwa sharti awe mtu ana uwezo wa kujizuia na kudhibiti matamanio yake.
viii.
Haitobatilika Swawm ya mtu atakayeamka na
janaba (lakini akishaamka akoge) au atakayeota mchana wa ramadhan akatokwa na
manii.
ix.
Kukoga, kupiga mswaki, kusukutua au
kusafisha pua kwa kutia maji puani bila kuzidisha.
08. BAADHI YANAYOSUNIWA KWA MFUNGAJI
1. Kula
daku.
Imepokewa
hadithi kutoka kwa Anas Ibn Maalik (Radhiya Allahu ‘anhu) kuwa amesema
Mtume (Swalla Allaahu ‘alahyi wa aalihi wa sallam): ‘’Kuleni
daku kwani hakika chakula cha daku kina baraka ndani yake’’ (Al Bukhariy na
Muslim). Na inasuniwa kuchelewesha kula daku mpaka kukaribia alfajiri.
2.
Kuharakisha kufutari (mara tu likizama jua).
Imepokewa hadithi kutoka kwa Sahl ibn Saad (Radhiya Allahu ‘anhu) kutoka
kwa Mtume (Swalla
Allaahu ‘alahyi wa aalihi wa sallam) amesema: ‘’Watu
watakuwa bado wapo katika kheri muda wa kuwa wanaharakisha futari’’ (Al
Bukhariy na Muslim).
3. Kuanza
kufutari kwa tende au maji.
Imepokewa hadithi kutoka kwa
Salmaan Ibn‘Aamir (Radhiya Allahu ‘anhu) kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alahyi wa aalihi wa sallam) amesema: ‘’Anapofutari mmoja wenu basi na afuturu kwa tende na kama hakupata
(tende) basi na afutari kwa maji kwani hakika ya maji ni kitoharisho
(kisafisho)’’ ( Wameipokea Maimamu watano).
4.
Kuzidisha kuomba dua.
Pia inasuniwa kwa mfungaji kuzidisha kuomba dua na hasa wakati wa
kufutari, kwani dua ya mfungaji na hasa wakati wa kufutari ni katika dua
zinazokubaliwa na Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Ta’ala).
09.
BAADHI YANAYOTAKIWA
AYAKITHIRISHE MUISLAMU KATIKA MWEZI WA RAMADHANI
1. Kisimamo
cha usiku (Swalah ya tarawehe)
Amesema Mtume (Swalla Allaahu
‘alahyi wa aalihi wa sallam):
من قام
رمضان إيماناً واحتساباً غُفر له ما تقدم من ذنبه
‘’Mwenye kusimama (kwa ibada) katika mwezi
wa Ramadhani kwa imani (thabiti) na hali ya kutaraji malipo toka kwa Allah (Subhaanahu wa Ta’ala) husamehewa yale aliyoyafanya katika
madhambi yake’’.
Na inafaa kwa wanawake kuhudhuria Swalah katika
misikiti maadamu watachunga na kufuata taratibu za dini (sharia). Na haifai kwa
wanaume kuwazuilia wanawake walio katika usimamizi wao kuhudhuria ibada hizo
bila ya kuwa na sababu za kimsingi zinazo kubalika kisheria, amesema Mtume(Swalla Allaahu ‘alahyi wa aalihi wa sallam):
‘‘wakiwaombeni
ruhusa wanawake zenu kwenda msikitini basi waruhusuni’’ (Muslim).
2. Kuzidisha
kusoma Qur-aan.
Mwezi wa Ramadhani ni mwezi wa Qur-aan na ndio mwezi
ulioteremshwa ndani yake Qur-aan, Amesema Allah (Subhaanahu wa Ta’ala):
إِنَّا أَنزَلْنَاهُ فِي لَيْلَةِ
الْقَدْرِ
‘’Hakika tumeiteremsha (Qur-aani) katika
laylatul-Qadr (usiku wenye heshima kubwa), (usiku wa mwezi wa ramadhani)’’
(97:1).
Na
شَهْرُ رَمَضَانَ الَّذِيَ أُنزِلَ
فِيهِ الْقُرْآنُ هُدًى لِّلنَّاسِ وَبَيِّنَاتٍ مِّنَ الْهُدَى وَالْفُرْقَانِ
‘’Mwezi huo mlioambiwa mfunge ni mwezi wa
Ramadhani ambao imeteremshwa katika (mwezi) huo hii Qur-aani…’’ (2:185).
3. Sadaka.
Pamoja na fadhila zake katika masiku yote huzidi
fadhila na thawabu zake katika mwezi wa Ramadhani. Na katika sadaka
zinazotiliwa mkazo katika mwezi wa Ramadhani ni kuwafuturisha waliofunga,
amesema Mtume (Swalla Allaahu ‘alahyi wa aalihi wa sallam):
من فطَّر صائما كان له مثلُ أجرِه غيرَ أنه لا
ينقص من أجر الصائم شيئا
‘’Mwenye kumfutarisha aliyefunga anakuwa na
malipo mfano wa malipo ya aliyemfutarisha na hayapungui malipo ya aliyefunga
kitu chochote’’. (Ahmad na Annasaiy).
4. Kufanya
Umrah.
Amesema Mtume (Swalla Allaahu
‘alahyi wa aalihi wa sallam):
‘’Umrah katika mwezi wa Ramadhani una
malipo sawa na Hijjah’’ (Muslim).
5. Itikafu
Itikafu ni kubaki msikitini bila ya kutoka
ukijishughulisha na ibada mbalimbali, inasuniwa kufanya itikafu na hasa katika
kumi la mwisho la mwezi wa Ramadhani. Imepokewa hadithi kutoka kwa Ibn ‘Umar
(Radhiya Allahu ‘anhuma) amesema;
كان رسول الله صلى الله عليه وسلم يعتكف العشر
الأواخر من رمضان .اخرجه البخاري
Alikuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alahyi wa aalihi wa sallam) akifanya itikafu siku kumi za mwisho za
mwezi wa Ramadhani. (Al Bukhariy).
6. Kuutafuta
usiku wa cheo (laylatul-qadr).
Zaidi katika kumi la mwisho la Ramadhani, imepokewa
hadithi kutoka kwa Mama ‘Aishah (Radhiya Allahu ‘anha) amesema: Amesema
Mtume (Swalla Allaahu ‘alahyi wa aalihi wa sallam):
‘’Utafuteni usiku wa cheo (laylatul-qadri)
katika siku kumi za mwisho za Ramadhani’’ (Al Bukhariy na Muslim)
Na amepokea Abu Hurayrah (Radhiya Allahu
‘anhu) kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alahyi wa aalihi wa sallam) amesema:
‘’Mwenye
kusimama katika usiku wa cheo (laylatul-qadri) kwa imani thabiti na kwa
kutaraji malipo kutoka kwa Allah (Subhaanahu wa Ta’ala) husamehewa madhambi alioyafanya (kabla ya hapo’’ (AlBukhariy na Muslim).
7. Toba.
Nako ni kurudi kwa Allah (Subhaanahu wa Ta’ala) kutokana na makosa aliyoyatenda mja na
kuomba msamaha kutoka kwake, kujuta na kuazimia kutokuyarudia tena makosa hayo.
10.
FADHILA ZA SWAUMU
1. Funga inamuokoa mtu kutokana na moto
Mtume (Swalla Allaahu ‘alahyi wa aalihi wa sallam) amesema:
"Swawm ni kinga itamukoa mja kutokana na moto (siku ya Qiyaamah)’’
Na katika hadithi nyingine
Mtume (Swalla Allaahu ‘alahyi wa aalihi wa sallam) amesema:
"Mwenye kufunga siku kwa ajili ya Allah Mwenyeezi Mungu
Atamuokoa uso wake kutokana na moto kwa umbali
wa miaka sabini"
2. Swawm ni kinga kutokana na matamanio
Amesema Mtume (Swalla Allaahu
‘alahyi wa aalihi wa sallam):
‘’Enyi kundi la vijana miongoni mwenu atakae kuwa na uwezo wa kuoa
basi na aoe, (kufanya hivyo) kutampelekea kuinamisha macho yake na kuhifadhi
tupu yake. Ikiwa hana uwezo wa kuoa basi na
afunge kwani hiyo ni kinga
kwake’’.
3. Swawm ni njia ya kumpelekea mtu peponi
Kutoka kwa Abu Umamah
(Radhiya Allahu ‘anhu) amesema kumwambia Mtume (Swalla Allaahu ‘alahyi wa aalihi
wa sallam);
“Ewe Mtume wa Allah Niamrishe mimi jambo
litakalonifaa mbele ya Allah”. Akasema Mtume (Swalla Allaahu ‘alahyi wa aalihi wa sallam) “Ni juu yako kufunga kwa hakika hakuna mfano wake"
4. Funga itamuombea mtu siku ya Qiyaamah:
Amesema Mtume (Swalla Allaahu ‘alahyi wa aalihi wa sallam
الصيام والقرآن يشفعان للعبد يوم القيامة، يقول
الصيام: أي رب، منعته الطعام والشهوات بالنهار فشفِّعني فيه، ويقول القرآن: منعته
النوم بالليل فشفعني فيه، قال: فيُشفَّعان
"Funga na Qur-aan zitamuombea mja siku ya Qiyaamah, itasema funga:
ewe Mola amejizuilia kutokana na chakula chake na matamanio yake wakati wa
mchana, basi nnamuombea msamaha, na itasema Qur-aan: amejizuilia kutokana na
usingizi wake wakati wa usiku ninamuombea msamaha. Atasema wamesamehewa’’.
5. Swawm ni kafara na msamaha kutokana na
madhambi:
Mtume (Swalla Allaahu ‘alahyi wa aalihi wa sallam) amesema:
: من صام رمضان
إيمانا واحتسابا غفر له ما تقدم من ذنبه
"Mwenye kufunga Ramadhaan kwa imani na akatarajia malipo atasamehewa
madhambi yake
aliyoyatanguliza"
11. YANAYOPASWA KUJIEPUSHA NAYO MFUNGAJI.
1. Tabia chafu na maneno maovu,
kama kusengenya, kusema uongo, na kadhalika.
2. Kuzidisha usingizi (kulala
kupita kiasi) ambao unampotezea Muislamu fursa ya kufanya ibada zaidi.
3. Kupoteza wakati mwingi katika
michezo na maongezi yasiyo na faida, na kuacha kuutumia wakati huo katika kazi
na ibada mbali mbali.
4. Kuacha kula daku au kuchelewa
kufuturu baada ya kutwa kwa jua.
5. Kufanya israfu katika vyakula
na vinywaji wakati wa kufutari.
6. Kufutari kwa vyakula vyenye
harufu ya kuchukiza, kama: vitunguu thaumu,vitunguu maji, doriani, na kadhalika
kwa kuhofia kuwaudhi Waislamu wakati mnapojumuika kwa Swalah.
7. Kutokuswali tarawehe kwa
utulivu na unyenyekevu.
12. YANAYOTAKIWA KWA KUMALIZIKA RAMADHANI.
1. Kutoa zakatul-fitri, nayo ni wajibu kwa kila Muislamu,
(mwanamume, mwanamke, mkubwa, mdogo, muungwana (huru) au mtumwa).
Watoto wadogo,Watumwa na pia Wanawake waliochini ya
usimamizi wa Wanaume itawalazimikia zakah hio wasimamizi wao. Ama Wanawake
wanaojitegemea itawalazimikia wao wenyewe.
Na inatakikana itolewe zakatul-fitri kabla ya Swalah ya iddi.
Imepokewa hadithi kutoka kwa Ibn ‘Umar (Rradhiya
Allahu ‘anhuma) amesema:
‘’Amefaradhisha
Mtume (Swalla Allahu ‘alayhi wa sallam) Zaka ya fitri (ya kumalizika Ramadhani)
pishi ya tende au pishi ya shairi kwa mtumwa na huru (muungwana), mume na mke,
mdogo na mkubwa katika waislamu, na akaamrisha (hiyo zakah ya fitri) itolewe
kabla ya kutoka watu kuelekea katika Swalah (ya iddi)’’. (Al Bukhariy na
Muslim).
Na wajibu ni kutoa pishi ya chakula maarufu katika mji
uliopo (ambayo ni sawa na uzito wa kilo mbili na gramu mia nne (2.4 kg)
takribani kwa nafaka kama mchele na mfano wake au thamani yake.
2. Takbir; inasuniwa kuleta takbir baada ya kuandama (kuonekana) mwezi
wa kumalizika Ramadhani, kuanzia kuchwa (kuzama) kwa jua mpaka wakati wa Swalah
ya iddi. Na inasuniwa kunyanyua sauti kwa wanaume njiani, masokoni na hata
majumbani.
3. Kuhudhuria swalah ya iddi, kwa wanaume na wanawake.
4. Inasuniwa kula tende kwa idadi ya (witri) au chakula chengine hafifu
kabla ya kutoka kwa ajili ya Swalah ya iddi al-fitri.
5. Inasuniwa kubadilisha njia wakati wa kwenda na kurudi kwenye Swalah
ya iddi. Imepokewa hadithi kutoka kwa Jaabir (radhiya Allahu ‘anhu)
amesema: Alikuwa Mjumbe wa Allah (Swalla Allahu ‘alayhi wa sallam) inapokuwa
siku ya iddi akibadilisha njia (ya kwenda na ya kurudia). (Al Bukhary).
6. Kuvaa mavazi bora zaidi anayoyamiliki Muislamu.
Na inatakikana kwa wale wenye familia kuwaandalia
mavazi mazuri watu wa familia zao (bila ya kufanya israfu).
7. Pia inasuniwa baada ya
kumalizika Ramadhani kufunga siku sita
katika mwezi wa mfunguo mosi (shawwali).
Amesema Mtume (Swalla Allahu ‘alayhi wa sallam):
من صام رمضان ثم أتبعه ستاً من شوال، كان كصيام الدهر
{Mwenye kufunga
Ramadhani kisha akaifuatilizia siku sita katika mwezi wa shawwali (mfunguo
mosi) inakuwa kama aliyefunga mwaka (mzima kamili).(Muslim).
Tanbihi:
Ni haramu kufunga
ndani ya siku ya Iddi. Imepokewa hadithi kutoka kwa Abu Said Al khudriy
(radhiya Allahu ‘anhu) :( Hakika Mjumbe wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allahu
‘alayhi wa sallam) amekataza kufunga katika siku mbili: Siku ya (iddi) alfitri
na siku ya (iddi) ya kuchinja (iddi l-adh‘ha).(Al Bukhariy na Muslim).
Na allah ni mjuzi
zaidi.
No comments:
Post a Comment