Muungano wa Asasi za Kiraia Juu ya Jinsia na
Katiba (GFC), umesema Katiba Inayopendekezwa imezingatia mapendekezo yao kwa
zaidi ya asilimia 90, hasa katika usawa wa kijinsia na haki za watoto.
Aidha, umewataka wananchi kuacha ushabiki wa
kisiasa na kufuata mkumbo wa kuipinga badala yake waisome na kuichambua kila
kipengele ili waielewe.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa
GFC, Victoria Mandari amesema wanaamini mafanikio yaliyofikiwa katika suala la
kijinsia pia limetokana na juhudi za muungano huo unaoundwa na asasi saba za
kiraia zikiwemo Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania (TAWLA) na Wanawake na
Sheria Afrika Mashariki (WLEA).
Amesema kwa sasa kuna kesi nyingi mahakamani za
migogoro ya ardhi na mali kutokana na utamaduni uliojengeka kwamba mwanamke
hawezi kumiliki mali na mirathi lakini kwa sasa haki sawa itakuwapo kwa sababu
Katiba hii ikipitishwa, inatamka wazi kuhusu usawa wa kijinsia.
Kwa upande wake, Mkurugenzi TAWLA, Tike
Mwambipile amesema ni vyema kila mwananchi akaisoma katiba hiyo inayopendekezwa
na kuielewa badala ya kufuata mkumbo ili muda wa kupiga kura ukifika aweze
kujua nini kinapendekezwa.