Thursday, July 31, 2014

RAISI KIKWETE KWA MARA NYINGINE TENA ATUNUKIWA TUZO YA KIMATAIFA YA NYOTA WA DEMOCRASIA AFRIKA MWAKA 2014




Rais Jakaya Kikwete kwa mara nyingine ametunukiwa tuzo ya kimataifa ya Nyota wa Demokrasia Afrika kwa mwaka huu.

Kwa mujibu wa barua aliyoandikiwa Rais Kikwete na kupokelewa Ikulu, Dar es Salaam, Rais Kikwete, amekuwa mshindi wa kwanza na kuwaacha wenzake mbali katika mchuano na marais watatu wa Afrika ambao walifikia mwisho mchuano wa kuwania tuzo hiyo.

Katika barua iliyochapishwa na  Mchapishaji na Mhariri Mkuu wa Jarida la The Voice, Pastor Elvis Iruh, akizungumza kwa niaba ya Kamati ya Tuzo 2014, amesema uongozi wa Rais Kikwete umekuwa ni hadithi ya kusifiwa ya mafanikio katika Bara la Afrika ambako hadithi za namna hiyo siyo nyingi.

Tuzo hiyo hutolewa na Jarida la The Voice na mwaka jana mshindi alikuwa ni Rais Bai Koroma wa Sierra Leone ambaye alikuwa ni mshindi wa pili wa tuzo hiyo, iliyotolewa kwa mara ya kwanza kwa Rais wa Kwanza wa Zambia, Mzee Kenneth Kaunda.

Miongoni mwa sifa zilizopelekea Rais Kikwete kutunukiwa tuzo hiyo ni kuwa msimamizi mzuri wa demokrasia, kuendelea kuhakikisha kuwa amani, utulivu na maendeleo vinaendelea kupatikana katika eneo la Afrika ambalo limepitia vipindi vingi vya migogoro na matatizo.

POLISI ALIYEFUKUZWA KAZI KWA UTOVU WA NIDHAMU AINGIA BAA NA SILAHA




Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Tarime, mkoani Mara linamshikilia aliyekuwa askari polisi wa kituo cha Moshi, aliyefufukuzwa kazi mwaka 2012 kwa utovu wa nidhamu kwa kuingia katika ukumbi wa baa akiwa na silaha.

Mtuhumiwa huyo anashikiliwa kwa tuhuma za kukutwa na bunduki aina ya riffle ikiwa na risasi tano, ambayo ni mali Kampuni ya Ulinzi ya Paroma Security, anayotuhumiwa kuitumia kufanya uhalifu katika maeneo ya mgodi wa Nyamongo.

Kamanda wa Polisi Tarime, Lazaro Mambosasa, amethibitisha kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo.

Amesema mtuhumiwa, alikuwa askari wa jeshi hilo Moshi, mkoani Kilimanjaro, na amekutwa akiwa na silaha hiyo baada ya kutoroka lindo lake na kwenda nayo katika ukumbi huo. 

Kamanda Mambosasa amesema kuwa Julai 29, walipata taarifa kutoka kwa raia wema za kuonekana mtuhumiwa maeneo ya Mtaa wa Magamaga, Kata ya Sabasaba, mjini Tarime akiwa na silaha hiyo yenye namba  58368 TZCAR 65963 ikiwa na risasi tano.

WAISLAMU JIANDAENI UCHAGUZI MKUU 2015




Waumini wa dini ya Kiislam nchini wametakiwa kujiandaa kwa ajili ya kujiandikisha upya katika Daftari la Kudumu la Wapigakura katika zoezi linalotarajiwa kuanza rasmi Desemba, mwaka huu.

Msemaji wa Jumuiya na Taasisi za Kiislam, Sheikh Rajabu Katimba, ametoa wito huo katika Baraza la Idd El-Fitri, lililofanyika katika viwanja vya Mwembeyanga, jijini Dar es Salaam.

Amesema ni wajibu wa kila muislamu kujiandikisha katika daftari hilo ili kujiandaa kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa mwakani.

Sheikh Katimba amesema awali ilidaiwa kuwa vitambulisho vya taifa ndivyo vitakavyohusika katika upigaji kura, lakini taarifa hiyo hazikuwa za kweli na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) yenyewe imezikanusha.

Nae, Mwakilishi wa Umoja wa Shule za Kiislamu, Sheikh Hashim Saiboko, amesema bado ipo dhuluma, ambayo inaendelea kutekelezwa kwa wanafunzi wa dini ya Kiislamu, hasa katika masomo ya dini.

Amesema masomo ya dini kwa sasa hayahesabiwi kwa wanafunzi wa kidato cha sita, hali inayosababisha wengine kushindwa kufikia malengo waliyojiwekea kutokana na somo hilo kutoingizwa katika rekodi ya alama

SHEIKH WA MKOA WA SINGIDA, SALUM MAHAMI AWATAKA UKAWA WAREJEE BUNGENI



Sheikh wa Mkoa wa Singida, Salum Mahami amewaomba wajumbe wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) kurejea bungeni na kuwapatia watanzania katiba itakayoendeleza amani na utulivu uliopo kwa miaka 50 ijayo.


Sheikh Salum ametoa nasaha hizo wakati akihutubia mamia ya waumini wa dini ya kiislamu wakati akizungumza na waumini hao katika uwanja wa Namfua mkoani hapo.


Amesema, UKAWA wasiporejea bungeni na kuendelea na msimamo wao, watakuwa hawaja watendea haki watanzania.


Amesema, wananchi wanashauku ya kuona wajumbe wote wamerejea katika meza ya kuijadili rasimu ya pili ya katiba ili kuwapatia watanzania katiba bora itakayowanufaisha wananchi wote.


Amesema, haoni sababu ya wajumbe wa bunge hilo maalumu kuendelea kuendelea kuvutana kwa hoja ya muundo wa serikali kuwa tatu au mbili kwani wenye haki ya kuamua muundo gani unawafaa watanzania ni wananchi wenyewe.


AL MADINA SOCIA SERVICE TRUST YAPONGEZWA KUWALISHA MAYATIMA!




Wananchi na wadau mbalimbali nchini wameipongeza Taasisi ya “Al–Madinah” kwa kujumuika kwa pamoja na zaidi ya watoto 500 walio katika mazingira magumu na mayatima katika kusherehekea siku kuu ya Eid l fitri.

Watoto hao kutoka katika vituo mbalimbali jijini Dare s Salaam walipata fursa ya kula na kufurahi kwa pamoja wakati wa karamu ya chakula cha watoto mayatima iliyoandaliwa na taasisi ya Almadinah Social Service Trust na kudhaminiwa na kampuni ya ufuaji wa umeme ya (IPTL).

Mkurugenzi wa taasisi hiyo Sheikh Ally Mubaraka aliyeandaa tukio hilo amesema, taasisi hiyo imegundua kuwa mayatima wengi hukumbwa na changamoto nyingi ambazo ni pamoja na mahitaji ya msingi yakiwemo chakula, makazi na malazi.

Wadau na wananchi mbalimbali jijini Dare s Salaam wameipongeza taasisi hiyo kwa tukio hilo la kuweza kuwakumbuka mayatima, na watoto wanaoishi katika mazingira magumu kwani nao wanapaswa kufurahi kama watoto wengine katika maisha yao.

Aidha, wameziomba taasisi mbalimbali nchini kuiga mfano huo ili kuwaondolea simanzi na majonzi watoto hao, ili waweze kuishi katika hali ya furaha na amani kama watoto wengine.