Monday, August 11, 2014

KIKONGWE (80) MIAKA 10 AISHI KWA KULA UDONGO.



Kikongwe Athumani Kulaba (80) mkazi wa Chanika jijini Dar es Salaam, amewashangaza wakazi wa eneo hilo alipobainika kuwa anakula udongo kama chakula kwa zaidi ya miaka 10.

Kwa mujibu wa kikongwe huyo aliyezungumza kwa shida, amesema kwa sasa amezoea hali hiyo, licha ya kupewa chakula kutoka kwa wasamaria wanaofika nyumbani kwake.

Amesema sababu ya kula udongo ni ugumu wa maisha alionao hasa baada ya kutelekezwa na aliyekuwa mwajiri wake na kutomlipa fedha zake.

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa Chanika, Mohamed Katungi amekiri kupokea taarifa hizo kutoka kwa jirani wa Kulaba.

Amesema baada ya jirani huyo kuona hali ya mzee inazidi kuwa mbaya, alimtaarifu mjumbe wa eneo hilo John Kanguya ili kumpeleka kituo cha afya Chanika ambapo amegundulika kuwa na Safura.

ALFRED MSOVELLA, BILA MARIDHIANO KATIBA MPYA NG`O!



Mkuu wa Wilaya ya Kongwa, mkoani Dodoma, Alfred Msovella, amesema kamwe katiba mpya haiwezi kupatikana bila kuwepo na maridhiano ya kweli kwani katiba ni mali ya wananchi na siyo mali ya wanasiasa.

Msovella, ameeleza kuwa ili kupata katiba mpya ambayo ni moyo wa nchi ni lazima pande zote zinazovutana kukaa meza moja kwa ajili ya kupata muafaka wa kweli.

Mkuu huyo wa mkoa, ametoa kauli hiyo wakati alipokuwa akizungumza na wazazi, walezi pamoja na wanafunzi wa shule ya msingi ya St. Ignatius, wakati wa mahafali ya tano ya darasa la saba yaliyofanyika shuleni hapo.  

Amesema kwa sasa kila kona wimbo unaoimbwa ni kuhusu mchakato wa vikao vya katiba mpya, ambavyo hata hivyo vinaonekana kuwa na mgawanyiko kutokana na kutokea kwa makundi ambayo hayakubaliani juu ya uendeshaji wa mijadala ya kujadili rasimu hiyo.

Awali kamati ya shule hiyo ilikuwa imemwalika Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Kassimu Majaliwa, ambaye alimkaimisha nafasi hiyo Mkuu wa Wilaya ya Kongwa, Alfred Msovella

AJIFUNGUA WAWILI WAGANDANA, WAFARIKI HAPOHAPO, MAMA MZAZI ANUSURIKA!



Neema Luswetula, mkazi wa Katoro wilayani Geita mkoani Mwanza amejifungua watoto wawili wenye jinsia tofauti wakiwa wamefariki huku wameungana sehemu ya tumbo na kifua.

Akizungumza katika wodi ya wazazi kituo cha afya cha Katoro, Mzazi huyo amesema kuwa alifika kituoni hapo Agosti 7 majira ya saa saba usiku, akiwa na uchungu na ilipofika saa 12:00 alfajiri alijifungua watoto wawili ingawa kwa bahati mbaya walikuwa wamefariki dunia.

Muuguzi wa zamu katika wodi ya wazazi, Joyce Michael, amesema kuwa Neema alifika na uchungu na kisha kupelekwa wodi ya wazazi na kwa bahati mbaya alijifungua watoto wawili wenye kilo 5.1 wakiwa wameshikana viungo vyao huku wakiwa wamefariki dunia.

Aidha, Muuguzi huyo ameongeza kuwa wakati akimzalisha Neema, amelazimika kuomba  msaada kwa mganga wa zamu, Dk. Daniel Izengo ili kunusuru uhai wa mama huyo, lakini watoto walikuwa wamefariki dunia  

Nae, Mganga wa zamu, Dk. Izengo, amesema Neema amejifungua watoto wawili walioungana viungo, na kuongeza kuwa kadi yake ya kliniki ilimtaka akajifungulie Hospitali ya Wilaya ya Geita.


WARIOBA AZIDI KUWASEKAMA WANA CCM!



Aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, a amesema si busara kutumia vibaya jina la Rais Jakaya Kikwete kuzima hoja muhimu kwa maendeleo ya taifa letu.

Akizungumza jijini Dar es Salaam, Jaji Warioba amesema hoja hujibiwa kwa hoja wala si kwa kauli ambazo haitasaidia maendeleo ya taifa.

Amesema kuwa midahalo kuhusu katiba mpya imefanyika mingi na jamii imeshaelewa lipi lenyemanufaa kwa taifa, hivyo wao ndio watakaokuwa wamwisho kuamua juu ya mustakbali wa taifa la Tanzania kwa maslahi ya kizazi hiki na kijacho.

Aidha, Jaji Warioba ameendelea kuwaasihi wajumbe wa Bunge hilo kutanguliza mbele hoja ya maridhiano ili wakamilishe kazi waliyopewa ya kuwapatia watanzania katiba yenye maslahi kwa taifa na sio kwa kikundi cha watu au chama cha siasa.


UCHUNGUZI WA UGONJWA WA MACHO BURE KUANZA LEO DAR !




 Uchunguzi wa maradhi ya moyo bure umeanza jijini Dar es Salaam leo ambako watoto 100 watakaobainika kuwa na maradhi hayo watapelekwa nchini India kwa matibabu.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mwenyekiti wa hospitali ya Regency ambako uchunguzi huo unafanyika, Dk. Rajni Kanabar amesema, watoto 100 wenye maradhi ya moyo kutoka Tanzania Bara na Visiwani watakwenda kutibiwa.

Kambi ya uchunguzi huo imeandaliwa kwa pamoja baina ya Hospitali ya Regency, Klabu ya Lions ya Dar es Salaam, na Fortis Escorts Heart Institute ya India India.

Aidha, Dk. Kanabar, amesema kambi hiyo ambayo imeanza leo itaendeshwa na mtaalamu bingwa wa maradhi ya moyo kutoka Fortis Escorts Heart Institute ya India, Dk. Ashutosh Marwah.

Dk. Kanabar, amesema uchunguzi huo vile vile utafanyika Zanzibar kuanzia Agosti 13 na 14 na kuwaomba watanzania wote kuchangamkia fursa hiyo ili wajue matatizo yanayowakabili watakapokutana na wataalamu.

Amesema wagonjwa 100 watachaguliwa kwenye kambi hiyo, kwa ajili ya kwenda kufanyiwa matibabu na upasuaji nchini India, kwa punguzo kubwa la gharama wakati wengine watafanyiwa bure.